Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi ya kuchangia hoja ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum asubuhi ya leo na kwanza kabisa nimpongeze Waziri na Naibu Waziri wake pamoja na Watendaji Wakuu wa Wizara ambao kwa kweli tangu Wizara hii imeundwa, wamefanya kazi kubwa sana hasa ya kuweka awareness katika mambo ya unyanyasaji wa kijinsia. Tunawapongeza sana na mwendelee kwa kazi hiyo njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bajeti yao pia ni shilingi bilioni 76 tu, ninaomba tu tuwape hiyo bajeti, na kwa hiyo, ninaunga hoja mkono ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa mwaka ujao wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi ya leo nitajikita katika maeneo mawili tu ambayo yote ni ya kujenga ustawi wa jamii yetu ya Kitanzania. Katika kusema hivyo, ninaelekea katika msingi muhimu sana wa ustawi wa jamii yetu ambao ni ujenzi wa familia iliyo bora. Ninaamini kwamba familia ikijengwa vizuri ndiyo msingi wa jamii ambao inaendeleo lakini pia ndiyo msingi wa ustawi wa Taifa zima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maarifa ambayo yanajenga msingi huu wa familia bora hayawezi kupatikana shuleni tu, wala hayawezi kupatikana katika taasisi za dini tu, maarifa haya kimsingi yanapaswa kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi ndani ya familia yenyewe. Kwa maana ya kwamba watoto kadiri wanavyokua wanapaswa kupata haya maarifa kutoka kwa wazazi wao na kwa jinsi hiyo tutajenga jamii ambayo ina ustawi unaokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hivyo, ninapenda kurejea kwamba sisi ambao tumebahatika kuwa wazazi tuna sababu ya kuchukua muda wa kutosha au kuutafuta huo muda wa kutosha kwa maana ya kwamba ni jukumu ambalo hatuwezi kulikwepa kwa kisingizio cha kazi nyingi, cha ufanisi wa mambo mengine yote isipokuwa kufundisha watoto wetu na tunapowafundisha watoto wetu katika familia tunajenga msingi wa kwamba familia inamhitaji baba, inamhitaji mama, inawahitaji watoto na kwamba hao wote ndicho kiungo ambacho kinaweza kikajenga familia iliyo bora na yenye ustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo ambalo mimi binafsi ukinichukua (Shukrani Manya) linalonikera, ni pale ambapo watoto wa kiume au akina baba tunatelekeza watoto wetu. Yaani ulipata mtoto kwa namna yoyote ile, halafu unamtelekeza, majukumu yote ya matunzo ya malezi anaachiwa mama. Hili jambo siyo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, sisi ambao ni wazazi, tuwafundishe watoto wetu, wanapokuwa wamefikia umri huo ambao wote tunaufahamu kwamba tendo la ndoa linapofanyika ndilo linaloleta watoto duniani, na kwa hiyo, kabla ya kuwaleta watoto duniani lazima watafakari kwamba kituo kinachofuata baada ya hapo ni malezi pamoja na matunzo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi hiyo, kama kijana wa kiume au wa kike huoni kwamba unayo nafasi au uwezo wa kufanya matunzo na malezi ya mtoto, basi kwanza usishiriki tendo linalomleta huyo mtoto duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwafundishe watoto kwamba watoto wanapokuja duniani watahitaji muunganiko wa baba na mama katika kuwalea na kuwatunza. Kwa hiyo, mmojawapo na hasa baba au huyu kijana wa kiume asikwepe akakimbia majukumu yake na kumwacha mtoto wa kike akisota peke yake katika matunzo ya mtoto ambaye ameletwa. Kwa jinsi hiyo, ninadhani sisi kama wazazi, tunayo sababu ya kuchukua muda wa kutosha kuiweka hii elimu kwa watoto wetu ili wajue kabisa kwamba ili tuweze kuwa na jamii ambayo ina ustawi lazima malezi ya watoto yaanze na wazazi wawili ambao wametamani kuwa na familia. Ni katika familia hii hii ambapo tutakataa ukatili wa kijinsia. Ni katika familia hii hii ambapo tutatoa elimu ya kukataa ushoga, na ni katika familia hizi hizi tutaweza kukilinda kizazi hadi kizazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pamoja na kupendekeza kwamba elimu hii itolewe ndani ya familia tuna sababu ya kuviomba vyombo vyetu vya habari viweke vipindi maalum kwa ajili ya elimu ya familia, yaani utakuta TV news media outlets nyingi haziweki kipindi hata kimoja katika jambo hili la msingi ambalo ndilo linalojenga ustawi wa jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pendekezo langu Mheshimiwa Waziri asubuhi ya leo ni kwamba, tuviombe vyombo vyetu vya habari, elimu hii ya ustawi bora wa familia viwe na kipindi maalum kwa ajili hii ili elimu hii iendelee kutolewa kila mahali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu hii itakapokuwa imekuzwa sana katika familia zetu, iwe ni nyumbani iwe ni katika taasisi za dini iwe ni katika media outlets maana yake ni kwamba itasaidia sana Taifa kupunguza watoto wa mtaani. Hakuna mtaa unaobeba mimba kwamba mtaa unazaa watoto wakawa wa mitaani, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, ni kwa sababu mzazi mmoja amekataa majukumu yake, hatimaye tunapata watoto wa mitaani. Kwa hiyo, hakuna mtaa wenye Watoto, watoto ni wa baba na mama; na elimu hiyo lazima ikuzwe katika familia zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ukiangalia nchi yetu ya Tanzania ukaitazama katika picha ya ujumla unagundua kwamba tatizo la udumavu wa watoto walio chini ya miaka 15 eti linapatikana katika Mikoa ya Kigoma, Katavi, Njombe, Songwe, na Rukwa, lakini mikoa hii ndiyo yenye utoshelevu wa chakula, yaani ni mikoa ambayo inapeleka chakula sehemu nyingine kwa wingi, lakini huko ndiko kuna udumavu wa watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachopungua hapa ni elimu ya lishe bora na katika hili nimtaje Mheshimiwa Lugangira ambaye kwa kweli kila mara anaposimama huwa anaongelea juu ya lishe bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe uzoefu binafsi. Wakati fulani nilikuwa ninawafundisha watoto kati ya umri wa miaka tisa hadi 15. Siku hiyo nikawatania kidogo nikawauliza, ninyi chakula chenu mnachokipenda ni nini? Wakanijibu, “Piza na baga” halafu baadaye ndiyo wakaniuliza, “Kwani wewe mwalimu chakula unachokipenda ni nini?” Nikawaambia, ugali, dagaa na matembele, ndiyo my best meal. Watoto wale walicheka wakagaragara. Wakanambia Mwalimu, matembele na dagaa! Wao wanataja habari ya piza na baga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani Ukoloni Mamboleo mpaka kwenye chakula? Yaani piza na baga, vyakula vya watu wengine huko ndivyo vinaonekana ni vyakula bora ndani ya nchi ya Tanzania. Tuna sababu kama nchi, sasa tuna utoshelevu wa chakula kupeleka elimu bora ya lishe katika jamii ya Kitanzania kwa sababu hii habari ya kupenda chakula cha wengine tukaacha vyakula vyetu vya asili, siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kuna msanii mmoja alisema yeye hajala ugali sijui miaka 20, na anaona kwamba hiyo ni sawa kabisa na inafaa. Katika jamii za Kitanzania leo watu wengine wanaamini kwamba kula maharage ni chakula cha wafungwa na kwamba wewe unakuwa mfungwa na kwamba ukila mboga za majani ni dalili ya umasikini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine hata wanaozalisha maparachichi wanaamini kwamba maparachichi na ndizi ni chakula cha biashara, wao hawali na kuna wengine ambao wanadhani kwamba ukila chipsi mayai kila wakati umekuwa na lishe bora kwa sababu chakula kile kina muonjo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Tanzania tunapenda sana unga wa sembe, lakini sio wote tunajua kwamba sembe imeondolewa nyuzi nyuzi (Fiber), na Fiber siyo muhimu kwa ajili ya afya zetu? Ninatamani tuwe na mwongozo wa Kitaifa juu ya nini tule kama Watanzania kwa sababu tuna utoshelevu wa chakula, lakini bado tunakula hovyo kwa sababu hatuna mwongozo mzuri wa nini tule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie dakika moja. Ninaomba ni-tease kidogo hapa. Hivi ni jamii ya Watanzania wangapi kina akina mama ambao wanajua mwanaume anapokuwa katika advanced age, mbegu za maboga ni chakula anachokihitaji sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wengi hawajui na akina baba wengi hawajui kuwa mbegu za maboga ndiyo zenye madini ya zink na selenium kwa wingi ambazo ndiyo zimeondoka kwa sababu mwanaume amekua, lakini hatujui. Kwa hiyo, mbegu za maboga ukienda kule supermarket hazinunuliwi, maana walaji hawapo. Mwanamke hajui, na baba hajui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo sababu ya msingi sana ya kuimarisha elimu ya lishe bora katika Taifa letu na ninapendekeza pia kwamba vipindi vya lishe bora virudi katika news outlet kama ilivyokuwa katika Redio Tanzania zamani “Kuleni chakula bora cha kuujenga mwili;” tulikuwa tunasikiliza sana hiyo chorus. Sasa hivi imeenda wapi? Hiyo, “Kuleni chakula bora cha kujenga mwili”, hiyo chorus iko wapi katika media outlets leo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante kwa nafasi. (Makofi)