Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uhai na akanipa afya njema jioni hii leo nikaweza kusimama katika Bunge letu hili Tukufu na kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia kumpongeza kwa kazi nzuri ambazo anaendelea nazo za utekelezaji wa Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi. Aya inasema, “Man la yashkurin-nasa la yashkurillah.!”. Mtu yeyote ambaye hatamshukuru binadamu mwenziwe basi hata Mwenyezi Mungu hataweza kumshukuru. Mimi ni nani, wao ni nani hata wasiweze kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia kwa mazuri ambayo ametufanyia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kuendelea kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoendelea kuletea maendeleo Taifa hili. Aliyekuwa haoni hataki kuona, asione, lakini sisi tulio wengi tunaiona kazi kubwa anayoifanya Mama Samia. Ni kazi ambayo imetukuka; ni kazi ambayo inaleta imani kubwa kwa Watanzania, hasa wanyonge, tukiwemo sisi wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anatokea mtu kibaraka aliyekuwa tayari amepigwa na laana na Mwenyezi Mungu anamkosea Mama Samia, anamkebehi. Tunasema Mwenyezi Mungu hatasimama nao watu kama hao. Hatutowapa nafasi watu madhalimu na wabaya ambao hawaoni jitihada ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeumia sana. Ninachangia Wizara hii ya Maendeleo na haya ninayazungumzia kwa ukali. Tumekerwa sana na watu hawa. Tunasema wakome! Mama Samia amezaliwa, ni mtoto ana wazazi wake kama walivyozaliwa wao. Haiwezekani na tunaiomba sana Wizara inayoshughulika na Mambo ya Ndani, Wizara yetu ya Ulinzi na Usalama, ihakikishe kwamba inachukua sheria mara moja kwa vibaraka wale ambao wamekosa nidhamu na utu. Ninathubutu kusema kuwa hawana hofu ya Mwenyezi Mungu. Haiwezekani! Wao ni nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi ni mtu ambaye ameshushwa na Mwenyezi Mungu. Uongozi hakujitengenezea, amepewa. Leo inakuwaje anakuja mtu anamchafua Rais wetu? Halikubaliki. Kama kuna vibaraka wanaona wana nafasi katika nchi hii kumchafua Mama Samia, wamechelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, salamu ziwafikie wale majeruhi wote ambao wanajaribu kuichezea nchi yetu. Tuko macho Tanzania, hatuchezewi na Mama Samia yuko vizuri, na jeshi lake ndiyo kina sisi hapa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze mchango wangu kwa Wizara hii, hizo zilikuwa ni salamu tu. Mchango wangu leo utajikita kwa vijana wetu Wamachinga. Bado tutaendelea kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ndugu zetu Wamachinga hawa ambao ni wafanyabishara ndogo ndogo, wakiwemo Mama Lishe, Baba Lishe, wale ndugu zetu ambao ni wajasiriamali washonaji wa nguo, pia bodaboda ambao ni vijana nguvu kazi ambayo Taifa inalitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nampongeza Mama Samia na kumshukuru sana kwa kuyaona makundi haya, kuyafikia, lakini pia kuyarahisishia maisha yao ya kila siku katika kujitafutia riziki. Hongera sana kwa Mama Samia na Mungu atamsimamia amtie nguvu. Wale wote waliokuwa na nia mbaya Mwenyezi Mungu atawalaani, Insha Allah. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama Samia ameweza kutoa fedha kwa ajili ya kuwekea mazingira mazuri ya kufanya kazi makundi mbalimbali yakiwemo kama haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameweza kujenga ofisi kila mkoa ndani ya Tanzania hii. Kama haitoshi, amewapa mtaji wa milioni 10 kila mkoa. Tunataka nini Watanzania? Tunataka nini kama si kumtia nguvu Rais wetu na kumshukuru kwa upendo wa dhati, lakini anafanya kwamba ni wajibu wake. Halafu watokee wachache tu waseme ooh Mama Samia! Nyie, hee; mshindwe na mlegee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi za mikoa 17 tayari ziko katika matengenezo ya kukamilika ili na wao sasa waweze kufaidika na zile shughuli zao mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Rais wangu, Mama Samia kwa kuendelea kuwaona machinga hawa, bodaboda, baba lishe, mama lishe lakini wale mafundi wa nguo, na bodaboda kwa kufikia zile nafasi za mikoa. Kama haitoshi, ninampongeza Rais wetu sana kwa sababu Ilani hii ameitekeleza 99% na sasa tupo mwezi Juni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mpaka nina furaha kwa kweli, amewapatia mtaji wa shilingi milioni 10 kila mkoa, lakini sasa ofisi za mikoa 17 zimekamilika na wengine wapo mbioni kukamilishiwa.
(Hapa kengele iIlilia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba dakika moja nimalizie, kwa sababu kuna mambo mazuri. Sasa hivi watu 78 ambao wamesajili kupitia mfumo wanasomeka kwenye mfumo, lakini kama haitoshi 601 tayari wameshakopeshwa tunataka nini? Kama siyo kumpa kura ya ndiyo Mama Samia, ikifika 2025. Mama Samia huyu huyu sasa hivi tayari kuna shilingi bilioni 1.1 hizo hela tayari zimeshaenda kwa hao ndugu zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengine 2,000 wanatarajiwa kupata mkopo wa shilingi bilioni 3.5 kwenye bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2024/2025. Haya ndugu zangu ndio maendeleo, halafu waje wengine hapa wawavunje moyo. Ndugu zangu machinga ninataka nitoe rai kwao, niseme Mama Samia ni kioo lakini Mama Samia mtu tena mwenye utu, tumshikilie, tumng’ang’anie na tumwombee kwa Mwenyezi Mungu, aendelee kumtia nguvu. Ninakuahidi Mama Samia tutaendelea kukutetea na hatakugusa mtu yeyote, Mwenyezi Mungu atakulinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zetu hawa machinga pia, wamebahatika sasa kazi zao kuingia kwenye mfumo wa kidijiti na kwa sasa hivi wameweza tena kuingia ndani ya mifumo hiyo kupitia vitambulisho vyao vya NIDA, lakini wameenda kuingia kwenye mifumo ya benki. Mwanzo hawa walikuwa mambo ya kukopa ni magumu, lakini sasa masharti ni nafuu, kwa sababu mtu mwenyewe anaweza kukopa na kujidhamini, nani kama Mama Samia? (Makofi)
WABUNGE FULANI: Hakuna.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, baada ya maelezo hayo ninaunga mkono hoja. (Makofi)