Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba; Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo; na Naibu Waziri wake Stanslaus Nyongo; Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara zote mbili; Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango; na Gavana wa Benki Kuu Ndugu Emmanuel Tutuba kwa hotuba nzuri ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli bajeti hii ni nzuri, inawagusa wananchi walio wengi, katika bajeti hii kuna hatua nyingi za kikodi ambazo zimewekwa ambazo sasa zinaenda kutusaidia kulinda viwanda vyetu vya ndani, pia inaenda kutusaidia kuweza kukusanya kodi zaidi, tunapokusanya kodi ndiyo tutaendelea kupata maendeleo na vilevile kuchochea uwekezaji. Tunasema hii bajeti ni nzuri, ni bajeti ya watu kwa sababu itatusaidia kutatua matatizo mengi ambayo yamo kwenye maeneo yetu na itatusaidia kuleta maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa pongezi hizi kwa Wizara hizi kwa kazi nzuri wanayofanya, Wizara hii wanahakikisha kwanza fedha zinapatikana, sidhani kwamba ni kazi ndogo kuweza kukusanya trilioni 56.49, kwa hiyo kazi imefanyika, vichwa hapo vimechemka wakaweza kuzipata na kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inapata hela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza vilevile kwa usimamizi mzuri wa sera za fedha. Hawa wamewezesha haya kufanikiwa kwa sababu ya ubunifu, uchapakazi, weledi na uadilifu wao. Pia, wamekuwa wasaidizi wazuri sana kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hivi, bado Taifa linawahitaji. Kwa hiyo, ninawaomba wananchi wa Jimbo la Iramba wamrudishe Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa sababu bado tunamhitaji; ninawaomba wananchi wa Jimbo la Ubungo wamrudishe Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, bado Taifa linamhitaji; tunaomba wananchi wa Jimbo la Kojani waweze kumrudisha Mheshimiwa Hamad Hassan Chande, aweze kuendelea kwa sababu Taifa bado linamhitaji; na tunaomba wananchi wa Maswa Mashariki wamrudishe Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo kwa kura nyingi kwa sababu Taifa bado linawahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamefanya kazi nzuri, tunaomba warudi na ikiwezekana ikimpendeza Mheshimiwa Rais awapatie nafasi nyingine kama hizi kusudi waendelee kulisaidia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inasimamiwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo makubwa. Kwa kweli leo hii Tanzania ukienda kila kata, ukienda kila mkoa, ukienda kila wilaya kuna mradi wa maendeleo unaoendelea au kuna hela zimeingia. Hii ni kwa sababu ya kazi nzuri ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Mkoa wa Kagera kwenye afya tuna halmashauri nane na zote tumejengewa hospitali za halmashauri; vituo vya afya 24; zahanati 40; na kwenye Bukoba Regional Referral Hospital tumejengewa jengo zuri sana la dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maji kuna miradi mingi imetekelezwa Mkoa wa Kagera ukilinganisha na upatikanaji wa maji wa 55% uliokuwepo 2015 leo hii tumefikia zaidi ya 70% huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia pia kuna Mfuko wa 10% ule wa Halmashauri ambao sasa unawasaidia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuendeleza biashara zao ambapo nao biashara zao zikikua ndiyo wanaweza kulipa kodi. Hapa wameweza kukusanya shilingi bilioni 12.86. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kuipa TARURA na TANROADS fedha za kutosha na barabara nyingi vijijini na mijini zinajengwa. Tumejengewa madaraja nane, barabara za lami na za changarawe mpya zinajengwa na tunajengewa daraja moja kubwa la Kitengule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu katika kipindi cha miaka minne tumeshuhudia matokeo makubwa sana katika Mkoa wa Kagera ukilinganisha na tulianza na madarasa 1,606, leo hii tuna madarasa 7,610 katika kipindi tu cha miaka minne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejengewa pia, shule mpya zikakamilika 12 za msingi, 19 za sekondari. Tumejengewa shule nzuri ya kisasa ya wasichana; itawalinda watoto wetu wa kike, watasomea pale, watakuwa Watanzania bora na watatimiza ndoto zao. Shule hiyo inaitwa Kagera River Girls Secondary School na sasa sisi akina ishomire tunajengewa chuo kikuu. Tunasema Mama Samia ahsante sana, hatuna cha kumlipa, tunangoja tukamlipe mwezi Oktoba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa pamoja na hayo mambo makubwa tuliyoyapata, tunaomba ikiwezekana waendelee kuangalia uwezekano wa kujenga masoko ya mipakani. Tuna uhakika wakijenga masoko mipakani na kule Mkoa wa Kagera tuna mipaka mingi, hii itachechemua uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu anapohangaika kutafuta fedha, hiki ni chanzo kimojawapo kizuri ambacho kinaweza kikaleta mapato. Wanategemea pato likue kwa asilimia sita kwenye mwaka ujao lakini kwa kufanya vitu kama hivi tunaweza tukakuta tunaruka mpaka tunafikia asilimia nane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo bado wilaya sita kati ya nane ambazo hazijaingia kwenye Gridi ya Taifa kwa maana ya Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Bukoba Vijijini, Bukoba Mjini na Muleba. Tunaomba nazo ziingizwe kwenye Gridi ya Taifa kwa sababu mnajua kwamba umeme ni uchumi na umeme unaweza kutusaidia kutoka hapa tulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanikiwa sana kwenye kilimo. Waheshimiwa, wote wanajua kwamba zao kubwa katika Mkoa wa Kagera ni kilimo cha kahawa. Watu wameteseka sana na bei ya kahawa ambayo ilikuwa chini ya shilingi 1,000, mwishowe wastani ukaja mpaka kwenye shilingi 1,100. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, amekuja Kagera mara kadhaa, amekutana na wakulima, amekutana na vyama vya ushirika. Serikali imeondoa tozo mbalimbali na sasa hivi bei imepanda kutoka kwenye shilingi 1,100 imefikia shilingi 5,000 kwa kilo moja. Tunasema, sasa ahsante sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, ahsante sana Mama Samia. Tunangoja tu tumlipe kwenye sanduku la kura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa kuwa huu ni mkutano wa mwisho wa Bunge la Kumi na Mbili, ninaomba niwapongeze wote tulio hapa kwa kuhitimisha kazi nzuri ambayo tulitumwa kufanya. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema pamoja na uhai wa kuweza kuyafanya haya yote tuliyoyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anazozifanya yeye kama kiongozi wa shughuli za Serikali ndani ya Bunge. Tunamwombea baraka tele ili wananchi wa Ruangwa wampe kura za kutosha na aweze kurudi hiyo Oktoba, 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kazi nzuri anazofanya. Tangu alipopewa nafasi hii kwa kweli ameitendea haki. Tunawaomba wananchi wa Jimbo la Bukombe wamrudishe Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko Bungeni kwa kura nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru Wenyeviti wote wa Bunge. Wamefanya kazi nzuri ya kuongoza shughuli zote za Bunge hili na tunawaombea wote wakarudishwe humu Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Naibu Spika, Mheshimiwa Zungu. Tunawaomba Watu wa Ilala wakampigie kura nyingi. Tunamjua ni mzee wa speed na viwango, aweze kurudi humu Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Katibu wa Bunge, Tume pamoja na Wakurugenzi na watumishi wote, kwa kweli wametuwezesha tukaweza kuyapata haya mafanikio tuliyofanikiwa. Bila wao tusingeweza kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Spika wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson Mwansasu, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani. Amekuwa kiongozi wa kuigwa, mwenye unyenyekevu, weledi wa kutosha, hekima na busara tele; ameliendesha Bunge hili kwa viwango vya kisasa na kwa ufanisi mkubwa. Tunaomba wananchi wa Jimbo Jipya la Uyole wamwone, wampe kura nyingi, ashinde na arudi Bungeni. Your future is even brighter. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakishukuru sana Chama changu Cha Mapinduzi kwa Ilani ambazo zimeendelea kutekelezwa ambazo zimeleta maendeleo katika Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Kagera walioniona, wakanichagua na wakanipa Ubunge nikafika hapa. Tumefanya kazi pamoja, kazi kubwa na nzuri. Ninawahakikishia... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante. Muda wako ulikuwa umeisha. Nilikuwa nakuacha umalizie.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia. Ninamalizia kwa kusema, ninawahakikishia kwamba bado nipo na nina nguvu za kuwatumikia. Niko njiani ninakuja twende kutafuta kura za Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mwenyezi Mungu awabariki Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote humu ndani. Kila mtu aende akashinde kwenye jimbo lake, tukutane hapa Desemba. Kwa Mama Samia tunasema, mitano tena, yajayo yanafurahisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)