Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kavejuru Eliadory Felix

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi hii ambayo umenipatia. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na nchi kwa zawadi ya uhai. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutubariki sisi sote kuwepo mpaka kwenye hii bajeti ya mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi ya pekee kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya pamoja na Makamu wake wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, kwa shughuli kubwa kwa ujenzi wa Taifa letu na Taifa letu linasonga mbele. Pili, ninawashukuru na ninawapongeza Mawaziri; Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Mwalimu Chande, kwa mafanikio na miradi mikubwa ambayo tunaona wamekuwa wakiitolea fedha na imetekelezwa majimboni. Wenye macho wote wameona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Waziri wa Mipango, Mheshimiwa Profesa Mkumbo, pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Nyongo. Hakika kwenye bajeti hii, kwenye Wizara hii, tumeona mipango mingi ambayo mmeiweka, kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mungu na ninawashukuru Wanabuhigwe, nimekuwa nao takribani kwa miaka mitano sasa. Tunajua wilaya yetu ilivyokuwa, katika uongozi huu wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaidiwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, ambaye ni Mwanabuhigwe, tumeona Buhigwe inayokimbia kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huduma za afya tumejengewa hospitali ya wilaya, imekamilika, ina vifaatiba, ina wataalam na tayari inatoa huduma. Tumepata vituo vya afya vinne; vitatu vimekwishakamilika na cha nne kinaendelea kujengwa. Serikali imetujengea zahanati zaidi ya 10 na shughuli bado inaendelea. Tunasema ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Buhigwe Oktoba tunatiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka kwenye afya; kwenye elimu tumeona shule mpya zimejengwa, shule za msingi na za sekondari. Kwenye bajeti hii nimeona kuna ujenzi wa Chuo cha TEHAMA ambacho kinaenda kujengwa katika Wilaya ya Buhigwe kwenye Kijiji cha Songambele. Buhigwe ikifika Oktoba tunatiki, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoka kwenye elimu; kwenye barabara tumeshuhudia, kupitia TARURA, tumechonga na kuimarisha barabara nyingi, vijiji vyetu sasa vinafikika na wakulima wanasafirisha mazao yao ya kilimo pasipo na shaka. Hongera sana Waziri wa Fedha, hongera sana Waziri wa Mipango, kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye huduma ya maji. Tuna vijiji 44 ambavyo hakuna hata kimoja ambacho kakijapata maji. Vyote vina miradi inayoendelea na mingine imekamilika. Tunasema ahsante sana. Wanabuhigwe ikifika Oktoba wako tayari kutiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwa wakulima. Tumeshuhudia pembejeo ambazo zimemwagika kwenye kilimo, tumepata mbolea ambayo tumekuwa tukiinunua ikiwa tayari Serikali imekwishalipia nusu ya gharama. Wakulima wa kahawa wamefaidika, wakulima wa tangawizi wamefaidika, wakulima wa mahindi wamefaidika, kila mkulima amefaidika. Kwa nini tusitiki? Oktoba tunatiki! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kwenye miradi ambayo sasa imeufungua Mkoa wetu wa Kigoma. Tumekuwa tukilalamika juu ya mkoa wetu kuunganishwa na mikoa mingine, tukitoka Kaskazini ya mkoa wetu kuelekea Mwanza tumepata barabara, ambayo imejengwa, Barabara ya kilometa 268 kutoka Kabingo katika Wilaya ya Kakonko, ya Mheshimiwa Kamamba ambaye ninaamini naye watamrudisha, imekuja Kibondo, imekuja Malagarasi, imekuja Kasulu, imekuja Manyovu. Nayo sasa imekamilika, wilaya zote hizo tunaenda kutiki mwezi Oktoba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi kutuunganisha na Tabora, tulikuwa tumebaki na kilometa 51 kutoka Malagarasi mpaka Uvinza. Sasahivi mkandarasi yuko pale, zimebaki tu kama kilometa 17, na hazifiki na kazi iko inaendelea. Sasa mkoa wetu umefunguka unaenda kuwa korido ya biashara, tunaenda kufanya biashara sasa na Burundi, Kongo, Zambia na nchi zote zinazopakana na sisi. Kigoma Oktoba tunatiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi tumeona ujenzi wa SGR ambao umeanza kutoka Tabora kwenda Kigoma, kilometa 506. Kama hiyo haitoshi kuna ujenzi wa reli ya kisasa, SGR, inayotoka Uvinza kwenda Msongati, kilometa 282. Wakandarasi wako site na reli hii inapita mpaka Jimbo la Buhigwe kwenye Kata ya Kajana na Kilelema. Kigoma mwezi Oktoba tunatiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, tunaona Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Kigoma mkandarasi yuko pale, majengo yako yanaota kama uyoga, uwanja unapanuliwa sambamba na mji ambao sasa uko chini ya Mheshimiwa Ng’enda Kilumbe. Lami iko inajengwa kila kona, ninaamini na Kigoma Mjini watatiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kuna ujenzi wa kiwanda cha meli na ukarabati wa meli. Kwenye bajeti hii tumeona fedha zinaenda kutolewa na tayari ukarabati wa meli umekwishaanza.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa. Wapi Taarifa?
Aah Mheshimiwa Jumanne Mtaturu.

TAARIFA

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajaribu kumpa Taarifa mchangiaji anayechangia vizuri, ndugu yangu Mheshimiwa Kavejuru kwamba, ukipewa mtihani ukafanya vizuri na ukapata matokeo lazima upate tiki. Kwa hiyo, ninakubaliana na yeye kwamba, tunatiki Oktoba itakapofika. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kavejuru, unaipokea Taarifa hiyo toka kwa Mheshimiwa Mtaturu?

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea hiyo Taarifa ya kaka yangu Mheshimiwa Mtaturu kwa mikono yote miwili. Mungu akubariki sana na wewe huko kwako wanatiki na wewe unarudi, Novemba tuko wote hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, upo ujenzi wa kiwanda cha meli. Zipo meli mbili, nne pale ziko zinajengwa, lakini ukarabati wa meli ambazo ni pendwa, MV Liemba na MV Mwongozo, tayari umeanza. Kwa hiyo, sasa wananchi wanaokaa kandokando ya Ziwa Tanganyika katika Mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na nchi jirani tukichukua Zambia, tuje na upande wa Kongo, Moba, Kalemie, Ubwari na Bujumbura, Kigoma wanaenda ku-enjoy. Muda si mrefu tutaenda kuongeza mapato na kuchechemua uchumi wa Kigoma kwa kupitia biashara kwa hiyo, Mwezi Oktaba, Kigoma inatiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa sababu kwa nini Kigoma tunaenda kutiki, kama shukrani yetu kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wake wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, ninarudi kwa wananchi wa Buhigwe. Ndugu zangu wananchi wa Buhigwe nimekuwa pamoja nanyi kwa unyenyekevu, tumefanya kazi wote kwa pamoja, wanaosafiri huwa wanaanza safari pamoja. Niko na nyie, tumelala pamoja, tumefanya kazi kwa pamoja, na wanaotafuta kuni ndiyo wanaoota moto pamoja. Ndugu zangu wakati umefika tena, wanasema chanda chema huwa kinatunzwa; anayefanya kitu kizuri huongezwa. Ninaomba waniongeze miaka mitano tena, nitaendelea kuwa mwaminifu mbele yao na mbele ya Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ninawashukuru viongozi wa ngazi ya wilaya, Mheshimiwa Kanali Michael Masala Justin Ngayalina, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kamati ya Ulinzi na Mkurugenzi Mbilinyi kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kusimamia miradi ambayo imeletwa na Serikali. Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Kigoma na Buhigwe Oktoba tunatiki. (Makofi)