Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia hotuba iliyopo mbele yetu. Awali ya yote nipende kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kusimamia na kulinda desturi za nchi yetu pamoja na utamaduni wetu. Siku zote amekuwa akikemea na kuonya na kuwasihi Watanzania tuendelee kubaki kwenye maadili na kuyasimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hotuba aliyoitoa juzi, ametoa hotuba nzuri kabisa na ametoa statement nzuri ambayo sisi kama Wabunge wake tuko nyuma yake, tunaifuata. Tunajua kabisa tuna Rais mwanamke hodari, mkakamavu, shupavu na ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kusimama na Rais wetu, kuungana mkono na Rais wetu. Niwaambie tu, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia tunaye na tunatamba naye. Mwaka 2030 ndipo tutakuja kuachana na Mheshimiwa Dkt. Samia. Kwa hiyo, niwaambie tu wale ambao wanajaribu kufanya majaribu tofauti tofauti ni kama wanapoteza muda wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu yuko vizuri, amefanya kazi kubwa sana kwenye nchi hii. Ndani ya miaka minne hakuna Kijiji, kata, wilaya, au mkoa ambao hauna alama ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ndani ya miaka minne amefanya mambo makubwa sana. Sisi Watanzania hasa Wabunge wake wa CCM tunaona fahari na tunayo mengi ya kwenda kuwaeleza Watanzania wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kwa kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia maadili kwenye nchi yetu. Napenda kuongea kuhusu Asasi za Kiraia. Tunazo asasi nyingi za kiraia kwenye nchi yetu; tunazo asasi zinazokuja kwa kificho kuleta fedha kwa ajili ya kuchafua siasa zetu; tunazo asasi zinazokuja kwa ajili ya kuharibu watoto wetu kwenye shule zetu, zipo; tunazo asasi kwa ajili ya kuharibu maadili yetu na tunazo asasi nzuri ambazo zinakuja kusaidia Watanzania kwa malengo yao wanayoyataka kuja kusimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumwomba Waziri wetu wa Maendeleo, dada yetu Mheshimiwa Dkt. Gwajima anayefanya kazi kubwa sana kwenye taasisi yake na Wizara yake hii. Namwomba atwambie ana mkakati gani sasa wa kuzichambua hizi NGO’s kujua NGO’s zipi ni bora na zipi siyo bora, na zipi zinaingia humu ndani kuharibu vizazi vyetu, zinaingia kuja kuharibu siasa zetu, zinaingia kupenyeza wanaharakati waje kuharibu siasa zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa aje na mkakati aliokuwa ameupanga ili tuweze kuzichambua na kuzijua zipi bora na zipi ambazo siyo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kuongelea suala zima la maadili. Kwenye Wizara hii pia kuna kitu cha maadili. Mimi naomba sana kwanza nianze kwa kukemea ukatili wa mtandaoni ambao unamdhalilisha mtu, utu wa mtu, na unampa fedheha mtu kwa kutoa siri au faragha zake kwenye mitandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naiomba TCRA pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, wakae pamoja kwanza kuleta sheria kali zaidi kuliko zilizopo na kwa kufuatilia hawa watu na kuwahukumu na tuone hukumu zao zinatangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kule China mtu akiiba wakimkamata wakichukua zile kamera zao wanatangaza kwenye vyombo vyao vyote vya habari jinsi alivyoiba mpaka walivyomkamata na mpaka alivyoenda kuhukumiwa kwa kuchomwa sindano ya sumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi hao watu wanaochafua watu kwenye mitandao na wanaofanya ukatili kwenye mitandao watakapokuwa wanakamatwa tunaomba baada ya hukumu zao tuonyeshwe kwamba huyu alifanya ukatili huu, Mahakama imefuatilia moja, mbili, tatu, ikathibitisha na imemchukulia hatua fulani. Labda itakuwa ni fundisho kwa wengine wenye kutaka kufanya tabia mbaya kama hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tunaamini hatua zinachukuliwa, lakini kwa sababu zinachukuliwa kisiri, labda watu wanajua kwamba, hizo hatua hazipo na wanaendelea kufanya hayo mambo kwenye mtandao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tu kwamba, nchi yetu ni nchi yenye maadili, nchi yetu ina misingi ya kimaadili, nchi yetu ina utamaduni wa kimaadili. Niombe, sisi kama viongozi wa nchi hii hususan Wabunge ni wa kwanza tuoneshe mfano wa kimaadili, sisi ndiyo tuwe wa kwanza kuweka maadili yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kuwa Mbunge leo na mimi nikawa sina maadili, ninafundisha nini kizazi cha kule nje? Maaadili ni pamoja na kuheshimu mamlaka zilizo juu yetu. Wewe ukiwa na maadili lazima uheshimu mamlaka iliyo juu yetu. Vitabu vya dini vimesema vya Kiislamu na Kikristo kwa maana ya msaafu na biblia, mamlaka na ziheshimiwe. Tumeongozwa toka kwenye vitabu vya dini, lakini leo unakuta Kiongozi au Mbunge yaani anaona anastahili kusema lolote lile bila kuangalia maadili yetu yalivyo. Niombe sana viongozi tuwe wa kwanza kuonesha mfano wa kimaadili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kiongozi mzima unakwenda unavi- blast vyombo vyetu vya usalama, halafu unasema una maadili, ni maadili gani? Bila vyombo vya usalama tusingekuwa hapa. Ninaomba tuchukue mfano, tutoe likizo ya mwezi mmoja, polisi tumewafungia mwezi mmoja, hakuna kituo cha Polisi, hamna Usalama wa Taifa, hakuna Jeshi, patakalika hapa? Hii nchi itakalika? Mimi ninaviheshimu sana vyombo vya usalama, ninaheshimu sana viongozi wote wa vyombo vya usalama, bila wao tusingekuwepo hapa, wanatulinda, wanafanya kazi ngumu na ndiyo maana leo tunajisifu, tunajidai kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani, lakini kuna watu hawalali kwa ajili ya kutengeneza hii amani ambayo ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo sawa kwamba Wabunge tunajua kila kitu, tunajua job instruction za viongozi wote, tunajua job instruction ya vyombo vya usalama, siyo sawa, tuache vyombo vifanye kazi kama Katiba ya nchi inavyoelekeza, tuache vyombo vifanye kazi kama sheria zilivyo zinavyoelekeza na sisi kama viongozi tuendelee kuwatia moyo. Pia, sisi kama Wabunge hatuwezi kuingilia utawala wa kuteua viongozi, Katiba inaeleza wazi nani anamteua nani na nani anamteua nani. Kwa hiyo, yule anayeteua ndiyo anayejua amteue nani kwa wakati huo na kwa nini amtoe na kwa nini amuweke mwingine, sisi haituhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhusike kwenye kuwahudumia wananchi wetu kwenye majimbo yetu tuliyoomba kura. Tuhusike kuja kuwasemea, kuja kuomba matatizo yao ambayo yapo kwenye majimbo yetu, tuje tuiambie Serikali iwatimizie wananchi wetu, lakini tusiingilie kazi za Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia kwa kusema sisi kama Wabunge tutaendelea kumlinda Rais wetu, tutaendelea kumtetea, tutaendelea kumsemea, nimesema mwanzo tu, Mheshimiwa Rais Samia aliingia kuwa Rais kwa nguvu za Mwenyezi Mungu, ile nafasi aliipata na sasa hivi tunaenda kupiga kura. Niwaambie tu Watanzania wanaonisikiliza, niwaambie watu wote kwamba, tutamchagua kwa kura nyingi za heshima kwa kazi aliyoifanya, hatutampa kura kwa sababu nyingine yoyote, Samia amefanya kazi kubwa anastahili kupata kura za heshima, kwa kazi aliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe Watanzania tusimame na Rais wetu, lakini Watanzania pia maadili yetu yatufundishe tuheshimu Marais wote wa nchi za jirani, tuheshimu Serikali zote za nchi za jirani, lakini wale wachache wanaotuvunjia heshima na kuingia kwenye nchi yetu kutuvuruga hakika hatutakubali. Kwa hiyo, ninawaomba vyombo vyetu vya usalama viwe macho na vifuatilie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo machache, ninaunga mkono hoja. (Makofi)