Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana. Jambo la kwanza niseme ninaunga mkono hoja Wizara ya Mheshimiwa Gwajima na jambo la pili nimpongeze kwa uwasilishaji mzuri. Pia nimpongeze kwamba vijana mtandaoni wanasema anafikika, kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri amekuwa aki-attend kwa wakati matukio ambapo yanatokea hususan mambo ya ukatili na mambo mengine, tunampongeza na nadhani wanafanya jambo zuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache tu ya kushauri kwenye Wizara hii, kwanza tufahamu kwamba Wizara hii haya yote tunayozungumza suala la maadili ya watoto au maadili ya watumishi au mmomonyoko wa maadili ni matokeo tu, ni matokeo ambayo yanatokana na malezi kutoka kwenye ngazi ya familia. Kwa hiyo, tunaweza tukazungumza mambo mengi kumhusu Mheshimiwa Gwajima na Wizara yake, lakini kiuhalisia ni Wizara nyingi ambazo zinahusika kuweza kumsaidia Mheshimiwa Gwajima kwenye suala la malezi kwenye Taifa letu. Yeye kama yeye ni matokeo tu ambayo anakutana nayo, lakini kuna suala la TAMISEMI, kuna Wizara ya Mambo ya Ndani, kuna Wizara tofauti tofauti zinahusika kwenye hili jambo kuhakikisha kwamba kama nchi inasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri, kwanza ninatamani sana, kwa sababu tu kwanza kama Taifa lazima tukiri kwamba kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili, sasa kama kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili nini kifanyike na sisi inawezekana ndiyo generation ambayo Mungu ametupa nafasi ya kufanya turning point kwenye kubadilisha haya ambayo tunayaona yaende kwenye mambo mema ambayo tunayataka. Kwa sababu kama unazungumza mmomonyoko wa maadili unazungumzia mtoto wako kwamba, mimi mtoto wangu yupo salama, lakini nikuhakikishie hutaweza kumzuia mtoto wako kuolewa na mtu ambaye hana maadili. Kwa hiyo, ni lazima wote tushikamane kuhakikisha kwamba tunapata Taifa jema na tunapata viongozi wazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwepo kwenye mjadala mmoja na wenzangu kwamba, kama tutafikia hatua hatuzuii hili suala la mmomonyoko wa maadili, tunaomba sasa hivi financing za fedha kutoka nje, kuna wakati tunaomba mikopo tunapata, kuna siku tutaanza kuomba na viongozi wa kusimamia hii mikopo, kwa sababu uwezo kama Taifa la kusimamia kuwa na viongozi wazuri baadaye tumeshindwa kuzoea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Gwajima huyu wa leo ambaye tunamzungumza siyo Gwajima aliyelelewa kwa haya ambayo sisi tunawalea watoto wetu, ni Gwajima ambaye amelelewa kwa misingi ya maadili na taratibu zote. Sasa ninaomba jambo moja, tunapozungumza suala la TAMISEMI, tunatamani wenzetu TAMISEMI wana mfumo kutoka nyumba kumi ambao unaweza kudhibiti mmomonyoko wa maadili kuanzia ngazi ya chini, kama familia haipo tayari, lakini kuna wajibu wa Balozi, kuna wajibu wa mtu wa nyumba kumi kusimamia kuhakikisha kwamba je, kuna jambo gani linaloendelea katika jambo husika, TAMISEMI wakasaidia kuhakikisha mtu anakua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mtoto kuanzia ngazi ya shule akipewa elimu nzuri akaenda akakua hadi Chuo Kikuu, ni vyema tukawa na mitaala mizuri ambayo inazingatia kulijenga Taifa letu lakini pili Mheshimiwa Waziri kuwa na special program kwa ajili ya mashule kuanzia shule level ya msingi, level ya sekondari lakini level ya vyuo vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mashule mengi kwa mfano, ninakupa sehemu ambapo unakuta kama Taifa tumemeguka. Mtoto amelelewa vizuri kwenye seminary school kuanzia yupo shule ya msingi na yupo sekondari, akishaingia chuo mtoto anakutana na uhuru. Lifestyle ya wanafunzi wengi wa vyuo ambao tunategemea baadaye waki-graduate ndiyo waende maofisini wamegeuka kuwa msiba kwenye Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ninaliomba Mheshimiwa Waziri, wewe pamoja na Maprofesa wa nchi hii, kwa sababu Wizara ya Elimu ni Wizara mtambuka kwenye suala la maadili, lazima tukae chini kama Taifa tuzungumze, tuwe na modality yetu kama Taifa na mataifa mengine yaweze kuiga, product gani tunaizalisha kutoka kwenye chuo kikuu husika, kuanzia kwenye maadili hadi uwezo wa mwanafunzi. Kwa sababu, mtu anaweza akawa na uwezo darasani lakini hana maadili na baadaye tukampeleka kwenye ofisi ndiyo haya Mheshimiwa Rais juzi alikuwa anazungumza, uzalendo kwa Watanzania na watumishi wa Serikali umepungua. Ni muhimu sana tuusimamie huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama Mheshimiwa Waziri lazima kuwe na program, kuwe na mkakati maalum wa kutoka kwenye Wizara kuhusisha Wizara ya Elimu kwa ajili ya kuweza kusaidia Taifa letu. Tuangalie product tunayoitoa vyuoni kuja kwenye kuihudumia jamii ni product ambayo inaendana sawa? Mambo ya kusema mtu akifika chuoni ana uhuru wa manyani wa kufanya anachojisikia results yake ndiyo hii, generation hii haitutaki tufanye hivyo! Tunahitaji kama Taifa tujifunge mkanda, kuzalisha kitu ambacho kitaenda kuwa na faida kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba tena Mheshimiwa Waziri kitu kingine, tunatamani kuwa na azimio lazima tuwe na declaration kama nchi kwamba this is the turning point kwenye suala la maadili twende kwenye moja, mbili, tatu. Kama tulishawahi kuwa na Azimio la Arusha na sisi kama Wizara lazima wakubaliane na wazazi wa nchi hii, wewe utazuia leo huyu kabakwa, utazuia yule kalawitiwa, huwezi kufanikiwa kwenye nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima sasa tuweke mkanda na mshikamano wa nchi yote kukubaliana kwamba ni kipi tunakifanya kwa ajili ya watoto wetu. Kwa hiyo, ni lazima kuwe na declaration (azimio la kitaifa) kwamba kuanzia viongozi wa dini, vyuo, taasisi mbalimbali, Bunge na NGOs zote tuwe na kauli ambayo huu ndiyo mwelekeo wa Taifa letu kuanzia sasa kwenye suala la maadili. Mtu asiyeenda hivi tutafanya moja, mbili, tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizo Wizara ni Wizara hii, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya TAMISEMI na nyingine nyingi ambazo zinahusika kwenye kutengeneza declaration kama nchi tukaamua kutoka hapa na kwenda hatua nyingine. Ninatamani sana hayo yafanyike kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Tofauti na hapo tutaendelea kulalamika kwa sababu unaongelea issue ya TCRA kwamba kuna changamoto kwenye mitandao, lakini yale yote ni matokeo ya jinsi mtu anavyolelewa kuanzia ngazi ya chini. Huku juu tutahangaika na kizazi ambacho tayari kimeshakomaa na tayari ni kizazi ambacho imekuwa sugu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu pia hata asubuhi nimezungumza hapa kwamba, kwa mfano vijana wanatumia pombe ambazo zimezidishwa content au wengine wanazidisha kunywa pombe wakiamini kwamba labda ndiyo njia ya kutoa stress kutokana na aidha amekosa ajira au kutokana na kesi zao zingine ambazo ni social interaction. Tunatamani kuwe na darasa kubwa sana la kutoa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya Mheshimiwa Waziri ninaiunga mkono (shilingi bilioni 76 alizoomba), lakini ninatamani investment kubwa ambayo inatakiwa aiweke ni kwenye kuelimisha jamii kwenye TV, redio na madarasa. Afanye namna awezavyo kuielimisha jamii wakati huo tunaunda modal tofauti kama Taifa la Tanzania kwa ajili ya kuijenga hii nchi yetu katika mfumo mpya kwa maana tuwe na declaration yetu ya maadili kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti na hapo, kama ambavyo tunajuta ukame kwenye maji, tunajuta ukame kwenye mazao na hali ya hewa; ndivyo ambavyo kuna siku tutajuta kwamba Taifa halina viongozi kwa sababu watu wote wamekuwa ni corrupt kwa sababu Mheshimiwa Waziri hatuwezi kukubaliana. Macho yako yanashuhudia watu wana Instagram account wanatangaza ushoga; macho yako yanashuhudia kuna hawa wanavaa nguo zisizokuwa na maadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tutabaki kuzuia huyu mmoja mmoja? Ni lazima tutafute mfumo ambao uta-unify Taifa kuhakikisha kwamba wote tunakuwa ni wamoja, lakini tunaisaidia nchi kuja kuzalisha Mawaziri na Marais ambao wana integrity kama ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anayo na kama ambavyo Marais wengine wamepita na kama Mawaziri wengine ambavyo wapo. Hatuwezi kupata Mawaziri kama nyie kama hatutakuwa na umoja wa kitaifa au azimio la kitaifa kuelekea kwenye suala la maadili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa muda. Nilikuwa na mambo mengi ya kuzungumza kwa ajili ya kuchangia, lakini mwisho kabisa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele, Mheshimiwa Festo yaandike.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nisisitize kama Taifa ni lazima tumlinde Mheshimiwa Rais kwa wivu mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama vijana, tuko tayari kuhakikisha kwamba tunamlinda Mheshimiwa Rais na hatuko tayari kuona mtu mwingine anaenda kinyume na kile ambacho Mheshimiwa Rais anafanya. Kazi kubwa anaifanya na amefanya kazi kubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu. Sisi kama Watanzania, lazima tuwe na wivu na Mheshimiwa Rais wetu. Wao wa-deal na Rais wao pamoja na nchi yao na sisi tu-deal na nchi yetu. Watuachie nchi yetu ibaki kuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)