Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa kwa mchango mkubwa na mzuri kwenye eneo zima la lishe. Ni kweli kabisa lishe bora ni jambo la msingi na ndilo ambalo linapelekea kutuhakikishia kama Taifa kulinda rasilimali watu. Aidha, ninamshukuru sana kwa kutambua jitihada zangu binafsi na tutaendelea kushirikiana katika kusemea ajenda hii ya lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nielekeze mchango wangu kwenye Wizara hii muhimu sana ambayo kimsingi inabeba muktadha mzima wa maendeleo ya jamii, lakini pia masuala ya wanawake, jinsia na makundi maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kuleta mageuzi makubwa katika sekta hii ya NGO’s, halikadhalika kuimarisha ustawi wa sekta yetu hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Doroth Gwajimba, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Jingu, pamoja na viongozi wote wa Wizara hii. Kipekee kabisa, ninapenda kutambua jitihada kubwa sana ambazo zimefanywa na dada yangu Vicky, Msajili wa NGO’s pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya NGO’s, Mama yangu Mwantumu Mahiza pamoja na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumesikia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, sekta hii ya NGO’s kwa mwaka 2024 peke yake imechangia shilingi trilioni 2.61 katika kutekeleza afua mbalimbali za maendeleo hapa nchini kwetu. Pia, sekta hii ya NGO’s imechangia moja kwa moja zaidi ya ajira 21,000 kwa Watanzania. Sasa pamoja na mafanikio haya ningependa kuishauri Serikali kupitia Wizara hii katika maeneo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, kutokana na mabadiliko ya misaada au ya utoaji misaada ya fedha kutoka Serikali ya Marekani pamoja na Serikali nyingine ambazo zinaendelea kufanya mchakato huo, ni muhimu sana Serikali ifanye tathmini ya hali ya kifedha ya NGO’s baada ya misaada hiyo kufutwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika hapa nimtambue na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi mwenye maono kwa sababu mwaka 2023 aliielekeza Serikali iharakishe mchakato wa kuanzisha mfuko wa NGO’s (NGO’s Basket Fund).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa sana wakati Mheshimiwa Waziri unahitimisha utueleze bayana kuanzishwa kwa mfuko huo wa NGO’s umefikia wapi hususan tukizingatia hali ya kiuchumi iliyoko hivi sasa kutokana na misaada mbalimbali kufutwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie fursa hii kuwasilisha ombi maalum na ninafurahi leo Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, Jerry Silaa, yuko hapa kwa sababu katika Sheria ya Taarifa ya Ulinzi Binafsi hakuna category inayoitambua sekta ya NGO’s. Kwa hiyo, hiyo inasababisha kwamba NGO’s zinatakiwa zilipe kujisajili katika mfumo wa taarifa binafsi. Jambo ambalo linakwambisha jitihada za sekta ya NGO’s.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninaomba niwasilishe ombi kwamba sheria ile ifanyiwe maboresho kidogo itambue category ya NGO’s na ziweze kupata msamaha wa kulipa kiwango hicho cha usajili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika kumekuwa na changamoto kubwa sana kwa upande wa TRA, kwa maana TRA wanatambua NGO’s kama vile ni biashara. Kwa hiyo, wanazitambua na kuzichukua NGO’s na biashara kama ni kitu kimoja; kitu ambacho kinaleta changamoto kubwa sana kikodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, niiombe sana Serikali, ninatambua tumeshapata fursa tumewasilisha kwenye Tume ya Kodi, lakini niiombe sana Serikali na Wizara hii itusaidie kuhakikisha kwamba TRA watofautishe kati ya NGO’s na biashara kwa sababu NGO’s hazifanyi biashara. Kwa hiyo, kuzichukulia kikodi kama vile nazo zinafanya biashara, ni jambo ambalo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nikiwa kama Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi ninayewakilisha kundi la NGO’s ninaomba niwasilishe shukrani zangu za dhati kwa sekta nzima ya NGO’s kwa ushirikiano mkubwa ambao wamenipa tokea nimeanza kuhudumu nafasi hii na halikadhalika kunifanya nimekuwa Mbunge wa kwanza aliyehudumu katika nafasi hii kupata utambuzi na ushirkiano ambao wamenipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakishukuru sana chama changu (Chama cha Mapinduzi) kupitia Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake chini ya Mwenyekiti wetu bingwa kabisa, Mheshimiwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Mama Mary Pius Chatanda pamoja na Makamu Mwenyekiti wetu bingwa kabisa m-NEC, Zainab Shomari kwa kuongeza nafasi ya Wabunge wa Viti Maalum wanaowakilisha kundi la NGO’s kutoka nafasi mbili na sasa kuwa tatu ambapo kutakuwa kuna nafasi mbili upande wa Tanzania Bara na nafasi moja upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaendelea kudhihirisha namna ambavyo chama changu (Chama cha Mapinduzi) kinatambua na kuthamini mchango mkubwa wa sekta ya NGO’s kwenye kuchangia maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuahidi kwamba nitaendelea kufanya kazi kwa kujituma, ufasaha na ufanisi na ubunifu na weledi mkubwa kwa maslahi mapana ya maendeleo ya Taifa letu. Halikadhalika ninaendelea kuwategemea sana mama zangu na viongozi wangu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania kutoka kila kona ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninakipongeza sana chama chetu kwa kuwa chama ambacho kinaongoza na kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kinaimarisha mazingira wezeshi ya wanawake kuweza kushiriki katika ulingo wa kisiasa na demokrasia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Chama cha Mapindizi kiko katika hatua za mwisho za kukamilisha mchakato wa kuwa na sera ya jinsia ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Mwongozo wa Dawati la Jinsia la Chama cha Mapinduzi, jambo ambalo litakwenda kuimarisha ushiriki wa wanawake katika siasa. Kwa kufanya hivyo, ndivyo ambavyo tutakuwa tunatekeleza falsafa za Four R’s za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kubwa pia kupitia Sera hii ya Jinsia ya Chama cha mapinduzi pamoja na Mwongozo wa Dawati la Jinsia la Chama cha Mapinduzi itapelekea kuwalinda na kuwawezesha na kuhakikisha kwamba Madiwani wa Viti Maalum na Wabunge wa Viti Maalum wataweza kutekeleza majukumu yao katika maeneo yao pasipo kupitia changamoto za kukwamishana kwa maslahi binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kuwashukuru sana viongozi wangu wa Serikali na Chama Mkoa wa Kagera na wilaya zote nane za Mkoa wetu wa Kagera kwa ushirikiano mkubwa ambao wameendelea kunipa katika kutekeleza majukumu yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hususan na kwa kipekee sana niwashukuru sana wananchi wenzangu wa Bukoba Mjini kwa ushirikiano mkubwa ambao wameendelea kunipa na niwaahidi ya kwamba tutaendelea kushirikiana kama ambavyo tumekuwa tukishirikiana, na niwatoe hofu kwamba tayari nimeshapata uzoefu wa namna ya kukabiliana na changamoto zenye mlengo wa kukwamishana kwa maslahi binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, nitumie fursa hii kuwatakia kila la heri wagombea wote wa Jimbo la Bukoba Mjini na niahidi nitatoa ushirikiano mkubwa kwa yule ambaye atateuliwa na chama chetu kugombea katika nafasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme kwamba ninaunga mkono hoja na tukutane site, na ahsante sana. (Makofi)