Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. Awali ya yote ninapenda kusema kwamba, ninaunga mkono hoja hii iliyoletwa na Mheshimiwa Dorothy Gwajima na ninampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Mwanaidi Ally Khamis kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuweza kumsaidia Mheshimiwa Rais katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nitumie nafasi hii mapema kabisa kuendelea kumhakikishia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari Samia Suluhu Hassan kwamba, sisi Wabunge wa CCM katika Bunge hili tutaendelea kuhakikisha yeyote yule hawezi akasimama na kumchafua Rais wetu na Serikali yetu, tutapambana naye kwa vyovyote vile itakavyokuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia eneo moja, eneo linalohusiana na ukatili dhidi ya watoto. Nimekuwa nikisoma hasa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) linasema nini kwenye eneo hili ambalo ni muhimu sana kwa watoto wetu. Taasisi mbalimbali zimefanya tafiti ili kugundua ni jinsi gani hali ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wetu mashuleni. Hali hii inavyokwenda na nikaangalia kwamba hakika Serikali imekuwa na juhudi kubwa sana katika kutafuta njia za kuwalinda watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na sheria kali kwa mfano, kama ile Sheria ya Sexual Offences Special Provisions Act (SOSPA) hakika sheria hii ni kali. Vilevile, kumekuwepo na mpango unaoitwa mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kumekuwepo na Dawati la Jinsia ndani ya Jeshi la Polisi, kumekuwepo, makongamano na maandiko mengi ambayo yote yanalenga kuhakikisha kwamba, visa vinavyowasibu watoto wetu vinapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ametuambia katika hotuba yake kwamba visa hivi vinapungua, lakini ukiangalia katika maandiko ya UNICEF wanasema visa vinaongezeka na hakika tukiangalia takwimu zinatisha. Nisingependa nichukue muda wako mwingi sana kuelezea takwimu ziko namna gani, lakini ningependa nizungumze juu ya hali ilivyo huko kwa wananchi hali ikoje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 17 nilipata nafasi ya kutembelea Kata ya Tandale katika Jimbo langu na pale niliongozana na Diwani wa Kata ile anaitwa Abdallah Chifu, kuongoza maandamano ya amani kuanzia Shule ya Msingi Hekima. Shule hii ya Hekima iko ndani ya Kata ile na nililazimika kufanya maandamano kwa sababu ya kwenda kwa jamii kupaza sauti juu ya kuongezeka kwa vitendo vya ulawiti na ubakaji kwa watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maandamano yale tulikuwa tunapita maeneo yote yenye watu wengi na tulikuwa tukisimama na mimi nilikuwa nikihutubia na nikipaza sauti. Takwimu zinaonesha huko nyuma kila mwezi angalau kisa kimoja kinaripotiwa katika shule ile, sasa hivi imekwenda mpaka kila wiki haikosi kuna visa vinavyoripotiwa na Mwalimu Mkuu pale anasema hatashangazwa akiona kwamba visa vile sasa ni vya kila siku. Ni kwa sababu gani? Kwa sababu jamii pamoja na sheria kali inaona kana kwamba jambo hili halipewi uzito unaostahili, ninaomba Mheshimiwa Waziri anisikilize kwa makini hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaofanya visa hivi wanasemekana wanaweza wakawa ndani ya jamii kwa maana ndugu, anaweza akawa baba mdogo, baba mkubwa, anaweza akawa kaka, anaweza akawa jirani, anaweza mpangaji, unajua nyumba zetu kule uswahilini, lakini yanapotokea mambo kama haya, jamii kwa maana ya ndugu wanakaa wanajadiliana na kumalizana. Mashauri mengine hayapelekwi mahakamani na kwa kuwa hayapelekwi mahakamani hata taarifa sahihi za matukio haya hatunazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa tulizonazo ni zile tu zinazoripotiwa katika dawati na nyingine zikapelekwa Polisi. Vilevile, hata zikipelekwa Polisi kesi hizi zinaahirishwa mara kwa mara kiasi kwamba jamii inapotea katika kujua kesi fulani imemalizika vipi, hivyo vitendo vinaendelea. Sasa wananchi wanasemaje? Hapa ndipo ningependa niende moja kwa moja kwenye mapendekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanasema kwamba, mashauri yote yanayohusiana na ukatili wa kijinsia iwe watoto wa kike, watoto wa kiume, wanawake, mashauri haya yasijadiliwe katika ngazi ya kijamii, kusiwe na mapatano na kama ikiwezekana ku-criminalize hatua yoyote ya watu kukaa kujadili kosa la jinai kulifanya kama vile ni kosa la madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wakashtaki Polisi na Polisi kesi iende Mahakamani na kesi ikienda mahakamani, wananchi wanataka iwe fast track isiwe kesi ichukue miaka miwili, miezi sita, kesi iamuliwe mapema na watu wote wanaotuhumiwa watangazeni, kwamba kuna kesi inahusiana na masuala ya ulawiti, ubakaji visa vya ukatili dhidi ya wanawake, yaani zile kesi zake zikienda Mahakamani itangazwe kwamba fulani fulani anashtakiwa na Jamhuri kwa kosa la kubaka, wananchi wajitayarishe wasubiri. Endapo itahukumiwa kwamba yule kweli ni mbakaji kuwe na list of shame watu waandikishwe, kwamba huyu amelitia doa, huyu ni mtu mchafu na agopewe katika jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezunguamzia suala moja muhimu sana kwamba, wanaopelekwa mahakamani kwa makosa kama haya, wahakikishe Serikali wanafanya mabadiliko katika sheria ikiwezekana Sheria ya SOSPA, masuala yote ya ukatili wa kijinsia yawe ni makosa ambayo hayana dhamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa haya kama hayana dhamana watuhumiwa wakirudi mjini huko watashindwa kuingilia mwenendo wa kesi kwa sababu akiachiwa kwenda huko wao wanarubuni wazazi, wanarubuni hata yule aliyefanyiwa vitendo vile, hata mahakamani haendi, mwisho wake kesi ile inakufa. Kwani kuna taabu gani kama mtu akiamua kwenda kubaka, kulawiti na akakamatwa, akashtakiwa kwa nini kesi yake isiwe haina dhamana (bond)?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho ninaomba hili dawati la jinsia, ninajua liko pale Polisi siyo sehemu yake, lakini yeye ni sehemu ya Serikali na Polisi ni sehemu ya Serikali. Ushauri wangu dawati hili liongezewe nguvu, ikiwemo liongozwe na Makamishna iwe kama ni Idara kwa sababu tatizo la visa hivi ni kubwa. Tupeni dawati hili lionekane kana kwamba ni moja ya sehemu ambayo itakuwa ni kimbilio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, narudia kusema kwamba, ninaunga mkono hoja hii na ninakushukuru sana. (Makofi)