Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Pia, ninaomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunipa afya njema ili niweze kuongea katika Bunge lako Tukufu katika kuchangia hoja iliyopo mbele yetu, Hoja ya Mapendekezo ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika, ninaomba kuunga mkono maoni ya Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamezungumza kuendelea kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ya maendeleo ambayo amekuwa akiifanya kwa ajili yetu sisi Wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo ambalo liko wazi kabisa dhahiri shahiri, mwenye macho haambiwi tazama; mwenye kusikia haambiwi sikia; na mwenye kugusa haambiwi gusa; yaani ile milango yote ya fahamu ambayo binadamu anayo inabaini na kutambua kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika, ninaomba niwapongeze Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Mawaziri na watendaji wote kwa hotuba nzuri ambayo wameiandaa kwa ajili ya bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imetekelezwa imebainishwa katika ukurasa wa 14 wa hotuba hii. Ninatambua Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi mbalimbali kwa fedha nyingi sana, matrilioni na matrilioni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze katika mkoa wangu wa Dodoma, ambao ndiyo Makao Makuu ya nchi hii ya Tanzania. Miaka 10 iliyopita ninaamini wengi wetu ni mashahidi, Dodoma iliyopo sasa siyo ile ya miaka 10 iliyopita. Kwa hiyo, ninaendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ya maendeleo ambayo tumeyapata katika Mkoa wetu wa Dodoma. Miongoni mwao, ninaomba niseme kwamba Serikali imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 3,093. Hili siyo jambo dogo kwa ajili ya maendeleo ya Wanadodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanadodoma, tuna kila sababu ya kuendelea kumshukuru, lakini pia kumwombea Mwenyezi Mungu, awe na afya njema, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwamba Mwenyezi Mungu akitujalia afya na uhai mwezi Oktoba tuhakikishe tunampa kura za Tsunami kwamba Dodoma ameipendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikibainisha tu baadhi ya miradi ni pamoja na ujenzi wa barabara ya mzunguko ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 221, na hivi juzi tulifanya ziara ya kuikagua na yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, tunaendelea kuishukuru sana kwa sababu ujenzi wa mradi huu una maana kwamba utapunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dodoma. Pongezi sana kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Msalato. Tunatambua kabisa kwamba huu utakuwa ni uwanja wa Kimataifa. Hivyo, ndege za kuingia na kutoka Mataifa mbalimbali zitafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo mradi wa uwekezaji mfumo wa umeme chini ya ardhi katika Mji wa Serikali ambao thamani yake ni shilingi bilioni 50.99. Pia ujenzi wa Mji wa Serikali ambao ni kivutio kikubwa sana katika Mji wetu wa Dodoma. Mwisho wa siku mimi naamini na kuna watu wanaweza wakajitokeza kwenda kufanya utalii katika eneo lile kwa jinsi ulivyojengwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwenye suala zima la huduma za kijamii ikiwemo elimu na afya, lakini nijikite zaidi kwenye elimu. Naendelea kuipongeza Serikali kwa kuwa na miradi mbalimbali ya kuhakikisha kwamba elimu pia inapewa kipaumbele kwa kujengwa miundombinu sahihi ili kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii naomba niseme wazi, dhahiri, shahiri kwamba, Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa wanufaika wakubwa sana wa ujenzi wa miundombinu hii, na hii imesaidia kuchagiza kwamba, yale mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia imefanya Mkoa wetu wa Dodoma uwe miongoni mwa mikoa ambayo imefanya vizuri sana katika mitihani ya Kitaifa na kuwa mkoa wa nne, hili siyo jambo dogo. Kwa hiyo, tunaendelea sana kuishukuru Serikali kwa kuhakikisha kwamba miradi ya kimaendeleo inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba nitoe ushauri kwamba, basi Serikali ione umuhimu wa kujenga nyumba za walimu katika shule zote, za sekondari pamoja na shule za msingi ili kuwawezesha hawa walimu nao kuwa katika mazingira bora ya utendaji kazi ili mwisho wa siku mafanikio zaidi katika suala la elimu yaweze kupatikana na hatimaye tupate wataalam mbalimbali kutoka katika shule hizo ambazo walimu wao wanawafundisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba nizungumzie suala zima la mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji. Mkoa wa Dodoma umekuwa ni miongoni mwa mikoa ambayo pia imefaidika na uwekezaji mkubwa sana ambao pia uwekezaji huu utasaidia kwanza, kupata ajira kwa wananchi wa Dodoma; kuongeza kodi pamoja na kipato kwa ajili ya wananchi wa Dodoma. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji pamoja na ufanyaji biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Dodoma tunajivunia viwanda mbalimbali vya usindikaji ikiwemo Kiwanda cha Mafuta cha Mainland cha kusindika mafuta ya alizeti ambacho kimekuwa kikisindika mafuta tani 250 kwa siku. Hili siyo jambo dogo. Hii maana yake nini? Ni kwamba tukiwa na viwanda vingi zaidi itasaidia kutokuagiza mafuta kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mkoa wa Dodoma tunalima sana zao la karanga, na kwa sababu hiyo, nilikuwa natamani niendelee kuishauri Serikali kuona namna bora ya kuboresha zile mbegu za karanga ili tuweze kuzalisha karanga nyingi na hatimaye tuweze kupata viwanda vya kusindika mafuta ya karanga, nayo pia itasaidia katika kuhakikisha upungufu wa mafuta unapungua nchini badala ya kutegemea kuagiza kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, pia tuna viwanda vya madini ya shaba ambayo pia inaongeza thamani. Pia ukitaka viatu Dodoma, tuna viwanda. Tuna kiwanda cha Jin’kui ambacho kiko kule Zuzu.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, mjue kwamba Dodoma sasa hivi ina viwanda vya kutosha. Ukweli ni kwamba, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameufanyia mambo mengi kabisa Mkoa wa Dodoma, na ninaamini na sisi hatutamwangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka kuzungumzia ni kuhusiana na mapato ya ndani, kwamba, katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri amezungumza kwamba, mapato ya ndani yamepanda kutoka shilingi trilioni 20.95 mwaka 2020/2021 hadi shilingi trilioni 29.83. Hili siyo jambo dogo. Kwa hiyo, tuendelee tu kuiomba Wizara iendelee kuhamasisha wananchi waweze kudai risiti na wafanyabiashara waweze kutoa risiti ili kusudi tuweze kupata mapato ya kutosha na hatimaye kodi hii itumike kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, badala ya kutegemea wafadhili au kutegemea ufadhili kutoka nje ambapo mwisho wa siku wakiamua kukata ufadhili wao, inakuwa ni mtihani kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo, naomba niendelee kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Dodoma kwa kunichagua mimi kuwa mwakilishi wao hapa Bungeni. Pia, naomba niwashukuru na waume zao, kwa sababu kama hao waume zao wasingewaruhusu kuja kunichagua, maana yake nisingepata nafasi hii. Kwa hiyo, naomba niwashukuru wote na nitaendelea kuwasemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba tena niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wote kwa kazi nzuri sana ambayo wanaifanya. Hakika mwenye macho haambiwi tazama. Sisi wananchi wa Dodoma tunamwahidi, sisi tuna deni na Waswahili wanasema, “dawa ya deni ni kulipa,” na deni hilo tutalipa mwezi Oktoba kwa kumpa kura za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipa fursa. Ninaunga mkono hoja. (Makofi)