Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi. Awali ya yote, ninapenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii jioni hii ya leo, lakini ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya katika Taifa letu kwa namna ambavyo ameendelea kusimamia Taifa na linakuwa na utulivu mkubwa. Pia, Mheshimiwa Rais kwa mambo ambayo anayapitia kwa kipindi hiki ni mambo magumu na hasa ukizingatia ni mambo ambayo yanatoka nje ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninajiuliza, kumbe mmomonyoko wa maadili huu ni karibu mataifa yote yamepata mmomonyoko wa maadili? Kwa sababu mtu wa kawaida tu kumzungumza Mheshimiwa Rais au mtu mzima, lazima uwe unaelewa unazungumza jambo gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hata hawa ambao bado wanaendelea kujadili jambo hili, ninaamini kwamba ni mmomonyoko wa maadili na wao inawezekana huko walikoanza hawakulelewa vizuri. Wangelelewa vizuri, saa zingine hata ukitaka kuzungumza jambo lazima ujue jambo hilo unataka kumweleza nani na amekukulia kwa kiasi gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, ndiyo Wizara ambayo inatengeneza sheria kwa ajili ya kulea watoto wetu. Hao watoto wa leo tunaowazungumza ndiyo watu ambao tunawategemea miaka ya baadaye waweze kuwa watu salama na watu sahihi ambao wanaweza kusimamia Taifa hili ambalo leo linatengenezwa katika miundombinu mikubwa na yenye gharama kubwa. Hata hivyo, matarajio yetu ambayo tunatarajia kuwarithisha miundombinu hiyo ni hao watoto wetu wa leo ambao tunawalea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa kwa sababu hali ya leo, malezi ya leo ambayo yanawalea watoto ni malezi ambayo yamechanganyikana. Malezi yamechanganyikana kwa sababu watoto wetu wa leo mambo wanayoyapitia katika mitandao na kwa sababu sehemu kubwa ya muda wao wanautumia kupita kwenye mitandao, kwa hiyo inakuwa ni vigumu sana kuelewa wazazi walitaka watoto wafanye kitu gani kwa sababu wazazi nao wamekosa nafasi nzuri ya kukaa na watoto wao kuwaelewesha, kuwaambia nini wakifanye na nini wakiache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wamewaachia mitandao ili watoto wajifunze maisha ya kuishi duniani kupitia mitandao. Kitu hiki mwisho wake tunachokuja kukivuna ndicho hiki ambacho leo tunakiona kwamba, mtu yeyote yule mwenye umri wowote ule anaweza kumweleza mtu yeyote yule kitu chochote kile bila kujali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama angekuwa amepitia maadili mazuri, kila unapotaka kumweleza mtu jambo ambaye amekuzidi umri, lazima wewe mwenyewe ujitathmini na uone hiki ninachotaka kumweleza huyu, kwangu mimi kinawezekana nikamwambia au siwezi kumwambia? Kama hulijui hilo na umepitia kwenye mitandao, umelelewa na mitandao hutajali. Chochote kile kitakachokuja kwenye kinywa chako utakisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii Wizara ya Maendeleo ya Jamii ndiyo Wizara ambayo inatunga sheria kwa ajili ya kulea watoto. Leo hii ukipita katika nchi yetu, kuna watoto ambao wamezaliwa hawana baba, hawana mama na ni yatima lakini wanaishi katika maisha yao hayo hayo wanayoyaishi; ya misukosuko, wanasoma kwa shida, wanakula kwa shida, wanalala kwa shida lakini wanaishi. Pia, muda huo wa kusema watapitia mitandao ya kijamii hawana kwa sababu hata uwezo nyumbani kwao wa kununua hizo simu ambazo zinaweza zikamfanya aweze kupita kwenye mitandao ya kijamii, hawana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu ambao wataendelea kusumbua Taifa hili sana kwa muda mrefu ni wale watu ambao muda wao mwingi wamekaa kupita kwenye mitandao ya kijamii au watoto wale ambao watalelewa, analelewa na wazazi wake lakini sehemu kubwa ya maisha yake analelewa na mitandao ya kijamii. Jambo analokutana nalo mle kwenye mitandao ya kijamii ndilo jambo analolichukua mtoto kulileta kwa mzazi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli pamoja na sheria ambazo tunazitengeneza hapa kwa ajili ya kulea watoto wetu, lazima tuangalie sheria hizo zitawafikisha wapi watoto wetu. Tukiwapa haki watoto zikazidi umri wao badala yake madhara yake tutakuja kuyapata sisi wenyewe wazazi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa imani yangu ninavyoamini...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maboto, muda wako umekwisha maana mlipewa dakika tano tano tu, ambao hamkuwa kwenye orodha mlipewa dakika tano... (Makofi)
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)