Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia leo Bajeti Kuu ya Serikali. Awali ya yote, ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa maeneo makubwa mawili. Kwanza, kunijalia afya na uzima katika kipindi cha miaka mitano nikiwatumikia akina mama wa Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ninamshukuru Mungu kwa kuijalia Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mafanikio makubwa ndani ya miaka mitan,o jambo ambalo kwa kweli linatupa ufahari na tunakwenda kwenye uchaguzi tukiwa na amani na tutatembea kifua mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwanza kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan kwa mambo makubwa aliyoyafanya katika Mkoa wa Tanga. Kusema kweli ni katika kipindi cha miaka minne ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mikopo ya akina mama, huduma za jamii, huduma za maji, huduma za afya, huduma za elimu zimeboreka na zimetoka kwa kiwango ambacho kwa kweli Watanzania wanaoishi katika Mkoa wa Tanga ni mashahidi mambo yanakwenda vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kumshukuru na kumpongeza sana Waziri wetu wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amekuwa Waziri wa Fedha kwa miaka mitano mfululizo. Hili jambo siyo jambo dogo, ameaminika, amefanya kazi nzuri. Mama yetu ameona ameweza kumsadia na ndio maana hakumhamisha, hakumwondoa, amempa Wizara ya Fedha kwa miaka mitano mfululizo. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu hongera sana, Mwenyezi Mungu akubariki zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Msaidizi wake Mheshimiwa Chande, Naibu Waziri, kwa kweli ni watu waunguana sana. Naibu Waziri ni msikivu, anatusikiliza sana humu ndani, anatusaidia mambo mengi. Kwa hiyo, kwa kweli Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya kazi nzuri ya kuunganisha watu wawili kuwaweka katika Wizara hii ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Mipango na Naibu wake Mheshimiwa Nyongo. Hawa wawili walikuwa wenyeviti wangu wa Kamati wakati naingia humu Bungeni, na Mheshimiwa Mkumbo ameniachia Uenyekiti wa Kamati baada ya yeye kuteuliwa kuwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni watu ambao nawafahamu uwezo wao, ukarimu wao, weledi wao, wamekuwa ni washauri wakubwa hata baada ya wao kuwa Mawaziri, bado wameendelea kuishauri Kamati yetu ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuendelea kufanya vizuri. Nawashukuru na ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitimisha Bunge la Kumi na Mbili na inawezekana mchango wangu ukawa ni mchango wa kuhitimisha Bunge kwa upande wangu. Nitumie fursa hii kwanza kuwashukuru sana akinamama wa Mkoa wa Tanga. Walifanya maamuzi sahihi kunileta mimi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamefanya kazi nzuri kwa ushirikiano na mimi kutekeleza mambo mbalimbali katika Mkoa wetu. Tumeshirikiana nao, tumefanya mambo mengi, tumefanya shughuli nyingi na hivi karibuni nimepita huko kwa ajili ya kufanya ziara katika wilaya zote tisa za Mkoa wa Tanga. Wakinamama wamenifanyia maombi, dua, na matambiko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni ishara kwamba bado wanatamani kuendelea kuwa na mimi binti yao Husna Juma Sekiboko kwenye Mkoa wa Tanga. Ninawashukuru na ninawaomba waendelee kuwa na moyo huohuo. Mitano ijayo tutafanya mambo kwa 5G kama ambavyo tumekubaliana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya salamu hizo sasa nijikite kwenye Bajeti ya Serikali. Kwanza nianzie na pongezi kwenye Bajeti ya Serikali ambayo nimeisoma; 18% ya Bajeti ya Serikali imekwenda kwenye Sekta ya Elimu. Hii ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba inanyanyua viwango vya elimu nchini. Pia, inatoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kuweza kupata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niseme kwamba bajeti ya kimataifa kwa viwango vya kimataifa tunatakiwa kila mwaka Serikali itenge 20% ya bajeti yake kuu ya Serikali kwenda kwenda kwenye elimu. Sisi tupo kwenye 18%; ni asilimia nzuri, kubwa na tunadhamiria kwenda kwenye viwango vya kimataifa. Tukiendelea kuongeza Bajeti ya Elimu kuanzia Elimu ya Msingi, Elimu Sekondari mpaka Elimu ya Vyuo Vikuu maana yake kwa miaka michache ijayo Tanzania itakuwa imefanya mapinduzi makubwa sana ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linaakisi maboresho ya elimu yanayofanyika kwenye elimu ya msingi na elimu ya sekondari. Tumefanya mabadiliko makubwa kwenye mitaala na Sera yetu ya Elimu. Kwa kweli kwa miaka michache ijayo tutaanza kunufaika na mabadilko haya. Binafsi sina hofu na wasiwasi na utekelezaji wa mitaala mipya. Ninaamini kwamba fedha zikiendelea kutoka kama ambavyo bajeti imepangwa vizuri, basi nchi yetu itaendelea kunufaika katika eneo hilo na hakika tutakwenda kwenye viwango vya elimu vile ambavyo tunavitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu dogo ambalo leo nilitamani kulitolea ushauri ni Elimu ya Juu (Elimu ya Vyuo Vikuu). Tumejenga vyuo vingi vizuri Tanzania vya binafsi na vya umma lakini tuna changamoto kubwa kwenye vyuo vyetu. Changamoto yenyewe ni kuhusiana na mitaala yetu ya elimu ya juu. Bado tunazalisha wanafunzi vyuo vingi kwa kutamani kupata ada kwa maana ya kutafuta fedha kufanya biashara, lakini bado hatujajikita katika kuzalisha wanafunzi au wahitimu kulingana na uhitaji wa changamoto zilizopo kwenye jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme ili twende na elimu ambayo inakwenda kunufaisha umma wa Watanzania, ili kupunguza ombwe hili la watoto wengi kuhitimu vyuo vikuu na kukosa ajira, ni lazima vyuo vyetu vya public na private viamue kulichukua suala la ajira kuwa ni jukumu la vyuo kuhakikisha kwamba kila chuo kinapozalisha watoto kinahakikisha kimewaandalia soko, kimewa-connect, kimewaunganisha na viwanda, taasisi na masoko ya ajira. Hili litatusaidia kupunguza ombwe kubwa la kukosa ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetembelea nchi kama Morocco. Morocco wanafunzi wao wanaozalishwa kwenye vyuo, kila chuo kimekuwa tasked kwamba 60% ya watoto wanaohitimu kwenye chuo hiko lazima waunganishwe na masoko ya ajira moja kwa moja. Wao wametoka nje ya boksi wanawaunganisha na masoko Ujerumani, Uingereza na Ufaransa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi kabla hajahitimu shahada yake tayari ameshaunganishwa wapi anakwenda kufanya kazi. Sisi hili Tanzania bado hatulifanyi kwa sababu vyuo vyetu vimejikita katika kutafuta ada zaidi. Utakuta hata kozi zinazotolewa sehemu kubwa wanafundisha sociology na education ambayo pengine hata kwenye kuajiri wapo walimu wengi mtaani bado hawajapata ajira. Wanafundisha kozi ambazo ni rahisi kupata wanafunzi ili waendelee kukusanya ada, lakini wanasahau kuwaunganisha hawa wanafunzi na masoko ya ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu; mitaala yetu ya Vyuo Vikuu inavyoandaliwa taasisi zinazoajiri zishirikishwe, ili ziweze kutoa qualities (vile vitu ambavyo wanavihitaji kwa mhitimu) ili mhitimu anavyomaliza masomo awe moja kwa moja anakwenda kwenye eneo ambalo anategemewa kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ufundishaji na utoaji wa kozi hizo ni vizuri vilevile kuwashirikisha waajiri, wahitimu wetu wakiunganishwa moja kwa moja wakati wa masomo na baada ya masomo na masoko ya ajira maana yake tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa ombwe hili la ukosefu wa ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu yetu lazima iwe ya kimataifa. Ni lazima tu-internationalize elimu yetu. Tukiweka elimu ya kimataifa maana yake hatutapambania tu nafasi za ajira zilizopo nchini bali tutaendelea kunufaika na nafasi za ajira ambazo zipo nje ya mipaka yetu. Leo tumeona VETA wameanza, wanaanza kuzalisha wachimbaji wa madini wanakwenda nje ya nchi. Sasa, tukienda kwenye vyuo vyote vya private na public (umma na binafsi) wakazalisha watoto kwa njia hiyo, maana yake mwisho wa siku baada ya miaka kadhaa pengine nchi yetu sasa tutakuwa tunaimba wimbo tofauti wa ukosefu wa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwenye simu za Waheshimiwa Wabunge hapa kila mzazi analalamika mtoto wake aajiriwe, lakini chuo kimemzalisha na hakihusiki. Baada ya mtoto kuhitimu chuo kimenawa mikono hakihusiki na huyo mtoto anakwenda wapi? Sasa ni lazima hivi vyuo viunganishwe vipewe jukumu la kuhakiksha kwamba, wahitimu wao wana-quality ya kuliwa na soko gani? Baada ya watoto kuhitimu wanakwenda kumezwa kwenye soko lipi la ajira?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatusaidia kuondoa kozi zile ambazo hazina ajira lakini vyuo viweze kuzalisha kozi ambazo zinaandaa wanafunzi moja kwa moja kwenda kwenye soko la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kusema hivi. Wakati tunaingia hapa 2021, moja ya kelele ambazo mimi binafsi nimepiga sana ni kuhakikisha kwamba Serikali inafanya mabadiliko katika mitaala ya elimu iweze kuajiri na watoto waweze kujiajiri. Leo tumeshapata mitaala mipya (nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan) ambayo watoto wanakuja na kozi tofauti kulingana na vipaji vyao kuanzia Shule ya Msingi mpaka Shule za Sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa bajeti zetu huko mbele tunapokwenda lazima tujikite sasa kwa hawa ambao wamekuja na elimu ya ufundi, amali, music, michezo na kadhalika; baada ya kuhitimu elimu ya sekondari maandalizi ya wao kwenda elimu ya juu yakoje? Ni vyuo vyetu hivi sasa vianze kujibadilisha mapema kabla hatujatengeneza huo msongamano wa wanafunzi ambao wamehitimu wakakosa nafasi ya kwenda kusoma kwenye elimu ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nikushukuru sana wewe binafsi, niushukuru Uongozi wa Bunge, nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu na Serikali nzima pamoja na Mawaziri wote kwa ushirikiano ambao tumepata katika Bunge hili kwa miaka mitano. Tunaomba Mwenyezi Mungu kwa kweli atusaidie turejee tuendelee kufanya kazi hii ya wananchi na Tanzania ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa njema na kuwa Taifa lenye ustawi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson na uongozi wote wa Bunge. Mwenyezi Mungu awabariki sana, ahsanteni sana. (Makofi)