Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mwanaidi Ali Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kutoa hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nipende kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini katika Wizara hii na kunipa nafasi ya Unaibu Waziri. Pia, niwashukuru watendaji wote ambao wako katika Wizara hii kwa ushirikiano ambao wananipa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye anatuongoza katika Bunge hili. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Spika na wewe pia Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote ambao wanatuongoza katika Bunge hili Tukufu kwa miongozo mizuri ambayo wanatupa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Kamati yetu ya Ustawi wa Jamii ambayo inaongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Fatma Toufiq kwa miongozo mizuri na maelekezo mazuri ambayo wanatupa katika Wizara yetu hii hadi tukafikia hii leo na tukawa na miongozo na sera mbalimbali ambazo zinawasaidia wananchi kuhakikisha tunakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kumsahau Waziri wangu, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima ambaye ananiongoza vizuri sana kuhakikisha Wizara hii tunaifanyia kazi. Hatulali usiku na mchana, tunapokea simu za wananchi na tunazijibu kwa umakini kabisa kuhakikisha kwamba wananchi wanaiamini Wizara yao, lakini wanamwamini Mheshimiwa Rais kama alivyotuamini sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru pia Mume wangu ambaye ananiongoza kwa miongozo mbalimbali na kunistahimilia katika kazi hizi za kujenga jamii, lakini na yeye kama mzazi basi tunashirikiana pamoja kunisaidia kuhakikisha wananchi nao wanaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa UWT pamoja na Wajumbe wote wa UWT Taifa kwa kunichagua na kuhakikisha ninaendelea vizuri katika kazi zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niupongeze Mkoa wangu wa Kusini na Wajumbe wote wa Mkoa wa Kusini kwa kunielewa na kunifahamu kazi ambazo Mheshimiwa Rais amenipa na wao kuwa wananikosa kwa mambo mengi ambayo yanafanyika katika Mkoa wangu, lakini tunakuwa tunashirikiana pamoja pale ninapopata wasaa wa kushirikiana nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru familia yangu kwa ujumla, lakini pia niwashukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; Katibu Mkuu na Watendaji wake wote kwa kutupa nafasi nzuri na miongozo mizuri, ushirikiano ambao tunafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha Wizara hii inakwenda vizuri na inakwenda salama na tunahudumia wananchi kama tulivyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, lakini ninapenda sasa nichangie hoja za Waheshimiwa Wabunge waliochangia wote na ambao waliochangia kwa maandishi na pia wale ambao wana fikra za Wizara yetu hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea hoja zenu na hoja zenu ni nzuri sana ambapo ninaamini kwamba Wizara hii sasa wameanza kuielewa. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipopata Urais aliona kwamba Wizara hii ilikuwa ndani ya Wizara ya Afya, lakini kwa vile yeye ni mama na vile yeye ni mzalendo na anajua uchungu wa akinamama na anajua uchungu wa watoto, akaona Wizara hii aiunde Wizara kamili ili vitendo vyote vinavyoonekana yale machungu yote ambayo wanawake wanayapata pamoja na watoto yaweze kuonekana na kufanyiwa kazi kuhakikisha kwamba watoto wa nchi hii na wanawake wa nchi hii, lakini wakiwemo na wanaume wanakuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia mambo mengi sana. Tukija kwenye hoja, mimi nitajikita katika hoja tatu katika mambo ya ukatili, mmomonyoko wa maadili lakini nitajikita katika wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge akiwemo Mheshimiwa Profesa Shukrani hapa, alieleza kuhusu malezi na makuzi ya watoto. Ni kweli kila mmoja ana familia katika nchi hii na familia ni taasisi katika kuleta ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, yapo madhara makubwa ya watumishi wenza kuishi mbali na watoto ambao wanapata madhara. Madhara haya ni kama yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, madhara ya watoto kuongezeka vitendo wa ukatili, kuingizwa katika vitendo vya kiudhaifu, kukosa malezi na kuathirika na mambo mbalimbali. Haya yote tunasema, mtoto anapozaliwa na mzazi wanapoungana kila mtu anatarajia mtoto na kila mtu anatarajia mtoto awe mtoto mwema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto ambazo zinawafika wazazi zinasababisha kutengana lakini jukumu kubwa anaachiwa mama na mama huyu ndiyo kila kitu. Anategemewa alifanikishe jambo hili, kwa hivyo anapata mzigo mkubwa sana na mama anahangaika kulea mtoto huyu hadi anapompa mahitaji yote ambayo yanastahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, sisi sote ni walezi humu ndani, lakini sisi sote tuna watoto na sisi sote tuna maadili ambayo ni ya Mtanzania na Utamaduni wetu wa Mtanzania. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan yeye ni mama, lakini ni mlezi. Siku zote anaposimama majukwaani anahimiza mila na desturi ya mtoto wa Kitanzania, lakini anahimiza tushikamane kuendeleza utamaduni wetu. Haya ndiyo yatatusaidia hapo mbele na mtoto wa Kitanzania tunamtegemea kuwa kiongozi wa kesho.

Mheshimiwa Naibu Spika, tusipomlea sasa hivi tukampa maadili mema, basi hapo baadaye tutakuwa na Taifa ambalo halina miongozo mizuri. Kwa hivyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, Serikali hii Mheshimiwa Hayati Nyerere, alipoianzisha aliandaa miongozo, sera, na kanuni katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kila nchi au tuseme mtaa kuna kanuni zake au kuna miongozo yake ambayo amepewa mtu aweze kujuana katika kijiji kile. Sasa ile miongozo tujitahidi tuifuate. Sisi ndiyo viongozi, kama vile tunavyohangaika kutafuta kura basi tuhakikishe ile mitaa na wale watu ambao wanaishi katika mtaa ule basi tunawajua na tunafahamu tabia zao ili tukimuona mtu ambaye ana ripoti mbaya, turipoti katika vyombo husika ili kukomesha ukatili na kukomesha udhaifu ambao unatokea katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie katika kipengele cha wazee. Wazee ni tunu katika Taifa letu na wazee ndiyo waliosababisha hadi leo tuko hapa tunaendesha Taifa hili kwa umakini. Wazee wetu tumewaundia sera kwa vile tunawajali. Tulikuwa tuna Sera ya Mwaka 2013, lakini tumeiboresha sera na tumeunda Sera ya Mwaka 2024. Sera hizi zinawawezesha wazee kupata haki zao zote stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anawajali sana wazee na kila time anapopata nafasi utamkuta anawatembelea wazee na kuwafariji. Hivi ndiyo tunavyotakiwa tuishi na kila mtu ana mzee wake. Kwa vile mtu ana mzee wake, haina haja ya mtu kumbeza mzee wake. Umlee kama yeye aliyokulea wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mtu ambaye anashindwa na kitu hiki. Mzee hahitaji makubwa kwa nini umtupe kwa maisha ambayo unaendelea nayo sasa hivi wakati yeye ndiye aliyekuwezesha hadi ukafika sasa hivi? Kwa hivyo, tuheshimu sana wazee na tuwajali sana wazee, tusiwabeze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiona mambo yanazidi tutaunda sheria. Kwa nini watoto hawalei wazee wao? Sheria hizi ziwakamate, ili tusione wazee wanahangaika wakapata taabu katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tuhakikishe katika majirani zetu, tuwaelimishe. Sisi ndiyo viongozi na ni mabalozi ambao tunatoa elimu mbalimbali kuhakikisha wananchi wetu wanafaidika na matunda ya Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo mama yetu ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Yeye ni mama na ni mlezi ambaye ana uchungu wa Serikali hii na ndiyo maana kila mara anahimiza upendo, uzalendo, ukakamavu, uhusiano mzuri katika mataifa na katika nchi yetu. Pia, anapoona jambo ambalo linamkasirisha basi utamwona sura yake inavyobadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mama hapendi kusema, lakini likimkera ndani ya moyo wake, neno lake moja tu na yeye anakwambia mtu anajua mwenyewe vya kum...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)