Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana. Niwapongeze Waziri na Naibu wake. Ninamwona Waziri anajitahidi sana, lakini bado tuna changamoto kubwa kwenye hii Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubakaji na ulawiti bado sana Tanzania. Hapa ninapoongea, kule Tarime, Halmashauri ya Mji wa Tarime, ndani ya mwezi mmoja kuna mtoto wa darasa la tatu ana miaka kumi tu; walivamiwa nyumbani kwao wakamfunga mama yake usoni wakampiga sana mama yule, ambapo amefariki na amezikwa siku kama nne hivi, wakambaka yule binti wa miaka 10. Haikuishia hapo, kuna dada mmoja anaitwa Esther Gaustine, huyo ni wa Kinyamanyoli; yule mama anaitwa Schola Magabe, ambaye wamemzika hata siku nne hazijapita, mtoto wake alibakwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Tulwa, Mtaa wa Kwa Kiogoma, kuna mama mmoja pia alibakwa, anaitwa Esther Gaustine. Wakamchoma visu, wakambaka akafariki. Mwenzake walimchoma visu, wakambaka, lakini akapona; siwezi ku-disclose jina lake hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mambo bado yanaendelea. Tunaomba sana, sheria zipo, lakini inaonekana enforcement haipo kabisa! Wanatoa elimu, lakini bado hayo majanga ni makubwa sana kwenye jamii yetu! Achilia mbali watoto wadogo ambao wanalawitiwa na kubakwa, haya mambo hatuwezi kuendelea kuyavumilia kwa Taifa hili la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na maswali, walishauliza hata Wabunge hapa. Wale akinamama ambao unakuta wamebakwa wamepata ujauzito, at a time inawa-affect kisaikolojia. Anabeba yule mtoto, wengine wanashindwa wanatoa mimba, lakini wengine wakizaa bado wanakuwa wanam-hate yule mtoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza swali hapa Bungeni; ninawaza kwa kina sana, kama ambavyo wameanzisha madawati ya jinsia kwenye vituo vya polisi, labda waanzishe tena madawati kwenye vituo vya afya, zahanati na hata hospitali. Kitengo maalum kabisa cha saikolojia kwa akinamama wajawazito ambao wanaweza waka-estimate ambao wamebakwa waweze kufanyiwa counselling wakiwa wajawazito, ili wasifanye abortion. Pia, hata wakishakuwa wamejifungua, kama wametelekezwa, waone jinsi gani wanawasaidia wasiweze, wengine, kutupa wale watoto au kuwanyanyapaa kwa namna yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafikiri inaweza ikasaidia wakati tukiangalia measures nyingine za kukomesha hili wimbi la ubakaji na ulawiti ambao unafanywa na ndugu zetu. Sijui ni kwa sababu ya depression ama kitu gani kingine? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru pia kwa Mji wa Tarime, tulikuwa tunapiga kelele Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo, lakini sasa hivi tunao wa kutosha. Changamoto ambayo tunaipata ni, tunashukuru wametupatia Maafisa Maendeleo ya Jamiii 11 wameenda kwenye kata zote nane na wengine wamebaki pale Halmashauri ya Mji, lakini hawana vitendea kazi kwa maana ya gari na pikipiki katika halmashauri ya mji, ili kuweza kuzunguka. Wapewe sasa kila kata, ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi, kama vile ambavyo kwenye Wizara ya Kilimo wameweza kuwapatia Maafisa Ugavi, basi na hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wapewe kwenye kata zao ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni changamoto ambayo inajitokeza sasa kwenye hii mikopo ya 10%, ambapo tunawapa vijana asilimia nne, wanawake asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili. Kule kwetu Tarime watu wenye ulemavu wamepata changamoto sana kwa sababu ya kile kigezo ambacho wamekiweka kwamba, ni lazima awe na shughuli fulani, ambayo anaifanya au biashara, unakuta hawana, kwa hiyo unakuta ile asilimia mbili haiendi kwa walengwa. Kwa hiyo, pale tunawaza, aidha hiki kigezo kiondoke au waboreshe waweze kutoa specific amount, kama ruzuku kwa hawa watu, ili sasa hata wawe na initial capital ya kuweza kufanya hizo shughuli kwa sababu, unakuta wengi, nikitoa sample ya pale Tarime, hawawezi kupata hii mikopo na inapita tu bila kunufaika wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kwenye mikopo hii ya 10% ni, watu wanaopewa, sheria iliyopo sasa hivi, wengine hawafanyi marejesho kabisa, hawarudishi na hatua ukichukua kali unasema umempeleka Mahakamani. Ukimpeleka kule ni kesi ya madai, anachoambiwa sana sana anapewa utaratibu upya wa kulipa. Wengine unakuta wanakiuka hata hiyo Amri ya Mahakama hawalipi. Kwa hiyo, unakuta fedha zinapotea, zinashindwa ku-revolve wengine waweze kupata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, labda wataangalia upi utaratibu mpya bora; aidha, watafanya mtu asipoleta afunguliwe kesi ya jinai, kama amechukua fedha kwa kudanganya, maana mtu kama amechukua kwenda kujiendeleza kiuchumi, ni lazima atafanyia kazi aweze kurejesha na wengine wapate, lakini ukichukua kwa ajili ya udanganyifu huwezi kupata hata hiyo ya kurejesha. Kwa hiyo, tuboreshe, wasiporejesha wafunguliwe jinai watu waogope, waweze kuleta marejesho ukizingatia kwamba, hizi fedha zinatolewa bila riba yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo, kwenye halmashauri ambazo hazina fedha nyingi. Kwa mfano, mapato ni shilingi bilioni mbili, nilishawahi kusema hata hapa Bungeni, 10% yake ni shilingi milioni 200 tu. Sasa, hii unakuta haitoshelezi ukilinganisha na halmashauri nyingine unakuta wanapata mapato ya shilingi bilioni 70 au 80, hapo10% yake ni shilingi bilioni saba au nane. Kwa hiyo, waangalie ile Mifuko mingine ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ipewe kipaumbele kwenye hizi halmashauri ambazo zina mapato madogo, ili wale wananchi na wenyewe waweze kunufaika, kama wengine wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kule kwetu, Halmashauri ya Mji Tarime, mapato yetu ni madogo sana hayafiki hata shilingi bilioni tano. Kwa hiyo, wahakikishe hizi zinaangaliwa, wakiwemo wazee ambao hawapati 10% zile kwenye hii Mifuko ya uwezeshaji waweze kunufaika, wazee wetu nao waweze ku-move mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu 2025 ni mwaka wa uchaguzi. Nipo kwenye Bunge la IPU na wewe mwenyewe ni Mjumbe, unajua kabisa tulikuwa tunaadhimisha miaka 40 kule, Bunge lililopita. IPU pamoja na UN Women waliweza kufanya tafiti za uwakilishi wa wanawake kwenye Mabunge; Wanawake Marais, Spika, Naibu Spika na Mawaziri, nitaenda kusoma hizi takwimu kabla sijaweka hoja yangu, ikizingatia mwaka huu 2025 Tanzania ni mwaka wa Uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia idadi ya Wabunge wanawake Tanzania, Kidunia tunashika nafasi ya 39, Kiafrika tunashika nafasi ya tisa na kwa East Africa Tanzania tunashika nafasi ya tatu. Kidunia nchi ya kwanza ni Rwanda na Kiafrika pia, ni Rwanda, wenyewe wana lower chamber na upper chamber. Kwa wastani wanakuwa wana 59% uwakilishi wa wanawake Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuja South Africa, kwa Afrika wana 44% wenyewe ni wa pili, wa kwanza ni Rwanda. Ethiopia wana 36% ya wanawake Bungeni. Kwa East Africa sasa Rwanda ya kwanza 59%, wanafuata Burundi 38%, hii ni kwa mujibu wa Januari; ninajua kuna baadhi ya nchi zimefanya uchaguzi, kama Namibia. Wanafuata Burundi 34.2%, sisi Tanzania tunafuata kwa 37.2% wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwa upande wa Mawaziri wanawake, Tanzania kidunia ndiyo tupo 65, Kiafrika tunafika nafasi ya 15, ya kwanza ni Ethiopia ina 45% ya wanawake Mawaziri. South Africa ina 43% ya wanawake Mawaziri, Madagascar ina 42% ya wanawake Mawaziri. Kwa East Africa Tanzania sisi ni wa nne, Burundi ni ya kwanza 33%, Kenya na Uganda walipata 30% wote na Tanzania tuna 28.6%. Mawaziri kwenye sekta nyeti, kama defence, Tanzania tumo, kidunia ni wanawake 21 tu ambao ni Mawaziri. Pia, ikasisitiza sekta, kama finance, madini, nishati na sekta nyingine nyeti (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye Maspika ni 23.7%. Tanzania tunashukuru sisi tuna Spika wetu mwanamke na ndiyo Rais wa IPU, Naibu Spika ni 32%. Kwenye Marais (Heads of State) 11%, Heads of Government ni 8.3%. Heads of State and Government ni Marais sita tu dunia nzima, kwa Januari. Kwa Afrika ni Rais mmoja tu, ambaye ni Dkt. Mama Samia, by then, kwa Januari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, tunajua kwenye uchaguzi huwa kuna unyanyasaji wa aina nyingi. Ninashukuru Tanzania tumetunga sheria ile, kama wakati wa kampeni wakifanya violence yoyote against women, watachukuliwa hatua. Pia, kuna hizi cyber bullying na ndiyo maana hata ukiona watu wana-react na mimi, in particular, jana nili-react sana kwa Rais kushambuliwa kwa cyber bullying ambazo zinamvua nguo kwa sababu, kwanza ni image siyo tu kwa Tanzania, kwa Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanamke pekee ambaye ni Head of State and Government kwa dunia katika wanawake ni sita tu. Kwa hiyo, lazima tuhakikishe tusiwafanye wanawake wajitoe kwenda front kwenye nafasi ya udiwani, ubunge na urais. Nimeona ACT wametangaza kuna mwanamke atasimama kupitia ACT nafasi ya Urais. CCM wameshampitisha Mheshimiwa Dkt. Samia kusimama kugombea nafasi ya urais. Lazima tuhakikishe mtu ukimpinga mtu, m-criticize kwa hoja na sera, siyo kumtweza utu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana…
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa. Mheshimiwa Mpembenwe.
TAARIFA
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Pamoja na mchango mzuri sana anaochangia Mheshimiwa Mbunge, Senior, ninataka nimwambie tu; anachosema ni sahihi. Wanawake wanapaswa wapewe nafasi ya uhakika, lakini kwa Tanzania nafasi ya Urais tayari tunaye Mama Samia. Ninashukuru sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Samahani Mheshimiwa Esther! hii ni Taarifa au approval?
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, unilindie muda.
MWENYEKITI: Unaipokea hii Taarifa?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa yake ninaipokea kwa sababu nina imani. Nimesema hapa ACT wameweka mwanamke, CCM wamesimamisha mwanamke; mama anaweza kuwa na advantage zaidi kwa sababu, yupo kwenye mamlaka, ataenda atauza alichokifanya, wananchi watapima. Wakiridhika na yale ambayo amefanya watamu-endorse. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, atakuwa Rais baada ya uchaguzi kufanyika, Tarehe 28 Oktoba, 2025. Kwa hiyo, niwaombe sana, tunaposimama kukemea cyber bullying, mimi jana nilisema ni activism wa haki za binadamu na wazungu wanasema, two wrongs don’t make right; mimi nikikukosea huwezi uka-revenge kwa kunifanyia ubaya, ndiyo eti unajilipiza niliyofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote ambaye anahisi amefanyiwa mabaya na Mamlaka ya Tanzania kuna mambo mbalimbali; kuna Mamlaka ya Kitaifa na Kimataifa, tuna mpaka Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, kama unahisi there is no justice, nenda, file. Hata hapa Tanzania tumeona kuna mtu alishawahi kufukuzwa kazi, akahisi hakutendewa haki, mawakili kutoka kwenye chama changu wakaenda Mahakamani ku-file, ili aweze kupata haki yake. Ukifanyiwa kosa usirudishe kosa kwa kumtweza mtu mwingine, hiyo mimi nitapinga, leo, kesho, mpaka ninaingia kaburini. Ahsante sana. (Makofi)