Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na ninamshukuru Mungu pia kwa kuwepo leo tena na kupata fursa hii ya kuchangia. Kabla sijaenda mbele sana unajua hii ndiyo Wizara kwetu ina-deal na NGOs na kuna mambo ya wanaharakati humu ndani. Nichukue nafasi hii kwanza kuwashukuru ndugu zetu wale Wakenya na niliwaambia kabisa saa hizi wanisikilize, nilikata kidogo maana tume-chat mpaka saa tisa, kwa hiyo nilikata kidogo nipo busy Bungeni, lakini niwaombe sana tukitoka hapo tutaendelea tena na mjadala wetu kama kawaida, kwa wale wote tu ambao wanatutukana, wale ambao wanatusifu lakini hoja inapingwa kwa hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninawashauri wale rafiki zangu wale Gen Z wale ambao tumeanza mazungumzo m-create group la WhatsApp waniinginze humo nitakuwa busy kidogo leo na kesho kwa sababu kuna rafiki yangu mwingine Mkenya yupo hapa anataka parachichi, kwa hiyo yupo shambani tutakuwa tunashughulika naye ili achume aje nazo huko. Kwa hiyo, ninaomba wanipe muda, kwa hiyo Jumamosi nitawajibu live, tutaendelea. Wakenya ni ndugu zetu, ni rafiki zetu, ni majirani zetu na hatuna namna ya kuwakwepa. Kwa hiyo tutaendelea, cha msingi hoja ijibiwe kwa hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kwenye mchango wangu sasa. Ninakushukuru sana na nimeisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nilisimama hapa mwaka jana nikaongea kuhusiana na mipango yetu, jinsi ambavyo inatakiwa iwaunganishe wanaume. Tutaongea hapa kutunga sheria kali, tutaongea hapa sijui Polisi waingilie kati, tutaongea hapa mipango yote tunayoipanga, tuta-inject fedha tunavyotaka kuweka katika kulea maadili. Kama familia hazijawa strong hili suala litatusumbua sana. Tunapoongelea familia ni somo dogo tu ambalo ukienda kule shule ya msingi wanafundishwa Family Tree ni nini. Wanasema pale anakuwepo babu, atakuwepo bibi, anakuwepo baba, anakuwepo mama, wanakuja watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatutaweka msingi kwenye familia, hili suala la maadili litaendelea kutusumbua kama ambavyo Mheshimiwa Waziri, anasema kwenye Ibara ya 29 kwamba ni mmomonyoko wa maadili kwenye nchi yetu umezidi na taarifa ya UN ameisema vizuri Mheshimiwa Tarimba, inasema kabisa kwamba vitendo vya ukatili vinaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilisema mwaka jana kwa uchungu hapa na nikafikiri labda nimeeleweka lakini ninaona mambo ni yaleyale. sasa kama we are serious tunataka kubadilisha hii jamii na tumeshasema hii Wizara ni mtambuka na kazi yake kubwa ni kujenga fikra mpya, tunaomba nyinyi wenzetu wa Maendeleo ya Jamii kwanza wenyewe wabadili fikra mpya. Mwalimu Nyerere alisema, tunajenga usawa wa kibinadamu, lakini kutokana na mambo ya mwingiliano wa dunia kwenye ule usawa wa kibinadamu tukaja kwenye usawa wa kijinsia, usawa wa kijinsia ni sehemu ndogo ya usawa wa binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kusoma hapa Sera ya Maendeleo ya Jinsia ya kwetu sijaona, pale palipoandikwa Sera ya Maendeleo ya Jinsia uki-click unapata Sera ya Maendeleo ya Watoto na uki-click ya watoto unapata Sera ya Maendeleo ya Watoto, kwa hiyo wakaliangalie hili ili tuweke taarifa sahihi. Nikaenda kwenye Sera ya Maendeleo ya East Africa ambayo sisi tumeridhia, inasema kabisa ili tuweze kuimarisha hizi haki za binadamu, tuweze kujenga usawa, usawa wa kijinsia, kuleta maendeleo endelevu lazima tuwahusishe wanawake na wanaume mabinti na vijana wa kiume.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 76 para ile ya 145 mfano kwenye taarifa bado inasema mkakati wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na sehemu nyingine kwa watoto, umemalizia kwa kusema, lakini mpango huu mpya tulichokiongeza ni kuunganisha au kuongeza zile Serikali za Mikoa, Wilaya ili ziweze kuwa part and parcel ya kutekeleza mpango huu. Pia, unasema: “Pia tunaongeza wanaume na vijana wa kiume katika kutekeleza afua hizi za ukatili wa kijinsia.” Hawa watakuwa mpango wa utekelezaji, mpango wao wa kuwalinda uko wapi? Wa kutokomeza ukatili kwa wanaume uko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watakuwa mpango wa utekelezaji, mpango wao wa kuwalinda upo wapi wa kutokomeza huo ukatili kwa wanaume upo wapi? Sielewi labda mimi ndiyo ninayefikiria tu sijui nyinyi wenzangu Wabunge humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sielewi, labda mimi ndiyo ninayefikiria, sijui ninyi wenzangu Wabunge humu ndani? Labda hivi ninavyofikiria kwamba katika society yetu leo, wanaofanyiwa ukatili ni wanawake pekee yao wanaume hawafanyiwi? Nami ninafahamu unapokuwa unategeneza mpango lazima utatengeneza malengo ambayo yatafikika yatakuwa na timeline, utayawekea resource utaweka mkakati, utaweka tunasema goals za ku-achieve ndiyo maana ya mpango. Maana yake ni kwamba sasa hapa mipango yetu au mpango wetu wa ukatili wa kijinsia ume-base kwa wanawake na hauna wanaume.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaweka mipango utaweka mikakati utaweka malengo utaweka goals za ku-achieve kwa upande wa wanawake, hawa wanaume ni vipi? Lawama imekuwa kubwa mitaani jamani sisi ni Wabunge tunakwenda tunafanya mikutano tunaomba tusikilizwe. Lawama imekuwa kubwa kwa sababu hawa wanaume wanasema kabisa hata wakienda dawati la jinsia wanaoangaliwa na kushughulikiwa ni wanawake zaidi wao hawasikilizwi ndiyo malalamiko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukubaliane, hivi hiyo familia unayotaka mama tu atetewe na mama ni malaika yeye hawezi kufanya kosa akamtendea kosa mwenziye. Huyu anakwenda wapi kujieleza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote riot imekuwa ni kugombania nafasi, lakini usawa wa kijinsia hakuna mwanamke anayetaka kuwa mwanaume na hakuna mwanaume anayetaka kuwa mwanamke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alivyoongelea usawa wa binadamu aliongelewa utu kama binadamu kwenye mahitaji ya muhimu wote tunatakiwa tupewe fursa sawa. Ni kweli Serikali imewekeza sana kwa wanawake kwa sababu waliachwa nyuma, lakini trend ilivyo sasa hivi Serikali mmefanya kazi kubwa mno ya kum-empower mwanamke, thank you very much. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanamke, sasa mwanaume anaachwa nyuma jamani watoto wa kiume wanaachwa nyuma. Moja ya usawa tunaosema ni kuwawekea miundombinu itakayowasaidia kuchangia maendeleo endelevu ikiwepo na elimu, lakini leo tunajenga shule zote tunazojenga mabweni na shule kubwa tulizozijenga nchi nzima mikoa 26 ni za watoto wa kike za bweni wa kiume hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu shule zilivyojengwa zile za wakoloni ni shule moja tu iko Mtwara ya wanaume ndiyo imejengwa tena ya bweni. Hatari imekuwa kubwa sana kwa watoto wa kiume kuliko hata hao wa kike: wa kike wamefungiwa kwenye hostels, wamefungiwa kwenye mabweni wa kiume wanarandaranda ndiyo wanaingiliwa kinyume cha maumbile, ndiyo wanalawatiwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa mimi sielewi, me I don’t understand ndiyo maana siku ile niliwaomba kama haiwezekani kwani hawa wanaume nao kwa sababu population yetu 50% ni wanawake of course na wanaume wanaweza kuwa wanaangukia huko huko. Kwa nini, tusiwe na watu wengine watakaowaangalia wanaume au taasisi au wizara nyingine? Kama tunafikiri hatuwezi kuchanganya au Waziri kwa nini asiwabebe wanaume wake kwenye wizara hii halafu tuwatoe hawa watu makundi mengine yaingie biashara ya umachinga ili a-relax kutujengea maadili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hamna namna kwa sababu hawa wanaona wanaonewa wanaamua kutekeleza ndiyo maana sasa hivi single mothers tuko wengi! Kwa sababu sheria inawalinda wakienda dawati wanatetewa wanaume wanaamua. Kwanza, after all wao moyo wao ni mdogo sijui I don’t know, sijui tusema ni mdogo au vipi wanaweza tu wakakimbia mtoto na asiumie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ule mzigo mzito wa akinamama wanaachiwa watoto pekee yao inakuwa shida kuwalea. Akinamama muda wote wanakosa muda wanatafuta hela wawalee watoto asimamie maadili kwenye familia alipe gharama zote za kulea mtoto is impossible. Wakati kuna mtu tu alitakiwa kukaa hapa kwa sababu hajatendewa haki hajaheshimiwa binadamu yeyote anataka utu wake uheshimiwe. Hajasikilizwa ameamua ku-avoid ameondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani huu uwezeshaji haya hawa wanaume kwenye mikopo ya 10% tumewaweka wanawake tumesema na vijana ok, ukienda in real sense ukiacha ile Halmashauri moja sijui ni ya Bumbuli huko ndiyo iliyofanya muujiza wa vijana wengi wa kiume kukopa kwenye mikopo ya vijana. Ukija hizi halmashauri nyingine zote ni kwamba mikopo mingi ilipelekwa kwa wanawake zaidi ya asilimia nne tulizopanga wa kiume hawapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya hawa wapo kwenye biashara ndogo ndogo za machinga wako kwenye bajaji wapo kwenye boda. Hao ndiyo tulisema wakopeshwe hii mikopo ambayo wametenga bilioni nane wamekopesha milioni 159. Uwezeshaji wa hawa wanaume kiuchumi upo wapi kwenye mipango hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri akisimama asitujibu kiwepesi kwamba jamani wote wanabebwa humo humo kivipi? Kama wote wanabebwa humo humo kwa nini huyu awe na mpango kamili halafu yule mwingine kwenye mpango hayupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani tuwaangalie watoto wa kiume ni species ambayo ni endanger kama species ya tembo wanatafutwa kila mahali wanaathiriwa kila mahali. Kwenye vita ikitokea wanaenda wao wanaisha ndiyo maana hata population yao ni ndogo kuliko tuwalinde. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ukisimama ninaomba unisaidie huo mpango wa wanaume, uwezeshaji wao, ukatili na mpango wao kuwawezesha kiuchumi upo wapi? Wewe ndiyo Waziri wa Maendeleo yetu ya Jamii, Jinsia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninashukuru sana sitakuwa na maneno mengi. Ninachomwomba Mheshimiwa Waziri hilo ndilo nilitaka kumwambia na ninaomba akisimama nisishike shilingi aniambie. Ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)