Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Gwajima pamoja na Msaidizi wake Naibu Waziri, Mheshimiwa Mwanaidi, wanafanya kazi nzuri sana sana hasa ya kufichua mambo na wakipewa tu taarifa wanawajibika, nimpongeze sana. Kwenye meza yake anawajibika kutoa yale yanayoonekana ni maovu na ukishayatoa yeye Mheshimiwa Bashungwa ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani naye pale anachukua nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, kuna maeneo mengi ambayo mambo mabovu yanatendeka, lakini niombe Serikali kila Wizara ichukue nafasi kama jambo limetendeka mashuleni Waziri wa Elimu anahusika, Waziri wa TAMISEMI anahusika, Waziri wa Mambo ya Ndani. Kwa hiyo, mambo haya yakitendeka maovu Wizara hizi nne zikishughulika pamoja basi hayo mambo yanaweza yakaisha haraka. Mara nyingi utaona Waziri Gwajima ameibua jambo, lakini linachelewa kufanyiwa kazi, nikutie moyo endelea na hayo mambo kuyaibua yapeleke sehemu ili kazi ifanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala la ndoa za utotoni. Suala la ndoa za utotoni ninakumbuka wazi kwamba, wenzetu hawa walituambia wanakusanya maoni, wakakusanya maoni halafu likabaki kimya. Waziri Ndumbaro alisimama na ninakumbuka aliulizwa na Spika wanaleta Muswada au wanaleta maoni? Akajibu tunaleta Muswada, Sheria ya Ndoa za Utotoni ni lini itafika mwisho wake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe elimu kidogo sana kuhusu suala zima la uzazi. Ninasikitika kusema kwamba wengi wanaelewa kwamba mtoto wa kike akishaona tu hedhi basi amekuwa anastahili kuolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisafiri na mama mmoja alikuwa anatoka Zanzibar. Wakati tunaongea akaonyesha ana machungu akasema mimi mtoto wangu ameona hedhi ana miaka 10; alilia sana. Sasa miaka 10 mnataka huyu mtoto akaolewe? Dalili za mtoto wa kike kukua ziko nyingi, wenzetu wanazitambua moja tu na wengi ni hao wanaume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto wa kike kujua kwamba huyu sasa yuko tayari kuingia kwenye kuolewa au kuingia kwenye ndoa; kwanza unamwangalia kiuno chake tunaita pelvic girdle zipanuke. Lazima unaangalia hiyo ambayo pia tunaita nyonga. Kwa hiyo nyonga zinapanuka ndiyo dalili mojawapo. Pia dalili nyingine kwa mtoto wa kike ni sauti kubadilika kuwa nyororo, ngozi kubadilika na nywele kuota kwenye sehemu za kwapani na sehemu za siri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanachukua dalili moja kwamba mtoto akiona hedhi ndiyo amekua; siyo kweli. Kwa hiyo niwaombe sana wale wanaofikiria kwamba mtoto akifikia ameona hedhi miaka 10 au 12, (watoto wa siku hizi wanapata hedhi mapema) basi aolewe. Juzi mliona kwenye magazeti baba mmoja amemchukua mtoto wa miaka tisa akamharibu mtoto aka-bleed mpaka akafariki; ndicho mnachokitaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wanaosema eti sheria zinasema mtoto akipata hedhi aolewe, watoto wao wako shuleni wanasoma; hakuna aliyempeleka mtoto wake akaolewe. Mheshimiwa Waziri watuletee ushuhuda hapa watoto wao wameolewa na miaka 12 au 13? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Sheria ya Ndoa irudi. Mheshimiwa Esther Matiko aliliongea sana jambo hili, lakini bado tunaangalia tu. Wewe mtoto wako wa kike miaka 10 unampeleka kwa mwanaume kweli? Hivi kwa nini tunashindwa kufanya maamuzi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yale maoni waliyokusanya Mheshimiwa Gwajima na Mheshimiwa Ndumbaro yamefikia wapi? Kwa nini bado tunashindwa kufanya maamuzi kama nchi? Hawa wachache waliokuja sijui wanasema hapana sheria; kuna tamaduni lazima tuziondoe. Watoto wanahitaji kusoma, kwa hiyo hilo Wizara ilisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka majibu, mtoto kuona hedhi siyo kwamba ndiyo yuko tayari ni kama mahindi wakiona yale mahindi yanapotoa zile nyuzi pale juu ndiyo mhindi umekomaa? Si bado unaona kwamba lazima ukae, ukomae ndiyo ule. Huwezi ukauvunja ule ukala, mahindi yale yanatoa maziwa maziwa tu. Tujipange kwenye hilo, ninamwomba Mheshimiwa Gwajima asimame kwenye nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumza ni kuhusu suala zima la ukatili na maadili. Yaani ni ukweli usiofichika ukatili ndiyo umezidi, ubakaji upo, wamesema wenzangu kulawiti watoto kunaendelea na sisi tulisema walete Muswada hapa tubadilishe sheria. Mtu analawiti mtoto wako ni kwa sababu wakati mwingine hayatugusi. Mtoto analawitiwa halafu wanasema huyu mtu anapelekwa kule? Tulisema walete tubadilishe sheria tuweke sheria kali kama wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaume hao wanaobaka wahasiwe. Pia, niliwaomba wakipelekwa kule; jana tumewasifia sana Polisi hapa. Wakipelekwa huko kabla hawajafika Mahakamani washughulikieni. Kuna dawa wawape, wawahasi wale wakae hivyo hivyo watatumia lile eneo lao kwa ajili ya kutoa haja ndogo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge tunaliona hili suala kama ni la mchezo lakini haya mambo yanaendelea. Hebu tulete sheria sasa haya mambo ya kubakana na ya kulawitiwa tulete sheria kali. Tukifanya hivyo mara moja watu watashika adabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje kwenye haya mambo ya maadili ya kawaida. Mavazi sasa hivi hovyo. Niwapongeze sana wasanii ambao mpaka sasa wao mavazi yao ni ya heshima akiwepo Darassa, Lady Jaydee na Ben Pol wanavaa mavazi mazuri, lakini nyimbo mbaya na mavazi mabaya kwa wengine wote, Wizarz wachukue hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi, ni aibu kuna wanawake wanacheza vigodoro na Dar es Salaam ndiyo inaongoza. Hivi kweli wanacheza nguo zile, ninasikia zile nguo wanazilowesha maji halafu wanavaa ili sehemu zao zile zitingishike. Jamani tunaona hayo kwenye ma-clip, Serikali iko wapi? Wakamate hao wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanavaa nguo za hovyo na hii singeli; singeli imekuja vizuri ila wameibadilisha wanacheza hovyo. Mheshimiwa Bashungwa asaidiane na Mama Gwajima wawakamate wale wanawake wote wanaocheza, wanatuaibisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanacheza unaona kabisa hii ni sawa. Ali Kiba anavaa vizuri, tunataka wanamuziki wanaovaa vizuri, tunataka wasanii wanaovaa vizuri. Kuwa msanii au kuwa maarufu siyo kuvaa nguo za ajabu na siyo kuimba nyimbo za matusi. Sasa haya mambo tukiwa serious right from the beginning watu watajua Tanzania sasa iko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine maadili hayo hayo wamesema hapa. Tunawafundisha nini watoto kama kuna dhehebu la dini linafundisha vitu vya ajabu? Fungia! Wakati ule Mheshimiwa Sagini amempeleka yule Mchungaji, Hakimu akamwachia. Mtu anawafundisha watoto wetu eti mimi ni Mungu ndani yangu kuna Mungu, wanamwachia! Mheshimiwa Bashungwa anamwachia? Hapana, wafanye sasa hivi, ninaomba wa-review madhehebu yote ya dini ya hovyo hovyo yanayosema uongo tuyafungie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wanaona yule wa madhehebu mmoja ametoka Kongo, wameona alivyotutukana? Yule wa Kongo anasema ametuibia hela ametudanganya alikuwa anaitwa nani yule? Nani…

WABUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo huyo…

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo huyo. (Makofi/Vicheko)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kiboko ya wachawi…

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo, anaitwa kiboko ya wachawi. Kiboko ya wachawi anatamba alivyotufanyia Tanzania na ndiyo hayo hayo yanayoendelea kwa Mama Zumaridi. Hivi vitu kwa nini tunaviangalia? Yaani ni aibu kweli halafu Mchungaji mzima unahubiri mbele unakatakata viuno kweli? Halafu mnasema huyo ni Mchungaji? No…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hussein, taarifa.


TAARIFA

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimwongezee mchangiaji kwamba kwa kweli kuna umuhimu sana wa kuangalia maadili yetu; leo kuna vijana wanasuka kama wanawake. Kwa nini isichukuliwe hatua ya kuwanyoa nywele tunapokutana nao barabarani? (Makofi/Vicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa unaipokea hiyo taarifa?

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea hiyo taarifa na ndiyo maana nimempongeza mwanamuziki mmoja. Wewe hujamwona yule mwanamuziki ametoboa masikio, anavaa vaa hereni. Ali Kiba anaishi katika maadili, lakini wengine wanavaa suruali wanaimba muziki, wameishusha chini lichupi linaonekana; nani anataka kuona? Nani anataka kuona chupi yako? Kwani nani asiyevaa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuangalie hivyo vitu jamani. Hebu tusimame kwenye maadili tuwe kama Wakorea jamani tusimame kwenye maadili. Wanapaka; yaani ni vitu vya ajabu. Wasimamie na hapo niwaombe sana. Mama Gwajima wasaidiane na Mheshimiwa Bashungwa na Mheshimiwa Bashungwa hayo ndiyo maeneo yake, awakamate tutengeneze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niombe sana Mheshimiwa Gwajima kama anavyofanya kuna hawa wanafunzi wetu wenye ulemavu hasa ulemavu wa ngozi na ulemavu wa miguu, vile vifaa tukisema wavifuate hospitalini au sijui kwenye sectors hawapati. Mafuta ya watu wenye u-albino ninaomba wagawiwe shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa vya watoto wenye ulemavu viende kwenye vyuo au mashuleni, hapo tutakuwa tumetengeneza. Hawana uwezo! Please, hebu viende mashuleni wagawiwe; kwanza ni wachache. Wagawiwe kama wanavyogawiwa wengine vidonge vile vya TB, vidonge vya HIV, wagawiwe pia mafuta mashuleni na vyuoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana. (Makofi)