Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa zawadi hii ya uhai na pamoja na kupata nafasi hii ya kusimama hapa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukurani kwanza kwa Serikali, Serikali imefanya vizuri sana na kwa mimi kama ni Mbunge wa kutoka Zanzibar basi ninaishukuru sana Serikali. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar wamefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajaribu kutaja sekta moja ambayo hii kwa kule kwetu itakuwa imekusanya vitu vingi sana ni sekta ya fedha za nje. Katika sekta hii ya fedha za nje, ninakushukuru sana Waziri, Mheshimiwa Dkt. Madelu hapa pamoja na ndugu yangu Mheshimiwa Hamad Hassan Chande wamefanya jambo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2021 tulianza na mkopo ule wa RCF (Rapid Credit Facility) ilifanya mambo makubwa sana kule Zanzibar, lakini tukaja na ECF tumefanya mambo makubwa sana kule Zanzibar, lakini kuna Boosting Primary Education tumefanya mambo makubwa sana. Isitoshe tokea kimeanza kipindi hicho tukitazama katika GBS (General Budget Support) hakuna mwaka ambao imesita na imekwenda kwa wakati na hiyo imefanyika kwa wakati na imeenda katika kiwango kamili. Kwa hiyo, Mheshimiwa ninakushukuru sana Mheshimiwa Dkt. Madelu na uongozi wote katika kufanikisha mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine niipongeze TRA, TRA imekusanya mapato mazuri kama trend inavyoonesha kwamba ilikuwa ikiongezeka hata kuvunja record ya quarter kwamba ziko quarter ambazo zimekusanya vizuri sana katika TRA. Nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali, lakini pia na ndugu yangu Yusuph Juma yuko pale amekusanya na amefanya kazi nzuri sana, ndugu yangu Mwenda. Kwa hiyo, tunawapongeza sana TRA kwa makusanyo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe shukurani kwa wale watu ambao sasa hivi wananisikiliza ndiyo walionileta hapa, shukurani zangu kwa wananchi wa Jang’ombe (Wapigakura wenzangu wa Jang’ombe) kwa kuniamini kwa kunileta hapa katika Bunge hili nafanya mambo ambao yanaifanya nchi yetu isonge mbele, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia, kwa kauli yao ambayo sasa wanasema mzungu wa nne tunaurejesha palepale. Kwa maana ya hiyo huu mzungu wa nne watakuja kuukuta tena katika meza hii kwenye hii mbao utakuwepo kwa mujibu wa maoni ya watu wa Jang’ombe ndiyo yako hivyo. Ninajua inawezekana ikawa wapo wanaopita kunusanusa, lakini tahadhari ninatoa tu kwamba usinusenuse kila kitu unaweza ukaja ukanusa sumu. Sasa ninawashukuru sana watu wangu wa Jang’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila wamenipa salamu, watu wa Jang’ombe wamenipa salamu hii hapa ambayo nimeiandika na hata ukipata kwenye Mitandao yote ya Jang’ombe utaikuta hii salamu wanasema: “Oktoba Tunatiki”, ila wameniambia nifafanue. Kufafanua kwamba Oktoba Tunatiki, kuna Msemo wa Kiarabu unasema: “Khalif tuarraf”, wewe ukitaka ujulikane upate umaarufu nenda kinyume, khalif tuarraf.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna watu wana khaalif hiki kitu ili wapate umaarufu, natoa kisa kimoja, kuna mtu mmoja aliona mwezi alipoona ule mwezi magharibi ndipo unapoandama akasema mwezi ule umeandama, kwa hiyo yule mtu alipewa sifa na watu wote wakaenda kushangilia pale, sasa pembeni kuna mtu anaitwa Hababel na yeye akaona kwa nini huyu anapewa sifa, akaona na yeye aseme kaona mwezi, mwezi unaandama mmoja tu, akasema na yeye kaona mwezi, lakini kaonesha upande wa kaskazini, anaambiwa Hababel mwezi unakuwa mmoja tu huku kwa nini unatuonesha mwezi, anasema huu mwezi kumbe Hababel alikuwa anataka ule umaarufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umaarufu huu unapelekea kumbe kuna watu wengine inawezekana wakawa hawaoni vizuri, kuna watu wengine wanakuwa wana tongotongo kwenye kope hizi, sasa anapogeukia yeye huwa anaona mwezi, mwezi ni mmoja tu Oktoba, tarehe 25 Oktoba ndiyo mwezi. Sasa kama kuna Hababel ana mwezi unaoandama kaskazini yeye huyo ni mwingine, au hawa waliotaja mwezi kwamba utakuwepo mwezi mwingine, naona labda tongotongo zao, kwa hiyo wananchi wawaone hawa watu ambao wana tongotongo hakuna mwezi mwingine, mwezi ni Oktoba na Oktoba tunatiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa ushauri kwa Serikali. Jana Balozi Mulamula hapa jirani yangu alizungumzia athari ya fedha za nje kutokana na uhusiano ambao tunao wa kimataifa. Sasa alisema kwamba zimeleta athari kwamba fedha hazikuingia, lakini tukakosa tukapata upungufu wa ajira watu 1,200 kutokana na fedha ya USAID.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yangu au niishauri ikajaribu kufanya utafiti, kuna baadhi ya fedha tunaweza tukaziona kwamba multilateral, lakini kumbe zikawa ni bilateral. Kwa maana gani? Tuna uhusiano na nchi fulani lakini zile fedha zipo katika mifuko mikubwa ya dunia, lakini ule mfuko wenyewe ukawa unachangiwa na nchi moja au ukawa unachangiwa na nchi mbili tu peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo litakalotokea katika ile nchi au kubadilika kwa sera ya ile nchi, au kubadilika kwa uongozi katika ile nchi unaweza ukaja ukatuletea shoti kama hii ambayo tuliyokuja kuiona. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali ikajaribu kutizama vile vitu ambavyo tunaweza tukaviona ni multilateral, lakini kumbe ni bilateral kwa sababu mchangiaji ni mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana ukaona kwamba ni international organization, multinational organization, lakini ikaja ikazusha hili tatizo. Kwa hiyo ili kuepuka tusiende huko kwenye kupata shoti za namna hiyo ninaishauri Serikali kufanya jambo hilo, huo ushauri wangu wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, tuna ndugu zetu hawa wa OSHA ambao wanashughulikia usalama na afya katika maeneo ya kazi, hivi sasa hivi mara nyingi sisi Wabunge hupiga makofi sana tukisema tumeondosha kodi ya OSHA, lakini kumbe wakati mwingine tunaikosesha haki ya binadamu kutopatikana. Kuwa na usalama na kuwa na afya katika maeneo ya kazi ni haki ya kibinadamu, kwa sababu pale anaweza mtu akafariki kutokana na mazingira yale ya kazi hapana usalama na wala hapana mazingira ya afya nzuri, pia panaweza pakatokezea jambo lingine likampa mtu ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaishauri Serikali tunasema kwamba Dkt. Kitila Mkumbo akitaja atakwambia investment imeongezeka katika nchi hii, ile huge of investment iliyoongezeka hivyo zile fedha zinazokwenda kule OSHA zinatosha kuja ku-cover haya mazingira? Au wanakuja wawekezaji wanawekeza sisi tunazuia kutoa kodi za OSHA tunasema kwamba tumepunguza halafu tunabakiwa na walemavu na vifo na mayatima au tunapata watu wenye magonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kukagua katika hayo maeneo, hii kodi au hii tozo tuichukulie kama ni haki au niishauri Serikali, basi tuweke percentage ya income tax ambayo inakusanywa iende katika OSHA ili iende ikaondeshe haya matatizo kwa sababu hii ni sawasawa na haki ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninazungumzia suala la kukuza ujuzi lipo kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Ridhiwan pia. Suala la kukuza ujuzi kwa soko la nje. Leo Tanzania tuna diplomasia nzuri na nchi nyingine na ile nchi inatamani itoe watu kwetu waende wakafanye kazi kule, lakini hatuna ujuzi wa kwenda kufanya kazi kule. Ninatoa mfano kesi moja, kesi ambayo aliizungumza Waziri wa Mambo ya Nje, tumepeleka watu, lakini watu waliofaa ni watatu katika watu mia na zaidi. Sasa hii tunaondosha fursa, tujaribu kuangalia, kukuza ujuzi kwa ajili ya soko la nje, kwa sababu tumejijenga vizuri kidiplomasia tuitumie hii fursa hata katika kufundisha Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo bidhaa moja adimu Kiswahili lakini pengine inawezekana uwezo au ujuzi wa kwenda kuifundisha nje haipo vizuri. Sasa tujaribu kuangalia katika sekta hizi ili tuweze kuingiza mapato kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni upotevu wa mazao na hili ninakusudia kwa Dkt. Kitila Mkumbo ni la kilimo hili. Tumewekeza matrilioni ya pesa kwa pamoja katika miaka michache. Tumetoka kwenye bilioni 200 tumekwenda mpaka kwenye trilioni, inafika wakati wa mavuno tunaweza tukapata majanga tunaita ya mvua na wavunaji inawezekana sasa wasipate mazao, kwa nini tusiwekeze watu waweze kuvuna hata kama kuna mvua, Serikali yetu inaweza kwa sababu tulishawekeza kwenye kilimo, tulishawahamasisha watu walime, lakini je, tunayo mipango endapo yanatokezea maafa, pamoja na maafa hayo lakini wakulima wetu waweze kulima wapate kile kitu, vinginevyo tukiweka mbadala wa kulipa ruzuku kwa majanga kama haya itakuwa siyo vizuri kuliko tukamwezesha huyu mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninazungumzia ajira kwenye michezo. Michezo inaajiri sana, turudi kule zamani, uwekezaji sasa umepungua katika taaluma ya michezo. Zamani ukimgusa kocha utaambiwa kasoma Ujerumani, kasoma Brazil, kasoma wapi, kwa hiyo hata timu zetu za Taifa zikiongozwa ingawaje sasa hivi zinaongozwa na watu wa hapa si wageni, lakini tujaribu kuangalia kwamba sisi timu zetu hizi kubwa kubwa tuna-import makocha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, hatuwezi kupata makocha wa kwetu? Kwa hiyo, taaluma kwenye michezo imepungua. Tujaribu kufanya kwa makusudi watu wapate taaluma ya michezo ili tusi-import hawa makocha na watatusaidia kuzalisha vipaji vingine. Pamoja na yote niseme kitu kimoja ambacho ninaishauri Serikali Kuu, kwamba wajaribu kuangalia wataalam wa michezo. Wataalam wa michezo wakapokee ushauri wao kwenye biashara kuna Baraza la Biashara moja kwa moja linakutana mpaka na Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku tunajua lipo Baraza la Michezo lakini lipo zaidi kama baraza lenyewe, sasa tunataka hawa wataalam wa michezo wapo wataalam wa michezo wamehusika mpaka kwenda kupata ule uwanja wa Arena wa Rwanda, baadhi ya washauri wametokea hapa hapa kwetu Tanzania. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali, ijaribu kukaa na wataalam wa michezo wapate ushauri, hawa wataalam wana mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninasema kwamba ninaunga mkono mia kwa mia, ninashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)