Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi mchana huu wa leo kuchangia hotuba ya bajeti na hoja zilizoletwa hapa mbele ya Wizara ya Fedha pamoja na Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila kitu aliyenijaalia uhai, afya, nguvu katika muda huu wote wa maisha yangu. Pia ninawashukuru wote wale walioniunga mkono na kunisaidia katika kuniongoza mpaka nikaingia ndani ya Bunge hili Tukufu, vilevile Waheshimiwa Wabunge wenzangu walionipokea mwaka 2022, wakanifundisha, wakanielekeza mpaka muda huu ninawashukuru Wabunge wenzangu nyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninampongeza Dkt. Mwigulu Nchemba, ninampongeza kwa hotuba hii aliyoiwasilisha hapa ambayo inatuonesha kwamba nchi yetu itakwenda kuwa na mafanikio makubwa baada ya utekelezaji wa bajeti hii. Vilevile ninampongeza Profesa Kitila Mkumbo kwa kutuwekea mpango madhubuti ambao utakwenda kutekelezwa sambamba na bajeti hii katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza pia wasaidizi wenu Mheshimiwa Chande, ninampongeza pia Mheshimiwa Nyongo, wote hawa kwa umoja wao wameweza kushirikiana wakaweza kutuletea mpango na bajeti hii ambayo ni mkombozi wa wananchi, hakika itakwenda kuwakomboa wananchi wetu kwa kipindi chote cha miaka mitano ijayo, nawapongezeni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana vilevile Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwingi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kusimamia vyema Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi tunayoimalizia 2020 - 2025. Hakika wamezitendea haki sekta zao walizozisimamia na hata sasa tumeona Tanzania nzima imekuwa ikiwataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Tanzania Bara, Dkt Samia amekuwa akitajwa kila sehemu, ukienda Zanzibar Dkt. Hussein Ally Mwinyi amekuwa akitajwa kila sehemu. Hii yote ni kutokana na utekelezaji wa Ilani waliyoifanya na kusikiliza kwa sababu kila Mkoa ameonesha hapa viongozi wote waliosimama wa Waheshimiwa Wabunge wameeleza katika maeneo yao kazi zilizofanyika. Hakika kazi walizozifanya ni za kutukuka na Insha Allah Mwenyezi atawajaalia, atawalipa mema kwa kile ambacho wamekitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na shukrani zangu, ninatoka Mkoa wa Kaskazini Unguja nikiwawakilisha wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao kwa hakika wamefarijika na jitihada za Marais wetu hawa na viongozi wetu hawa waliomo ndani ya Serikali na zaidi viongozi hawa wametokana na Chama Cha Mapinduzi. Chama Cha Mapinduzi kimetuwekea misingi imara ya kuwapata viongozi wazuri ambao watatuletea maendeleo sisi wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa hapo nianze kwa kusema ndani ya Mkoa wa Kaskazini hususan wanawake wa Mkoa wa Kaskazini tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuhakikisha viongozi hawa wanarudi madarakani ili waweze kuendeleza yale waliyoyapanga wananchi waweze kupata manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru tena Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuja kutufungulia kituo chetu cha ujasiriamali pale Mkoa wa Kaskazini Unguja cha wanawake na alipokuja akatuasa mambo mengi na alitoa kauli pale akasema kwamba viongozi watapimwa kutokana na utendaji wa kazi waliyoifanya. Akatushajihisha akatuambia kwamba katika kituo kile cha ujasiriamali ambacho kitakuwa kinafundisha ushoni, akatuahidi kutoa vyereheni vitano, lakini kwa uzalendo wake mama huyu alitupa vyerehani 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kuonesha kwamba anawiwa na changamoto za wananchi kukosa ajira, kwa sababu kituo kile kinapokea vijana wengi ambao wanakuja kujifunza pale, wakitoka kujifunza watakwenda katika maeneo yao kwenda kuyaendeleza na hatimaye watapata kipato. Sasa kwa hilo ninampongeza sana, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia vyerehani vile, tunamshukuru na tunamwahidi tutazifanyia kazi kwa kadri ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea vilevile kumshukuru tena Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ziara zangu nilizokuwa ninatembelea nilikuwa nimepitia katika dawati la jinsia pale Mahonda, wakanieleza changamoto nyingi wanazopambana nazo, lakini mwisho wa siku wakasema wanashukuru sana kwa sababu kuna watoto ambao walikuwa wanapatikana na shida kidogo, basi walikuwa wanapeleka kituo cha polisi na nikaona bora nitembelee, nikatembelea kituo cha polisi na nikatembela Kituo cha Polisi cha Mkokotoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Mkokotoni kimejengwa upya, kilijengwa tangu miaka ya ukoloni lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akawapelekea pesa kikajengwa upya kituo kile kipo vizuri na makamanda wa pale waliniambia niwaletee shukrani zao kwa Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa hili ninaomba amwambie Mheshimiwa Rais kwamba zile pesa alizopeleka wakajengewa kituo kile cha polisi, basi wanamshukuru sana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo ni kizuri, kituo kina miundombinu ya kisasa kwa sababu hapo mwanzo ilikuwa hata wale watoto wanaokinzana na sheria walikuwa wanawekwa pamoja na mahabusu watu wazima, lakini kwa sasa kituo kimejengwa, kina miundombinu mizuri hata mahabusu ya watoto ipo nimeiona ipo vizuri. Kwa hiyo ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri ampe salamu hizi Mheshimiwa Rais kwamba makamanda wa Kituo cha Polisi Mkokotoni wanamshukuru sana kwa lile alilowafanyia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea mbele, ninashukuru tena kwa Mheshimiwa Rais ametupatia majiko ya gesi kwa ajili ya wananchi wetu, kwa hiyo na kwa Mkoa wa Kaskazini ninashukuru wamepata, ametupa mashuka mama, tumekwenda kupeleka kwenye hospitali zetu, pia na hilo tunashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hiyo Mkoa wa Kaskazini tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuzisaka kura tuhakikishe tunamrudisha tena mama huyu na pamoja na Mheshimiwa Dkt. Mwinyi wapate kura za kishindo. Tunashukuru sana kwa kazi zote walizotufanyia pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye hii bajeti ya Serikali pia naishukuru kwa sababu ukiiangalia hata vile vipaumbele vyake vilivyowekwa pale vinamlenga mwananchi wa kawaida moja kwa moja atanufaika. Vipaumbele hivi vitawasaidia wananchi kupata ajira, kwa sababu kuna kuwastawisha wananchi kwa miradi yote na mipango na ajira, kila kitu. Sasa haya yote wananchi wananufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye sehemu ile ya ajira, watafaidika wananchi, tukiangalia bajeti iliyokwisha ya 2025/2026 tuliona kwamba ajira kwa mujibu wa Ilani yetu ya Uchaguzi kipindi kile walikuwa wamesema ajira 8,000 wananchi watapatiwa, lakini utekelezaji wa Ilani ile umevuka kwa sababu kuna ajira zimetoka 8,000 na nukta nane. Sasa kwa sababu hiyo tunashukuru sana Serikali, tunashukuru sana kwa kazi zote zilizofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hayo kila nikiendelea mimi nitakuwa ninashukuru tu, lakini yote ni kwa sababu kazi kubwa imefanyika ya kuleta maendeleo ndani ya nchi yetu. Ninashukuru sana uongozi wa Chama changu Cha Mapinduzi kwa muda wote unijaalia nikaingia humu ndani ya Bunge hili Tukufu, ninawashukuru sana uongozi wa Kaskazini Unguja, wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, UWT kwa pamoja, mama yetu Mama Mary Chatanda anatusimamia vyema, tunashukuru tunaendelea mpaka muda huu tunapokamilisha bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. (Makofi)