Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia na mimi nafasi ya kuchangia kwenye hii Wizara muhimu sana. Awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema, imempendeza leo nisimame kwenye Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyofanya kazi nzuri na njema sana kwenye Taifa hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inahusu wanawake pia. Ninapenda kuchukua nafasi hii nimpongeze sana Mwenyekiti wa Wanawake Tanzania, Mheshimiwa Mary Chatanda, pamoja na Makamu Mwenyekiti wake Mheshimiwa Zainab Shomari, amekuwa akipita kila mkoa kuhakikisha anaongelea wanawake, watoto na makundi ya watu maalum. Hongera sana Mheshimiwa Mary Chatanda pamoja na timu yake yote kwa ujumla. Mungu asimpungukie kwa muda wake na nafasi kubwa anayoitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimempongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwa, kwetu Mkoa wa Mbeya amefanya mambo makubwa kwa maana ya kwamba, kila Wizara inaposimama hapa kuchangia michango yake, kila mahali anaongelewa ambavyo amefanya kazi kubwa na njema kwenye Wizara hiyo. Kwenye wizara hii Mheshimiwa Rais ametusaidia sana, kwa Mkoa wa Mbeya amewajali pia, wanawake ambao wanajifungua, kwa maana ya Jengo la Mama na Mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wilaya ya Kyela amejenga Majengo ya Mama na Mtoto manne, Mbarali majengo manne, Rungwe pamoja na Busokelo majengo tisa, Chunya majengo sita, Mbeya Jiji majengo saba, lakini Mbeya Jiji hapa amejenga jengo kubwa sana, pale Meta, ambalo limegharimu fedha kiasi cha shilingi 11,300,000,000; pamoja na hayo, amenunua vifaa muhimu sana, kwa ajili ya wanawake na watoto, vya zaidi ya shilingi bilioni tano. Hongera sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa, amekuwa akijali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza sana Wizara hii. Ninampongeza Mheshimiwa Gwajima, Waziri, Naibu Waziri wake na Wizara yote kwa ujumla, wanafanya kazi njema sana. Ninaomba jambo moja, wawatazame wazee wa Taifa hili. Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, ni msikivu, ana busara na hekima, kwa majengo haya yote ambayo ameyajenga, kwa ajili ya afya za wanawake na Watanzania wote kwa ujumla, hawezi kushindwa kujenga angalau kila wilaya moja hostel, ili kuwatunza wazee pale kwa sababu, kuna wazee wengine ambao hawana msaada wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba, Serikali inatoa hizi Fedha za TASAF, lakini mzee yule anakuwa hana mtu yoyote wa kumsaidia, yamkini hata kwenda kuzifikia fedha zile! Fedha zile zinachukuliwa na wajanja; anakosa fedha, lakini kama kuna viongozi ambao wana roho ya huruma wakamfikishia fedha zile, akapewa, anapita mtu anamwomba akamnunulie japo sukari kwa sababu, yeye hana uwezo. Matokeo yake kijana anaweza akapotea na fedha na ndani hamna kuni, maji, sukari na kitu chochote cha muhimu. Kwa hiyo, niombe sana kwenye Wizara hii wawajali wazee. Pamoja na kwamba, wameonesha kuwajali, lakini angalau hostel ijengwe katika kila wilaya moja, litakuwa jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Watanzania Baba yetu wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alituachia misingi imara sana ya amani, upendo na mshikamano. Misingi hiyo ni ambayo Watanzania tunaendelea kukua nayo, ninaomba kutoa angalizo jambo moja; katika misingi hiyo kwa upande wa wazazi, baba na mama, mke anapokuwa mjamzito, awe baba awe mama, anategemea apate mtoto ambaye ni mwenye busara na hekima na awatii wazazi vile ambavyo wamemwongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine maadili yameporomoka sana. Maadili hayo ni sisi wenyewe wazazi ambao tunatakiwa tuyalinde. Natamani nishauri jambo moja kwa Watanzania, unajua kiumbe tangu kinaingia ndani ya tumbo, tunapaswa kuombea watoto wetu kuanzia akiwa ni kiumbe kipo ndani ya tumbo. Tuendelee kumwomba Mwenyezi Mungu mtoto huyo aje atoke na awe ni mtoto wa aina gani, vile ambavyo mzazi yeyote anapenda mtoto wake atoke akiwa salama na afuate yale anayofundishwa na wazazi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulizuka maneno mbalimbali kwamba, Wabunge wakisimama Bungeni kazi yao ni kumpongeza Mheshimiwa Rais. Sisi Wabunge tunasimama hapa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uhalisia wa kazi zake nzuri anazozifanya. Mheshimiwa Rais, pamoja na kazi nyingine tunazoziongelea, angalia miradi mikubwa ambayo ilikuwa imeachwa Awamu ya Tano; Bwawa la Mwalimu Nyerere lilikuwa 32% tu, lakini Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kadri anavyoweza zikatolewa fedha zaidi ya shilingi trilioni 6.58 likakamilika na sasa umeme upo wa kutosha. Nani kama Samia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo SGR sasa hivi imekuwa ni mtelezo tu. Tunakwenda Dar es Salaam, Morogoro; wanakwenda wanafanya kazi na wengine wanarudi kufanya kazi hapa. Yote hiyo ni kwa sababu, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesimamia hayo. Kipindi cha Awamu ya Tano zilitolewa karibu shilingi trilioni nne, lakini sasa hivi miradi inayoendelea kwenye SGR Mheshimiwa Rais ametoa zaidi ya shilingi trilioni saba, ujenzi wa SGR unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuongea jambo moja muhimu na makini sana. Kuna maneno ambayo yalikuwa yakipita kwenye mitandao, Mheshimiwa Rais wetu ametwezwa sana utu wake. Ninatamani kukemea sana hili jambo. Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mama mnyeyekevu, ana busara na hekima na ni msikivu sana. Mheshimiwa Rais wetu tunampenda sana, hatutaki mtu yeyote aguse mboni ya jicho lake. Maana kwa kutweza utu wake kwenye mitandao wanagusa mboni ya Mheshimiwa Rais na wamegusa mboni ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa, majirani zetu wa Kenya, wanapata wapi ujasiri wa kumtukana Mheshimiwa Rais wetu hapa nchini? Wanapata wapi ujasiri wa kusema watakuja hapa Tanzania wafanye wanavyotaka? Wao wakiwa na misukosuko kwao kule hawajawahi kuona Mtanzania yeyote ametoka hapa kwenda kufanya vurugu kwao, wao wanaingiaje hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Wizara husika, ambayo inashughulikia watu ambao ni watovu wa nidhamu, kuwakamata haraka mara moja na kuwadhibiti, ili wajue Tanzania tupo imara na macho. Hakuna kitendo kimeniuma na kimewaumiza Watanzania, kama mtu kumtukana Mheshimiwa Rais wetu. Ninajua hata sasa hivi wanaweza kuhamia kwenye Bunge hili ili waweze kututukana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeshazoea, Wabunge, watukane wanavyotaka, lakini Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wamwache mama wa watu. Wamwache aendelee kufanya kazi, maana tunajua anafanya kazi nzuri, anafanya kazi njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi tumempitisha kwa mara nyingine tena, ili awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia kipindi hiki mpaka miaka mitano ijayo na atakuwa Rais hata wafanye nini, hakuna mtu wa kupinga. Tunakwenda kwenye kampeni, tukutane site. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayupo mtu wa kumsemea vibaya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mimi na Watanzania wote tutakuwa mstari wa mbele. Tunampenda na tunamtegemea Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu, ni mama bora, mwema na amefundishwa maadili, watu wamemtukana kwenye mitandao, amenyamaza kimya ni kwa sababu, ni mstaarabu. Ni mama mwema sana na ni bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Ninaamini ujumbe umefika kwa ndugu zetu hao Wakenya na hata hawa ambao Watanzania wanagusagusa haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na ninaunga mkono hoja. (Makofi)