Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa mwisho katika hotuba hii ambayo inakwenda kuhitimisha muhula wa miaka mitano wa uhai wa Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali, niweze kumpongeza sana Waziri wetu wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. Hongera sana kwake na Naibu wake, ndugu yangu Mheshimiwa Chande, ambaye sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu katika chama chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze vilevile jirani yangu Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Nyongo. Hakika ukimjumlisha na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda; hawa watu wamefanya kazi vizuri sana. Lazima niwapongeze na tuwapongeze, wameifanyia kazi Tanzania, wameipendezesha Tanzania, wameisaidia Tanzania uchumi wake kuweza kukua. Pia, hapa lazima nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuwaona wao ambao hakika wameweza kumsaidia na hakuna mtu ambaye anaweza akabisha kwamba Tanzania hii sasa imepiga hatua kubwa sana kiuchumi na inafahamika kimataifa, siyo kama tulivyoikuta mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukiangalia maandiko yanaonesha katika nchi 42 za Sub-Sahara Africa, Tanzania kwa uchumi ni nchi ya saba. Ni hatua moja kubwa sana na hali hii inatuonesha kwa sababu kuna maandiko mengine yanasema, kwenye Afrika nzima sisi ni miongoni mwa nchi 10 na wengine wanasema ni nchi ya 11. Vyovyote vile itakavyokuwa, 10 na 11 haziko mbali. Hivyo, hongera sana. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Baraza lako lote la Mawaziri kwa sababu wameweza kuiheshimisha Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana juzi wakati nikiwa katika ziara zangu kule jimboni, wananchi wa Kinondoni wameonesha kuridhika sana na utendaji wa Serikali na utendaji wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wenyewe wanasema wanasubiri mwezi Oktoba ili Kinondoni iweze ku-tick na ninaamini Dar es Salaam na Tanzania nzima tunakwenda ku-tick. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa katika kuchangia kwangu nizungumzie njia mbadala ya kuchangamsha uchumi kupitia Jiji au Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba Dar es Salaam ni eneo ambalo ndilo lenye msukumo mkubwa wa shughuli za kiuchumi na biashara katika Tanzania yetu. Pia, hata mapato ya Taifa makubwa sana yanatokea Dar es Salaam ambapo Dar es Salaam peke yake tunachangia zaidi ya 17% ya pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023, Dar es Salaam ilichangia takribani shilingi trilioni 32.1 kati ya shilingi trilioni 188.8 ya pato la Taifa. Kutokana na ukubwa huu wa uchumi wa Dar es Salaam na mchango wa Dar es Salaam, kuna haja ya kuiangalia zaidi Dar es Salaam na hasa katika maeneo ambayo yakifanyika yanaweza yakachagiza zaidi uchumi wa Taifa kwa maana ya pato la Taifa na vilevile uchumi ambao utaweza kwenda kusaidia mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ningependa zaidi nizungumzie suala la barabara kwa sababu barabara ni moja kati ya vitu muhimu sana vinavyoweza kusaidia uchumi ukakua haraka. Usafiri na usafirishaji ni ingredient, ni vitu muhimu sana katika masuala mazima ya uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Dar es Salaam tuna kilometa zaidi ya 2,000 (to be precise ni kilometa 2,206). TARURA hivi karibuni walifanya upembuzi wakaona ni barabara gani muhimu ambazo kama zitaweza kutengenezwa zinaweza zikasaidia sana kuibadilisha Dar es Salaam iendane na ukuaji wa uchumi, itengeneze matumaini kwa investors wanaokuja pale, kuuona mji kwamba una barabara ambazo hakika zinaweza zikasaidia usafiri na usafirishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kilometa 756 ambazo tunaweza tukaziita barabara muhimu. Kati ya hizo, kilometa 44 ziko Kinondoni na tunafahamu vilevile kwamba kuna Mradi wa DMDP II ambao huu sasa unakwenda kujenga takribani 30% ya barabara zote hizo nilizozitaja ikiwa ni sawa na kilometa 225.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hesabu zinaonesha itatuchukua si chini ya miaka sita kuweza kumaliza kuzitengeneza hizo barabara za kilometa 225. Sasa ukizichukua barabara za kilometa 756 ambayo ndiyo mahitaji yetu, ukiondoa 225 tunabakiwa na kilometa karibu 500 na zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi kwa kutegemea bajeti ya Serikali ya kila mwaka itatuchukua miaka mingi sana na kwa hali hiyo haitawezekana kuchepusha uchumi wetu kwa haraka zaidi. Tunachohitaji ni maendeleo ya haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia ametuonjesha ni kwa jinsi gani Tanzania inaweza ikapiga hatua za uchumi wa haraka kwa haya ambayo ameyafanya katika kipindi cha miaka minne. Ninaamini Serikali inaweza ikaangalia njia mbadala ya kutafuta fedha. Ukiondoa huu Mradi wa DMDP hesabu zinaonesha kwamba, tunahitaji takribani shilingi trilioni 1.89 ili Barabara za Dar es Salaam ziweze kutengenezwa zote hizi kilometa 700 na ushehe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, Serikali iangalie siyo lazima iwe kwa mwaka huu, lakini hata kwa mwaka ujao katika mipango yetu, tukaweka utaratibu wa kuangalia alternative sourcing ya fedha; siyo lazima tuitoe kwenye bajeti yetu. Kuna watu wengine ukiwashauri kwamba hata tukienda kukopa ni vizuri tu kwa sababu Dar es Salaam inahitaji ijengwe sasa hivi kwa mafanikio ya sasa hivi kwa Tanzania ya sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusisubiri tudundulize, (kudunduliza lugha yangu ya Tanga kidogo ngumu). Kile kidogo kidogo mpaka upate nyingi halafu uje ujenge hizo barabara zote, hiyo itatuchukua miaka mingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam lazima liwe Jiji la matumaini; Jiji ambalo wawekezaji watakapokuja waweze kuona kweli pale ndipo Dar es Salaam. Sasa hivi Dar es Salaam ikifika usiku maeneo machache sana utakuta kuna taa za barabarani; hapana haipendezi. Hivyo, hata huu mradi kama Serikali itaona ni vizuri kutafuta njia mbadala za kutafuta fedha, barabara za Dar es Salaam zikajaa taa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda miji ya watu vilevile tunakuta hata business names yaani majina ya biashara yamewekewa taa. Kuna kitu wanaita neo signs. Tukienda Dubai, tukienda Nairobi, tukienda South Africa tunaona lakini kwetu Dar es Salaam ukiweka business name yako (jina lako la biashara) kwa kuweka taa au kwa maandishi makubwa kesho unatozwa kodi. Ningeshauri vitu vingine vidogo vidogo ambavyo vinakwamisha kutufanya Dar es Salaam tukue kwa haraka lakini tuupendezeshe mji wetu vilevile, tuko katika zama nyingine tuweze kufikiria na tuwe na mawazo mengine nje ya box.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda zaidi nizungumzie Dar es Salaam na ushauri wangu ni kwamba, tuiangalie zaidi Dar es Salaam ili Dar es Salaam iweze kuchangia zaidi kwenye uchumi wa Taifa letu kwa manufaa ya Tanzania nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Ninaunga mkono hoja hii na ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Rais kwa yale aliyoyafanya katika Jimbo la Kinondoni ambayo nisingependa kuyarudia, ninataka nimwambie, wana Kinondoni tuko tumeridhika sana na kazi yake. Tunasubiri mwezi Oktoba twende tuka-tick. Hilo hatuna mashaka lakini tuwaombee Mwenyezi Mungu awajaalie Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge hili ambalo wamefanya kazi iliyotukuka ambayo hakika wametuleta katika mafanikio makubwa ya uchumi wa Taifa hili, basi Mungu awajalie waweze kurudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona Kinondoni mimi nipo ndugu yenu Tarimba Abbas, mwananchi; Mwananchi wa Tanzania, siyo Mwananchi Yanga maana yake wengine nikisema mwananchi wataingia wasiwasi. Nitakuwa pamoja na nyie Mwenyezi Mungu akijaalia katika kipindi kingine cha miaka mitano. Bi idhnillah, Assalamu alaykum wa rahmatullahi taala wabarakatuh. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)