Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii. Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ndiyo huwa tunaiimba kwenye Wimbo wa Taifa pale tunaposema wake kwa waume na Watoto, kwa hiyo Wizara hii ni Wizara muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yao kwa jinsi ambavyo wamejiandaa hadi wametuletea taarifa nzuri kwenye hotuba na tumeielewa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakiri kabisa kwamba jina la Wizara hii linasadifu kabisa maendeleo ya Taifa letu. Ninaomba nianze kwa kutoa tafsiri rahisi za baadhi ya maneno machache. Jamii ni watu wanaokaa pamoja kwa kushirikiana na Watanzania wanaishi kwa kushirikiana ndani ya Taifa letu hata kwenye harusi, kwenye misiba tunasheirikiana na hili halina ubishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa maana yake ni muunganiko wa watu wenye utamaduni, mapokeo na historia yao, umoja wa Taifa hutegemea sana lugha na lugha yetu ya Kiswahili imetujengea umoja ambao hautikisiki. Umewasikia baadhi ya watu katika nchi jirani wanajivunia Kiingereza, sasa ningependa kuwauliza hawa ndugu zetu, hivi Wachina Taifa ambalo linapambana kimkakati wa kibiashara na Marekani leo lipo katika dunia ya kwanza kimaendeleo, hivi Wachina wote wanazungumza Kiingereza? Hao wenzetu bado wapo nyuma sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana ya nchi ni eneo la ardhi pamoja na eneo lililofunikwa na maji ambalo lipo ndani ya mipaka rasmi. Mipaka yetu hii tulirithi kutoka kwa wakoloni na ndiyo maana ili tushirikiane vizuri na nchi jirani tumekuwa tunapambana, tunajitahidi kuanzisha mitangamano ili tuweze kushirikiana kimataifa, tuweze kufaidika kibiashara na mambo mengine. Sasa hawa ndugu zetu ambao wanaanzisha chokochoko ambazo zinataka kutuvunjia umoja wetu ambao wa ushirikiano na nchi jirani wana maana gani, wanatupeleka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nilivyokuwa ninaangalia jinsi wanavyozungumza, wanambeza Rais wetu, kiongozi wetu, wanazungumza maneno machafu, matusi na nini, ninasikitika na ninashangaa. Ninatoa wito kwa viongozi wao, wawaite hao watu wawafokee, wawaweke katika tabia ambazo zitakuwa ni nzuri. Labda katika jambo hilo ninaomba nimsikitikie Ndugu yetu mmoja ambaye amevamia mada ambazo hazielewi vizuri kwa sababu hata Serikali yenyewe bado hajaijua vizuri kwa sababu yeye mwenyewe hajawahi kufanya kazi Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, amehoji mambo mengi ambayo hayaelewi vizuri. Tafsiri yangu kwa kweli kwa yale aliyoyasema ninahisi anahitaji zaidi kuelimishwa, watu wakae naye, wamwelimishe hatua kwa hatua, ninaamini ataelewa. Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imempa Rais mamlaka yenye kinga katika kuongoza nchi yetu na kuteua wasaidizi wake kwa kadri anavyoona inafaa na anapoteua au kutengua hahojiwi na chombo chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana, nimpe mfano kwa nyakati tofauti tangu tupate uhuru, wamekuwepo kwa mfano, Wakurugenzi wa Usalama wa Taifa ambao wamekaa kwa miaka 10 -15 katika Madaraka, lakini wapo ambao wamekaa muda mfupi, hiyo ni hiari na muono wa kiongozi wetu mkuu wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mifano michache, tangu tupate uhuru mwaka 1961 nchi ilikuwa na Mkurugenzi wa Usalama anaitwa Emidio Mzena, alikaa miaka 15, lakini mwaka 1975 akateuliwa Dkt. Laurence Gama akakaa miaka mitatu tu, mwaka 1978 akateuliwa Dkt. Hassy Kitine tena alikuwa kijana mdogo wa miaka 35 akakaa miaka mitatu tu na mwaka 1980 akateuliwa Dkt. Augustine Mahiga ana miaka 33 wakati ule anateuliwa, Mheshimiwa Rais aliona kwamba hawa watakuwa ni wasaidizi wangu ambao watanisaidia kazi. Kwa hiyo, kwa muda ambao anaona Mheshimiwa Rais kwamba huyu anafaa kunisaidia kazi hawezi kuhojiwa na chombo chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nilishangaa sana nilipokuwa ninamsikiliza Ndugu yetu, lakini nikajiuliza maswali mengi, hivi motive ilikuwa ni nini? Nchi hii ilimruhusu Ndugu yetu akazunguka kwa helikopta majimbo yote Tanzania, hivi kulikuwa na motive gani kwenye hiyo ziara? Labda kulikuwa na mambo fulani ambayo yanaandaliwa ambayo pengine angependa kuyafanya katika mwaka 2025. Ninadhani niachie hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye Wizara. Wizara hii kwa jina lake lilivyo ndiyo inayostahili kuratibu mikopo yote ya makundi yote ya jamii. Mikopo ambayo inatolewa na halmashauri ile ya 10%, mikopo ambayo inatolewa na Idara ya Vijana pale Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna mikopo mingine ipo Ofisi ya Rais sijui kwenye Mradi wa SELF na mikopo mingine ipo kwenye Wizara nyingine na Mashirika mengine. Hii mikopo yote, fedha yote ile ilitakiwa ipelekwe kwenye Majiji yetu, kwenye Halmashauri zetu, kwenye Miji yetu ili wale Madiwani na zile Kamati za mikopo za Halmashauri ambazo zinawajua vizuri zaidi watu kuliko wao watu ambao wapo kwenye Wizara, Makao Makuu huku ndiyo wangehusika kutoa hiyo mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaishauri Serikali nzima wakakae waweze kuiweka mikopo yote kwenye Mfuko mmoja na mikopo hiyo itolewe kwenye Halmashauri na taarifa ziratibiwe kupitia kupitia Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Tukifika hapo tutakuwa tumesaidia nchi yetu kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tuitetee sana hii Wizara, hii Wizara ni miongoni mwa Wizara ambazo zina bajeti ndogo, lakini vilevile niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuitetee sana Serikali. Pia ninawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kukitetea Chama Cha Mapinduzi ambacho kimetuleta humu ndani, bila vikao vya Chama Cha Mapinduzi wengi wetu tusingekuwemo humu ndani. Tunafahamu, wapo watu hapa waliongoza kura za maoni, lakini wapo ambao hawakuongoza kura za maoni, lakini waliteuliwa na Chama Cha Mapinduzi kuja humu ndani, tukitetee sana Chama Cha Mapinduzi ili nchi hii iendelee kuongozwa na chama ambacho kimeendelea kuihakikishia nchi hii amani, usalama na utengamano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutakikosa Chama Cha Mapinduzi inawezekana kabisa nchi hii ikaingia kwenye matatizo makubwa sana kama ambavyo yameanza. Watu wa nje wametoa macho, 2025 hii wametoa macho kutaka kuisambaratisha nchi hii. Kwa hiyo, ninaomba kila mtu awe makini anachozungumza, anachowasilisha kwenye jamii, awe makini sana nacho kwa sababu nchi yetu sasa hivi mpaka tuvuke Mwezi Oktoba tumalize uchaguzi mkuu tutakuwa tumepitia misukosuko mikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)