Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru kunipa fursa hii ya kuchangia. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya katika jamii yetu hususan kwa umaalum wao waliokuwa nao maana Wizara yao inagusa moja kwa moja wanawake, watoto na jamii nzima kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee sisi tukiwa kama Wabunge Wanawake hatuna namna na hatuna maneno mazuri, ushirikiano wao kwetu umekuwa mkubwa na wamekuwa wakifanya ufuatiliaji wa karibu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri maana yeye ni Waziri kwa wanawake kati yao ni wa mwendokasi. Pia, nimshukuru kwa namna anavyokwenda na Naibu Waziri wake. Naibu Waziri wake muda mwingi anakuwepo Bungeni, msikivu, mtulivu, mtu ambaye anatusikiliza, anasikiliza na kufanya papo kwa papo kutatua matatizo ya wanawake tunapomletea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nina mambo matatu ambayo nitakwenda kuyazungumza. Wanawake wa Zanzibar, Mkoa wa Magharibi wameniteua kunileta hapa Bungeni kuzungumza zaidi mambo yanayowahusu wanawake na kero za watoto na Tanzania kwa ujumla. Kwa hiyo sitosita kufanya hivyo kila nitakapopata nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumpongeza Katibu Mkuu wa Wizara na Watumishi wote kwa namna wanavyofanya kazi vizuri na Waziri na Naibu Waziri na ndiyo maana Wizara imepata ufanisi mzuri wa kufanya kazi. Niwapongeze Wakuu wa Mikoa wote Tanzania na Wakuu wa Wilaya. Mara nyingi shughuli nyingi za kijamii na matatizo mengi ya wanawake na watoto, utatuzi wake huanzia kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Wamekuwa wakichukua fursa hii kila inapobidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitamani niseme mambo mengi ninayojua kupitia Wakuu wa Mikoa wetu na Wakuu wa Wilaya. Mheshimiwa Rais wetu hakuwahi kukosea namna anavyoteua Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Tumeona kwa namna ya kipekee nilitamani kuyasema yale wanayoyafanya lakini ninafikiri Mheshimiwa Waziri na Naibu wake ni mashahidi hata kuna watoto wanaotelekezwa mitaani au kutupwa; Wakuu wa Mikoa bado wanawachukua kuwaweka ndani ya nyumba zao na Wakuu wa Wilaya. Niwapongeze, tunawaona kwenye mitandao namna wanavyoihudumia jamii. Hakika Mungu alipitisha roho ya kuwateua kupitia Mama yetu Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, 2024/2025, zaidi ya shilingi bilioni 67 ndiyo zilikuwepo kwenye Wizara hii, lakini kwa sasa tunaongea ni shilingi bilioni 76; ongezeko la shilingi bilioni nane. Tunamshukuru Rais wetu kwa kuupa umuhimu wa kipekee kwamba Wizara hii ni Wizara iliyobeba wanawake, watoto na kero zote zilizokuwepo ndani ya jamii. Tunasema ahsante na tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ambayo sisi kama Wabunge tunapaswa kuyawasilisha kwa Wizara ili kuona tunaboresha vipi na kuweza kufanya kazi vipi ndani ya Tanzania yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni mifumo ya uchangishaji wa fedha kwa watu wenye matatizo. Mheshimiwa Waziri ni Mama jasiri, hatuna mashaka na uongozi wake, angalia mifumo sahihi ya uchangishaji wa fedha. Kuna watu binafsi mara nyingi wanajitokeza labda kuna mtoto anaumwa na jamii yetu ya Tanzania ni watu wanaoishi kwa huruma na kuhurumiana, wanaishi wakiwa na nguvu ya pamoja ya kusaidiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa wanaweka mitandaoni namba za simu wanasema changia mgonjwa ni huyu. Mheshimiwa Waziri hili tunalileta kwako, mtu yeyote ndani ya mtandao anapoweka namba ya simu ya kuchangia iwe imepata kibali kutoka ndani ya Wizarani. Mheshimiwa Waziri alichukue hili wawe wanakata vibali na namba hiyo wawe wanaitoa wao ikiwa ni namba ya simu iwe imesajiliwa chini ya Wizara yenu na ikiwa ni namba ya Benki iwe imetoka kupitia Wizara yenu. Ikiwezekana kufanya hivi kwa mtu, wako wanawake wengi wanajitolea ndani ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wana vyombo binafsi vya TV wanaenda kuibua kero za wananchi na wananchi wengi na jamii yetu ya Tanzania huwa wanaguswa wanachangia. Mheshimiwa Waziri alichukue hili na namna ya pekee ya kulitatua, mtu anapotaka kuchangisha jamii ya Tanzania, kibali kiwe kimetoka chini ya Wizara yake. Atafute namna ya kuliweka ili likae vizuri liende. Maana yake nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba mtu huyo wakati anachangisha watamfuatilia mwisho wa kufunga mjadala wa kuchangisha alichangisha shilingi ngapi? Je, zilikwenda kwa mhusika? Bado liko chini ya dhamana ya Wizara. Ninadhani tuweke mambo yetu yaende sawa ili Watanzania wanufaike na Tanzania yao na michango inayotolewa na Watanzania wenzao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo kwangu lilinifanya leo nisimame ni mwenendo mzima wa wanafunzi katika shule zetu. Mheshimiwa Waziri muda mwingine kama hakualikwa ataalikwa Naibu Waziri au Waziri mwingine yeyote na muda mwingine Wabunge wa Viti Maalum au Wabunge wa Majimbo tunaalikwa mahafali ya shule watoto wa nursery wadogo mpaka watoto wa primary. Mheshimiwa Waziri nimesimama hapa kwa masikitiko makubwa, watoto wale sasa hivi kwenye mahafali zao kutoka shule za nursery kwenda primary wanafungwa kanga za kiuno wanafungwa tena ili kiuno kikaze wanafungwa kanga mbili Waziri atoe tamko tena atoe tamko kali kwa walimu na kwa shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaelewa kwamba kuna Wizara ya Elimu lakini suala la malezi ni juu ya Wizara hii. Haiwezekani watoto wetu wa kiume, watoto wa kike wadogo tena baya zaidi mtoto wa kike akishafungwa ile kanga kiunoni na macho anapeleka juu anakata viuno laiti ni kiasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, kuna watoto wetu wa kiume wanakata viuono mpaka inafika wakati unasema imekuwaje? Mheshimiwa Waziri hili halihitaji fedha, hili hatuna sehemu ya kuwaambia Mama Samia aongeze fedha, inahitaji karipio lake na tamko lake; wasituchezeshee watoto wetu viuno. Kuna michezo shuleni ya watoto wanapofanya mahafali wawape debate za kushindana juu ya kujibu, maswali itatufurahisha zaidi. Kengele imelia, hiyo ni ya kwanza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la watoto kuamshwa alfajiri. Mheshimiwa Waziri mtoto anakwenda nursery anaenda kujifunza kushika kalamu siyo kuandika, kushika penseli anaenda kujifunza (a) inaandikwaje? Hivi mtoto unamkuta anasubiriwa na basi la shule? Haya tumeamua kuyaleta kwa Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Elimu tumeshasema tumechoka tunalileta kwake kwa ujasiri wake hili asijadiliane nao; tunamtaka atoe tamko. Wanawake wa Tanzania tupo nyuma yake kwenye matamko haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiingii akilini mtoto wa nursery anasubiria basi la shule. Amka alfajiri fanya mazoezi, saa 10.30 mfikirie mtoto yule kutoka saa 10.30 alipokwenda barabarani kusubiri basi, ameamka saa ngapi kujiandaa? Wakati huo anamwacha mama yake na baba yake wamelala kitandani; huyo mtoto anaenda kutafuta nini? Tusaidiane kurekebisha muda wa mabasi kuchukua watoto kwenda shuleni. Mheshimiwa Waziri hili tunatumia nguvu kubwa kama Serikali na tunatumia nguvu kubwa kama Wabunge kuona vitendo vya ubakaji vinaondokaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya vitu vinavyoleta ubakaji ni pamoja na mifumo mibovu ya usimamizi wa watoto wetu juu ya kwenda shule. Mheshimiwa Waziri hili ni dogo lifanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la watoto waliopata matatizo ambapo wazee wao wamekorofishana na mama akaamua kuchukua begi kwenda nyumbani kwao. Mheshimiwa Waziri kuna tatizo kubwa na katika sehemu ambayo tunapaswa kutunga sheria iwapo mtoto akapotea, akabakwa, lakini mazingira yale kama wanatuhusisha sisi kama walezi au wazazi tuna sehemu ya kuwajibishwa kwenye sheria ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mama amekorofishana na mume wake ametoka; mama anakaa Kariakoo baba anakaa Tabata. Kwa hiyo mtoto yule anaenda kuishi na mama Kariakoo, shule Tabata. Kwa hiyo, bado yule mtoto ule mfumo wa kuamshwa saa 10 za usiku aende shule mbali. Mheshimiwa Waziri katika kesi zinazokuja lazima tuangalie kwa kina chanzo cha tatizo la mtoto limesababishwa na nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya matatizo tunasababisha sisi wazazi tuliowazaa watoto. Mtoto unamtengenezea mazingira magumu. Wewe umekorofishana na mume wako, ni wewe, lakini ushindani wako na mumeo unatengeneza kumuadhibu mtoto. Waziri, shule zimejengwa mpaka chini ya nyumba zetu. Mheshimiwa Rais anaendelea kujenga shule, hakuna sababu ya watoto wetu kupata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia hayo machache ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)