Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali pamoja na Wizara ya Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kuweza kunipa uhai na kusimama leo mbele ya Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tukiwa tunakaribia kuvunja Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninaomba Mwenyezi Mungu anisaidie na awasaidie Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wote ambao wameifanya kazi hii kwa weledi mkubwa ndani ya miaka mitano, kwa kuhakikisha kwamba wanamsaidia au tunamsaidia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendesha mambo yake kwa weledi na kwa umakini mkubwa kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yamefanya tuendelee kutambulika na kufahamika kote ulimwenguni, ni kwa ajili ya umahiri wa Mama huyu mwanamke hodari, mwanamke shupavu, mwanamke mwenye maono, mwanamke mwenye malengo ambaye ndiye ametufikisha hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kokote Tanzania inaposimama leo hii, haiachi kumteua au kumchagua mtu yeyote kuhakikisha kwamba anasimama kwa niaba ya Taifa letu la Tanzania. Aliyeyatengeneza haya sio mwingine bali ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hongera sana mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo na kutoa shukurani kwa Mungu, ninaomba niendelee kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amemwaga fedha kona zote za Taifa letu la Tanzania, kuanzia mijini hadi vitongojini. Ndiyo maana Mbunge yeyote atakayesimama katika Bunge hili hawezi kuacha kumpongeza, hata wale ambao walikuwa hawajaona maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wengine walikuwa hawajaona maji ya bomba katika Taifa hili, lakini leo watu wameona maji ya bomba, wameona umeme, wameona barabara nzuri, wameona vituo vya afya, wameona huduma za jamii za kila aina, zikionekana katika Taifa letu la Tanzania. Sio mwingine bali ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayasema haya kwamba mama amemwaga fedha nyingi sana kwa sababu mimi mwenyewe nikiwa ni shahidi juu ya mambo hayo, amemwaga kwenye barabara; kwa mfano Jimbo langu tu la Mchinga ametuletea shilingi bilioni 11; kwenye maji, shilingi bilioni 18; afya, usiseme; nishati, amehakikisha kwamba vijiji vyote vya Jimbo la Mchinga vimepata nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Jimbo la Mchinga lina vitongoji 236. Kati ya vitongoji hivyo 181 leo hii vinawaka umeme na ni maendeleo, kwani bila umeme hakuna maendeleo. Kwenye elimu ametoa shilingi bilioni 17.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ndicho yeye amekipa umuhimu mkubwa katika Taifa letu. Bila chakula hakuna kitu. Kila mwanadamu anategemea chakula. Leo hii kwenye kilimo ametuwekea shilingi bilioni 31.3. Hii tangu anaanza kulihutubia Bunge letu, hili aliweka kipaumbele kwenye kilimo, na ndiyo maana bajeti ya kilimo ilitoka kwenye shilingi milioni 290 kule, ikaja mpaka trilioni. Hii yote ni kazi ya Mama Samia Suluhu Hassan na ndiyo maana leo ninaposimama kuzungumza, nina kila sababu ya kumpongeza kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo sasa hivi tumekuwa wa pili barani Afrika kwa uzalishaji. Haya yote ni kwa ajili ya maono mazuri ambayo ameyaonyesha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hongera sana Mama. Tuna kazi kubwa; na siyo kubwa, tarehe ikifika tunachukua, tunaweka, waaa! Kwa nani? Kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya katika Taifa letu la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Makamu wa Rais, amekuwa ni msaidizi mzuri sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yeye ndiye aliyekuwa msimamizi mzuri wa Shughuli za Serikali Bungeni. Bila kusimamia vizuri Shughuli za Serikali Bungeni, wakati mwingine kuna baadhi ya mambo yanaweza yasiende sawa, lakini kila jambo liliweza kwenda vizuri. Ninampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ninampongeza Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa uwasilishaji wako mzuri wa bajeti yetu ambayo ni bajeti inayojipambanua kwa kila eneo, pamoja na Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu wa Wizara, na watendaji wote, bila kumsahau Profesa ambaye yuko pembeni yake ambaye wao wenyewe wanaitana kaka mdogo, kaka mkubwa. Waendelee kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaweka wao; amejua jinsi wanavyoweza kuchapa kazi, na akaona hakuna matata. Kazi hii wanaiweza vijana kutoka Singida. Hongera sana kwa vijana wa Singida, Mama anawaamini na anawapenda sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefanya kazi kubwa na nzuri katika kuliongoza Bunge. Kazi aliyoifanya katika kuliongoza Bunge hili pamoja na Naibu Spika ni kazi zenye viwango, na kila mtu anaziona kazi hizo. Hongereni sana; na wakisaidiwa na Wenyeviti wao, wamefanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wewe Mwenyekiti Mwanyika ambaye ni Mwenyekiti wangu katika Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, hongera sana, umefanya kazi nzuri. Tunaamini tunamaliza hili Bunge, tutarudi huko majimboni, na tukirudi majimboni kwa kazi hizi zilizofanyika, hakuna mtu atakayesema, huyu hawezi. Wote tunaweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, uongozi ni wote. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba hapa au Mama Samia Suluhu Hassan ana mwenza wake na hata sisi Wabunge tuna wenza wetu. Tunawapongeza sana Wabunge hawa wenza wa Wabunge; mwenza wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba anamsaidia kwa hali na mali, na mambo yake yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niwaambie, Mama Samia ni Rais. Pamoja na Urais wake, anazungukwa na walinzi chungu nzima, lakini ikifika usiku anaenda kulala. Akishaenda kulala, kwanza anamtegemea Mungu, na mwenza wake ndiye anayeweza kumfariji, hata kama akiwa na misongo ile, mwenzi ndiye mtu wa kwanza kumpa faraja. Bila yeye mambo hayaendi vizuri. Hongereni sana wenza wa viongozi, na hongereni sana wenza wa Wabunge kwa kusaidiana na Wabunge hawa. Endeleeni kufanya hivyo, tunawategemea sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka nije kwenye kilimo. Kama nilivyosema, Mheshimiwa Mama amefanya kazi kubwa kuongeza bajeti, na ndiyo maana kilimo kimepanda kupita kiasi. Leo Tanzania inategemewa na Afrika katika suala zima la kilimo. Sasa Mama amehimiza kilimo, na watu wamelima vizuri na wamelima kwa bidii. Korosho wamelima sana, ufuta wamelima sana kupita kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kutokana na changamoto zilizojitokeza, juzi tulikuwa na mnada wa ufuta. Ufuta ulipanda mpaka shilingi 4,000.00. Sasa hivi bei ya ufuta kwa ule mnada wa kwanza imeshuka mpaka shilingi 2,700.00. Nini ninachotaka kusema?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusitegemee soko moja, pamoja na kwamba ninajua Serikali inafanya kazi kubwa na nzuri ya kutafuta masoko, tuendelee kutafuta masoko ili wananchi hawa waliojitokeza na waliojipambanua kulima kwa bidii, juhudi na maarifa, itakapofika wakati wauze mazao yao kwa bei ambayo itakuwa ni nzuri na wataifurahia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni barabara. Mimi kwangu kule tunalima ufuta. Ninamwomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, yeye ndiye Waziri wa Fedha, kule wamelima ufuta lakini hauwezi kutoka Mipingo kuja hapa kwenye maghala, wala hauwezi kufika pale Mkwajuni. Ninaomba anisaidie fedha ili waweze kuleta ule ufuta kwenye vituo vya kuuzia. Mheshimiwa tafadhali ninakuomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye afya, tumepunguza tozo kuhusu vileo ili kuleta ushindani. Kuna kitu kinaitwa energy. Energy ni shida, na ni tatizo. Energy inauzwa madukani na wanaokunywa ni watoto wadogo. Wanakunywa energy kwa malengo yapi? Kama wanaweza sasa hivi umri wa miaka 13 ku-boost ile nguvu ije, wakifika umri wa miaka 28 watakuwa katika hali gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, energy jamani zinaharibu hao watoto. Tutengeneze kitu mbadala. Tuweke mikakati ya kupunguza haya ma-energy. Ni hatari, watoto wanaangamia. Tunategemea vijana ndio wanaotutegemea sisi baada ya kuondoka, vinginevyo ni hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja kwa 100%, na ninawatakia Wabunge wenzangu kila la heri. Ninaamini wote tutashinda. Ninawashukuru sana wapigakura wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Mkoa wangu wa Lindi. Ninawashukuru wote, ninaamini sote tutarudi. Ninawashukuru sana Wanamchinga kwa ushirikiano mkubwa walionipa katika kipindi cha miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru ninyi viongozi wote, Wabunge, watumishi na wasiokuwa watumishi kwa ushirikiano mkubwa mlionipa. Mungu awabariki, inshallah tutarudi tena Bunge lijalo. Sina mashaka hata kidogo tutarudi sote humu Bunge lijalo kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa muda huu, nawe Mwenyezi Mungu atakurudisha. (Makofi)