Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kuwa mahali hapa siku hii ya leo nikiwasilisha bajeti yetu kama nilivyofanya awali asubuhi na sasa ninahitimisha. Ninaomba kuhitimisha hoja yangu ili bajeti hii iweze kupitishwa kwa ajili ya kwenda kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameendelea kuniamini na kuniamini pakubwa sana kuja kuanzisha hii Wizara ambayo awali haikuwepo, lakini akaona umuhimu wake kwenye majira ya nyakati za sasa. Akasema ianzishwe na akanileta mimi na nimeweza kwenda nayo miaka minne, akiendelea kuniamini hadi muda huu ambapo ninakuja kuwasilisha bajeti hii kwa mara ya nne hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kazi yangu pekee yangu ni kazi yetu sote. Tumekuwa tukija humu, tukipata miongozo na maelekezo yenu Waheshimiwa Wabunge. Tumekuwa tukipata maelekezo ya kamati pamoja na wadau wengi wa maendeleo hadi kuipambanua na sasa inaeleweka pakubwa kiasi kwamba, ninajivunia kupata maswali mengi tunapokuwa tunakuja kuwasilisha hotuba zetu hapa, kinyume na miaka iliyopita ambapo maswali yalikuwa machache sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliwashukuru viongozi mbalimbali asubuhi. Ninaomba nisirudie, shukurani zangu zisajiliwe, kama ambavyo niliwasilisha kwenye muhtasari wa bajeti yangu asubuhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaomba kipekee niwashukuru Wabunge wote waliotoa michango yao siku hii ya leo jioni, ningeweza kuwasoma wote, wako 17 wamezungumza na wengine wamenipatia kwa maandishi. Inawezekana nisiweze kuhitimisha kujibu hoja zao zote na kufafanua, lakini niseme tumezipokea na tutazifanyia kazi. Ninawahakikishia tutazileta kwa maandishi, ili ziweze kuwa kumbukumbu sahihi za michango yao kwa siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Kamati yangu, ambayo imeleta hoja karibu 10 za Kamati. Vilevile nazo tutazifanyia kazi na kuziwasilisha kwa maandishi, endapo sitafanikiwa kuzijibu zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kama utangulizi, hoja ambazo zimewasilishwa hapa ni nyingi. Mheshimiwa Naibu Waziri ameanza kuzizungumzia nyingine awali, ninamshukuru sana na ninaunga mkono majibu aliyoyatoa. Ninampongeza sana kwa ushirikiano wake. Nitapita kwenye baadhi ya hoja, ninaweza nikarudia alizozisema kwa nia njema ya kuendelea kuongeza, kujazia na kufafanua zaidi yale yote ambayo yamesemwa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja kubwa ambayo imejitokeza kwenye mjadala wetu huu wa jioni ni suala zima la maadili. Hii ni hoja ambayo imeendelea kujitokeza kila tunapokuja hapa kuwasilisha hotuba zetu na Wabunge wamekuwa wakitupatia miongozo, maelekezo na michango mizuri sana, ambayo imekuwa ikitusaidia kwenda kuboresha utendaji wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, muda tu ni mdogo. Awali ya yote ninaomba, kupitia Bunge lako Tukufu, niweke kumbukumbu sahihi, ili tuweze kwenda vizuri na hoja yetu hii ninayoihitimisha. Huu mmomonyoko wa maadili ambao tumekuwa tukiusema kila siku;
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme machache kupitia Mwongozo wetu wa Taifa wa Maadili na Utamaduni wa Mtanzania, ambapo kuweka kumbukumbu sahihi, mwongozo huu Wizara yenye dhamana ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kwa sababu maadili yetu ni zao la tamaduni na mila zetu tulizozirithi, hivyo wamefanya kazi kubwa na nzuri. Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Wizara nyingine, sisi sasa ni washirika katika kuhakikisha kwamba, jamii inapata mwongozo huu na kuutumia, lakini haiwezi kupata mwongozo huu, kama hauwezi kupita kwenye machinery za Serikali ambazo sisi wote humu pia, ni wahusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasema vizuri kuhusu machinery hizo, maadili yametafsiriwa hapa kwamba, ni “tabia njema, misingi, kanuni na taratibu zinazofuata mienendo inayokubalika katika jamii, ambayo inaongoza uhusiano katika makundi ya jamii husika na maadili yanamtaka mtu kufanya kitu kilicho sahihi, mahali sahihi, kwa wakati sahihi. Kimsingi maadili ni zao la mila na desturi za utamaduni wa jamii inayohusika”, mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo kisa na mkasa cha suala zima la maadili kumomonyoka ni malezi ya watoto wetu huko kwenye familia, tunawaleaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote ni wazazi. Kwa bahati mbaya tumekuwa na watoto ambao hawana malezi mazuri na wenyewe wamebarikiwa kuzaa watoto, wameendeleza kukata ule mnyororo wa maadili. Kwa sababu, hawakuruthishwa na wenyewe hawawezi kuendelea kurithisha, lakini dalili zake ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, dalili zake sasa ni mabaya yote tutanayoyalalamikia sasa hivi humu ndani na siku zote; ubakaji, ulawiti, sanaa mbalimbali mbaya, hizi cyber bullying ambazo zimekuja na utandawazi zinazompa mtu asiye na maadili, ambaye hakuruthishwa tabia njema, ujasiri wa kufanya vitu vibaya, ambavyo hawezi kumfanyia baba na mama yake waliomzaa. Hapa pamebaki tu wawachukue wazazi wao waliowazaa wawafanyie cyber bullying, kama wamekuwa na ujasiri wa kwenda kufanya cyber bull kwa viongozi hadi wa Taifa na kiongozi namba moja wa Taifa. Huu ni ujasiri mkubwa utokanao na malezi mabovu kwa baba zao, mama zao, babu zao na bibi zao, hili hakika ni janga.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya masuala ya mavazi mabaya na watoto kunengua viuno yametajwa hapa. Huduma za mafundisho ya baadhi ya dini au baadhi ya viongozi wa dini, ambayo yamekuwa ni tata, yote haya ni zao la mmomonyoko wa maadili na malezi mabovu kwenye msingi wa familia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo ni nini tunacho sisi katika mapambano hayo? Tanzania ni nchi mojawapo nzuri sana katika kutengeneza sera, miongozo na mikakati, lakini ni lazima nikiri hapa na ninyi ni mashahidi, machinery yetu ya Serikali, Wizara hizi za Kisekta, ni kutengeneza miongozo, ndiyo kama huu hapa mwongozo mwingine nimetoka kuusoma. Tuna mwongozo mwingine ambao unahusiana na masuala ya malezi, uendeshaji wa vikundi vya wazazi vya malezi na matunzo ya mtoto wa Mei 25; tuna viongozi wa miongozo ya malezi na makuzi ya maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuzingatia dini mbalimbali, hii hapa; tuna Kitini cha Wawezeshaji Kuhusu Majadiliano ya Mila na Desturi, hii hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, tuna mkakati kabisa wa kutokomeza ukatili ambao ni zao la mmomonyoko wa maadili Kitaifa kwa wanawake na watoto, watoto wa kiume na wa kike. Kwenye Mashirika Yasiyo ya Kiserikali tuna miongozo vilevile na mingine sijaibeba, shida yetu ni wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uzoefu wangu wa kufanya kazi Serikalini miaka yote mpaka nimekuwa Mbunge, tumetengeneza Sera ya Decentralization by Devolution, ambapo Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tumepeleka wataalam kule. Tuna Maafisa Utamaduni tumewaweka pale ma-custodian wenye dhamana ya masuala ya maadili, tuna wataalam wa Sheria, wa Maendeleo ya Jamii, wanaoshughulika na Habari, kila mtaalam yupo kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto yetu moja, ambayo ninaomba niikiri hapa, ili tushirikiane ni miongozo hii. Huenda katika baadhi ya maeneo inawekwa kabatini, lakini tuna machinery yetu ya Serikali za Mitaa inayoendesha vikao rasmi, ambavyo vinaanzia ngazi ya kata (WADC) na Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kule kwenye kata ndiyo Wenyeviti, tuna Kamati za Baraza la Madiwani na Full Counsel nimefuatilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona vipaumbele vya ajenda mbalimbali bado ni changamoto. Ili tuweze kutoka hapa tulipo tufikirie hata kuja na Sheria ya Maadili sasa, ambayo itatekelezwa na kufungamanisha mambo yote ya maadili huko mbele ya safari. Ni lazima tukubaliane kufanya ajenda ya maadili na mmomonyoko wa maadili kuwa kipaumbele katika halmashauri zetu, kwenye majukwaa yetu rasmi ya kuweka ajenda za vipaumbele mezani. Vinginevyo utamkuta Afisa Utamaduni anafanya mengine, hana mkakati aliouwasilisha, lakini hoja za vipaumbele zimepita na kwa kawaida bajeti itakwenda na vipaumbele vilivyowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe, tumefanya kazi ya kuandaa hii miongozo, tumeisambaza, tushirikiane kufanya mapinduzi ya ajenda kwenye machinery zetu, ili mikakati yetu kwenye halmashauri zetu ifuate local context pale walipo, tutaweza kutoka kwa haraka. Hata hayo mambo ya malezi na makuzi watayasikia kwa haraka, masuala ya kuna Sheria gani watasikia kwa haraka, masuala yote ya kuhusu kwamba, tuvaaje, mila na desturi ziweje, tuongee vipi, watayasikia kwa haraka badala ya kubakiza kwenye sera hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, muda ni mdogo, mambo ni mengi. Ningependa kusema machache kuhusu hoja za Kamati, tumezipokea; na kuhusu masuala ya maendeleo ya vyuo vyetu kuwa ya ubia, ndiyo. wakati muafaka umefika wa kufikiria hizi hosteli zetu zijengewe pamoja na ushirikiano wa Sekta Binafsi ziweze kuwa nzuri, ili mapato haya yaongezeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jesca Msambatavangu ameongelea tena suala linalomuumiza sana kuhusu ushirikishwaji wa wanaume katika masuala yote ya Wizara hii. Nimhakikishie, tumeanza vizuri, Wizara hata haikuwepo miaka iliyopita, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya jambo kubwa kuileta hii Wizara akaanza na hawa wanawake, ambapo changamoto ilikuwa inaelemea sana, lakini kadri tunavyokwenda tunaona kwamba, takwimu zinabadilika, wanaume pia, wanakatiliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie, kwenye mikakati yote ya kutetea watoto wa kike kuanzia kwenye madawati ya ulinzi shuleni, kwenye hayo Mabaraza ya Watoto, Sheria yenyewe ya Watoto, Mabaraza na Madawati ya Vyuoni ni watoto wa kiume na wa kike. Hata Iringa, 19 Novemba, mwaka jana 2024, nilienda kwenye Kongamano la Wanaume kwa siku yao ya Wanaume Duniani, Tarehe 19 Novemba. Huu ni mwanzo wa safari ya kufika kule, kutengeneza vizuri mchango wa wanaume na kuzifanyia changamoto zao vilevile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kitabu changu cha Hotuba nimeonesha pale kwenye Ukurasa wa 55, Aya ya 104, inayosema, “tuna sekta nyingine zinatoa mikopo vilevile, ambayo inahusisha wanawake na wanaume. Mfano, kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, mifuko hii 75 ikijumuisha 63 inayomilikiwa na Serikali na mifuko 12 iliyo chini ya Sekta Binafsi hadi Aprili 2025, mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 3.5 imetolewa, ambapo kiasi cha shilingi trilioni 1.7, sawa na 49%, imetolewa kwa wanawake na kwa upande wa wanaume zilitolewa shilingi trilioni 1.8, sawa na 51%.”
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonesha kwamba, kuna mtandao mpana wa upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa wanaume pia, siyo kwa wanawake pekee yao. Kutokana na changamoto za mila kandamizi zinazowaathiri zaidi wanawake ndiyo zilitengenezwa programu chache, kwa ajili ya kuwanyanyua hawa wanawake waende kwa kasi zaidi, lakini kama vile haitoshi Dkt. Samia Suluhu Hassan akaona hapana, isiwe kesi, ninatengeneza Mfuko mwingine wa wafanyabiashara ndogondogo ambao unahusisha mtu mmoja-mmoja na wala siyo kikundi, wanawake na wanaume. Takwimu zilizoko hapo za Machi, zilikuwa ni kama shilingi milioni mia moja na kitu zimetolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi kwenye eneo hili, record inasema tayari wafanyabiashara ndogondogo 601 wameshapata mkopo wenye thamani ya shilingi bilioni 1.1, lakini kuna maombi 2,092 yanaendelea kuchakatwa yenye thamani ya shilingi bilioni 3.5. Leo tumeomba shilingi bilioni 12, wakitupitishia ina maana Mwaka wa Fedha unaoanza Julai, wanaume wafanyabiashara ndogondogo kumekucha kuchere, nawakaribisha waje wajisajili, wabebe fedha, Wizara yao imewakumbuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ni mengi, lakini nimeyapokea, tutayaandika na tayari yameshaandikwa hapa, tutayahariri na kuyawasilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache sana, ninaomba kutoa hoja, tupitishiwe bajeti yetu tukatekeleze.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaafiki.