Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ninaomba kuchukua fursa hii kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa kuzungumza na kwa maandishi. Kwa niaba ya Wizara ana Sekta ya Afya tumepokea maoni, tumepokea ushauri na tumepokea hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa unyenyekevu mkubwa na kwa dhamira ya utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, michango iliyotolewa hapa ni michango takribani ya Wabunge 59, lakini nimeshuhudia namna ambavyo kila Mbunge alitamani kuzungumza kwa niaba ya wananchi wake. Hakika Wabunge wa Bunge hili wamedhamiria kwa dhati kabisa kusimamia wananchi waliowaleta hapa Bungeni, ninawapongeza sana sana Waheshimiwa Wabunge kwa kazi kubwa na kazi nzuri hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa ufafanuzi wa hoja za Kamati ya Kudumu ya Afya na Masuala ya UKIMWI, pamoja na hoja za Waheshimiwa Wabunge, ninapenda niwatambue Waheshimiwa wote waliochangia; Wabunge 59 waliochangia hotuba yangu na kati ya Wabunge hao Waheshimiwa Wabunge 50 wamechangia kwa kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wanne wamechangia kwa maandishi akiwemo Mheshimiwa Thomas Kampala Maganga.
Mheshimiwa Spika, nimthibitishie kwamba kwa hoja alizozitoa Wizara ya Afya itashirikiana na Wizara ya Ujenzi ili kusudi tuweze kuona ni namna gani tunaweza tukatengeneza njia nyingine ya kuunganisha kutoka pale Daraja la Jangwani kuelekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Tumepokea hoja hii kwa mikono miwili kabisa.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja za Wizara wamewasilisha maoni, lakini wamewasilisha ushauri na hoja zilizojikita katika maeneo makubwa tisa; eneo la Bima ya Afya kwa wote, Wabunge zaidi ya 16 wamechangia kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, wakiwawakilisha wananchi wao katika maeneo yao ambapo Waheshimiwa hawa Wabunge na wawakilishi wa wananchi wanatoka.
Mheshimiwa Spika, ipo miundombinu ya kutolea huduma ya afya; Wabunge zaidi ya 38 wamezungumzia kuhusu miundombinu, kuhusu ujenzi wa hospitali, lakini wapo waliopongeza kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi hiki cha Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi ndani ya Serikali tunatambua kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia, atakumbukwa na huu ndiyo ukweli. Inawezekana wapo Watanzania wasiotamani kusikia maneno haya, lakini tunawaambia ukweli, toka Taifa hili lipate uhuru vituo vya afya vilikuwa ni 7,000 tu vya Serikali, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake amejenga vituo vya afya 3,530. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maono haya tunakiri kabisa kwamba dhamira ya Baba wa Taifa katika ndoto dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi. Kama Baba wa Taifa angekuwa hai leo, yeye mwenyewe angekuwa ni shuhuda wa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi hii ni nchi inayobeba misingi ya ujamaa na huo ndiyo ukweli. Nchi hii inabeba misingi ya ujamaa na tunaweza kwa namna moja au nyingine tukawa tume-overlap au bado tupo nyuma, lakini ukweli ni kwamba Taifa hili ni Taifa ambalo viongozi lazima tujitoe tufanye kazi kwa bidii kwa ajili ya wananchi, lazima tujitoe. Kwa hiyo, ukiangalia takwimu, Watanzania watamkumbuka Mheshimiwa Rais Samia, kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunasema nchi hii ni nchi ya kijamaa. Nchi hii ni nchi ya kusaidiana, nchi hii ni nchi ya kutegemeana, nchi hii imebeba misingi ambayo sisi viongozi wa kuteuliwa ni lazima tufanye kazi kwa bidii. Hakuna neno lingine, hakuna neno linguine, tunapofanya kazi kwa bidii tukakusanya kodi itasaidia Taifa letu kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine Waheshimiwa Wabunge wanabeba ajenda za wananchi, wanakuja hapa Bungeni wanazungumza kuhusu kero zinazowakabili wananchi na sisi ndani ya Serikali tunaziona kabisa kero hizi zina mantiki na pengine tunasema tumechelewa sana kutekeleza au kwenda kuwasaidia wananchi katika maeneo ambapo Waheshimiwa Wabunge wanatoka katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, haikubaliki hata kidogo, haiwezekani Mkoa kama Shinyanga ambao kuna wadau wa maendeleo, ambao kuna wadau wa madini, leo hii tunalia kwamba tunahitaji shilingi 200,000,000 ya kutengeneza chumba cha Dialysis na viongozi wa mkoa pale wapo, Mganga Mkuu wa Mkoa pale wapo, tuna wadau wa maendeleo pale wapo, zipo benki. Tunajiuliza wakati mwingine ni lazima tuwajibike, tuziangalie kero za wananchi kama kero zetu sisi wenyewe viongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi kweli leo hii Mkoa kama wa Shinyanga wanasubiri bajeti ya mwaka ujao wa fedha kuomba shilingi 200,000,000 au 300,000,000 kuokoa maisha ya Watanzania ambao figo zimefeli na pale kuna viongozi, hii haikubaliki. Ninawaambia ninawapa mwezi mmoja watu wa Shinyanga, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge amezungumza hapa haikubaliki, haikubaliki hata kidogo.
Mheshimiwa Spika, nchi hii ni ya kijamaa ni lazima tujipange, tujikusanye sisi wenyewe tutafute fedha. Mwalimu Nyerere alikwisha sema Taifa hili haliwezi kuendelea bila kushirikisha wadau wa maendeleo, si maneno yangu ni ya Mwalimu Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo tunakaa kujadili shilingi 200,000,000 kuokoa maisha ya wananchi ambao figo zimefeli na pale kuna viongozi wa mkoa, tuna madini pale, tuna wadau wa madini, tunashindwa kama mkoa hata kuhitisha harambee tukawaomba wadau mabenki ambayo yamekuwa yakifanya kazi ya kusaidia kujenga majengo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wangu, viongozi wa Wizara ni lazima wajipange, kweli kweli sitakubali, hili ninalisema wazi sitakubali. Ninatoa mwezi mmoja katika maeneo haya, wakishindwa kujipanga nitawaweka kando, nitawaweka kando. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rufaa yeye na timu yake, haiwezekani Watanzania waendelee kufa tunasubiri Bunge lijalo kujadili maombi ya shilingi 200,000,000 ambayo hata wadau wa maendeleo tukiwaomba wanaweza kutupatia hizo fedha. Hii haikubaliki na wakati wangu siwezi kuiruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesema hapa nchi hii ni nchi ya kijamaa. Yapo mambo ndani ya Wizara yanatokea ambayo wakati mwingine hayapo hata kwenye bajeti na ndiyo maana tumekuwa tukisisitiza sana sana kwa Watanzania tuwape viongozi nafasi ya kutusaidia kama Taifa. Tusiwa-frustrate viongozi wetu wa kitaifa, kwa sababu kwa takwimu za Wizara ya Afya, Watanzania zaidi ya 40,000,000 walifika kwenye vituo vyetu vya afya na hospitali mbalimbali nchini, zaidi ya Watanzania 40,000,000 kwa mujibu wa takwimu.
Mheshimiwa Spika, kama wewe hukwenda hospitali yupo ndugu yako aliyekwenda hospitali na Watanzania hawawezi gharama za hospitali, ni kubwa sana hawawezi. Ninatoa takwimu ya haraka, takwimu ya haraka kabisa; kwa mwaka huu peke yake JKCI wametoa msamaha kwa Watanzania waliokwenda pale hospitali, msamaha wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.9 kwa wenye changamoto za moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni Taifa gani ambalo linaweza kutoa msamaha wa aina hii ndani ya Afrika Mashariki, ndani ya Afrika tujiulize Taifa lipi tukafanye tafiti. Ocean Road Taasisi ya Cancer ambayo Mheshimiwa Devota ameizungumza hapa. Kwa mwaka huu peke yake mpaka hapa niliposimama wametoa msamaha wa zaidi ya shilingi 12,000,000,000, Ocean Road. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda pale MOI msamaha wa matibabu zaidi ya shilingi 7,000,000,000; ukija Muhimbili Mloganzila msamaha wa Watanzania waliokwenda. Kwa sababu hatuwezi kuwaacha Watanzania wanakufa tukasema eti walipe fedha, haiwezekani na ndiyo maana kwenye kila kituo chetu cha afya, kwenye kila zahanati, kwenye kila hospitali zetu zote tumeweka wataalam wa ustawi wa jamii. Huduma za afya ni gharama kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda Muhimbili; ninaomba nikutaarifu, msamaha wa Watanzania waliosamehewa ni zaidi ya shilingi 19,000,000,000, msamaha na hii haipo kwenye bajeti yoyote, haipo kwenye bajeti yoyote. Ukienda KCMC zaidi ya shilingi 6,000,000,000, ukienda Benjamini Mkapa zaidi ya shilingi 4,000,000,000. Tunazungumzia karibu shilingi 60,000,000,000 mpaka 70,000,000,000 ya msamaha.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana tunasema viongozi wetu wanahitaji utulivu, fedha hizi zinatoka wapi, hazipo kwenye bajeti. Wakati mwingine hospitali hizi zinatamani kufanya mambo makubwa, lakini itafanyaje hayo mambo makubwa? Kwa sababu Watanzania wanaingia kwenye misamaha.
Mheshimiwa Spika, haiwezekani mgonjwa yupo kitandani, yupo katika hali mbaya ukamwacha kumhudumia na hana fedha, tunafanyaje. Kwa hiyo, niseme tu kwa uwazi, Watanzania wanahitaji kuendelea kuwaombea viongozi wetu wa kitaifa kwa sababu misamaha hii inatoka kwao. Niendelee kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya kwa niaba ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge 18 walizungumzia kuhusu dawa na vifaatiba na Wabunge 12 wamezungumzia kuhusu huduma za kinga ikiwemo chanjo, mifumo ya TEHAMA, MSD, sera ya afya na Taasisi ya TMDA pamoja na TBS. Kwa upande wa kikanda; idadi ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia ni kama ifuatavyo: Kanda ya Kati Wabunge saba, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Wabunge saba, Kanda ya Ziwa Wabunge 11, Kanda ya Kaskazini Wabunge wa nne, Kanda ya Magharibi Wabunge tisa, Kanda ya Mashariki Wabunge tisa, Kanda ya Kusini Wabunge wa nne na Zanzibar Wabunge wa tatu.
Mheshimiwa Spika, michango iliyotolewa ina ujumbe mmoja mkubwa kwamba, ujumbe wa uboreshaji wa huduma za afya. Wananchi wanataka huduma ziwe karibu, wananchi wanataka dawa na wananchi wanataka watumishi katika maeneo mbalimbali ya vituo, hospitali, zahanati na hospitali za kanda ziwe na vipimo, ziwe na mifumo inayosomana na ziweze kugharamiwa bila kuangusha kaya katika umasikini.
Mheshimiwa Spika, majibu yangu yatazingatia maeneo ya Bima ya Afya kwa wote, dawa na MSD, TEHAMA, miundombinu na rasilimali watu, ushirikiano wa sekta binafsi, kinga, sera, taasisi na mwongozo wa bei elekezi ya matibabu, Bima ya Afya kwa wote na ulinzi wa makundi maalumu.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea hoja kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, utekelezaji wa sheria hii ulianza rasmi tarehe 26 Januari, 2026. Baada ya kutangazwa kuanza kutumika kwa kitita cha mafao ya huduma muhimu. Awamu ya kwanza imeanza kwa wananchi wasio na uwezo wanaogharamiwa na Serikali. hadi tarehe 16 Aprili, 2026 kaya 172,297 zimefikiwa na wananchi, 463,228 wamesajiliwa katika awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu utambuzi wa kaya zisizo na uwezo, Tanzania Bara ina kaya 3,917,457 zisizo na uwezo kwa mujibu wa takwimu za NBS. Hadi sasa kaya 900,228 zimetambuliwa katika Mwaka wa Fedha 2026/2027. Serikali imekamilisha utambuzi wa kaya zilizobaki na inaendelea kuchambua vyanzo vipya fedha ikiwemo kodi ya bidhaa za tumbaku, tozo kwenye bima ya vyombo vya moto na mapendekezo ya miamala yaliyotolewa na Mheshimiwa Kingu, tutakwenda kuyafanyia kazi na tayari tumekwishakutana na wadau hawa na tunaamini wenzetu wa Wizara ya Fedha tutazungumza nao, tutakaa nao.
Mheshimiwa Spika, imani yangu kwa namna nilipokutana na wadau hawa, kama tutakwenda kutekeleza namna ambavyo Mheshimiwa Elibariki Kingu, alivyoshauri, basi inawezekana kabisa kama makusanyo ambayo Mheshimiwa Kingu ameshauri na kwa namna ambavyo mimi mwenyewe nimekutana na wadau hawa, tukifanikiwa kulitekeleza hili pengine tutamshauri Mheshimiwa Rais kwa mwakani, Watanzania wasichange hata senti tano kwa sababu tutakuwa na fedha za kutosha kuhudumia Bima ya Afya kwa wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili ninaomba nimthibitishie kwamba tumelibeba na tutakwenda kulifanyia kazi. Serikali pia imepokea hoja kuhusu huduma bila malipo kwa watoto chini ya miaka mitano na wazee wenye zaidi ya miaka 60. Sera hii inaendelea kutekelezwa ili haki iweze kuwa ni endelevu, makundi haya yanaingizwa kwa awamu katika Bima ya Afya kwa wote ili huduma ipatikane kupitia mfumo unaolipika, unaofuatilia na unaodumu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Bima ya Afya kwa Waheshimiwa Wabunge, utoaji wa bima hiyo unasimamiwa kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha Sheria ya National Assembly Administration Act, Sura 115. Kupitia sheria hii Bunge huingia makubaliano maalum na NHIF ili kutoa huduma za Bima ya Afya kwa Waheshimiwa Wabunge na wategemezi wao kupitia zabuni.
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa mujibu wa Sheria ya NHIF na Bima ya Afya kwa wote, fao la wazazi linalowahusu watumishi wa umma na sekta rasmi na binafsi hutolewa kwa utaratibu wa kuchangia asilimia sita ya mshahara kila mwezi, asilimia tatu kutoka kwa mwajiri na asilimia tatu kutoka kwa mtumishi. Kwa msingi huo utaratibu uliopo kwa Waheshimiwa Wabunge, haujumuishi wazazi kama Kundi la wategemezi ndani ya bima hiyo maalum.
Mheshimiwa Spika, dawa MSD, EP-prescription na bei elekezi za matibabu. Serikali inatambua hoja za Waheshimiwa Wabunge kuhusu dawa, vifaatiba, form II C, prescription zinazotumika nje ya vituo na ushiriki wa community pharmacies. Dhamira yetu ni kuhakikisha takwimu na uhalisia wa magonjwa vinakutana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha EP-prescription. Mfumo huu utamwezesha mtoa huduma kuona dawa ilipo kituoni kwa wakati halisi, kuandika dawa kwa generic name na kwa kuzingatia miongozo ya tiba.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa na changamoto, wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wao wamekuwa wakinifikia, wakilalamika baadhi ya vituo vyao kukosa dawa. Ukweli ni kwamba kumekuwa na changamoto, baadhi ya madaktari katika baadhi ya maeneo wamekuwa wakiandika dawa kutumia mifumo ya generic name na wakati mwingine dawa zinakuwepo kwenye vituo lakini wanaandika dawa nyingine wakijua kabisa kwamba dawa ya kutibu ugonjwa husika ipo kwenye kituo. Sasa haya wakati mwingine yanafanywa kwa makusudi, pengine wakishirikiana na baadhi ya watu, pengine wadau walioleta hizo dawa ambazo wao wanataka kwenda kuzitoa.
Mheshimiwa Spika, nikuthibitishie zaidi ya 70% ya dawa tunazo MSD na hatuna changamoto ya dawa. Hili nimefanya vikao vya kutosha na MSD, tumekwishakubaliana na tumekwishaweka redline kwa Mganga Mfawidhi wa Wilaya na Mkoa pamoja na vituo vya afya; wale ambao watakwenda kinyume na makubaliano tuliyokubaliana tutamweka pembeni, hakutakuwa na mjadala kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo eneo hili tunakwenda kulifanyia kazi kwa ufasaha kabisa, lakini hii tunaamini itakwenda kupunguza over prescription, matumizi yasiyo sahihi ya brand, ghost dispensing na mianya ya dawa kuingia kwenye mnyororo usio rasmi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu MSD hadi kufikia mwezi Aprili, 2026 deni la MSD kwa upande wa utunzaji na usambazaji wa bidhaa za miradi Msonge, limefikia shilingi bilioni 220.6. Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara ya Fedha inaandaa mpango maalum wa kulipa deni hili. Vituo vya kutolea huduma vimeelekezwa kuingia makubaliano na MSD ya kulipa madeni yao ikiwemo kupitia mifumo ya NHIF.
Mheshimiwa Spika, kuhusu wafamasia, Serikali inatambua kuwa mfamasia si mtunza store pekee. Mfamasia ni mtaalam wa matumizi sahihi ya dawa, ufuatiliaji wa stock, ushauri wa kitaalam na udhibiti wa rasilimali kubwa ya afya. Kutokana na maelekezo niliyoyatoa siku nilipofanya kikao MSD tarehe 28 Machi, 2026 Wizara imeshaanza kupitia miongozo, ili wafamasia wote wawe ni sehemu ya menejimenti katika hospitali na vituo na pendekezo la kuifanya famasia kuwa kurugenzi kamili, liko kwenye ngazi ya maamuzi sasa hivi tunavyozungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea kwa uzito hoja ya kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa tiba na bidhaa za afya nchini. Wizara itaendelea kuvutia wawekezaji, kuimarisha viwanda vilivyopo na kuhakikisha maamuzi ya Serikali yanazingatia ubora, yanazingatia usalama na thamani halisi ya fedha. Tumepokea maono na ushahidi uliotolewa na Mheshimiwa Shabiby. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba nimthibitishie nimekwishafanya vikao na wenzangu. Tunajua kwamba mchakato wa ujenzi wa viwanda vya dawa, Serikali inatamani kufanya, lakini wapo watu wasiolitakia mema Taifa hili, wamekuwa wao ndiyo kikwazo kikubwa cha kutotekelezwa uzalishaji wa dawa hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu hawa hawalitakii mema Taifa hili. Ninataka nimthibitishie, tumekubaliana na wenzangu wa MSD kwa sababu orodha wanayo tutawafuatilia. Mchakato wa ujenzi wa viwanda vya dawa si maamuzi ya Mchengerwa. Mchakato wa ujenzi wa viwanda vya dawa si maamuzi ya Wizara ya Afya. Mchakato wa ujenzi wa Wizara ya Afya ni maamuzi ya mamlaka.
Mheshimiwa Spika, yeyote atakayejaribu kukwamisha mchakato huu, tutashughulika naye wala hatutamwacha. Hili ninalisema wazi kabisa, nimekwishasema mara kadhaa, hatutarudi nyuma hata kidogo. Haiwezekani kwa Taifa hili lenye miaka zaidi ya 60 bado tuko chini ya 16% ya uzalishaji wa dawa. Huku tukitambua changamoto tuliyoipata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wa COVID-19 tulipata changamoto nyingi, lakini tunayo majanga chungu mzima ambayo yanaendelea katika dunia hii. Ni lazima tuzalishe dawa sisi wenyewe kama Taifa. Kwa hiyo, ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Shabiby niko imara, niko imara kweli kweli kwenye hili wala asiwe na wasiwasi.
Mheshimiwa Spika, ndani ya Serikali tumejipanga vizuri na nilipoingia katika Wizara hii, jambo la kwanza ambalo Mheshimiwa Rais alinikabidhi ni kuhusu uzalishaji wa dawa. Niliunda timu ambayo ilihusisha Wizara mbalimbali. Kwa maombi yangu, kwa mamlaka, mwenyewe Mheshimiwa Rais, lakini kwa maombi yangu kwa Waziri Mkuu, tunao wataalam kutoka Wizara ya Viwanda, tunao wataalam kutoka TRA wapo kwenye Kamati hii.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nimthibitishie hivi nimesimama, ndani ya miezi mitatu ya kutangaza mchakato wa kuanza kuzalisha dawa sisi wenyewe; juzi nimezindua hub ya Mloganzila ya uzalishaji wa dawa na tayari tumekwisha wakabidhi wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali na tumekwisha saini hati ya makubaliano na kampuni kubwa duniani kutoka Ujerumani ya Sartorius ambayo kwa mara ya kwanza Taifa letu tutakwenda kuzalisha chanjo sisi wenyewe kama Taifa. Kwenye hili hatutarudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mwongozo wa bei elekezi ya matibabu, Wizara inaendelea na zoezi la ukokotoaji wa gharama za huduma za afya kwa kuzingatia kitita cha Taifa cha huduma muhimu za afya. Katika kazi hii, Wizara inashirikiana na mshauri elekezi kutoka Shirika la Afya Duniani na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu. Matokeo yake yatasaidia kuweka bei elekezi zenye ushahidi, zinazolinda mwananchi na kuwezesha huduma kuwa endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika TEHAMA bima ya afya kwa wote haiwezi kufanikiwa bila mfumo wa kidijitali unaosomana. Bila mfumo imara ongezeko hilo linaweza kuleta madai yasiyothibitishwa, udanganyifu, ucheleweshaji wa malipo na shinikizo la mfuko. Serikali imesimika afya eHMS katika Hospitali Za Rufaa na Mikoa, Kanda Maalum na Taifa na GOTHOMIS katika ngazi ya msingi.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeanzisha health data universal kwa mara ya kwanza kabisa, tunakwenda kuanzisha kanzidata ya afya nchini, kwa mara ya kwanza kabisa, ili kuwezesha mifumo mbalimbali kusomana, kupokea na kutuma taarifa, kutoa rufaa kidijitali na kujenga misingi ya kanzidata ya kitaifa ya afya. Tunataka dai la bima lizaliwe kutoka huduma halisi iliyothibitishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na udanganyifu mkubwa. Labda niseme, kuna wakati wenzetu wa bima wamekuwa wakipokea kila mwaka madai kutoka kwa mdau wetu wa afya mmoja ambaye aliwekeza shilingi 300,000,000 pekee lakini watu wa bima ya afya kutoka sehemu fulani, walikuwa wakimlipa huyo mwekezaji aliyewekeza kwenye kituo cha afya, ujenzi na vifaa kwa thamani ya shilingi 300,000,000. Kila mwaka alikuwa akilipwa shilingi 2,000,000,000. Sasa hili halikubaliki.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu tunatambua kwamba mchakato huu unahusisha mpaka watu wetu ndani ya Wizara, wataalamu huko kwenye mifumo, ndiyo maana tumeamua kuja na robust system ambao hautachezewa na hakutakuwa na Mtanzania mwenye uwezo wa kuuchezea. Tutakwenda kuokoa fedha, tutakwenda kusababisha NHIF iweze kuwa imara na iweze kudumu miaka na miaka.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunataka dai la bima lizaliwe kutoka huduma halisi iliyothibitishwa, dai lizaliwe kutoka prescription halali, rufaa izaliwe kutoka uamuzi wa kitabibu na malipo yawe audited, miundombinu, vipimo na rasilimali watu.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamewasilisha hoja muhimu kuhusu miundombinu na watumishi. Serikali itaendelea kuimarisha huduma za msingi, hospitali ya wilaya, hospitali za rufaa na mikoa, hospitali za kanda na hospitali za Taifa ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kutoka Muhimbili na kuongeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea ushauri kutoka kwa Wabunge mbalimbali ambao wamechangia kuhusu eneo hili. Tutazingatia ushauri, tutazingatia maono yao Waheshimiwa Wabunge na yale ambayo wametamani tuyafanye katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wa Kanda ya Ziwa hasa kule Mkoa wa Mara tumewasikia. Mheshimiwa Waitara tumemsikia, Mheshimiwa Ghati na Mheshimiwa Dkt. Mahera tumewasikia. Ni lazima tuiboreshe hospitali hii ya Baba wa Taifa, hakuna mjadala kwenye hili.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, lazima twende kwenye hospitali zote zilizopo mipakani tukaziboreshe ili ziwe imara kwa sababu zitakwenda kuongeza utalii tiba, lakini zitakwenda kuimarisha utolewaji wa huduma za afya katika maeneo yetu na kule Rukwa Mheshimiwa Aeshi Hilaly. Nimekusikia na nimekwishatoa maelekezo ndani ya mwaka huu tutahakikisha huduma za dialysis zinafanyika katika Mkoa wa Rukwa pamoja na maoni yako, maono yako na ushauri wa Mheshimiwa Mzindakaya ambao ameutoa kwa Bunge hili na Serikali tumeusikia na tunakwenda kuufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninatambua kwamba mambo ni mengi na bado Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza mambo mazuri ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Erick Shigongo kuhusu vita ya homa ya ini. Tumelipokea hili, lakini kwa sababu ya muda tutatoa maelezo kwa maandishi kutokana na muda. Pia, Mheshimiwa Hokororo tunatambua kule Mtwara kuhusu ujenzi wa kituo cha afya, tumelipokea hilo. Pia na Waheshimiwa Wabunge wote wote ambao wamezungumza kwa niaba ya wananchi katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba nimalizie. Watanzania wanahitaji huduma bora za afya na kwenye hili hatuwezi ku-compromise hata kidogo na nimekwishawaeleza wenzangu, wakati huu ni lazima tufanye kazi kama mchwa. Sisi tuliyopata bahati ya kusimama na kuteuliwa kwenye vyeo mbalimbali tunao Watanzania zaidi ya milioni 60 wenye uwezo mkubwa. Sisi tuliopata bahati ni lazima tufanye kazi kwa bidii, hakuna mjadala kwenye hili, hakuna mjadala hata kidogo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikiri kwamba hoja zote ambazo zimetolewa zina umuhimu na kwa niaba ya Wizara ya Afya ninawashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa maoni kwa ushauri wao na hoja zao. Ninaomba Bunge lako Tukufu liendelee kuiunga mkono Wizara ya Afya katika utekelezaji wa bajeti hii, kwa sababu tunachokifanya si kazi ya mwaka mmoja ni kuweka misingi ya historia mpya ya afya nchini. Historia hii itakumbukwa kama kizazi kilichoamua kwamba afya ya Mtanzania isiwe bahati, afya ya Mtanzania isiwe hisani, isiwe uwezo wa mfukoni pekee bali ni haki inayolindwa na mfumo imara wenye utu, teknolojia, nidhamu na uwajibikaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii, ninaomba kutoa hoja.