Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Hotuba ya Bajeti iliyoletwa na Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Mipango na Uwekezaji. Mimi naungana na Wabunge wenzangu kwanza, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi na uhai, ametulinda sasa tunapokwenda kukamilisha miaka mitano. Kipekee ninamshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninaungana na Wabunge wenzangu kumshukuru sana kwa namna ambavyo ametuletea miradi mingi katika majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata bahati ya kuwa Mjumbe wa Kamati ya Tamisemi kwa kipindi chote cha miaka mitano kwa hiyo, nimezunguka sana kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo. Ukiangalia miradi mikubwa inayotekelezwa kwenye kila kona ya nchi yetu hakuna ubishi Mheshimiwa Rais anakwenda kupata kura za kishindo mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru pia, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Mawaziri wote. Wameendelea kunipa ushirikiano, kama Mbunge wa Jimbo la Nachingwea na kuhakikisha kwamba Nachingwea inaendelea kupiga hatua kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia, viongozi wangu wa chama, Wilaya ya Nachingwea na wana-CCM wenzangu wakiongozwa na Mwenyekiti wetu Mwalimu Longinus Nambole kwa namna walivyonipa ushirikiano. Ninawashukuru pia, wapigakura wote wa Jimbo la Nachingwea. Ninaendelea kuwashukuru viongozi wangu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Lindi wakiongozwa na Alhaji Hassan Jarufu, Mwenyekiti wetu bingwa, kwa namna walivyonipa ushirikiano, wakanifundisha na kunielekeza kuhakikisha kwamba, ninatimiza majukumu yangu ya Kibunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuishukuru familia yangu iliyonivumilia nyakati zote wakati ninatimiza majukumu yangu, ikiongozwa na mke wangu kipenzi Eva Bipaulo Komu. Wamefanya kazi kubwa ya kunivumilia, lakini pia, kuniombea na kuhakikisha kwamba, ninatimiza majukumu yangu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kujielekeza kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 ni ya viwango, ni bajeti ambayo inaendelea kujibu shida na matatizo ya nchi yetu. Ninaendelea kuunga mkono hoja hii maana unaweza ukahutubia sana halafu ukashindwa kuunga mkono hoja. Ninaunga mkono kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nachingwea kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna ambavyo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba anavyoitendea haki Wizara hii na tukienda kwa Mheshimiwa Profesa Mkumbo kwa namna ambavyo anaendelea kuweka mipango sawasawa kuhakikisha nchi yetu inakimbia kimaendeleo, pamoja na Manaibu wao na wataalam wote. Ni wazi kwamba, jambo hili ni kwa sababu ya kiutaratibu tu, lakini ilikuwa tayari tuwe tumeshamaliza na bajeti hii tumepitisha, ili kazi kubwa ambayo iko kwenye mipango iende ikatekelezwe. Tukisema Mheshimiwa Rais mitano tena, tunamaanisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa kwamba, nimezunguka maeneo mbalimbali nikiwa na Kamati ya TAMISEMI kukagua miradi ya maendeleo, sasa hapa nitajielekeza kidogo kwenye Jimbo langu la Nachingwea. Mwaka 2020, 2021 na 2025 tumepokea zaidi ya shilingi bilioni 101 katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Kiasi hiki cha fedha hakijawahi kupatikana kwa kipindi kama hiki tangu enzi za uhuru. Ninarudia tena, kiwango hiki cha shilingi bilioni 101 hakijawahi kupatikana kwenye Jimbo langu la Nachingwea kwa kipindi kama hiki tangia uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili sasa, tunamwambia Mheshimiwa Rais hana tatizo kule Nachingwea na sisi hatuna deni na yeye. Tumekubaliana na hii nasema kwa ujasiri, wananchi nimewatembelea nimewaaga ninakuja hapa kwenye Bunge la Bajeti na wakaniambia kaseme, sisi 2025 tunakwenda na Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatolea mfano tu kwenye eneo la elimu, hapa tumepata shilingi bilioni 5.9 tumejenga shule mpya za sekondari tano, za kisasa, nzuri kabisa. Hizi shule tulizoea kuona aidha vyuo au za misheni ambazo zilikuwa nzuri, leo tunashuhudia ni shule za sekondari ambazo zinamilikiwa na Serikali, nzuri, zikiwa kwenye viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tumepata shule mpya za kisasa za msingi tatu, hizi shule ni za mfano. Kwenye ziara yangu nilikwenda sehemu moja nikamkuta mama akanitolea ushahidi, saa tisa usiku mtoto anatamani kwenda shule, saa tisa usiku. Ni kwa nini anatamani kwenda shule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yaliyowekwa yanamfanya mtoto huyu apende kusoma. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii kubwa ambayo ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo la elimu bila ada, tumepokea zaidi ya shilingi bilioni saba. Hili ni jambo kubwa na hapa sasa imeendelea kutoa morali kwa wanafunzi na walimu kwa sababu, inajumuisha pia, fedha ya madaraka. Walimu wa Nachingwea sasa wana morali ya kufundisha na kazi hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata Shule ya VETA yenye thamani ya 1,400,000,000. Haya mambo tulikuwa tunayaona tu maeneo mengine, lakini leo shule hii mpya ya kisasa ya ufundi inajengwa na kazi hiyo inaendelea kwenye jimbo langu la Nachingwea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la afya tumepokea zaidi ya shilingi bilioni saba, eneo hili nitakwenda polepole kidogo. Wakati tunaingia mwaka wa fedha 2020/2021 tulikuwa na kituo cha afya kimoja, hiki ndicho kilikuwa kinafanya kazi na kulikuwa na kituo kingine cha pili ambacho kimsingi ilikuwa ni zahanati, lakini ilipewa hadhi ya kituo cha afya. Sasa ninapozungumza tunavyo vituo vya afya vizuri na bora, ambavyo vinatoa huduma zote sita. Maana yake ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia uhuru mpaka Mwaka wa Fedha 2020/2021 tulikuwa na kituo cha afya kimoja ambacho kilikuwa kinafanya kazi. Ongezeko la vituo vya afya vitano katika miaka minne na nusu, miaka mitano, hili ni jambo kubwa. Viko vituo vya afya vingine ambavyo vinaendelea na ujenzi na viko kwenye hatua mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la barabara, tumepokea zaidi ya shilingi bilioni saba. Kazi hiyo inaendelea, lakini hii haijumlishi barabara zingine ambazo zinaendelea kutekelezwa; kwa mfano ujenzi wa Barabara ya kutoka Ruangwa kuelekea Nachingwea kwa kiwango cha lami, mkandarasi yuko site na kazi hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la maji tumepokea zaidi ya 4,700,000,000 na hii haijumlishi Mradi mkubwa wa Maji kutoka Nyangao kwenda Nachingwea, ambao pia, unapeleka kwenda kulisha kwenye Jimbo la Ruangwa, zaidi ya shilingi bilioni 100. Hili ni jambo kubwa na huyo ndiye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye tunasema mwaka huu tunakwenda kumlipa wema kwa kumpa kura nyingi za ndiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nimeona Wabunge wenzangu wananiambia kwamba, kwao wataongoza kumpa kura za heshima, za ndiyo, Mheshimiwa Rais. Kule Nachingwea tumekubaliana tutampa kura nyingi za kishindo na tutaongoza kwenye majimbo yote Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la nishati. Wakati tunaingia mwaka wa fedha 2020/2021 vijiji 57 ndiyo vilikuwa na umeme na Nachingwea ina vijiji 127, vijiji 70 vilikuwa havina umeme. Sasa hivi ninavyozungumza vijiji vyote 127 vina umeme muda wote na kazi za wananchi za kujiletea maendeleo zinaendelea. Huyo ndiye Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo nako Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana na upo wimbo kule wenzetu tunaimba; ni kanuni tu vile haziruhusu, ningeunganisha hapo ungeuona huo wimbo ambao unamsifia Mheshimiwa Rais. Korosho ndiyo dhahabu ya Kusini. Rais amefanya uwekezaji mkubwa kwenye eneo hili na ametupa pembejeo bure kwa miaka minne yote mfululizo; hili ni jambo kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa sasa pia niende kidogo na Mheshimiwa dada yangu Dkt. Thea Ntara, alikuwa anasema kule Lindi sasa nyumba; nafikiri yeye alipita miaka ya zamani; nyumba zilizopo kule si dhaifu tena, kule wananchi sasa wamechangamka na maendeleo yanakwenda. Tunachokubaliana hapa ni kwamba maendeleo ni hatua. Wapo wengine bado wanaendelea, lakini watu wengine wamekwenda mbele sana. Kwa hiyo kazi kule inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea pia zaidi ya shilingi bilioni tatu na milioni 700 kwa ajili ya kujenga jengo la utawala, kazi hiyo inaendelea. Huyo ndiye Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo yule ambaye anasema kwamba tunakwenda na uchawa tu wa kusema mama Samia mitano tena; mama Samia amefanya. Ametekeleza na mengine ambayo hayakuahidiwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Ukiingia leo kwenye Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea, hospitali kongwe imefanyiwa ukarabati mkubwa, tumetumia zaidi ya shilingi milioni 900. Unakwenda majengo yameota, mapya, ICU mpya na ya kisasa; ndizo ICU zinazotumika ndugu zangu huko duniani, leo ICU ile ipo Nachingwea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujajenga ICU ili kuhakikisha kwamba watu wetu wanapata maradhi ya kwenda ICU, tunajenga ICU ili kuwa na utayari pindi yanapotokea maradhi ambayo yanahitaji mgonjwa kuwa na uangalizi maalum, tunampeleka kwenye hiki chumba. Huyo ndiye Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu; kwa wale waliotoka zamani Nachingwea leo wakiingia asifike usiku, vinginevyo basi awe na namba ya ndugu yake ili kuhakikisha kwamba anapata mawasiliano. Akifika mji unapendeza kwa mataa na barabara za lami zinaendelea. Kwa hiyo asije akashangaa shangaa akajikuta anapita wakati hapo ndio kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninaona umewasha microphone; wananchi wa Jimbo la Nachingwea, hawa ni watu wema sana, wamenipa ushirikiano kutimiza majukumu yangu ya Kibunge. Wapo wengine ambao wananiambia Mheshimiwa Mbunge, bado tunakuona una nguvu na ninawaambia Mwenyezi Mungu, akipenda wakati ukifika Chama changu Cha Mapinduzi kikinipa ridhaa nitarudi tena kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwatumikia wana Nachingwea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)