Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Ninamshukuru Mungu kwa afya na uzima. Ninaomba nitoe mchango wangu katika hii Wizara ya Afya. Nami niungane na walio wengi kupongeza juhudi za Waziri katika hii Wizara ya Afya na Naibu Waziri wake. Kwa muda mfupi ambao wameingia kwenye Wizara hii wameonyesha uwezo mkubwa. Ninaomba niwapongeze kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanasubiri kuona imani ambayo wanayo juu yao kuona ni namna gani watapambana kuhakikisha kwamba wanapunguza gharama za matibabu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuja na Sera ya Bima ya Afya Wote. Kwa kaya yenye watu sita, ni shilingi 150,000. Ziko Kaya masikini ambazo hazina uwezo kabisa wa kumudu shilingi 150,000.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri waangalie namna Serikali itakavyosaidia kaya hizi. Wako watu ambao 150,000 kwao hawajawahi kuiona. Waende vijijini wataona. Wabunge tuko hapa, kuna watu ambao hata 50,000 hawajawahi kuiona, maisha ni magumu. Mtu kama huyu 150,000 kwa ajili ya bima ya afya hataweza. Tuwatambue ili Serikali iweze kuwasaidia watu hawa, washirikishwe, waingie kwenye bima ya afya ili wasaidiwe na Serikali.

Mheshimiwa Spika, ninaomba nizungumze. Nimesikia kuhusu upanuzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, sijasikia kuhusu upanuzi wa Hospitali ya Ocean Road. Watanzania zaidi ya 5,000 na kuendelea wanaingia ndani ya Hospitali ya Ocean Road ili kupata matibabu. Ugonjwa wa saratani hivi sasa mpaka watoto wadogo wanapa, na kwa bahati mbaya ni magonjwa ambayo mengine ni ya kurithi.

Mheshimiwa Spika, Serikali ifanye kitu Ocean Road. Mgonjwa mmoja wa chemotherapy kupata matibabu yake dripu moja ni shilingi 10,000,000, shilingi 20,000,000, shilingi 30,000,000 na kuendelea. Je, Mtanzania wa kawaida anaweza? Kama Serikali imeweza kutoa ruzuku kwenye mbolea, dizeli na petroli, Serikali ione namna gani itawasaidia wagonjwa wa saratani waweze kupata matibabu bure.

Mheshimiwa Spika, linguine, Hospitali ya Ocean Road ni ya zamani, ina vitanda 200 na havitoshelezi kabisa. Wagonjwa wengi wanalazimika kuondoka kwa sababu hakuna sehemu ya kulazwa. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, kwa nini kama Muhimbili ...

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, taarifa, taarifa.

SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza ninaheshimu sana mchango wa dada yangu anayechangia na ninampenda sana dada yangu Mheshimiwa Devotha, ila ninatambua anachojaribu kusisitiza. Niseme tu, kwenye eneo la bima na watu wasiojiweza tayari Serikali imetengeneza mkakati na ilishatenga hela kwa ajili ya kuhudumia eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, labda tuseme ni kwa kiwango gani? Kama watapatikana wote hilo ni jambo lingine, lakini ukienda kwenye Hospitali yetu ya Ocean Road, leo Hospitali yetu ya Ocean Road imefanyiwa kazi kubwa, imewekwa vifaa vikubwa ambavyo leo imekuwa ni kitivo cha rufaa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa investment iliyofanyika pale.

SPIKA: Mheshimiwa taarifa hutakiwi kuchangia.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, dada yangu ninatambua mchango wake, lakini nilisema tu nimwongezee hayo.

SPIKA: Mheshimiwa Mollel, taarifa ina utaratibu wake. Mheshimiwa Devotha unapokea taarifa? (Makofi)

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, nimemsikia lakini ninachosema, kupanga ni jambo lingine kutekeleza ni jambo lingine pia. Tunachosubiri na Watanzania wanachokisubiri ni kuona ni namna gani Serikali inasaidia kaya hizi maskini na zenyewe zinufaike na bima ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninazungumza suala la Ocean Road. Tumesikia Serikali ina mpango wa kuboresha Hospitali ya Muhimbili. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri waone ni namna gani wataboresha na kusaidia Hospitali ya Ocean Road. Wagonjwa zaidi ya 5,000 na kuendelea kila mwaka wanatibiwa pale Ocean Road. Mheshimiwa Waziri, kwa nini asiache legacy? Kwa nini asifunge macho Hospitali ya Muhimbili inaenda kutanuliwa, tayari pale kuna Hospitali ya Jakaya Kikwete, kuna Hospitali ya MOI, kwa nini Mloganzila isitumike wakawapa Ocean Road ambao hawana eneo wakafanya huduma zote pale za upasuaji, vipimo, chemotherapy, mionzi na huduma zote zikaenda Mloganzila?

Mheshimiwa Spika, ninamshauri Mheshimiwa Waziri, aone namna gani wataisaidia Ocean Road. Tuna wagonjwa wengi wa cancer na kupitia utaratibu huo wa kuipa fursa Ocean Road, nchi nyingine zozote zilizoendelea zina Cancer Institute ambazo zina mashine za kutosha zinafanya kila kitu wenyewe. Ocean Road wanategemea operations zikafanyike Muhimbili. Kwa nini tusiwe na kitengo ambacho kinajitegemea na kufanya huduma zote? kwa usikivu wa Mheshimiwa Waziri ninaoujua ninamwomba muitazame Ocean Road kwa jicho la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matibabu ya saratani ni ya bei kubwa mno. Watanzania hawawezi kumudu. Kama kweli tumeweza kutoa gharama kwenye petroli na dizeli, basi tuondoe gharama za matibabu ya cancer kwa watu wanaoumwa ...

SPIKA: Mheshimiwa Devotha, muda wako umekwisha. Malizia, halafu unga mkono hoja.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, ninamalizia kwa kuomba Serikali iondoe gharama za matibabu kwa wagonjwa wa cancer. Ahsante sana.