Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BENJAMIN L. NGAYIWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kukushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika mjadala wa kujadili hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa wakati wa kufungua ama kuzindua Bunge letu la Kumi na Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakupongeza kwa kuteuliwa kwako kuwa Naibu Spika wetu. Pia ninampongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa nafasi hiyo ambayo anaitumikia. Nichukue fursa hii pia kuwashukuru wapigakura na wananchi wenzangu wa Jimbo la Kahama Mjini kwa imani yao kubwa waliyonipatia kwa kunichagua kuwa mwakilishi wao Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni siku njema ambayo tunajadili hotuba ya Mheshimiwa Rais, lakini ni siku pia ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake. Kwa hiyo, tunampongeza na kumwombea maisha marefu huko aliko, aendelee kututumikia Watanzania kwa moyo wote kama ambavyo ameonesha kwa kipindi chote.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii ya Mheshimiwa Rais ni hotuba ya kwanza kabisa aliyoitoa tangu tulipomaliza uchaguzi wetu mkuu tangu Oktoba, 2025. Hotuba hii iliakisi na kugusa maeneo karibu yote muhimu ya kisekta katika kuonesha Dira ya Maendeleo ya Taifa letu na kuinua hali ya uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote ni mashahidi, Mheshimiwa Rais alipogusia kwa mfano, katika sekta ya ujenzi aliposema na ninamnukuu hapa anasema; “Tutaongeza pia bajeti na uwezo wa TARURA katika kuboresha barabara za ndani na za vijijini ili kuhakikisha zinapitika mwaka mzima na kuwa wakulima wanaweza kuyafikia masoko kwa urahisi.”
Mheshimiwa Naibu Spika, humu Waheshimiwa Wabunge tulimpongeza kwa kumpigia makofi mengi sana, ikionesha kwamba shida kubwa au sehemu kubwa ambayo inatakiwa tuelekeze nguvu zetu ni katika kuboresha miundombinu yetu hasa barabara za ndani na zile za vijijini. Mheshimiwa Rais ameonyesha dhamira hiyo ya kuongeza bajeti kwa TARURA.
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA hii ikiwa na umri wa miaka minane, kwa kweli imefanya kazi nzuri sana, lakini bado tunatakiwa kuendelea kufanya kazi iliyo bora zaidi na katika kuonesha kwamba tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais katika adhima yake ya kuboresha hali ya miundombinu yetu ambayo yeye anatamani ipitike kwa mwaka mzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi ninawaomba tu watendaji wetu katika ngazi zote kwamba Mheshimiwa Rais anapohangaika usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo, basi na sisi tuoneshe ile nia thabiti na dhamira ya kwenda kumuunga mkono katika kusimamia shughuli hizi za maendeleo ili wananchi wetu waweze kufaidika na jitihada hizi za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijielekeza katika ukurasa wa 25 wa hotuba ya Mheshimwa katika sekta ya madini, pia Mheshimiwa Rais ameonyesha kutambua mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya Taifa letu. Katika hotuba yake inaonesha kwamba kiwango cha mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa, kiliongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 mpaka kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameonesha utayari wa kuwaunga mkono na kuwa-support wachimbaji wadogo kwa kuwawezesha kuwapatia vifaa vya uchimbaji kama vile vya uchorongaji, lakini na taarifa za jiolojia kuonesha kwamba madini yanapatikana wapi? Kwa wingi gani? Ni madini ya aina gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaiomba tu pia Wizara yetu ya Madini iende ikasimamie vizuri eneo hili kwa kuhakikisha kwamba ile mikopo ambayo Serikali inaenda kuitoa kwa wachimbaji wadogo, iende basi kwa walengwa ambao kweli wana uhitaji, mikopo isiende kwa wachimbaji ambao tayari wana uwezo wa kujiendesha wao wenyewe na kuendesha shughuli zao za uchimbaji, na tuende tukawaangalie wale vijana ambao wapo katika hali za kati ambazo sasa wanataka kupambana kuweza kuona kwamba wanaongeza tija ya uzalishaji katika sekta hii ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba hata asubuhi wakati wa michango ya Waheshimiwa Wabunge walieleza kuhusu masuala ya mirabaha ambapo wachimbaji wanaonekana wanatozwa mirabaha mara mbili pale ambapo wanakuwa wameshatoa mawe juu, lakini pale ambapo wanakuwa wameshachenjua dhahabu na penyewe pia dhahabu inaenda kutozwa mrabaha tena kwa mara nyingine.
Mheshimiwa Niabu Spika, kwa hiyo, tuende tukaangalie maeneo haya ili wachimbaji wetu, sisi kule usikumani tunaita wasitegemee tu miganyalo. Miganyalo ni zile posho ndogo ndogo zinazopatikana kwa wachimbaji hawa wadogo wanapokuwa wanachimba katika maeneo yao hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada kubwa ambazo anazifanya na hotuba hii iende ikawe dira kwa taasisi zote za Serikali, taasisi binafsi, Wizara zote, tuweze kwenda kupita humu ambapo Mheshimiwa Rais wetu ameonesha dira kwamba sasa tunataka kuelekea upande gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)