Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama nilivyosema hapo awali ninawapongeza viongozi, lakini nisimsahau Katibu Mkuu Jingu ambaye yeye ndiye anayeendesha Wizara, kwa maana ya utendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa Wizara hii ni Wizara muhimu sana kwa kuweka Taifa letu la sasa, la kesho na kesho kutwa. Tusipokuwa na msingi kwa kumsaidia Wizara hii basi tutakuwa hatuna Taifa hapo mbele kwa sababu tunapozungumzia mwanamke, tukizungumzia mtoto na jamii nzima, basi tunakuwa tumeweza kujua ni namna gani tunaweza tukaandaa Taifa letu kuwa bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninapenda kuzungumzia suala la bajeti. Tusipoipatia Wizara hii bajeti ya kutosha; kwa sababu tunafahamu hapa walipata fedha za maendeleo 31.95% hii ni namba ndogo sana. Bunge linapopitisha bajeti kimsingi bajeti zile zinaenda kusaidia Wizara kufanya mambo yale ambayo tumewaambia wafanye. Tunapowapa chini ya 50% utekelezaji wao hasa wataalam unakuwa mbovu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kuwa Wizara hii inaendesha vyuo vya ustawi wa jamii. Tunafahamu na hata Kamati imeeleza hapa, kwamba mabweni, vyuo, bado ni chakavu. Tunahitaji kujenga na kuwapatia fedha za kutosha na tukifahamu kabisa kwenye mabweni tunakuwa tumemsaidia mtoto wa kike. Anapokuwa anasoma katika mazingira mazuri, basi yale mambo yasiyomfaa hawezi kuyafirikia kwa sababu yuko katika eneo ambalo linamsaidia aweze kusoma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema kwamba Wizara hii ndiyo inayotengeneza wanawake wa kesho, mama wa kesho, viongozi wa kesho. Basi tunaomba tuwapatie fedha sawasawa na jinsi walivyoomba na kuwafanya ndugu zetu hawa wataalam waweze kufanikisha yale ambayo wameyapanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna eneo la mikopo ya wafanyabiashara ndogo ndogo. Tunaomba sana ninajua kwamba bajeti anaisema na sisi tunapitisha vifungu hapa, lakini utekelezaji wake unakuwa mdogo. Mwisho wa siku hawa watu wanaanza kuona Serikali kama haifanyi kazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Rungwe sijaona, labda aje aniambie anapotoa majibu; kwamba kuna Wamachinga wamepata mikopo. Kwenye takwimu zake inaonyesha kwamba aliomba bilioni nane, lakini watu waliopata tu ni milioni 197. Tunaomba basi, kama bajeti inataka bilioni nane basi at least isogee ili watu hawa wafanyabiashara ndogo ndogo waweze kufanikiwa, maana hao ndio wengi wanaofanya uchumi wetu, hasa kwenye halmashauri zetu, uweze kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudi tena kwenye suala la maadili. Sisi kama Taifa, kwanza sisi viongozi tunaamini kwamba tukitengeneza familia bora kwenye ngazi ya familia, basi Taifa linapata viongozi bora. Leo hii tukianza na sisi viongozi, hatujui watoto wetu wanacheza na nani, hatujui watoto wetu wanaongea na nani, tuko bize na siasa, kwa sisi wanasiasa. Viongozi mbalimbali maofisini unatoka nyumbani saa 11 asubuhi unarudi nyumbani saa tano usiku, hujui mtoto wako anaongea na nani, amekula nini na anafanya nini. Nimesema tunatengeneza viongozi wa kesho. Tusipowasimamia sisi tukasema kwanza Serikali ije, tunaanza kwanza sisi Serikali inafuata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna maadili mabovu kabisa kwenye jamii zetu. Tunaona jinsi ambavyo watoto wetu wanaishi na wadada wa kazi ambao hata huyo dada maskini ambaye tumesema hapa na wenzangu waliotangulia asubuhi, hata mishahara yao tunawakopa hatuwapi. Si tu kuwakopa tunawapa pia mishahara midogo sana; na elimu zao wengine ni ndogo kabisa kuliko hata watoto wetu. Unategemea huyo ndiye ahakikishe mtoto wako amekula vizuri, uhakikishe mtoto amempeleka shule, wala huwezi kujua mtoto amerudi shule saa ngapi. Tunakuja kupata kizazi ambacho tunakilaumu, tunasema watoto hawatusikii sisi, kumbe watoto ni watoto wa kinadada. Mtoto analelewa na dada asubuhi mpaka jioni, mzazi hujihusishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia masuala ya shule za boarding, tunafahamu kabisa kwamba ni vyema watoto wasome shule zote, ni haki, lakini mtoto ambaye ana miaka mitatu anawekwa boarding, hili ni suala la hatari sana kwa kiazi kijacho. Mtoto anaangalia TV channels ambazo hatuzifahamu asubuhi mpaka jioni bila kuangaliwa na wazazi wala walezi ambao wamepewa. Hiyo siyo sawa. Matokeo yake sasa ndiyo tunapata hao watukanaji wa kwenye mitandao. Niseme tu kwamba, tusipokuwa na maadili mema kama Taifa tutalaumiana, tutalaumu Serikali, lakini mwanzo wa ujenzi wa familia ni wewe mzazi ambaye umetengeneza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mheshimiwa Mbunge hapa amezungumzia suala la akinababa wanaozalisha wanawake na kuacha watoto. Hili ni suala ambalo sasa limekwishakuwa kama mazoea na single mothers imekuwa kama ni jina la uhalali kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafahamu kwamba tumekuwa tunamrushia Mheshimiwa Waziri, ma-message mbalimbali akinamama wakiteseka kabisa. Mtu anazaa na mtu kwa makusudi. Anajua kwamba yeye ni mume wa mtu, anazalisha halafu anafanya siri. Akina dada waliozalishwa waseme waume zetu walikowazalisha ili wawe wazi, ili watoto hao waweze kutunzwa kwa sababu kosa siyo la mtoto. Mapenzi wamefanya wao wawili, lakini watoto hawapelekwi shule, watoto wanapata shida hawana bima za afya, akinababa wazima kabisa na vyeo maofisini wanazalisha watu na kujificha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri alisimamie hilo, kwa sababu hatimaye tunaacha watoto wenye vinyongo vikubwa kabisa na kuja kutiliana sumu na watoto tuliowazaa kwenye ndoa kwa sababu tu wana uchungu waliofanyiwa na baba zao ambao hawakutaka kuwatunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo pia akinamama ambao pia wanawaza vibaya. Mama anazaa mtoto nje halafu anatupa mtoto. Kwani alipokuwa anazaa kwa nini hukuwa na kinga? Kwa sababu kuna sayansi zinaendelea na wakati mwingine wanawapeleka kwenye vituo vya kulelea watoto, ninafikiri si sawa. Tupeleke watoto kwenye vituo wale walioshindikana kabisa, ambao wamepata bahati mbaya ya kufiwa na amebaki na bibi ambaye ni mzee, tuwapeleke basi kwenye hivyo vituo. Lakini wamezaa kwa mapenzi yao kwa makusudi wanakuja kuwaweka watoto katika hali mbaya na hatimaye tunawaita watoto wa mitaani. Mtaa haujawahi kuzaa mtoto hata siku moja. Tuhakikishe tunawalinda hawa watoto kwa nguvu zote, maana hilo ndiyo Taifa la kesho (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mitandao; haki za watoto kwenye mitandao. Kuna watu wanapiga picha bila hata kuziba nyuso za wale watoto. Sheria ipo; uwezi kum-expose mtoto kwenye mtandao hata kama unataka apewe matibabu, hata kama unataka asaidiwe. Ni lazima ufiche sura yake kwa faida yake na kwa ulinzi wake na usalama wake. Ninaomba kwa picha kama hizo azitolee matamko. Tumemwambia tangu asubuhi atoe matamko. Awe tu mama matamko, tunamruhusu kabisa. Kwa sababu hatimaye tunahitaji usalama wa hawa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna cyber crime na bullying kwenye mitandao. Hili suala si la Mama Samia kwa kwa sababu ni Rais wa Tanzania, ni suala la haki ya mwanamke kulindwa. Leo hii tunakwenda kwenye uchaguzi, tulitunga sheria hapa, kwamba tunahitaji kulinda haki ya mwanamke. Leo hii unawezaje mwanamke mwenzetu akamtukana mwanamke mwingine? Hii haitakubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala wala si suala la kisiasa, ni suala la hifadhi na hadhi ya mwanamke anayotakiwa kulindwa nayo. Wanawake wenzetu wengi wengi wengi; wewe fikiria kama Mheshimiwa Rais anaweza akafanyiwa vile nini mtu wa kawaida anashindwaji kufanyiwa hivyo? Anafanyiwa vitu vibaya, anaweza akafanyiwa masuala ya ngono na yakarushwa kwenye mtandao na hao wanaume wanaofanya hivyo wapo, lakini pia wanaotukana kwenye mitandao wapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema vizuri sana kiongozi mmoja hapa asubuhi, kwamba Wizara ya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na Wizara yake Mheshimiwa Waziri, ni lazima tusimamie haki za wanawake wote akiwemo na Rais wetu ambaye ametukanwa. Hili nimeliona kwenye mitandao wakiendelea kusema, kwamba nyinyi mnaosema mna njaa. Suala la njaa lipo katika haki na staha ya mwanamke yeyote katika Taifa hili. Tunaomba tulindwe kama wanawake. Tusipokuwa wakali mwisho wa siku tutajenga Taifa ambalo kitu kikifanyika kidogo tu unarushwa kwenye mtandao. Kitu kikikosewa kidogo tu unarushwa kwenye mtandao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sheria zichukue mkondo wake kwa kulinda hadhi ya mwanamke yeyote anayesemwa vibaya kwenye mtandao. Hata kama umegombana na mume wako, hana mamlaka ya kurusha chochote, kwamba huyu mwanamke nimemwacha kwenye mtandao. Tunahitaji privacy ya ndoa, tunahitaji privacy ya wanawake, kwa sababu tunajua mwanamke akilindwa Taifa linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia mambo mengi sana. Mwaka jana nilizungumzia suala la ombaomba, hasa wale wazee wanaotembea na vijana wadogo. Muda wa saa za shule mzee ameshika fimbo na anavutwa na mtoto wa darasa la pili au la tatu au la nne kwenda kuomba kwenye baa. Ninaomba watoto hawa na wazazi hawa wapigwe marufuku; na tutoe tamko kabisa, kwamba, hakuna kutoa fedha kwa mzee huyu kwa sababu zile fedha hazimsaidii yule mtoto. Hiyo ni biashara ya yule mzee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa wana future yao ya kesho. Leo hii saa saba mchana anatembea na mtoto baa anakwenda kuomba fedha. Huyu mtoto atasoma lini, anapata afya gani? Watoto ni wachafu, unaona kabisa watoto ni wadhaifu. Ninaomba litolewe tamko kwa watoto hawa. Nilisema mwaka jana na mwaka huu ninarudia. Ninaomba Mheshimiwa Waziri alichukulie hatua suala hili (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, tunaomba kabisa Mheshimiwa Waziri asimamie nafasi yake kama Waziri. Tuko nyuma yake kuhakikisha kuwa haki ya mtoto wa kike pamoja na wanawake viongozi na wanawake wa kawaida inalindwa sawasawa na sheria na kanuni la Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, ninaunga hoja katika bajeti hii. Ahsante. (Makofi)