Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, niunge mkono hoja. Pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama leo katika Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia hoja tuliyonayo mezani ya Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyoweka kwangu kuniteua ili niweze kumsaidia katika nafasi hii ya Unaibu Waziri wa Afya. Ninamwahidi Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba, nitaitumikia nafasi hii kwa unyenyekevu mkubwa, kwa heshima kubwa. Nitajituma ili kuhakikisha kwamba ninaweza kutimiza yale maono. Imani aliyoiweka kwangu nitailipa kwa imani kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa kuteuliwa kutumikia nafasi hiyo ili kuweza kumsaidia Mheshimiwa Rais kwenye nafasi hiyo ya Umakamu wa Rais.
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri na kubwa anayofanya. Wote tumeona jinsi gani anafanya ili kumsaidia Rais katika nchi yetu. Ziara anazofanya, jinsi anavyosikiliza wananchi katika hoja zao na shida zao. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa, mtu kazi. Ninasikia fahari, ninasikia furaha kufanya kazi na Mheshimiwa Waziri. Miongozo yake maelekezo yake, lakini msimamo wake wa kuhitaji matokeo kwanza ananipa hamasa na tija ya kuendelea kutumika zaidi. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakupongeza wewe kwa kuchaguliwa kuliongoza Bunge hili Tukufu, Naibu Spika lakini na Wenyeviti wote wa Bunge, kwa jinsi ambavyo mnaliendesha Bunge hili kisasa kabisa. Hongereni sana ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawapongeza pia watumishi wote wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Makatibu Wakuu, CMO, Wakurugenzi wote wa taasisi, lakini na watumishi wote wa afya katika nchi hii. Ukiwa na maumivu au ukiwa unaumwa huwezi kupata furaha. Ninawahakikishia watumishi wote wa afya, kazi yao ya wito watalipwa na Mungu. Waendelee kuchapa kazi kwa bidii kubwa sana, sisi tunawategemea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shukrani na pongezi zote tulizopewa humu zinawastahili wao watumishi wa afya, kwa sababu pale ambapo wananchi wanahitaji shida yoyote, tukiwaomba wanaitekeleza kwa wakati. Kwa hiyo, watumishi wote wa afya nchi nzima wanastahili pongezi hizo na shukrani na waendelee kuchapa kazi ili ile azma ya Mheshimiwa Rais aliyoisema ya kuacha tabasamu kwa Watanzania pindi atakapoondoka mwaka 2030 iweze kufikia. Huwezi kupata tabasamu ukiwa na maumivu.
Mheshimiwa Spika, ninakishukuru sana Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniteua niweze kupeperusha bendera katika nafasi hii, lakini kipekee wananchi wa Jimbo la Muhambwe ambao wameendelea kuniamini kwa awamu nyingine hii ya pili. Ninawahakikishia wananchi wa Muhambwe kwamba niko gado niko na nguvu zangu kabisa za kuwatumikia kuliko mwanzo. Nitasimamia yale tuliyokubaliana ili tuweze kuyatekeleza Muhambwe kwa ajili ya maendeleo, tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru pia wasaidizi wangu wote wanaonisaidia, Katibu wangu Juliana, dereva na wasaidizi wote. Wao wamesababisha kazi yangu iwe rahisi kwa kunisaidia kwa karibu sana. Ninawashukuru sana na Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho siyo kwa umuhimu, familia yangu ikiongozwa na mume wangu Sadock Mugendi na watoto wangu, kwa ushirikiano wanaonipa, upendo wanaonipa na maombi yao yamenifanya niendelee kufanya kazi zaidi na wakati wote nisikie kama sijachoka, ili niweze kutimiza majukumu yangu. Waendelee kuniombea na kunivumilia. Nipo kazini ninachapa kazi kutimiza maono ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitajikita sasa kwenye kuchangia baadhi ya hoja, lakini hata hivyo ninaendelea kuishukuru Kamati yetu ya Bunge kwa michango yao na hoja zao wanazotupatia kwenye Kamati. Zinaendelea kutuimarisha na kuona wapi tuongeze bidii. Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa sana, michango yote ya Waheshimiwa Wabunge tumeipokea kwa umuhimu wake mkubwa na tunawathibitishia, hata kama hoja haijajibiwa hapa leo, ninaomba niwahakikishie tumeziandika hoja zote na changamoto zenu, kwa sababu michango yao inawakilisha Watanzania wote. Tutaifanyia kazi kwa umuhimu wake mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, basi nijielekeze kwenye hoja chache. Hoja ya kwanza ni huduma za mama na mtoto ambao Wabunge wangu wamechangia. Hapa kipekee ninamshukuru Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kweli yeye ndiye kinara wa kupunguza vifo vya mama na mtoto katika nchi hii. Tumejionea akiendelea kupewa tuzo, akiendelea kutunukiwa tuzo mbalimbali kwa sababu ya jinsi ambavyo ameamua kwa dhati kabisa kupunguza vifo vya mama na mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sikusudii kurejea takwimu kwa sababu wengi wamezitaja, isipokuwa nitaenda kwenye hoja ya ombi la mama kujifungua kwa staha, lakini na kuwa na mwambata. Waheshimiwa Wabunge ninaomba niwathibitishie tumeshalifanyia kazi jambo hili. Kati ya vituo 8,019, tayari vituo vyetu 1,244 vinatoa huduma hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuhakikisha kwamba vituo vyote viweze kutoa huduma kwa sababu kwa mujibu wa takwimu za WHO zinaonyesha kwamba, pale mama anapokuwa na mwambata basi mambo mengi yanakwenda vizuri zaidi. Kwa hiyo, ninawathibitishia tunalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia jinsi gani hatujafanya vizuri kupunguza vifo vya watoto wachanga ambao tumepunguza kwa digit moja kutoka vifo 25 katika vizazi hai 1,000 mpaka vifo 24 kwenye vizazi hai 1,000. Ni kweli, lakini ninawahakikishia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaliona hilo na pale 2018 WHO walipoleta tathmini na kusema ni lazima tuwe na vyumba au wodi kwa ajili ya kuhifadhi watoto wachanga waliozaliwa chini ya uzito pungufu, kwa maana ya njiti.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2018 tulipoanza tulikuwa na vyumba 14 nchi nzima ambavyo vinaweza kutunza watoto wachanga. Leo hii tuna vyumba 438 nchi nzima. Huu ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kipindi hiki cha Awamu ya Sita ili kuhakikisha kwamba watoto wachanga wanakuwa salama hata kama watazaliwa na uzito pungufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hajaishia hapo, mwaka huu 2026 tunajenga vituo 37 na kwa ubora zaidi vituo hivi navyo vimeboreshwa. Kwa mujibu wa utafiti wa WHO imeonyesha kwamba, mama anapojifungua mtoto ambaye ana uzito pungufu na akatengwa kuishi na mtoto wake, basi chance ya mtoto kufariki ni kubwa kuliko akiwa na mama yake. Akina mama wengi wanaojifungua watoto njiti wanapata sonona (depression) pale unapomtenga yeye na mtoto wake.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo mwongozo wa WHO ni mama anapojifungua mtoto chini ya uzito akae na mtoto wake. Kwa hivyo, vituo hivi 37 vimezingatia vigezo hivyo. Vinajengwa nchi nzima vituo 37 kwenye hatua mbalimbali. Vituo 17 kwenye hospitali za mikoa, lakini vituo 20 viko kwenye hospitali ngazi ya halmashauri.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji huu unaendana na uwekezaji wa vifaa kwa maana ya Radiator Warmer, kwa ajili mtoto anahitaji joto, CPAP na Oxygen Concentrator kwa sababu mtoto anahitaji oksijeni. Lakini Phototherapy kwa sababu watoto wengi wanatengeneza manjano ili waweze kupata matibabu.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji huu utapelekea tupunguze vifo vya mtoto mchanga kwa 50% na tutafikia vifo 12 kama ambavyo malengo ya maendeleo endelevu yanataka, kwa maana ya SDGs. Tukipunguza kwa 50% ninaomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge, tutapunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa sababu kwa sasa tuna vifo 43 kati ya vizazi hai 1,000. Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kwamba vifo hivi vinasababishwa na vifo vya watoto wachanga, kwa maana ya 0 – 28. Kwa hiyo, uwekezaji huu wa vyumba au wodi za watoto wachanga utapunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa 50%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakwenda kufikia lengo la SDGs la kuwa na vifo 25 kwa vizazi hai 1,000 vya watoto under five. Ujenzi huu unaendelea mahali tofauti tofauti Waheshimiwa Wabunge, wakienda kwenye majimbo yao watajionea.
Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi wamechangia kuhusu huduma ya dharura. Huduma ya dharura ni huduma mgonjwa anayoipata ndani ya saa moja, tunaita Golden Hour. Hii ni saa ambayo mgonjwa akipata huduma, basi umeokoa maisha yake kwa 60%. Kumtoa kwenye eneo la dharura, kumpa oksijeni, kumpa maji na kumpa huduma zote za msingi anazotakiwa mgonjwa kuzipata kwa dharura.
Mheshimiwa Spika, tumefanya nini? Mwaka 2021 tulikuwa na vyumba au wodi za dharura saba tu nchi hii. Leo tunavyoongea tunazo 125. Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kuokoa maisha ya Watanzania ndani ya Golden Hour waweze kupata huduma muhimu. Nimewasikia Waheshimiwa Wabunge wengi wakisema jinsi gani huduma za dharura zinapatikana pale pale mapokezi anapokuwa sawa ndiyo anajulikana aende wodi gani. Hii itakwenda kuokoa maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hiyo, tumeongeza magari ya dharura (ambulance). Mwaka 2021 tulikuwa na magari 540. Hadi Machi, 2026 tunayo magari 1,267. Ikiwa hiyo haitoshi, tumenunua boti saba kwa ajili ya maeneo ya majini ambazo zimepelekwa kwenye maeneo tofauti tofauti ili nao waweze kupata huduma za dharura kupitia boti.
Mheshimiwa Spika, mwisho, tumetoa pikipiki 300 nchi nzima kwenye halmashauri ambazo zinaenda kutoa huduma za chanjo nchi nzima ili Watanzania waweze kupata huduma bora.
Mheshimiwa Spika, wako Wabunge wengi pia wamechangia hoja ya rasilimali watu. Ni ukweli usiopingika huwezi kutoa huduma bila kuwa na rasilimali watu, lakini hapa ninampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kuanzia mwaka 2021, mpaka leo ameajiri watumishi wa Sekta ya Afya 53,633. Hii ikiwemo watumishi 5,000 ambao wameajiriwa mwezi Januari kupelekea ahadi yake aliyotoa wakati wa kampeni.
Mheshimiwa Spika, hivyo sasa, tunao watumishi wa Sekta ya Afya nchi nzima 182,430. Tunaendelea kuongeza watumishi hawa hasa mabingwa na bingwa bobezi. Kupitia Samia Health Super Specialization, wako watumishi 1,483 wanaosoma ndani ya nchi na nje ya nchi ambao wanasoma kwa ajili tuendelee kupata watumishi mabingwa.
Mheshimiwa Spika, kumtengeneza Daktari Bingwa Bobezi inachukua zaidi ya miaka 10 mpaka 14. Kwa hiyo, Wabunge wanaweza wakaona siyo rahisi sana kuwapata, lakini Serikali imeamua kwa dhati kuhakikisha kwamba tunawapata watumishi wao. Hata hivyo, tunaendelea kuwaomba viongozi wetu Wakurugenzi wa Halmashauri waendelee kuwaruhusu watumishi wanaotaka kujiendeleza katika fani mbalimbali ili tuweze kupata watumishi wa kutosha kwenye hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunao mpango wa kufanya msawazo kwa ajili ya hospitali za kanda ambazo zimeonekana bado zinatoa huduma chache za kibingwa, ikiwemo Hospitali ya Lindi ambayo bado inatoa huduma tatu, Hospitali ya Sumbawanga inatoa huduma tano na Hospitali ya Tabora inatoa huduma sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba tuwaahidi Waheshimiwa Wabunge, tulikuwa na mpango huo, kwa hivyo tutafanya msawazo ili tukabiliane na hiyo changamoto. Kwa sababu, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alituelekeza wakati akihutubia Bunge, kwamba tuongeze huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba, hapo awali nchi hii ilikuwa na huduma nne tu, lakini sasa Wizara ya Afya tumejipanga chini ya Waziri wetu, mtu kazi na tumeshatoa mwongozo kutoka huduma nane mpaka 17. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ninawathibitishia kwamba tupo kazini kuhakikisha kwamba huduma hizi zinafika kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutaenda mbali zaidi, kwenye hospitali za halmashauri tunataka wawe na huduma tano. Lengo ikiwa ni kwamba huduma za kibingwa ziweze kupatikana kuanzia katika ngazi ya halmashauri. Kwa hivyo, tunaendelea kujipanga kuhakikisha tunatimiza malengo na maono ya Mheshimiwa Rais ambaye amekusudia tupeleke huduma za kibingwa kwa Watanzania ili tupeleke huduma kwa Mtanzania. Amesema Watanzania wasizifuate huduma, bali huduma ziwafuate Watanzania. Kwa hivyo, kwa kufanya hivyo madaktari hao bingwa watakwenda kuwahudumia Watanzania kule walipo kuanzia kwenye ngazi ya halmashauri.
Mheshimiwa Spika, ili uweze kutoa huduma za kibingwa unahitaji mambo kama matatu au manne. Kama nilivyoanza kueleza, unahitaji rasilimali watu wenye weledi wa kufanya kazi, unahitaji miundombinu yenye uwezo wa kuwezesha hiyo huduma ifanyike na unahitaji wataalam...
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, malizia.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, unahitaji wataalam wenye huduma bobezi.
Mheshimiwa Spika, tumeendelea kuboresha huduma za miundombinu kwenye hospitali zote za rufaa, hospitali maalum na hospitali za mikoa. Waheshimiwa Wabunge, ninaomba niwathibitishie, hata kama hapa haujatajwa, lakini ninaomba niwaambie kila mkoa una kitu umepata.
Mheshimiwa Spika, nimepanga kwa mikoa michache hapa niwaelezee, lakini kwa sababu ya muda ninaomba waridhie niseme michache. Kwanza tuna Hospitali ya Mkoa ya Kitete ambao umepangiwa shilingi bilioni 4.5 kwa sababu ya jengo la watoto wachanga, lakini tuna shilingi bilioni 3,000,000,000 kwa sababu ya kumalizia jengo la mama na mtoto. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Tabora tumewasikia na tumelifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunayo Hospitali ya Rukwa, tunayo shilingi bilioni 2.1 ambayo shilingi bilioni moja inakamilisha jengo la damu salama na shilingi bilioni 1.5 unaanzisha jengo la hospitali mpya. Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Rukwa tunakwenda kutekeleza hiyo miradi. Rukwa wanayo shilingi 542,000,000 ambayo tunaenda kuanzisha huduma ya Dialysis, itanunua mashine na itafanya ukarabati wa chumba. Tunayo pia shilingi bilioni 4.7 ambayo inakwenda kujenga jengo la taaluma kwenye Chuo cha Afya kilichopo Sumbawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Dodoma tunayo shilingi bilioni 4.7 kwa sababu ya jengo la watoto wachanga, lakini tunayo shilingi 7,000,000,000 kwa ajili ya Benjamini Mkapa kwa ajili ya kuendeleza huduma za upandikizaji figo. Tunayo shilingi 2,000,000,000 kwa sababu ya Hospitali ya Mirembe.
Mheshimiwa Spika, tunayo shilingi bilioni 4.7 kwa sababu ya jengo la taaluma katika Chuo cha Mpwapwa; Hospitali ya Mara, hospitali ya kumbukumbu...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, maelekezo ya kiti muda wako umekwisha.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, ninaomba Wabunge waridhie kwamba tupo hapa na nitawasikiliza na kuwaonesha nini wamepangiwa kwenye mikoa yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)