Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja mbili zilizopo mezani. Kwanza nianze kuunga mkono hoja zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kuiongoza nchi yetu vyema. Kwa kuwa Serikali ni ya Chama Cha Mapinduzi na yeye ndiye Mwenyekiti wetu; kwa kweli kwa namna ambavyo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa miaka hii minne imetekelezwa kwa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia kaka zangu Waheshimiwa Mawaziri wote; Mheshimiwa Kitila Mkumbo, kwa sababu yeye ndiye mkubwa, Mheshimiwa Mwigulu ni mdogo wake; lakini wote kwa kweli ni marafiki zangu, pamoja na Naibu Mawaziri wote kwa kazi njema wanayoifanya katika nchi yetu. Nimekuwa nikisema, kwamba anayefanya kazi njema amekuwa akifanya ibada. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu ataendelea kuwalipa na awaongoze katika majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja hizi zote mbili ninataka kusema kwamba imeonesha umahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa miaka minne ambayo ameiongoza nchi yetu. Nikinukuu kitabu cha Waziri wa Fedha, katika ule ukurasa wa 20 yeye amesema kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imekuwa ikitekeleza, ikiendelea na ile vita vya wale maadui watatu; ujinga, umaskini na maradhi. Ninataka niseme kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na huu mchakato wa vita ulianza tangu kipindi hiko, lakini kipindi hiki hii vita imepigwa kwa kishindo kikubwa sana, kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye eneo la ujinga kila Mbunge huku ndani amesema namna shule shikizi zilivyojengwa, shule za msingi, shule za sekondari pamoja na zile za chini na za A level. Vilevile vyuo vya kati, vyuo vya ufundi, VETA, vyuo vikuu na namna ambavyo mafanikio makubwa katika sekta ya elimu yamefanyika. Hapo ndipo tunasema kwamba kishindo kwenye hili eneo la huyu adui ujinga Dkt. Samia ametekeleza kwa kishindo kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa umaskini, kama ambavyo tunaona, pamoja na mambo mengine yote, lakini ninaangalia lile eneo la Watanzania walio wengi, wakulima, kwa kupeleka ruzuku ya mbolea; na kule kwetu tumesema viuatilifu; kwa namna ambavyo uzalishaji umeongezeka na kuongeza fedha za kigeni kwenye yale mazao ya kimkakati. Unaona kabisa kwamba hayo matokeo yamewafikia wananchi moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la maradhi, ukiacha zahanati zilizojengwa kila Mbunge hapa amekuwa akisema, pamoja hospitali za wilaya za kisasa, kama alivyosema Mbunge aliyomaliza kusema sasa hivi. Tumeona Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kujenga hospitali katika kila halmashauri. Hapo sasa tunaona kwamba kwa kweli amepunguza vifo vya watoto wachanga na akinamama wajawazito wakati wa kujifungua; na kwa ajili hii anatambulika duniani. Kwa hiyo ndiyo maana tunasema kwamba kwa hawa maadui watatu, pamoja na kwamba ilianza wakati ule, lakini katika kipindi hiki hawa maadui wamepigwa kweli kweli. Kama ni Nduli Idi Amin haya maadui matatu yamepigwa kuliko ilivyokuwa Nduli Idi Amin. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze sasa kwenye hizi hotuba zote mbili. Nikianza na baadhi ya maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha amesema, baadhi ya maeneo mahususi ya kipaumbele, ule ukurasa wa 71; yeye ametuambia kwamba moja wapo ni kuimarisha sekta za uzalishaji zenye matokeo chanya katika kukuza uchumi, katika kukuza uchumi. Hapa ninaomba nijielekeze kwenye mambo machache yafuatayo; hasa nikijielekeza katika Mkoa wa Mtwara. Ninaamini moja ya sekta ambayo imo na ambayo imewekewa kipaumbele ni miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninaomba sana na niishauri sana Serikali yangu sikivu. Reli ya Kusini, niliuliza swali hapa kwamba je, Serikali inafahamu nguvu ya uwepo wa reli ya Kusini? ikajibu imeshafanya tathmini na inafahamu na kwamba ina matokeo chanya mengi na hasa katika kuzingatia kwamba tutaunganisha na Liganga na Mchuchuma; lakini na zile fedha zilizotolewa na Serikali kwenye bandari yetu ya Mtwara.
Mhesimiwa Mwenyekiti, ninatambua, kwamba kwenye Ilani yetu ambayo tayari imeshatolewa tutaitumia 25 – 30 hii reli ya Kusini imeandikwa mara kadhaa. Nimpongeze sana Mwenyekiti wa mchakato ule wa Ilani, Profesa Kitila Mkumbo, kwamba hii ameitambua na hivyo Serikali imefanya tathmini na kuona matokeo ama matokeo chanya yatakayoletwa na reli ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu chake cha mpango ameandika kwa mistari miwili tu; kwamba Serikali inaendelea na mchakato wa ujenzi wa reli ya Kusini katika hataua za awali zile kilometa 1,000. Ombi langu hapa ni kwamba, badala ya kuendelea na ule mchakato wa PPP ninaomba Serikali kwa yale mataokeo chanya yatakayotokana na reli ya Kusini Serikali ione haja ya kujenga yenyewe; huyu mwekezaji aje kushughulika na mambo mengine, ikiwemo operations kama itaonekana inafaa. Kwa sababu tukisubiri PPP hii itachukua karne nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili naomba sana, wakati anataka mipango ya nchi yetu iendelee kama ilivyo na ili tuendelee kupata fedha zingine ili Watanzania tuendelee kuneemeka katika sekta zote, hasa sekta za huduma ya jamii ambayo kwenye vipaumbele ipo, reli ya Kusini ni muhimu sana ikazingatiwa na kujengwa na Serikali katika mipango ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninaomba katika hiyo hiyo miundombinu ni Mradi wa LNG. Ninataka niseme, wananchi wa Mtwara na Lindi wamekuwa na matumaini kwa muda mrefu. Sasa ninaomba haya matumaini kwa kipindi hiki yasiishie hewani. Ninaomba nitumie fursa hii kumpongeza sana mama yetu kipenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan; yeye alifufua majadiliano yale ya mkataba na ninaamini yanaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninaomba nishauri; ushauri wangu ni kwamba, ninaomba juhudi ziongezwe katika kutafuta gesi asilia na mafuta hasa Mtwara na Lindi. Siyo tu juhudi hizo zikiongezwa ziishie hapo, ninaomba juhudi hizo pia ziongezwe katika kusambaza gesi asilia katika taasisi na kwa wananchi. Kwa sasa taasisi zilizounganishwa ni chache, lakini na wananchi waliounganishwa; ninazungumzia hasa wananchi wale wa mahalia, yaani wa Mtwara na Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua huku Dar es salaam maeneo ya Masaki na Oyster Bay sawa wamepata lakini ni muhimu wananchi wa Mtwara wakayaona haya matunda kwa sababu mnakumbuka hii gesi huko nyuma ilituletea madhara. Kwa hiyo juhudi ziongezwe katika kusambaza gesi asilia kwa taasisi zilizopo Mtwara na Lindi lakini na wananchi, kama Wabunge wengine walivyosema; kuona namna hiyo ya kuharakisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo likifanyika na lile la kwanza likafanyika itakuwa imepelekea pia matokeo chanya. Ninaomba pia uhamasishaji ufanyike kwa namna yoyote ile kupitia Wizara, uhamasishaji ufanyike wa kuona namna ya kupata wawekezaji watakaotuwezesha kuwa na viwanda vile tulivyokuwa tunavitarajia. Tuliambiwa kutakuwa na viwanda vya mbolea, basi uhamasishaji huo uendelee kufanyika, viwanda vya mbolea na viwanda vingine vinavyotokana na gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona pwani ilivyo pale, pwani sasa ardhi inakwisha kwa ajili ya viwanda. Kwa hiyo ninaamini na uhamasishaji huu ukifanyika wawekezaji watakuja watajenga viwanda vinavyotokana na gesi asilia katika maeneo ya Mtwara na Lindi. Kwa sababu mnafahamu viwanda vya Korosho vimekufa. Hata hivyo nimpongeze pia Mheshimiwa Bashe kwa juhudi kubwa anayoifanya sasa ya kufufua na hasa kutuletea zile kongani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii malighafi ya gesi tunayo Mungu ametupa na wakati ndio sasa. Inawezekana huko mbele kutokana na teknolojia tukawa tunataka vitu vingine sasa vya kidijitali zaidi, inawezekana gesi ikapitwa na wakati. Hatutaki kufikia huko. Ninatamani sana kizazi hiki tulichopo humu ndani tukaona matokeo ya gesi ile asilia inayopatikana Mtwara na hasa katika kuitumia hiyo malighafi kama ambavyo tumekuwa tukiamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninaomba nishauri kwa Wizara ya Fedha; pamoja na mambo mengi yote ambayo kama nchi tunajua kwamba Mheshimiwa Mwigulu amekuwa akifanya vizuri, lakini ninamwomba sana, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa; zipo fedha kwenye maeneo mawili; ya kwanza ni fedha ya Mfuko wa Maji, tunajua inakwenda kwake, lakini ninaomba itoke kwa wakati ili na sisi watu wa Mtwara tunufaike nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hasa kilio changu kwenye maeneo mawili, ule Mradi wa Makonde ambao umetengewa shilingi bilioni 84.7 umekuwa ukisuasua. Nina uhakika hizi fedha za Mfuko wa Maji zikienda kwake zikaenda kwenye Mradi wa Makonde ina maana ile changamoto, ule mradi utatekelezwa kwa wakati; lakini hata ule Mradi wa Mto Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, nivumilie dakika moja. Fedha za export levy zinapokwenda Mfuko Mkuu tafadhari sana tunaomba zirudi ili zikaendeleze zao la korosho. Kwa sababu tunajua wao wanatupa hivyo viuatilifu, lakini mambo mengine kama vile utafiti, mbegu bora na mambo mengine hata yale maghala zitatusaidia sana kuhakikisha zao la korosho na dhahabu hiyo ya korosho itakuwa inatuletea fedha za kigeni kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninaomba niunge hoja mkono na niwapongeze sana Mawaziri kwa kazi nzuri, ahsante sana. (Makofi)