Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii adhimu na adimu ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya bajeti ya mwisho katika kipindi chetu cha kuhudumu katika Bunge hili. Ninamshukuru Mungu kwa neema ya uzima aliyonijaalia mpaka leo nipo imara na nipo tayari kwa mitano tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nianze kwa dhati kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Jemedari Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kweli amesimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na nchi yetu imeendelea kupaa kimaendeleo katika ramani ya dunia. Rais Dkt. Samia kwa kweli anastahili maua yote. Hakuna wa kumfikia; kwa hiyo, mitano tena inamstahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza vilevile Makamu wa Rais Dkt. Mpango kwa namna anavyomsaidia Mheshimiwa Rais katika majukumu yake. Nikiendelea ninampongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu Dkt. Doto Biteko. Ninawapongeza sana Mawaziri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande na watendaji wote wa Wizara hii kwa jinsi wanavyofanya kazi iliyotukuka ya kuisaidia Wizara ya Fedha ikaweka katika medali hii iliyokuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee ninaomba nimpongeze sana Spika wetu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ambaye ni Rais wa Mabunge ya Dunia kwa jinsi alivyotuendesha katika majukumu yetu kwa miaka mitano yote iliyopita kwa umahiri na uhodari wa pekee. Mheshimiwa Dkt. Tulia anaweza na anaweza kabisa. Niwaombe tu wananchi wa Uyole waitunze tunu hii na kuipatia stahiki yake inapofika mwezi Oktoba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Naibu Spika Comrade Zungu na yeye kwa jinsi alivyosaidiana na Spika. Ninawapongeza Wenyeviti wote; wamefanya kazi nzuri sana iliyotukuka kutuongoza sisi katika Bunge hili kipindi chote tumekuwa na nyie. Ninawashukuru na kuwapongeza Wabunge wenzangu wote kwa jinsi tulivyoshirikiana na insha Allah kwa uwezo wa Mungu, sote tutarudi tena hapa kwa kasi kubwa zaidi tuendeleze yale ambayo yalikuwa labda yamebaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kutoa shukrani pia kwa watu wangu wa Mkoa wa Mjini ambao kwa mamlaka yao waliyokuwa nayo ndiyo wamenileta hapa kuwa Mbunge wa Mkoa wa Mjini, kwa maarufu wananiita Asha Mshua. Nimekuja hapa kutumika, wenyewe wameniona nikiwa na magongo matatu, gongo moja, lakini sikurudi nyuma, uongo kweli? Kwa hivyo, watu wangu ninasema ahsanteni sana na ninaamini watanipatia tena nafasi hiyo ya kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hii bajeti kusema kweli bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 imeonesha dira ya kujinasua kiuchumi na kuelekea kwenye kujitegemea asilimia kama nchi. Pamoja na kuwa ni bajeti ya maono pia imeonesha dhamira ya dhati kupunguza utegemezi wa misaada ya kigeni. Pia, imetoa nafasi kwa matumizi ya kilimo hai, kuelekeza ukombozi katika uagiziaji wa mbolea, kemikali na viuatilifu sumu kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo shida kutengeneza viuatilifu salama; ni kujiamini na kulifanya kazi suala hili. Kilimo chetu ambacho ndio uti wa mgongo kinakwenda kupaa, ili mradi tukiongeza nguvu katika kuhimiza kilimo cha style hii ya kilimo hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti pia imegusia nchi kutengeneza wenyewe dawa au kununua kwa mapato yetu ya ndani. Watanzania tuwatibie wagonjwa wetu badala ya kusubiri. Kwa mara ya kwanza Serikali imeondosha utegemezi kwa misaada ya kigeni. Mfano, Serikali kujitolea kununua dawa za ARV ni jambo la ukombozi mkubwa sana na limeonesha ukomavu wa Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii imejikita sana katika kukamilisha miradi elekezi na kuimarisha rasilimali yetu katika sekta za kijamii. Mfano, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo. Jambo zuri kabisa na la muhimu nikwambie Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ni hili la kuahidi hapa Bungeni kwamba Uchaguzi Mkuu unakwenda kugharamiwa na sisi wenyewe kwa fedha zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia katika hatua hizi juzi Daraja la Kigongo – Busisi (Daraja la JPM), limezinduliwa na mwenyewe Mama Samia. Huu ni ukombozi mkubwa sana wa miradi mikubwa kama hii ambayo tunaahidi tunakwenda kuimalizia. Hii inasaidia kufanya urahisi katika maeneo yale na kwa hivyo kunyanyua kuichumi na kuwaondolea kero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine zuri sana ambalo Wizara ya Fedha wamefanya ni kule kuchambua na kuimarisha relation baina ya TRA na wafanyabiashara na kuwaondolea ile bughudha ya kukamatwa au kufukuzwa ila kuwaongezea elimu ambayo inawapelekea wao watalipa kodi kwa hiyari. Kwa hivyo, kodi nyingi itakwenda kupatikana na ni wajibu kulipa kodi kwa sababu kodi ndio misngi wa maendeleo. Hao wote tunawaona wameendelea, wanalipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa ninavyofahamu mimi, kule ukikwepa kodi adhabu yake inakuwa kubwa unaweza hata ukafungwa. Kwa hivyo, hapa TRA na wenzetu watachukua lugha laini watubembeleze mpaka tufahamu umuhimu wa kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo ambalo linaikumba hii Wizara ya Fedha. Ninataka ni-quote agizo fulani hapa kwamba, “wapo watu wanadai fedha kwa miaka mingi na hawalipwi mpaka wengine wamekufa”. Ninashukuru kwamba tatizo hilo lilikuwepo kwa wateja wa FBME lakini wameanza kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo pia wafanyakazi wanadai haki zao za msingi kutoka kwa Mwajiri TTCL. Wafanyakazi 283 tangu 2018 ambapo wafanyakazi hawa kiongozi wao ni Fidelis Msamila na wenzake hao 283. Hawa watu baadhi yao wengine hata wameshafariki na ni-quote reference ya madai yao; “CMA/BSM/ILA/R.592/2023”. Hawa watu wanadai fedha zao; hebu Mheshimiwa Waziri akaangalie. Bajeti yetu nzuri namna hii kwa nini watu wengine waendelee kuteseka? Hebu kafanye uchunguzi hawa watu walipwe, tusitie doa bajeti yetu ambayo ni nzuri kupita kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miradi, sina cha kuongeza sana. Ninaridhika na speed inayokwenda na kwa maana hiyo ninasema kwamba kwa kweli mitano tena ndio inamstahili Mama Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wote. Kwa kweli Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amefanya kazi nzuri ya kuhudumu bila kutetereshwa kipindi chote kile; wewe my boy you are really my son. I admire and appreciate you, and I love you. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwamba kuna maboresho katika mifumo ya kodi na ku-harmonize mifumo ya kodi. Tumeona hilo ni jambo linakwenda kusaidia kwa hiyo kutakuwa hakuna ubabaishaji. Kwa hivyo, niseme kwamba kwa kweli kwa hakika hasa hii bajeti yetu imetengenezeka vizuri sana. Niombe tu kwamba tuendelee kuunga mkono Serikali yetu, yale ambayo hayajakamilika tuweze kuyamaliza na tukumbushane wajibu wa kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema ahsanteni sana. Wote wamenipenda sana, wameniuguza sana, mpaka wakanipa ile tittle kwamba, mimi Miss Bunge. Ninasema ahsanteni sana, ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)