Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. Kwanza, kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na nchi kutujalia afya njema sote tukiwa wazima tukiendelea kutimiza majukumu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya kutetea, kulinda na kutupigania Watanzania kama Amri Jeshi Mkuu. Tunamtia moyo tunamwombea na tunamhakikisha kwamba tupo bega kwa bega na yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana pia Wizara hii ikiongozwa na dada yangu Mheshimiwa Dkt. Dorothy pamoja na Naibu Waziri lakini Watendaji wote wakiongozwa na Katibu Mkuu kwa kazi kubwa ambayo mmekuwa mkiifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Gwajima, mara nyingi amekuwa aki-respond kwenye mitandao matukio ambayo wananchi wanayaripoti wanaya-post wanakuwa wakiku-tag. Kwa kweli umekuwa ukiitikia kwa haraka sana na kufanya ufuatiliaji, hilo nikupongeze, lakini haitoshi kwa Mheshimiwa Dkt. Gwajima pekee yake kufanya hii kazi. Sisi sote kama Watanzania kama wazazi ni wajibu wetu kulinda maadili kulinda mila zetu, kulinda tamaduni zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mmomonyoko wa maadili, mmomonyoko wa tamaduni zetu unaanzia kwenye ngazi ya familia. Familia nyingi tumekuwa aidha hatutimizi wajibu wetu kutokana labda na kazi nyingi ambazo tunazo au kutokana labda na uzembe au kutokana na utandawazi ambao umekithiri duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika ukiangalia watoto wengi ambao wako mitaani hawana makazi wanafanya kazi wengine wanarandaranda ni watoto ambao wamezaliwa na baba na mama. Kutokana na sababu mbalimbali zikiwepo magovi kati ya baba na mama au ikiwemo na malezi ambayo watoto hawa wamepatiwa tunajikuta kuna watoto ambao hawana makazi maalum, tunawaita watoto wa mitaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ni jukumu letu sisi kama wazazi kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwalinda watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na vitendo sisi wote ni wazazi, sisi sote ni walezi, lakini utandawazi unatupelekea hata malezi ya watoto wetu yanakuwa magumu. Sasa hivi watoto tunawalea kwa katuni, haki za watoto kila mtu anazitambua, mtoto ana haki ya kuishi, mtoto ana haki ya kupata elimu, mtoto ana haki ya kupata matibabu, mtoto ana haki ya kwenda shule, mtoto ana haki ya kupata mlo kamili na malazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haki nyingine ambazo tunataka kuziiga kutoka kwenye nchi za wenzetu. Mtoto wa miaka mitatu, mtoto wa miaka mitano unakuta anam-control mzazi wake mtoto anashinda kwenye TV yeye ndiyo anaamua aangalie kipindi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu unakwenda kwenye familia nyingine unataka hata kuangalia taarifa ya habari wewe ni mgeni mtoto ndiyo ana mamlaka ya ile remote na mzazi wake anakwambie, enhee! Yaani unajua anapenda kweli kuangalia katuni hayo ni malezi kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wetu humu tumelelewa na wazazi ambao wamekwenda na walikuwa ni wafanyakazi, lakini tulikuwa hatuna malezi ambayo tunayo sasa hivi ya kumdekeza mtoto anakuwa kama yai. Mtoto hata kumkaripia hata Biblia inasema kiboko ni haki ya mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na malezi ambayo mimi kwa kweli, mtoto analilia simu eti mpe achezee anataka kuangalia sijui nini, mtoto anajua na ku-download hivi kama mtoto anajua ku-download hizo katuni atashindwa ku-download vitu vingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watoto wetu sasa hivi wamekuwa so creative, wanajifunza vitu vingi wepesi wa kunasa. Watoto toka shule wanafundishwa kutumia kompyuta leo wewe mama unamwachia mtoto simu achezee. Mtoto unaweka password anakuangalia unavyofungua anaifungua badala ya kuangalia katuni anakwenda ku-search vitu vingine. Hayo ndiyo malezi ambayo sasa hivi sisi kama wazazi tumewalea watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huu mmonyoko wa maadili unasababishwa kwanza kabisa na ngazi ya jamii ngazi ya familia. Kwa hiyo, sisi kama wazazi tutimize wajibu wetu hawa watoto wa mitaani, mtaa unazaa kama alivyosema Mheshimiwa Jesca, pale mtaa unazaa? Mtoto anazaliwa na baba na mama, lakini kwa sababu hatuna malezi mazuri, ukiondoka leo duniani mtoto akaenda kwa mtu mwingine hawezi kukaa na ile familia kwa sababu malezi ambayo umempa siyo malezi ambayo anaweza mtu mwingine akayavumilia. Kila anachokitaka mtoto unafanya! Uzungu mwingi, tunaacha mila na desturi zetu, tunaacha mila ambazo tulikuwa tunafundishwa sisi na wazazi wetu, tunafuata utandawazi, utandawazi hatuwezi kuukwepa, lakini kuwe na mipaka kwenye familia zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto anataka kitu, je hiki kitu kina manufaa? Mtoto anakwambia mimi leo siendi shule mimi leo mtoto sitaki kula ugali ninataka kula burger, sitaki hiki na mama unafuata baba unafuata baba anavyotaka. Sasa kama sisi wazazi tunakuwa driven na watoto wetu unategemea tutakuwa tunamlaumu mama Mheshimiwa Dkt. Gwajima, hapa tutakuwa tunalaumu Serikali, lakini malezi sisi kama wazazi tumewajibika kwa kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana wazazi niwaombe sana wanawake na akinababa wote Tanzania tutimize wajibu wetu kuwalea watoto wetu katika misingi ambayo sisi tulilelewa. Hatuwezi kufanana sana kwa sababu hatukuwa na teknolojia kubwa kipindi kile hatukuwa na mambo ya mitandao, lakini walau basi vile vitu vya msingi tuwapatie watoto wetu kitu kikiwa kibaya mwambie asikifanye kikiwa kizuri mwambie akifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwenda kwenye hatua ya pili, kwenye mchango wangu wa pili, tumeona kuna tafiti ambazo zimefanywa kuna utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka wa Fedha 2022/2023 imebainisha kwamba ukeketaji kwa wanawake na wasichana miaka 15 mpaka 45 umepungua kutoka 10% mpaka asilimia nane kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunaona kwamba vitendo hivi vinafanyika, kuna mikoa ambayo bado vitendo hivi vipo. Kwa mfano; Kwa Mkoa wa Dodoma imepungua kutoka 47% mpaka 18%, hawa wanaweza kusema kwamba wamefanya vizuri sana. Singida kutoka 31% mpaka 20%, Mara kutoka 32% mpaka 28%, lakini Manyara bado kuna tatizo kutoka 58% mpaka 43%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi na Mheshimiwa Waziri ukeketaji wa wanawake unafanyika kwa watoto wadogo. Mtoto mdogo amezaliwa anakeketwa bila yeye kujua. Kwa hiyo, ninaomba sana, mamlaka ambazo zinazidi kusimamia kuendelea kuelimisha umma wa Watanzania ambao bado mila hizi zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kumnyima haki lakini pili ni kumpa maumivu, ni kumtengenezea maumivu baadaye atapata uzazi pingamizi atakapokuwa mtu mzima vitendo hivi havikubaliki. Kumekuwa na taasisi mbalimbali Asasi za Kiraia ambazo zinaelimisha ambazo zinapigana kupinga ukatili huu wa ukeketaji kwa sababu huu ni ukatili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuombe sana zile Asasi za Kiraia ambazo zinajishughulisha na masuala mazima ya kupinga mila potovu zisizofaa kuendelea kuelimisha jamii ambazo bado zina utamaduni huu kwa sababu huo ni ukatili kama ukatili mwingine. Mtoto hajui lakini hata kama ni msichana wa miaka 15 hana hiari ya kufanya kile kitendo cha kukeketwa. Tunaomba waendelee kuelimisha, kuhamasisha katika jamii ambazo ukeketaji bado unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tumeona kuna unyanyasaji katika mitandao wanawake wengi wanadhalilika kwenye mitandao, wanaume wengi wanadhalilika kwenye mitando. Tumekwenda mbali Watanzania mpaka tunafikia ya kudhalilisha hata viongozi wetu wa kitaifa kwenye mitandao hili halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kabisa sheria zipo TCRA Mheshimiwa Jerry afuatilie watu ambao wanadhalilisha viongozi wanatweza utu wa viongozi wetu hatutakubali kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kupigana, tunaendelea kupambana kuhakikisha kwamba staha ya mtu inaendelea kulindwa, staha ya Mheshimiwa Rais wetu inaendelea kulindwa tutapambana kwa hali na mali kuhakikisha kwamba mtu hatwezi utu wake kwa sababu anastahili heshima hata vitabu vitakatifu vimesema mwenye mamlaka na apewe heshima yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, ninaunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)