Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya Bajeti Kuu ya ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Waziri wa Wizara ya Fedha, na pia Wizara ya Mipango kwa mwaka huu 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kujiunga na wachangiaji wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha hapa, nina afya nzuri baada ya miaka mitano kutumikia Bunge hili na kuwatumikia waliotupigia kura kutuleta humu Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na kutoa shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mambo mengi aliyotufanyia. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwetu Jimbo la Uyui tunamwona kila siku kwa alama alizoziweka. Naweza kuzitaja hapa alama hizo ambazo pia wenzangu mkumbuke kuhusu pongezi hizi tunazozitoa kwa Mheshimiwa Rais. Kwanza, ni afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipoanza, hatukuwa hata na kituo kimoja cha afya, tunamaliza na vituo vinne vya afya katika Jimbo langu, lakini hatukuwa na hospitali ya Wilaya; Mama Samia ametujengea hospitali mpya ya Wilaya, hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumejenga zahanati nane mpya katika kipindi cha uongozi wa Mama Samia Suluhu Hassan. Haya siyo mambo madogo kwa Wanauyui. Kuhusu maji, Jimbo la Tabora Kaskazini zamani, siku hizi linaitwa Uyui, lina vijiji 58 vinatumia maji ya Ziwa Victoria, lakini tuna vijiji 98, na vijiji 71 vina maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa miji 28 kujengwa, maji yakienda Urambo yatatitirika maji katika Jimbo la Uyui na hivyo vijiji zaidi 72 kwa ujumla vitapata maji, na hii itakuwa zaidi ya 89% ya vijiji vyote kupata maji katika Jimbo la Tabora Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, tulipoanza kulikuwa na Kata zaidi ya 10 hazina sekondari, leo Kata zote 19 za Jimbo la Tabora Kaskazini zamani, siku hizi Jimbo la Uyui, zina sekondari na nina sekondari moja imebaki ya ziada naipeleka katika Kata ya Mabama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumejengewa Kituo cha VETA ambacho hakikuwepo. Tumejengewa shule za upili wa juu, yaani form five na form six tatu, na tumejengewa shule za msingi moja lakini tumekarabati shule nyingi, madarasa mengi, tuna madarasa mengi sasa kuliko idadi ya wanafunzi. Tuna tatizo dogo tu la madawati ambalo tumejitahidi kuyajengea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la nyumba ambalo nililisemea ndani ya Bunge, Serikali inisaidie kujenga nyumba kwenye bajeti inayokuja, nimeziona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umeme. Jimbo la Uyui vijiji vyote 98 vina umeme, na vitongoji 15 vina umeme; na juzi Naibu Waziri hapa amenipa orodha ya vitongoji 86, vingine vitapata umeme katika Jimbo la Tabora Uyui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, kulikuwa kuna matatizo ya ruzuku. Tuna ruzuku ya mbolea, na mbolea ya ruzuku. Ruzuku ya mbolea ilikuwa ya msimu uliopita. Serikali ya Mama Samia ilijitolea kuwalipa wananchi walionunua pembejeo kwa bei kamili, akawalipa ruzuku na tumeanza kulipa. Wamebakia watu wachache ambao hawajalipwa, lakini tunaendelea kulipa. Mwaka huu pembejeo zote zinanunuliwa kwa bei nusu. Serikali imelipa nusu, pongezi sana kwa Mheshimiwa Mama Samia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tumbaku, Jimbo la Tabora Uyui huwezi kuongelea chochote kuhusu biashara bila kutaja neno la tumbaku ambalo Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara analipiga vita; lakini tumbaku tumeilima miaka mingi na ni zao la biashara kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulianza na matatizo makubwa sana miaka mitano iliyopita. Tulikuwa hatuna wanunuzi, leo tuna wanunuzi 12 wa tumbaku. Ilikuwa huwezi kulima tumbaku mpaka upewe mgao. Sasa tunalima tumbaku kwa nguvu yetu. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri Bashe na hongera sana kwa Mama Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utawala bora. Halmashauri ya Uyui ilikuwa haina majengo, tumejengewa majengo mapya pamoja na ukumbi mpya; pia tunajengewa Mahakama. Kwa muda huu wa Mama Samia Suluhu Hassan, tunampongeza sana na tunamshukuru sana. Pamoja na ukumbi huo, mahakama inajengwa pale Uyui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia iko miradi ya Kitaifa ambayo inatugusa moja kwa moja, kama Bwawa la Kufua Umeme kule Mwalimu Nyerere. Bwawa lile linatoa umeme ambao unafika mpaka vijijini kwetu. Bila bwawa hilo, umeme usingewaka vijijini, na umeme wa REA ungekuwa hadhithi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, uko mradi wa reli ya SGR ambao tunatoka sasa Dodoma saa tatu, tutaenda Tabora kwa saa mbili au saa moja na nusu. Hii tuna imani kwamba, likishaisha mradi huu wa SGR, Tabora itanufaika ikiwemo Jimbo la Uyui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia liko daraja la Kigongo Busisi ambalo limefunguliwa jana. Daraja lile ingawa lipo pembeni kwa kanda ya Ziwa, litaingiza fedha, lakini fedha zile zinakwenda centralized kule Benki Kuu na hiyo itatusaidia sisi kupata mgao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bajeti ya mwaka huu, kwa sababu tunaiongelea, mimi ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Mheshimiwa Kitila na Naibu Mawaziri wote wawili kwa kazi nzuri waliyoifanya kuandaa bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni ya watu, na kama utaona huko mbele, kuhusu mpango wa kumalizia miradi ambayo ilikuwa imebakia mwaka 2024, na miradi ambayo ilitoka huko nyuma, tunampongeza sana Mama Samia kujiandaa pia kutoa ahadi alipoingia madarakani kwamba atamalizia miradi hii, watu hawakuamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza sana Mama Samia, miradi moja moja inakamilika. Bwawa la Mwalimu Nyerere limekamilika, Daraja la Busisi limekamilika na reli ya kati inaenda vizuri. Tunampongeza sana kwa kutimiza ahadi hiyo. Ni utu kutimiza ahadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR, Daraja la Busisi nimesema, lakini kwenye afya amefanya vizuri sana. Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi nzuri sana ya kujenga vituo vya afya, hospitali, pia vifaa vya tiba vimenunuliwa vingi. Tumeendelea kupata elimu bure, REA imeendelea na barabara zimeendelea kujengwa. Hizi zilikuwa ni ahadi za mwanzo za Mama Samia Suluhu Hassan ambazo amezitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kuwasahau watu hawa ambao nimewataja; Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Kitila, bajeti hii ni nzuri. Ngoja niyaseme yale ambayo yametugusa Wanauyui moja kwa moja. Amesamehe kodi ya ongezeko la thamani, viuatilifu vya dawa za mashambani za wakulima, pongezi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amesamehe pia VAT kwa ununuzi wa bima, amesamehe pia VAT kwa mafuta yanayotengenezwa hapa nchini, amesamehe VAT kwenye lami ili tujenge barabara, amesamehe VAT, magazeti sasa hawatakuwa wanazunguka meza kusomea magazeti mezani, watakuwa wananunua kwa sababu yamepungua bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Mheshimiwa Rais amesamehe VAT kwenye matanki ya mitungi ya gesi tunayopikia majumbani. Mimi nimekuwa mpenzi wa wazo la Mheshimiwa Rais la kupeleka nishati safi, nimekuwa nagawa mitungi ya gesi bure katika Jimbo langu na majiko; na kwa kupunguza bei, nitayagawa mengi zaidi. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Mama Samia Suluhu Hassan, kwani jambo la kupeleka nishati vijijini lilikuwa na kasoro kubwa sana kwetu. Watu wanakuwa na macho mekundu wanaambiwa wachawi, halafu wanauawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imegusa mpaka bodaboda, imegusa mpaka bajaji. Hii ndiyo bajeti ya watu, bajeti ya wananchi, tunaita sisi bajeti ya wananzengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina salamu kwa wananchi wa Uyui waendelee kuniamini, tuliyoyafanya mengi sana wameyaona, lakini yako mengi ambayo tumeyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kuhusu mikataba ya wakandarasi. Tuna mikataba ya wakandarasi wa hapa nchini wazawa na mikataba ya wakandarasi wa nje.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu unisikilize. Sisi wakandarasi wa ndani tukifanya kazi kama wakandarasi, tusipolipwa tunangojea mwaka, miaka miwili mpaka mali zetu tulizoweka benki zinachukuliwa. Tukilipwa hatutakiwi kuongeza riba yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi mzawa akiweka riba yoyote kwenye mkataba wake, anakuwa black listed, hapati tena kazi, lakini wenzetu wakandarasi wa nje wakichelewesha malipo yao, wanawekewa riba, wanalipwa na riba. Kwa nini tusifanye mikataba iwe sawa kunyanyua wazawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo muhimu sana. Kama kweli wewe ni mzalendo, ni ndugu yangu, na unatupenda sisi ndugu zako wazawa, tusaidieni wakandarasi wa Tanzania tuweze kulipwa kwa wakati unaofaa, pia kama tutacheleweshewa malipo na sisi tulipwe hata kidogo kupunguza gharama ya mabenki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko pia suala la kupata mapato mengi kutoka kwenye makampuni ya ulinzi. Makampuni ya ulinzi binafsi hapa nchini hayana sheria na hayana kanuni. Matokeo yake hayajulikani mapato yake. Ningeshauri sheria ile ya sekta ya ulinzi binafsi, iletwe Bungeni hapa; niliiandika mimi kama Muswada binafsi, lakini ulichukuliwa na Serikali kwamba utaletwa na Wizara ya Mambo ya Ndani. Hiyo sheria haijaletwa mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ile itatusaidia kupata mapato, kwa sababu makampuni yanajulikana. Pia kutakuwa na mamlaka ya kuongoza makampuni haya. Sasa hivi hayapati kazi kwenye Kimataifa kwa sababu hayana classification. Mamlaka hii ya sekta binafsi ya ulinzi itayapanga makampuni haya kwa mpango wa madaraja, na italeta faida nyingi kupata mapato ya Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushuru sana kwa muda wako, ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Athuman Almas Maige kwa mchango wako.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.