Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii kuu ya Serikali. Awali ya yote nipende kumshukuru sana Mungu wa mbingu na nchi, muweza wa yote ambaye ametukirimia na kutufanikisha kuwepo katika Bunge lako hili Tukufu. Pongezi zangu za pili ziende kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri sana ambayo anawafanyia Watanzania. Hakika amefanya kazi hii na kuzidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Mawaziri hawa wamefanya kazi nzuri. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, pamoja na msaidizi wake Hamad Hassan Chande na Mjumbe wa Kamati Kuu, Waziri wa Mipango Profesa Kitila Mkubo pamoja na Naibu wake Stanslaus Nyongo na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa; niwapongeze sana kwa kazi nzuri za kusimamia Wizara zao vizuri sana, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matunda haya tunayoyaona ni juhudi za Mheshimiwa Rais kwa kumshauri vyema, lakini pia kwa kusimamia Wizara zao vizuri; na ndiyo maana Taifa la Tanzania katika Afrika Mashariki na Kati ni Taifa ambalo kwa sasa ni la kuigwa na ni la mfano. Ndiyo maana hata jana tumeshuhudia Mheshimiwa Rais akifungua daraja katika historia ya nchi hii lenye kilometa tatu; na daraja hili halipo mahali popote katika nchi hizi za Afrika Mashariki na Kati isipokuwa hapa Tanzania. Hongera sana kwa Waheshimiwa Mawaziri, hongera sana kwa watendaji wote wa Serikali, hongereni sana Watanzania na hongera sana Waheshimiwa Wabunge kwa kupitisha bajeti za Serikali hata hii miradi ikaweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni bajeti yangu ya mwisho kuchangia katika Bunge hili. Nianze kuwashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Kwa kipindi chote ambacho nimekuwa Mbunge hapa tumeshirikiana vizuri sana na wamenishauri vyema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ukiwa kama Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo umekuwa Mwenyekiti wetu mzuri sana. Mheshimiwa Spika, amekuwa Mheshimiwa Spika wa viwango na amekuwa Mheshimiwa ambaye kwa kweli sisi Watanzania tunajivunia; pamoja na Naibu Spika, Wenyeviti wote wa Bunge, watendaji wote wa hapa Bungeni na wafanyakazi wengine wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa niipongeze Serikali kwa yote ambayo imefanya katika sekta nyingi kule jimboni kwangu. Wananchi wangu wa Jimbo la Busokelo kwa takribani miaka mitano wameshuhudia miujiza na maajabu ambayo yamefanywa ndani ya Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi. Hapo awali katika sekta ya afya tulikuwa na kituo kimoja tu cha afya. Hivi ninavyozungumza tuna vituo vipya vya afya vitano na vingine vitatu vinaendelea kujengwa. Zaidi ya yote tulikuwa na zahanati zisizozidi tano hivi ninavyozungumza katika kipindi cha miaka hii minne takribani mitano tuna zahanati 14 mpya na zote hizi zimetekelezeka chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ametujengea hospitali ya wilaya nzuri sana ambayo ina vitendea kazi vyote na huduma za upasuaji zinafanyika pale katika Halmashauri ya Busokelo. Zaidi ya yote ametufanyia kazi ya kuwa na jengo zuri bora la kisasa. Ninasema lile jengo la halmashauri linaweza likawa ndilo jengo la kwanza kwa hapa Tanzania maana lina vyumba zaidi ya 205.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni kazi kubwa na nzuri sana ambayo Mheshimiwa Rais wetu mpendwa ametufanyia sisi Wanabusokelo; na sisi tunasema ifikapo Oktoba ya mwaka huu panapo majaliwa tunatiki kwa mama, tunatiki kwa CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya elimu, hivi ninavyosema tuna shule mpya sita. Katika hizo shule sita, shule mbili ni za vipaji maalum, kwa maana kuna shule ya wasichana maalum na wavulana maalum, kwa maana ya Busokelo Boys na Busokelo Girls. Hizi ndizo shule pekee zinazofanya vizuri sana katika Halmashauri ya Busokelo na Wilaya ya Rungwe kwa ujumla na Mkoa wa Mbeya; zimefanyika kipindi cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mikakati yetu sasa tunataka tuwe top ten kitaifa. Kwa hiyo shule hizi ni kielelezo tosha kwamba elimu katika Jimbo la Busokelo imepaa sana na inafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la barabara; tumekuwa na barabara ambayo tangu enzi na enzi ilikuwa haina lami. Hivi ninavyosema tayari Mkandarasi yupo site. Barabara hii ya Katumba – Suma – Mwakaleli – Mbambo mpaka Tukuyu yenye kilometa zaidi ya 83; na tunamshukuru Sana Mheshimiwa Rais, tunamshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha, alikuja kule akiwa pamoja na Waziri wa Ujenzi wakati huo, waliona ile barabara; na hatimaye hivi ninavyosema anashuhudia. Wamenituma wananchi wangu wa Busokelo wanasema ya kwamba tunawashukuru sana tena sana. Barabara hii ni mkombozi mkubwa sana wa wananchi kule kwa sababu wanalima, wanafuga. Pia kuna viwanda vya gesi ya asilia kwa maana ya carbon dioxide gas, vyote vimefanyika katika kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais. (Makofi)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Festo Richard Sanga.

TAARIFA

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, nichukue nafasi kumpongeza Mheshimiwa Mbunge anachochangia barabara anayoisema ni barabara ambayo mimi nimesoma shule ya kidato cha tano na sita kwenye jimbo lake, lakini barabara hii inaenda kuunganisha hadi Makete. Kwa jitihada hizi ambazo Mbunge wa Busekelo amefanya, ninaona kabisa Wanabusekelo wakienda kumchangua tena kwa mwaka 2025. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Fredy, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, nimeipokea kwa mikono miwili, nami nimwombee kwa wananchi wa Makete ile barabara ile ya kilometa tisa ambayo alikuwa anazunguka zaidi ya kilometa 200 na kwa juhudi za mimi na yeye na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI nayo inafunguliwa. Kwa hiyo, wananchi wa Makete wamwone kwa jicho la karibu ili ifikapo Oktoba apate nafasi tena ya kurudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nizungumze pia suala zima la hizi barabara za mijini, kwa mfano pale Kandete Mjini kulikuwa hakuna lami, hivi sasa kuna lami na mataa yanawaka. Sisi kule tunasema ndiyo Dar es Salaam ya Busekelo kwa pale Kandete Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Lwangwa Mji ambapo ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri kulikuwa hamna lami, hivi sasa kuna lami na mataa yanawaka usiku na mchana, sisi ile tunasema ndiyo Dar es Salaam ya Busekelo. Sasa tuseme nini zaidi ya kumwombea Mheshimiwa Rais kusema mitano tena inamhusu na tumwombee afya njema ili ifikapo Oktoba sisi Wanabusekelo tutatiki kwa CCM na viongozi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya maji, kulikuwa kuna changamoto kubwa sana katika suala zima la maji Kandete Mjini, Lwangwa Mjini na maeneo mengine. Hivi sasa ninavyosema ambayo ndiyo Dar es Salaam ya Busekelo maji yanatoka masaa 24, imefanyika kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ukienda Lwangwa hivyo hivyo na maeneo mengine mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna vijiji 56 havina umeme lakini sasa vijiji vyote 56 vina umeme, tunazungumza habari za vitongoji sasa. Kwa hiyo, ni habari njema kwa Wanabusekelo wote kwamba Mheshimiwa Waziri wa nishati ametuthibitishia ndani ya wiki mbili vitongoji 15 ambavyo vilikuwa vimebaki vitakwenda kupelekewa nguzo na vitakuwa na umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo za kilimo, sisi kule wananchi wetu ni wakulima na ni wafugaji na wote tunashuhudia Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Fedha kutoa fedha kwenye sekta ya kilimo. Nilikuwa Mbunge katika Bunge lililopita, bajeti ya kilimo ilikuwa siyo zaidi ya bilioni 200. Hivi sasa tunazungumza zaidi ya trilioni, matrilioni kwenye kilimo. Kwa kweli ni mabadiliko makubwa na ni mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Mbeya tulikuwa tuna changamoto ya Airport, Uwanja wa Kimataifa wa Songwe, hivi sasa wenzetu majirani ndege za Malawi zinatua pale, Zambia na Kongo zinatua pale. Kwa hiyo, hii itakuwa ni lango muhimu la Nyanda za Juu Kusini. Kiwanja hiki kitakuwa ndio mkombozi wa mikoa lakini pia wa nchi hizi ambazo nimezitamka. Haya yote yameshafanyika chini ya Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mengi ya kusema, lakini natindikiwa kwa sababu furaha ikizidi unaweza ukaharibu, zaidi tu ya kusema tunawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wote kwa kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, kazi yenu imeonekana. Mheshimiwa Profesa Kitila, yeye ni mwalimu wangu; na Mheshimiwa Dkt. Lameck Nchemba, yeye ni mwalimu wangu na siku zote wamekuwa wakinifundisha namna ya kuweka mambo sawa Jimboni. Leo ninashuhudia kwamba na ninyi niwaombee kwa Mwenyezi Mungu insha Allah ifikapo mwezi Novemba waweze kurudi tena katika eneo hili la viwanja vya Bunge na wawe Wabunge tena pamoja na wasaidizi wao wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja na ahsanteni sana Waheshimiwa Wabunge kwa muda wenu wote ambao tumekuwa hapa Bungeni kwa kushirikiana kwa pamoja na niombe kwa Mwenyezi Mungu aturudishe tena ikimpendeza na impendeze iwe hivyo ifikapo Oktoba mwaka huu. (Makofi)