Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana na nianze kwa mpongeza sana Waziri wetu Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima na msaidizi wake Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamisi, pamoja na Watendaji wote wa Wizara hii, kusema ukweli wanatutendea haki wanafanya kazi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza kwa sababu chache niseme tu chache. Kwanza, kabisa tulikuwa tunapiga kelele tupate ile Sera ya Wazee irekebishwe ile ya 2003 tuwe na toleo jipya. Niwapongeze kwa sababu wameshafikia hilo na tunawaomba baada ya hii sera sasa twende tukarekebishe sheria ya wazee ili mambo ya wazee yaende sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana Shirika Help Age, hili ni Shirika linalo-deal na wazee hapa nchini, kusema ukweli ninawashukuru na ninawapongeza. Serikali pia ninaipongeza kwa sababu kuna vitu vichache wamefanya nimshukuru sana mama yangu Mheshimiwa Jesca, Mbunge wa Iringa ameongea sana kuhusu watoto wa kiume nami pia nitakazia kwenye wazee, akinamama na wanaume. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona kuna vitu vizuri wamefanya kwenye zile kambi za wazee kuna kambi 13, bado wanawahudumia na private sector ina kambi 15 ambayo inahudumia hawa wazee. Kwa hiyo, mchango wangu mkubwa utahusiana na suala la wazee hapa nchini kwa sababu ni balozi wa wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee ni watu muhimu mno sana kwenye jamii yetu na ni kwa nini ni muhimu, wazee ni watu wenye hekima sana wazee ni watu wenye uzoefu na wameshatoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Taifa hili ikiwa ni pamoja na kuziendeleza familia zao na jamii ya Kitanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye kitabu kitakatifu ambacho ninakiamini mimi cha Biblia nimesoma kuna mistari kama 100 inayotuambia kwamba wazee ni muhimu na tutumie hekima zao na kwenye kitabu kimoja. Kwa mfano; nitatoa tu mfano, Musa alivyozidiwa na ubishi wa wana Israeli alipokuwa anawapeleka kwenye nchi ya ahadi yalitokea matatizo pale baba mkwe wake alimwambia akachague wazee 78 wamsaidie kufanya hiyo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa inaonesha umuhimu wa wazee kuanzia zama hizo kwenye vitabu vitakatifu tunaambiwa, kwenye kitabu cha Ayubu 12:12 inasema “Hekima ipo kwa watu wazee, maarifa kwao walioishi muda mrefu” kwa hiyo hata kwenye vitabu vya Quran nina hakika tunaelekezwa kwamba tutumie hekima ya wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, wazee siyo watu wa kubeza, wazee ni watu muhimu sana, hata huku Bungeni tusije tukabeza wazee. Kwa mfano, kuna Mzee Profesa Muhongo utambeza umekuwa nani? Kuna Prof. Kabudi, kuna Mama Ishengoma, kuna wazee na mimi Mzee Ndakidemi utanibeza na uzee wangu huu kwamba mimi sifai. Kwa hiyo, tuwe makini wazee wanahitajika, mwendo ni mdogo, lakini wana mambo mengi wanayoweza kusaidia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme, pamoja na umuhimu wa wazee hapa nchini, lakini bado wana changamoto nyingi kubwa ambazo nitaiomba Serikali itusaidie kwa sababu hizi changamoto zinaathiri ustawi na maisha ya hawa wazee wetu hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza kwa wazee wetu hapa nchini ni ukosefu wa kipato cha uhakika na kutegemea familia. Wazee wengi wakishazeeka kama mzee hana pension, kama mzee ametoka kwenye familia maskini, sasa hukuwaandaa watoto ukiwasomesha vizuri, ukawatafutia kazi nzuri, kwa vyovyote kutakuwa na shida ya kipato. Kwa hiyo kuna changamoto ya hawa wazee kupata kipato cha kuwasaidia, ndiyo pale tunakuja sasa tunapiga kelele tunasema familia hizi TASAF tumepeleka kule iwasaidie, lakini tunatakiwa tufanye vitu vya ziada ili kuwasaidia wazee wanaotoka kwenye familia maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano hapa hata Mheshimiwa Jesca ameongea hapa, Nne vijana, Nne akinamama, haya wamenisaidia, sasa mtu ambaye amewajibika kuliko mtu yeyote kwenye familia zetu za Kiafrika hapa Tanzania ni baba, mwanaume mzee, anapokuwa ameishiwa nguvu husaidiwa na Serikali kwamba naye awe kwenye hili kundi la watu maalam kwa sababu hii Wizara pamoja na Makundi Maalum na Wazee wapo pale, mimi sioni kama tunawatendea haki hasa hizi familia ambazo ni maskini, ambazo huwa hazina kipato badala ya kuwasaidia ili nao wawe kwenye lile kundi, wa-generate income ya kuwasaidia waishi, tunawaacha unawapa akinamama, vijana na watu wenye ulemavu, mimi ninafikiri hapa kuna kitu tunatakiwa tubadilishe kwenye sera zetu na sheria zetu ili tuwasaidie na hawa wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya pili ni ya wazee kukosa pension. Huku kwetu Tanzania Bara wazee hawapati pension na hii ni changamoto, kule Tanzania Zanzibar wamejiongeza vizuri sana. Rais wa Zanzibar hata juzi aliongeza pension, walikuwa wanalipwa ukishafikia miaka 70 ulikuwa unalipwa shilingi 20,000 sasa hivi Mheshimiwa Rais Mwinyi kule Zanzibar amesogeza kidogo anawapa shilingi elfu 50. Sasa jamani hawa wazee siyo wengi, wazee wa hapa Tanzania Bara siyo wengi kiasi hicho, ni nini kinaishinda Serikali yetu kila siku tunapiga kelele hapa tusiwape hawa wazee ambao hawajiwezi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameshafanya kazi nzuri, wamefanya kazi nzuri, wame-identify watu ambao hawajiwezi na tunajua namba yao. Sasa inatushinda nini hao watu karibu 5,000 kuwapa pension ili nao wawe na maisha, waweze kupata pesa ya kununua sukari, aweze kujikimu, aweze kupata pesa ya kumpatia dawa? Ni nini kinatushinda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni kushindwa hawa wazee ambao hawajiwezi, ambao hawana bima ya afya, wengi wanashindwa kulipia matibabu, akiugua hana namna ya kwenda hospitali ili apate tiba. Sasa ninaomba hawa wazee wanahitaji wasaidiwe bima ya afya na wameshafanya kazi nzuri, wame-identify watu ambao hawajiwezi, katika hao 46% wameshawapa vile vibali vya kupata tiba, 54% hawajapata hivi vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, nashauri Serikali tujitahidi wazee wote wapatiwe bima za afya ili wakienda hospitali waweze kupata misaada kwa magonjwa kama pressure, kisukari, kansa, miwani, hivyo ni vitu ukishazeeka lazima unavaa miwani, wengine wakishidwa kutembea yale magogo wanatakiwa wapate pesa ya kuwasaidia kuyanunua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mwisho ambayo ni ya kawaida ni msongo wa mawazo. Wazee wengi wakishazeeka, watoto wameondoka wameoa wameenda kujitafutia kazi huko waliko, bahati mbaya unabaki wewe na mama, mama akitangulia au baba akatangulia, mzee utabaki kule ndani huna wa kukusaidia, huna wa kukufulia nguo, huna wa kukuletea kuni, huna wa kukupikia, unapata msongo wa mawazo na mara nyingi wanaishia kupoteza maisha hao wazee kwa sababu ya msongo wa mawazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali tuhamasishe vijana wetu, tuwafundishe kupenda wazee wao, kama mzee amezeeka angalau tumpelekee hata mtoto akae naye kule, mashirika ya dini, dini zetu zote hizi mbili ziwashauri vijana, sasa hivi kumetokea mtindo mbaya vijana wanazaa mtoto mmoja, wawili, usitegemee kama kijana wako ana mtoto mmoja ama wawili atakupa mtoto Hapana! Wewe utabaki hivyo hivyo maana na yeye ana hamu ya kukaa na mtoto wake. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali tuwe na program maalum za kusaidia hao wazee, kwa mfano, tunaweza kupata watu wanaowafundisha kisaikolojia, kuwatibu kisaikolojia, wawashauri namna ya kuishi, namna ya kushiriki katika jamii na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee ni watu muhimu sana, wazee bado wanahitaji sana huduma za watu ambao wanawazunguka, tukiwepo wananchi wote kwenye jamii tunatakiwa tuangalie wazee. Niendelee kushauri, Waziri aweke nguvu kwenye wazee, kwenye bajeti yake ametenga bilioni 12 kwa ajili ya yale makundi maalum, anaratibu vitu vyao ikiwa ni pamoja na siku ya wazee duniani, lakini nina wasiwasi kwenye hizi bilioni kumi ni kiasi gani….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Profesa malizia.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)