Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mungu muumba wa mbingu na nchi kwa kupata nafasi hii tena niweze kuzungumza leo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa tarehe 20 Juni, bado siku saba twende tukawe raia wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichoko mezani ni Bajeti Kuu yenye trilioni 56.49. Nizungumze bila mashaka, kwanza nimwombee sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania azidi kuwa na imani na nchi yake ameiweza na kila kitu kinaonekana. Hata jana mimi nilikuwa Mwanza tumeshuhudia ufunguzi wa daraja. Kwa hiyo, hakuna shaka, hakuna tatizo kabisa na Watanzania wanamwelewa sana kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, nikushukuru wewe tumekuwa na wewe miaka mitano hapa ndani ya Bunge, ukweli mimi siyo mnafiki wala sipendi maneno ya uchawachawa Mungu akubariki sana tumekuwa nawe umetusimamia vizuri sana kwa nafasi yako. Nikuombee tu kwa wananchi wako wakuhukumu kwa haki wasije wakakufanyia maneuver ambayo hayaeleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninaomba nimshukuru Waziri wa Fedha, kwenye bajeti yake ninakumbuka kuna maneno mengi nilishauri ya kimataifa na kitaifa, lakini tukiwa tunazungumzia leo trilioni 56 ninajua zote hizi zitapitia mkononi mwake na ninamwombea hata awamu ijayo aendelee kuwa Waziri wa Fedha kwa sababu hana baya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe tu mimi kwenye Jimbo langu ninazo kilometa 102 ambazo ziko kwenye michakato mpaka sasa hivi na ninajua kutokana na hii bajeti tunayoizunguzia hapa zinaenda kutekelezwa. Kwa hiyo, anikumbuke anapofika Mbogwe mitandao isigome itiki moja kwa moja kama tunavyoenda kutiki Oktoba ili Wananchi wa Mbogwe waweze kupita kwenye barabara za lami ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nimeiomba hapa ndani na ikakubali zikatekelezwe sasa mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakaporudi tena huku kwa sababu nina imani kuliko mtu yeyote yule kama maandiko yanavyosema imani ni kuwa na uhakika na mambo yale uyatarajiayo. Kwa hiyo, barabara hizi zikimalizwa nitakuwa na raha lakini pia na wenzangu niliowaacha huko Mbogwe watakuwa na amani sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kipaumbele changu hapa tunayo maboma ambayo yamejengwa na wananchi; tuna maboma ya madarasa na maboma ya zahanati ni mpango wa Mwaka 2020 - 2025 kwenye Ilani yetu tuliahidi tukiwa tunatafuta kura kwamba hivi vitu tunaenda kuvikamilisha. Kwa hiyo, niiombe Serikali pale tutakapoanza tu makusanyo ya kodi hizi utekelezaji uangalie kwenye mambo hayo mawili miundombinu ya barabara, maboma pamoja na afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, uniruhusu niwashukuru Wabunge wenzangu ambao nimekuwa nanyi ndani ya Bunge hili miaka mitano, hakika tumezoeana nina imani kila mmoja atam-miss sana mwenzake. Kwa sababu miaka mitano ni safari ndefu kweli, tumeishi kama nyumba moja familia moja na mimi niwaombe tu Wabunge wenzangu huko mwendako Majimboni Mungu awabariki sana na wakafanye kazi kwa kujiamini kwa sababu kazi kwa kweli imefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, japo kuwa miaka mitano hii imekuwa na changamoto kwetu. Kwanza, kupotelewa na Rais wa Awamu ya Tano, hilo janga lilikuwa kubwa sana na kwa vile sasa hatujaanguka hapo, sina hakika kama tena jaribu lingine linaweza likatokea likatuangusha. Lazima twende kwa pamoja lakini vilevile tuendelee kuipa support Serikali yetu, hii ni nchi yetu sote si nchi ya mtu mmoja. Hata ikitokea bahati mbaya wengine wasirudi lakini kwa kuwa tumekuwa wazoefu wa kuifanya hii kazi ya uwakilishi tusisite kutoa ushirikiano kwa Serikali, kwa sababu maendeleo yanaanzia na Serikali za Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli huko kwenye halmashauri zetu unakuta kuna halmashauri zingine zinakuwa na sheria ngumu sana, lakini kumbe ni uelewa tu unakuta. Kuna sheria huwa zinapitishwa pasipo Madiwani wengine kujua kwamba wanachokitengeneza ni kitu gani. Matokeo yake halmashauri ile inakuwa na mambo magumu na inafanya watu kuichukia Serikali, kumbe ni kitu ambacho kimetengenezwa halmashauri tu na watu wachache ambao wana maslahi pengine binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zinapopita sheria hizo (by law) zinaenda kuwa kero Serikali kwa ujumla inataka kuchukiwa lakini kumbe Serikali tuliyonayo ni nzuri sana kwa sababu nimeiishi kwa miaka mitano. Nina uhakika sasa Serikali nzuri na Chama Cha Mapinduzi ni kizuri hakuna matatizo kabisa. Kwa hiyo, niwaombe watu wema wote wale walio na ndoto ya siasa na kule maendeleo na mabadiliko kwenye Taifa hili ni vyema waamini tu kwamba Chama Cha Mapinduzi kwanza kina viongozi makini sana ambao wanapenda haki, wana misimamo wanategemea nchi ipige hatua na ndiyo maana hata mimi mwenyewe niko kwenye chama hiki tunaendelea kulisongesha kuhakikisha kwamba tunapambana kutoka kwenye umaskini tulio nao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ninaomba uniruhusu nizungumze na wananchi wangu wa Jimbo la Mbogwe, wananchi wa Mbogwe mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, niombe kabisa kama vile walivyonizaa walivyonilea kati ya vitu ambavyo sitavifanya ni kuwa na kundi. Nitaendelea kuwa na misimamo yangu kwa sababu ninamwamini Mungu yaani haipo sababu hata ya kutengeneza safu. Kwa hiyo, wanichagulie Madiwani ambao watakuwa wanawafaa wao kwenye kata zao, kwenye mitaa yao, kwamba kwa vile wanaishi nao hao Madiwani wanawajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana nimeshasikia maneno maneno kwamba mara huyu hatakiwi na Mbunge, mara huyu ndiyo anatakiwa na Mbunge, mimi sina mtu na sina mambo hayo. Kwa hiyo, wachaguane kwa kufahamiana. Ushauri wangu tu, wanipe Madiwani waaminifu na wakimwona mtu siyo mwaminifu haipo sababu ya kumwingiza kwenye siasa za nchi ya Tanzania, kwa sababu ukweli ni kwamba tumechelewa sana kwenye nchi yetu na sasa hivi ni wakati muafaka na Mungu tunamwomba sana, hata watumishi wa Mungu tunawaomba watusaidie sana tupate viongozi waaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema kwa sababu ukifikiria Mbogwe mwanzoni ilikuwa haikusanyi kwanza mapato, ni kwa nini tulikuwa hatukusanyi? Tulikuwa tunakusanya mwisho milioni 700, nimeingia mimi bilioni 3.2 mpaka sasa hivi tumekusanya. Kwa hiyo, utagundua kwamba kulikuwa na mchwa au tulikuwa Madiwani wengine wabaya. Kwa hiyo, wakawahukumu kwa haki kwa kuwauliza kwanza kwa nini huko nyuma pesa zilikuwa hazionekani na miradi ilikuwa haiendi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawape majibu ili wawachague kwa haki na mimi sitaki nimtaje mtu hapa ila tu niiache hivyo. Kwa vile watu wa Mbogwe ni waelewa sana watakuwa wamenielewa kwamba ninamaanisha nini, wanipatie Madiwani wazuri ili kusudi Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania izidi kupiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho ninataka nikishauri hapa, katika Serikali yetu ya Tanzania kwa maana ya halmashauri zetu, tunao Wenyeviti wa Halmashauri kila Wilaya na Mwenyekiti wa Halmashauri anaenda mara mbili kwenye Halmashauri. Ni kwa nini wakati mwingine zinatokea hati chafu? Ni kwa nini halmashauri zingine zinatokea hati safi? Huyu Mwenyekiti kwa nini anaenda mara mbili kwa wiki anafanya nini? Kwa nini asitoe ripoti mapema kwenye Serikali pale kabla haijatokea hati chafu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Mwenyekiti kazi yake ni kwenda mara mbili kuikagua Halmashauri ili yeye akabaini na kutoa ripoti kwenye Serikali kwamba hiki kitu kinaenda hivi na hivi, kwa nini akae kimya tu huyu Mwenyekiti? Mpaka mwishowe tunakuja kupata ripoti mbaya za CAG. Kwa hiyo, hili Serikali iliangalie sana kwa ujumla kwa sababu ukiangalia hasara nyingi zinaanzia halmashauri,
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali Kuu inatuma pesa zinaenda kupokelewa halmashauri, miradi inayojengwa ya mabilioni ni kodi za wananchi wanazolipa kidogo kidogo, lakini ni kwa nini inakuja kutokea hasara halafu watu hao wasichukuliwe hatua? Halafu ni kwa nini tuendelee kupanga bajeti kila wakati? Wakati mwingine tunaletewa shoti na watu ambao wanaeleweka. Kwa hiyo, ushauri wangu Serikali ijaribu kuchukua hatua mapema sana kwa hawa Wenyeviti wa Halmashauri pale hasara inapotokea kwenye halmashauri yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwezekana kama vile wanavyowajibishwa kwenye nchi zingine, anakamatwa anawekwa kwa kesi ya uhujumu uchumi pamoja na wale alioshirikiana nao. Kwa sababu sisi Wabunge mara nyingi tunakaa tu huku Dodoma, Serikali inazidi kutoa miradi na tunaomba barabara sijui na nini, lakini pesa pale zinapofika hapo ni kwa nini zinapotea na Mwenyekiti yupo hapohapo? Halafu tuanze sasa kuilaumu Serikali au aanze kulaumiwa Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, lazima Serikali hili suala iliangalie sana. Kwa mamlaka haya ya kisiasa Mwenyekiti anapokuwa Halmashauri ifahamike shughuli zake ni nini na nini anapaswa kufanya nini ili inapotokea shoti wawajibishwe mapema haraka iwezekanavyo, tusiendelee kula hasara kwenye Taifa letu ili maisha yaende vizuri kuhakikisha kwamba tunapiga hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kuwashukuru Mawaziri wangu ambao nimekuwa nanyi miaka mitano, hakika miaka mitano hii ilikuwa safari ndefu. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Chande, Naibu Waziri wa Fedha; nimshukuru sana Mheshimiwa Profesa Mkumbo, ameendelea kunipa ushirikiano hapa; lakini pia brother Mheshimiwa Nyongo ameendelea kunipa support kwenye Wizara yake. Kila nilipokuwa ninakwenda na shida walikuwa wananisikiliza vizuri. Pia nisimsahau Mheshimiwa Ridhiwani, mtu wangu wa nguvu sana Waziri ambaye nilikuwa kila nikienda kwenye Ofisi yake ananipa ushirikiano na ninaweza kutimiza majukumu ya wananchi wangu. Hakika mimi sikuwa chawa, nilikuwa mwakilishi, nimefanya kazi hii kwa umakini mkubwa kwa kujiamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikutaka kabisa kuwa chawa wa mtu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale palipokuwa na ubaya nilikuwa ninasema hapa kuna ubaya, pale palipokuwa vizuri, ninasema vizuri na nitaendelea kuwa hivyohivyo. Kwa hiyo, Mawaziri ninawaombea sana Mungu awabariki sana na Mheshimiwa Rais awakumbuke kwenye Serikali yake ijayo ili tuje tuzidi kupiga hatua kuhakikisha kwamba tunasonga mbele kuisukuma nchi yetu ili tuweze kutoka kwenye wimbi la umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa …
MWENYEKITI: Malizia, muda wako umeisha.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba ninakushukuru, lakini pia Waziri wa Fedha, nchi yetu tuko kwenye biashara za umoja kwenye hizi nchi East African Community Benki zetu bado riba ziko juu sana atusaidie…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maganga, usichangie tena malizia kwa kuunga mkono hoja.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia kwa kuunga mkono hoja. Mheshimiwa Waziri afanye juu chini inavyowezekana ili kusudi tuweze kufanya ushindani vizuri, riba zishuke, tufanye biashara wengine, wengine haipo sababu ya kuja huku kwenye siasa. Ninakushukuru sana. (Makofi)