Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuweza kukaa ndani ya Bunge hili kwa miaka mitano. Ninamshukuru sana Mungu kwamba ametupa afya, lakini pia tuwaombee wale wote ambao walituacha kipindi hiki, basi Mwenyezi Mungu awaweke mahali pema Peponi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwashukuru sana Wabunge ambao ni Mawaziri; Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Chande wanafanya kazi nzuri. Wanapiga kazi nzuri. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu anajua hiyo Wizara ni nyeti, lazima kutakuwa na mawe kila kona, lakini akaze mwendo na aendelee. Ninajua tunamaliza Bunge, lakini Serikali bado ipo. Kwa hiyo, mawaziri bado tunawategemea watafanya kazi katika maeneo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na eneo la elimu. Kwanza, ninapongeza sana, kuna maeneo makuu mawili ambayo yamefanyiwa kazi kipindi cha miaka mitano. Moja ni la mikopo. Tulikuwa na mikopo kama shilingi bilioni 464, lakini mpaka sasa ikapanda kufikia shilingi bilioni 787.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, suala la mikopo mnajua lilikuwa na kelele miaka miwili iliyopita, lakini tuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia, mikopo hii ilivyoongezeka, kelele ziliisha. Niwaambie, vyuo vikuu vilitulia. Vurugu hakuna vyuo vikuu. Wahadhiri pia walitulia, ingawa wana changamoto kidogo nitazisema, lakini mikopo imefanya vyuo vikuu vimetulia, na niseme Serikali ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ni muhimu katika elimu lililofanywa ni uboreshaji wa mitaala. Mheshimiwa Rais alipotoa yale maagizo kwamba mitaala iboreshwe na imefanyika hivyo, niseme Waheshimiwa Wabunge baada ya miaka 10 wanafunzi wetu hao, vijana wetu wataweza kujiajiri kwa sababu ya lile eneo la amali. Kwa hiyo, hata kelele za ajira zitapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo kubwa lililofanyika katika kipindi hiki kubadilisha mitaala na ilikuwa ni nguvu ya Rais kusema kwamba ninataka mkarudie, hebu mfanye review, rudieni mitaala, mwone kwamba tunaifanya vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tulikuwa tunalalamika humu ndani kwamba elimu yetu haitusaidii. Kwa hiyo, suala la mitaala ni muhimu sana, na ninampongeza sana Rais kwamba aliliona hilo na akaona ni muhimu mitaala hiyo ibadilishwe. Kwa hiyo, uboreshaji wa mitaala utaleta ajira baada ya miaka 10. Tuvute subira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine sasa nije kwenye maombi kwa huo upande wa elimu. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nimefurahi sana kwamba yupo hapo. Suala la madeni ninamwombe sana sana Mheshimiwa Waziri chonde chonde, mimi ninapenda bado nirudi kuwa mwakilishi wa vyuo vikuu. Ningekuwa hapo karibu labda ningempigia magoti au ningegaragara kama wanavyofanya Wangoni, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mwigulu madeni ya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu, hebu wamalizane nao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, pale Chuo cha Ushirika wanadai shilingi bilioni 1.1 lakini ukienda SUA wana madeni, ukienda UDOM wana madeni, na ukienda Open University wana madeni. Hebu tumalizane nao hawa watu. Wanafanya kazi kwa utulivu, hutaweza kusikia sijui kuna migogoro au wanagomagoma. Ninamwona Mheshimiwa Waziri anaandika hapo. Ninakushukuru, akalifanyie kazi hilo suala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali kwa ujumla ikaangalie sana retirement age. Bado wahadhiri wanalalamika hasa maprofesa. Vyuo vyetu nimekwambia mara nyingi hakuna maprofesa.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu tulikuwa sote pale chuoni wakati wewe unasoma Ph.D, tunagongana gongana kwenye corridor. Maprofesa ni wachache mno. Unapishana tu na ma-Assistant Lecturer. Retirement age mwiangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hivyo kwa sababu ninaamini Waziri wa Utumishi yupo, Mheshimiwa Simbachawene ananisikia. Tuangalie retirement age ya wahadhiri. Ubongo hauzeeki haraka. Mtu akiwa profesa au daktari kule chuo kikuu hubebi mizigo, hubebi matofali kule, ni akili tu inafanya kazi. Kwa hiyo, niwaombe mwangalie retirement age hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa upande wa elimu, wenzangu waliongea. Ninawaomba sana tuangalie namna gani tunaondoa kuamsha saa 10 ya usiku watoto wa chekechea mpaka darasa la tatu. Tufanye kama wenzetu. Korea na Japan wanaanza masomo saa tatu, mbona wanafanya vizuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watoto wadogo kuwabeba saa 10 ya usiku kwenye magari; nimelisema hilo na mwenzangu alilisema, ninafikiri ni Mheshimiwa Neema. Niwaombe jamani hili tuliangalie litatuletea balaa. Tuangalie kabisa hawa watoto wadogo wanaosoma, wapelekwe shuleni kuanzia saa moja na nusu, lakini siyo saa 12. Wenye shule wanapenda wao wanawabeba tu kwenye magari lakini waangalie na akili ya watoto. Hilo ninaona nimelimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la afya. Mimi niombe, kuna tatizo kubwa sana la ugumba. Kuna wanawake wengi wanashindwa kupata watoto. Ninaomba Hospitali ya Benjamin pamoja na Hospitali ya Muhimbili waboreshe kitengo kile cha IVF, wanawake wasaidiwe. Kwenda kupandikiza watoto jamani ni gharama kubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanawake wanaopata hilo tatizo linawa-affect mpaka kwenye ubongo. Akili yao haiko sawa. Tuwasaidie, tunaposema family planning, tuiingize huko. Hata kuwasaidia hawa, tena ikibidi bure. Kupandikiza mtoto ni shilingi milioni 15 au milioni 20, hawawezi. Waziri wa Afya akaliangalie hilo, upandikizaji wa watoto uwe bure au walipe fedha ndogo sana. Hili jambo tunaliona tu dogo, lakini sasa hivi ni suala kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, wanaume wanaona aibu kwenda hospitali na kusema mimi sizai. Kwa hiyo, hospitali iweke kitengo kitakachoweza kushirikisha wote: wanaume na wanawake ili mtu aweze kupata mtoto. Kutokupata mtoto ni umaskini kama umaskini mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine Mheshimiwa Waziri nizungumze kuhusu ardhi. Mimi ninatoa tu maoni yangu kuhusu ardhi. Jamani Wizara ya Ardhi hebu ilete programme ya kuondoa nyumba zote za nyasi na nyumba zote za matope. Wakipanga hiyo programme, wanaweza kuwaambia wananchi kwamba, kila mwananchi afyatue matofali, ajenge nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakusanya fedha kutoka kwenye zao la tumbaku, na madini. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu atafute fedha, watu wa namna hiyo wanaambiwa jenga nyumba nzuri, Serikali pelekeni mabati. Ni aibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilikuwa ninaangalia takwimu, yaani tumefikia wakati takwimu mikoa ambayo inaongoza kwa nyumba ambazo siyo bora; ninaomba mnisikilize. Lindi, Tabora, Mtwara, Ruvuma, na Rukwa. Sasa mpaka mimi ninashangaa. Mtwara wanalima korosho, sasa mjue kwa nini wananchi wa kule nyumba zao bado ni za nyasi. Ruvuma ninajua wilaya zinazotuangusha kule, ninazifahamu, Namtumbo ni mojawapo, pamoja na Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nyumba za nyasi mpaka leo, halafu nyumba zinazoezekwa kwa udongo Singida, na Dodoma; Singida ni kwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. Hebu tuwasaidie. Tupeleke bati tuwahamasishe nyumba za matofali…
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, peleka bati.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
TAARIFA
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Massare.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba Singida sasa hakuna nyumba ya tembe hata moja. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Amandus Chinguile, unaipokea?
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei. Nimepita huko, ila sasa ndiyo hivyo Mheshimiwa Mbunge si anaona aibu; lakini Singida, Dodoma, Manyara, Shinyanga, na Simiyu, tuwapongeze wale ambao mikoa yao hakuna nyumba za nyasi. Mkoa unaoongoza ni wa Mheshimiwa Waziri, Mkoa wa Njombe ni bati tupu; Kilimanjaro bati, Dar es Salaam na hata Kagera pamoja na Katavi. Tena mpaka nimeshangaa hata Katavi kumbe wako juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ni kampeni inaweza ikafanyika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu tuondoe hili. Tafuta fedha kila mahali. Mwone Waziri wa Madini wakupe fedha, ziko kule. Waziri wa Kilimo anasema anapata fedha nyingi za kigeni kutoka kwenye tumbaku, mbane alete hizo fedha wananchi hawa wapate bati.
La mwisho, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu leo ndiyo unisaidie hili la mwisho. Ninaomba sana, nilikuomba sana kuhusu wale ma-DC na ma-RC. Hebu uende ukaongee na mkuu wa nchi, wapate ile HS. Andika hapo. Wapate ile HS, Wakuu wa Wilaya wanalalamika mno. Tumalizane nao lile deni wanaita hand shake Mheshimiwa Kikwete alisaini. Sasa ninakuomba ukamalize na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nikushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)