Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa ruhusa yako saa hizi. Nimesimama hapa katika Bunge hili Tukufu ili kuweza kuichangia hotuba ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ninapenda sana kuichangia hii, maana ina mambo mbalimbali, hii Wizara tamu kama nini. Wale viongozi wangu kule mbele walipo na wao ni wazuri, watamu sana. Maana Mheshimiwa Waziri wangu pale na Naibu wake, Mheshimiwa Mwanaidi, wanafanya kazi kubwa. Ninasema siku zote Mheshimiwa Mwanaidi, saa zote ukimwita; leo ukimwita anakwambia mimi sasa hivi sina nafasi niko huku. Anaangalia Wizara yake, jinsi anavyofanya kazi pamoja na Waziri wake. Akija hapa anatoa maswali asubuhi kisha anatoka anakwenda kufanya kazi zake za wanawake. Kwa hiyo, ninawapongeza sana, waendelee kuifanya kazi vizuri katika Wizara yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi Mheshimiwa huyu alivyokuwa ana maono. Ninasema huyu kaanza kuyaona maono toka huko anakotokea Mheshimiwa Rais. Tupo pamoja kipindi kile Mbunge na Mwakilishi Jimbo la Makunduchi, tunafanya kazi basi yeye ana maono, hapa nikifanya hivi itakuwa hivi yanakuwa kweli na hapa nikifanya hivi inakuwa hii, inakuwa kweli. Sasa hivi ameshakuwa Rais anafanya vitu kweli. Kwa hiyo, ninampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wanaombeza, waache wambeze na yule sisi kwetu kazaliwa hana matatizo, tena kazaliwa mtoto wa tumbo, mjukuu wa mbavu. Mwenyezi Mungu amwondolee shari, ampe heri, amjaalie kila la heri ndugu yangu, aendelee na kazi zake vizuri na viongozi wenziwe waliomzunguka Mheshimiwa Dkt. Samia. Mheshimiwa Dkt. Samia ana imani toka huko anakotokea, mpaka hivi sasa anaendelea na kazi. Ninasema haya kwa sababu mimi mwenyewe ninamjua A to Z, ninamjua Mheshimiwa Dkt. Samia. Kwa hiyo, waache wao wabeze, wafanye maneno yao wanayomsemesha yeye mwenyewe katulia na anaangalia, siyo kama hajui kusema yule, anasema tena akisema neno lake moja utatafuta uvungu ujitie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuchangia sasa. Kuna suala hili la akinababa wale ambao wanabaka watoto huko nje au kuwalawiti, wanaume hawa wanawalawiti watoto wetu wale ambao hawana akili, maana akili hawana. Wanawaona hawa mbumbumbu basi huyu mimi ndiye atakayenifaa. Maana anaona yule mwenye akili yake, anaona mimi pale nitaenda chukua mzigo wa UKIMWI au maradhi mengine, lakini ninakwenda kwa huyo uliokuwa mbumbumbu hajafanywa chochote. Anakwenda kule anamsemesha na yule analaghaiwa, anacheka tayari anamwingilia na kisha pengine kashamjaza mimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimba ile aliyokwisha kumjaza sasa, siyo yule kama atamshughulikia, atashughulikiwa na wazee wake, baba au mama au familia. Mtoto yule atazaa atakwisha na kama ataulizwa basi anasema, mimi kanifanya jambo hili Fulani, lakini akiendewa yule mwanaume tayari na yeye anakataa au kama hakukataa ndiyo lile tulilolisema la kuhusu familia. Familia wakae wazungumze ili yule apate kumwoa, hamwoi. Anangoja mtoto akue, aje tena kumfanyia kitendo kingine, anamtia mimba nyingine na hili lipo mimi ninaliona, limo ndani ya nyumba yangu nitasema. Akisha kumtia mimba ile nyingine yeye yule anakimbia haonekani kabisa. Sasa pale tayari tushakuwa na mizigo miwili, baada ya yule mtu tunayemlea (mwathirika) yule halafu na yule mtoto wake wa mwazo uliyelea, aliyezaa na hivi sasa hivi tunalea mimba nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili aweze kulea, ninamwomba Mheshimiwa Dorothy na ninaiomba Wizara yako ifanye kazi juu ya suala hili la hawa watoto wanabakwa huko mitaani na wanaume waliokuwa hawajitambui (hawajijui). Hawa wanaume hawa wapo na ninasema hili siyo kama wale wanaume waliokuwa wana akili zao tuliokaa humu Bungeni kuzungumzia sheria zetu humu Bungeni. Wanaume hawa wapo huko mitaani wanafanya vitendo vibaya kwa watoto wa wenzao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, wakae kitako, pamoja na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wapange jinsi mtu kama huyu anayemlawiti mtoto au kumbaka, kisha akamwachia na ulezi kama huo. Kwa hiyo, hilo ndilo ninalolisema kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili, ninasema hivi katika taarifa yako, taarifa yako nimekaa nimeiangalia kwa kina nzuri, haina mbambamba nitasema, tena ile inasema tukutane site na site yenyewe ndiyo hii hapa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, amesema kwamba kuna kampeni ya watoto wanaozurura mitaani. Watoto hawa wapo, wanazurura mitaani tena na wazee wao, mtoto anaachiwa anaambiwa nenda kwenye gari ile pale, mzazi kajificha nyuma na mambo hayo yapo sana sehemu za Dar es Salaam. Anakwenda kwenye gari anakwenda kuomba akishapata ile pesa anampelekea mzazi, wale watoto bado wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mpaka hivi sasa hii kampeni hii tuliyonayo kama haijafanyika basi ifanyike, imefanyika izidi kufanyika ili hawa watoto waache kuombaomba kwenye magari, mitaa na barabara. Utaogopa wewe binafsi mtoto anavyokujia utaogopa, ninasema huyu mtoto akipigwa na gari huyu, kweli huyu mtoto ana mzee? Kumbe ana mzee wake anamwangalia, kakaa huko, yeye huku anakwenda kuombaomba. Mheshimiwa Waziri, hili suala lipo kwa hiyo hii kampeni ifanyike, tena ifanyike kampeni ya kitaifa, wanaoweza tushirikiane twende ili hili suala liweze kutoka. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa, tafadhali.
TAARIFA
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimpongeze mama yangu kwa mchango wake mzuri, nilitaka kumpa taarifa tu, siyo tu kwamba wazazi ndiyo wanawasindikiza watoto kwenda kuomba, lakini kuna watu wapo Dar es Salaam biashara yao ni hiyo. Wana nyumba, watoto wanaishi kwenye nyumba hizo, mchana wanawapeleka kwenda kuomba, usiku wanawafuata wanakusanya zile fedha, ndiyo mradi wao. Kwa hiyo, ni vizuri akapata taarifa hii ili aishauri Serikali vizuri juu ya kudhibiti uhalifu huu wa kutumia watoto kufanya biashara. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa unapokea Taarifa ya Mheshimiwa Saashisha?
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea taarifa ya mwanangu, huyo yeye ndiyo kazi yake kunipiga mataarifa nikizungumzia katika Wizara hii, kwa hiyo mimi ninapenda sana anipe taarifa halafu niendelee. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri kampeni hii iendelee kufanyika ili tuweze kuwadhibiti hawa watoto wetu pamoja na wazee wao, waweze kukaa katika majumba yao wafanye shughuli zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubakaji na ulawiti umepungua na haya unasema wewe katika taarifa yako ya kazi kwamba haya masuala yamepungua. Haya masuala Mheshimiwa bado hayajapungua, hayajapungua yapo (ubakaji na ulawiti). Juzi tu hapa nchi hii yetu hii ya Tanzania, kalawitiwa mtu, alivyokwisha kumlawiti mbele na nyuma kisha wakamuua, wakaenda wakamtupa mwituni, baadaye wao wakakimbia. Mtoto yule mwanamke amekutwa mwituni amefariki katika Tanzania hii na nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo bado hili suala lipo, tuzidi kupanga sheria. Nilisema humu ndani, sheria hii tuipange iweze kupatikana japo wanaume wawili tu wanaobaka wale, wawili tu wakahasiwa hawa, wakishahasiwa hawa watu wawili, wakajulikana na wanaume wenzao hili suala litaachwa. Sheria imeletwa tumeitunga humu Bungeni, lakini ninasema hii sheria wala sikuifurahia sana, kwa sababu sikuijua, na hii sheria ilikuwa tuipitishe kwa uzuri ili hawa wanaume wanaobaka wakamatwe watiwe ndani miaka 30. Wakishatiwa ndani miaka 30, wapigwe shindano, wakishapigwa shindano wamekwisha wanarudi majumbani mwao wanaenda kulala, ndilo lililobakia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama si hivyo hapa kila siku tutakuja hapa tukaizungumzia Wizara hii, tukaisema Wizara hii, lakini hili suala bado lipo na linafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nawashukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wangu, Mheshimiwa Mwanaidi. (Makofi)