Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie hoja hizi mbili ambazo ziko Mezani kwetu. Nianze kwa kuwapongeza hawa Mawaziri wawili; Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji pamoja na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye ni Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mawaziri hawa ni wachapakazi, ni wasikivu, wanafikika, na kila muda wapo tayari kurekebisha mipango yao ili kusikiliza mahitaji ya watu, lakini pia wana bahati ya kupewa wasaidizi ambao nao ni wasikivu vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ndugu yangu Mheshimiwa Hamad Chande, ni Naibu Waziri msikivu, mnyenyekevu na muda wote yupo tayari kusikiliza kero za sisi Wabunge. Vilevile kaka yangu Stanslaus Nyongo ni Mbunge mahiri, mchapakazi. Hata alipoteuliwa kuwa Waziri, hajapandisha mabega juu. Bado tunaye tunatamba naye na tunashirikiana naye. Kwa hiyo, hongereni sana Mawaziri na Manaibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee, nichukue nafasi hii kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake mapana na jinsi anavyoendelea kuchapa kazi na kutusaidia sisi Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jana tu tumeshuhudia kazi kubwa ikitendeka, na Afrika Mashariki jana ilizizima tulipokuwa tunashuhudia uzinduzi wa Daraja la Busisi. Kama alivyosema hapo Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alikuta daraja hili limetekelezwa kwa 24%, lakini kwa maono yake, kwa ujasiri wake ametekeleza kwa 100%. Hongera sana Mheshimiwa Rais. Tunamwomba Mwenyezi Mungu ampe afya njema na umri mrefu ili tuendelee kunufaika na busara zake na uongozi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utahusu katika maeneo matatu. Sehemu ya kwanza ni kuhusu sekta ndogo ya korosho. Ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa inayoifanya katika uwekezaji wa sekta hii ndogo ya korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia miaka minne mfululizo wakulima wa korosho wakipata pembejeo kwa ruzuku ya 100%. Tumeshuhudia pia Mheshimiwa Rais anafanya maamuzi magumu kwa kutoa 100% ya Export Levy, kwamba yote ipelekwe kwenye tasnia ya korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, msimu huu Wizara ya Kilimo na Bodi ya Korosho imeajiri Maafisa Ugani 500 ili kwenda chini kuwasaidia wakulima wa korosho. Siyo hivyo tu, tumeshuhudia msimu uliopita kwamba minada yetu imeendeshwa kidigitali kupitia TMX. Kwa hiyo, hongera sana kwa Mheshimiwa Rais, uwekezaji wake tunauona katika sekta ya korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina mambo mawili tu ya kushauri. Kazi hii nzuri ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais, matunda yake yanaanza kuonekana. Kwa mfano, usambazaji wa pembejeo kwa 100%, mwaka 2024 kulikuwa na ongezeko kubwa sana la uzalishaji wa korosho. Tumetoka tani 315,000 na tumefikia tani 525,000 Kitaifa. Hata hivyo, takwimu hizi haziendi sambamba na ongezeko la ubanguaji wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaiomba Serikali sasa ifanye mipango wa kuwa na mpango na vivutio maalum wa kuhakikisha sasa tunatoa kipaumbele kwa wabanguaji wetu wa ndani ili tulinde ajira za wanawake na vijana. Si hivyo tu, ni pamoja na kuongezea thamani korosho yetu ambayo itakwenda kupata bei nzuri huko nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii bei ambayo tumeipata miaka miwili hapa nchini kwetu inawezekana ni kwa sababu wenzetu wazalishaji wa korosho Afrika Magharibi wameamua kuzuia korosho yao isiuzwe nje ikiwa korosho ghafi, wanabangua. Kwa mfano Benin, Ivory Coast wamefanya hivyo. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali yetu ijikite sasa ili na sisi tuwe na mipango ya kuhakikisha kwamba ubanguaji unafanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwa hatua nzuri ambazo imeanza kuzichukua. Tuna kongani ya Kiwanda cha Korosho pale Malanje. Kama tulivyoona kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huu, kuna mwekezaji amepatikana, atabangua tani 100. Hiyo ni hatua nzuri, tunataka wabanguaji wengine wapatikane ili korosho yetu yote tubangue ndani na tupeleke nje korosho na karanga ili wakulima wetu wanufaike na mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mwaka 2024 tumeshuhudia uchache au upungufu wa maghala baada ya uzalishaji kuongezeka. Kwa hiyo, naomba Serikali iweke mpango maalum wa kujenga maghala katika maeneo yetu, tusiwe na maghala ya wilaya tu, twende hadi kwenye ngazi ya tarafa ili tuhakikishe kwamba korosho ikitoka kwa mkulima iende ghalani siku ya tatu iende mnadani na hatimaye mkulima, korosho yake ifike mnadani mapema na apate bei ambayo inaridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ningeshauri Wizara, Bodi ya Korosho na vyama vikuu vya ushirika watengeneze mpango wa kuongeza maghala katika maeneo yetu. Mimi ningeshauri kwenye Jimbo langu la Nanyamba, tungeweza kuweka ghala pale Kiromba, tungeweza kuweka ghala pale maeneo ya Hinju na maghala makubwa tukaweka pale Nanyamba Mjini ili kuhakikisha kwamba korosho ikitoka kwa mkulima inapokelewa, na baada ya siku chache inakwenda mnadani na siyo kama tulivyoshuhudia mwaka 2024, tulipoona korosho yetu inaloana na mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho ikiathirika na mvua hata ubora wake unaathirika na hatimaye kupata bei ambayo ni ndogo inapopelekwa mnadani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ulikuwa ni kuhusu Mtwara Corridor. Mtwara corridor ni mpango ambao ulianzishwa huko nyuma na viongozi wetu wa Tanzania, Malawi, Msumbiji na Zambia; na lengo lake kubwa ilikuwa ni kuhakikisha kwamba Bandari yetu ya Mtwara inaunganishwa na barabara, reli na usafiri wa maji; na kukawa na mipango mizuri sana ambayo imewekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuubeba mpango huu sasa na kuanza kuutekeleza. Tumeshuhudia sasa Barabara ya Uchumi kutoka Mtwara Nanyamba - Newala mpaka Masasi inajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kuna maboresho makubwa yanafanyika katika Barabara yetu ya Mingoyo - Mtwara na Mingoyo – Masasi. Sasa hivi tumeona kwenye mpango wetu kwamba tuna ujenzi wa reli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, hili suala la ujenzi wa reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay sasa tuutekeleze, tuongeze kasi ya utekelezaji na matawi yake ya Mchuchuma na Liganga. Wananchi wa maeneo hayo wanasubiri sana mradi huo ili uboreshe maeneo yetu na hatimaye Bandari yetu ya Mtwara iweze kutumika ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo, tutakuwa tumeifungua Mtwara, tutakuwa tumeifungua Lindi na vilevile Liganga na Mchuchuma, sasa chuma kitakuwa kimepata sehemu ya kusafirisha. Siyo hivyo tu, tutapata mzigo kutoka nchi za Malawi, Msumbiji, na Zambia ili ipelekwe kwenye Bandari yetu ya Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana kwamba sasa uwe muda wa utekelezaji wa mradi huu, ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la mwisho ni kuhusiana na sekta ndogo ya gesi. Ninaipongeza Wizara na Shirika la TPDC kwa kazi nzuri ambayo inafanywa. Vilevile ninaipongeza Serikali kwa kuamua sasa kufanya mashauriano na wale wawekezaji ili mradi wetu wa LNG uweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali kwamba kwa kipindi kilichobaki sasa hivi tuongeze kasi ya mashauriano, tuongeze kasi ya majadiliano ili mradi utekelezwe. Wenzetu wa Msumbiji majirani zetu wanaekwenda kwa kasi sana. Ni muda mwafaka sasa na sisi twende kwa kasi ili gesi yetu ya Mtwara, na gesi yetu ya Lindi iweze kuchakatwa pale Likong’o Lindi na hatimaye tupate fedha nyingi za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninashauri kwamba kasi ya mashauriano iongezwe. Vilevile kupitia TPDC tuongeze kasi ya kuongeza vituo vya CNG ili gari zetu ziweze kutumia hiyo gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kuna mradi wa kusambaza gesi asilia nyumbani. Tumeanza Lindi na Mtwara, lakini kaya ambazo zimenufaika ni chache sana. Ni muda mwafaka wa kutenga fedha za kutosha ili gesi hiyo isambazwe, siyo Mtwara na Lindi pekee, kuwe na line mbalimbali. Twende hadi Masasi, iende Tunduru mpaka Songea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuwe na route nyingine ambayo inaenda mpaka Dar es Salaam na maeneo mengine. Taasisi za umma zipewe kipaumbele, vilevile hospitali za umma zipewe kipaumbele, na maeneo mengine ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango cha usambazaji wa gesi hii asilia nyumbani, sasa hivi kasi yake ni ndogo sana. Sababu kubwa ni kwamba hazijatengwa fedha za kutosha kwa ajili ya mradi huo. Ninaiomba Serikali, naiomba Wizara na kupitia TPDC fedha za kutosha zitengwe ili gesi hii ipelekwe nyumbani na hatimaye Serikali ipate fedha za kutosha, na vilevile ili wananchi wetu wanufaike na gesi yao ambayo ipo ya kutosha kwa maeneo ya Mtwara na Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu sisi Wanananyamba, hatumdai Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatudai yeye, na tumejiandaa kwamba mwezi Oktoba tunatiki na tuna kapu kubwa la kura zake ambazo tayari tumeziandaa kwa ajili ya kujaza kura kwa ajili ya Mama Samia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, ninaunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)