Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sasa kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha wote kuwa ndani ya nyumba hii ya mipango na kutunga sheria za nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumtakia heri, kumtakia fanaka, kumtakia afya njema, kumtakia weledi na maarifa makubwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika siku yake leo ya kuzaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kwa lengo moja la kuongea na vijana wa Tanzania, kuwaelezea kwa nini wanapaswa kumwombea na kumlinda kwa wivu mkubwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, duniani kote wanasiasa hupenda kuwekeza katika vitu ambavyo vinaonekana kwa macho na vinatoa majibu kwa haraka. Ni Tanzania pekee chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mama yetu amewekeza kwenye taaluma ambayo haionekani na ambayo matokeo yake hayatokei kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, nitaenda kwa ufupi, lakini nitatamani kugusa namna ambavyo ameikuta elimu ya Tanzania sehemu ilipo na pahala anapoipeleka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 nilisimama hapa mwanzoni kabisa na nilimwuliza swali Mheshimiwa Profesa Ndalichako kipindi hicho akiwa Waziri wa Elimu, nikamwambia Mheshimiwa Waziri, humu ndani tunasikia taarifa, habari nyingi za kuhusu wale waliofaulu mitihani yao; waliofaulu darasa la saba wakaenda form one, waliofaulu form four wakaenda form five, waliofaulu elimu ya juu ya form five na six wakaenda vyuoni, vipi wale ambao huwa wanatemwa na mfumo darasa la saba, hawafanikiwi kusonga mbele, wanaishia hapo; form four hawafanikiwi kwenda mbele wakaishia hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati natafakari majibu ya Mheshimiwa Profesa Ndalichako kipindi hicho Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nilimsikia kwenye vyombo vya Habari, akiielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufanya mapitia ya mitaala ya elimu na sera ya elimu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema ni nini? Mwaka 2021 Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuta changamoto kwamba watoto wanaohitimu Darasa la Saba ni takribani 1,900,000. Katika watoto hao, ni watoto takribani 900,000 peke yake wanapata fursa ya kwenda Kidato cha Kwanza. Watoto milioni moja takribani wanabaki mtaani, wanabaki vijijini wanakuwa ni mzigo kwa familia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2023 wakati Serikali inafanya mapitio ya Sera na Mitaala ya Elimu, baada ya maboresho yake na kuanza mapema mwaka jana, 2025, ninavyozungumza sasa, hii habari ya kuwaacha nyuma watoto milioni moja wanaohitimu Darasa la Saba inaisha mwaka huu wa 2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2027 Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassana ameamuru kupitia mabadiliko ya sera na mitaala, watoto wote wanaohitimu darasa la saba wanakwenda elimu ya lazima mpaka form four, ule mzigo wa watoto milioni moja waliokuwa wanabaki darasa la saba kuanzia mwakani haupo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie vijana wa Tanzania, wanalo jukumu la kumwombea na kumlinda kwa wivu mkubwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia takwimu za kidato cha nne, wanaohitimu ni kati ya wanafunzi 500,000 mpaka 560,000 nchi nzima. Hawa wanafunzi 500,000 wanaohitimu kidato cha nne wanaokwenda kidato cha Tano ni takribani 100,000 mpaka 150,000. Wanafunzi zaidi ya 300,000 miaka hii yote ya nyuma walikuwa wanabaki mtaani, wanabaki kuwa mzigo wa familia na wazazi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza kwenye elimu ya kati, amejenga vyuo vya kati vya VETA, tunazungumzia ndani ya miaka minne ya uongozi wake, ameshakamilisha na vinatoa mafunzo vyuo 33.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma tulikuwa tunazungumzia vyuo 47 tangu kuumbwa kwa Tanzania. tulikuwa na vyuo vya VETA 47. Ndani ya miaka minne ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejenga na vimeshaanza mafunzo vyuo 33. Tunavyozungumza sasa, Mama ameshatoa shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 65. Vyuo 64 vya wilaya na chuo kimoja cha mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nini anachotazama Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan? Anachotazama ni kwamba dunia imeshabadilika, dunia sasa haimthamini mwanadamu kwa idadi ya digrii alizonazo, inamthamini mtu kwa ujuzi (competence). Wewe umebobea, unao uwezo wa kufanya nini? Kutatua changamoto gani kwenye jamii? Dunia ndiko inapoelekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuwekeza kwenye elimu ya kati, amejenga vyuo vya kati, amejenga vyuo vya VETA bado anatoa mikopo kwenye baadhi ya course kwenye vyuo vya kati. Nataka niwaambie Watanzania wanaonisikiliza, kwamba tunalo jukumu la kumwombea na kumlinda kwa wivu mkubwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye elimu ya juu. Tulikuwa tunazungumzia watoto wanaojiunga na vyuo vikuu takribani 100,000 mpaka 120,000. Tunavyozungumza sasa kwa mwaka ule wa kwanza, acha wanaoendelea na masomo, wanajiunga zaidi ya watoto 205,000. Kwa nini? Kwa sababu miundombinu ya vyuo imeongezeka, wakufunzi, Maprofesa walimu vyuoni wameongezeka, vifaa vya kufundishia vimeongezeka na ufaulu wa watoto kwenye mashule yaliyoboreshwa nao umeongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea hapa, watoto wa maskini wamesoma bure kuanzia elimu ya msingi mpaka sekondari mpaka form six, sasa wanakwenda chuo kikuu. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwaka 2021, na kwa bahati nzuri, nimekuwa kwenye Kamati ya Elimu, na nimeshuhudia bajeti kila mwaka 2021 humu ndani tulipitisha bajeti ya takribani shilingi bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu pekee.

Meshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza sasa Serikali inatumia na imeshakopesha wanafunzi takribani bilioni 919, mategemeo yangu, bajeti ya mwaka 2026/2027 tutakwenda kwenye zaidi ya shilingi trilioni moja kadhaa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu pekee. Mikopo hiyo inakopesha zaidi ya watoto 250,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka vijana wanielewe kwamba tukisema tunamlinda Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunamaanisha kitu gani? Pamoja na mikopo hiyo ya elimu ya juu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaona mbali, ameona dunia inataka wasomi, dunia inataka watu wenye ujuzi (competence), Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunavyozungumza sasa anatoa Samia Scholarship, anapeleka watoto wa Kitanzania mpaka nje ya nchi. Zaidi ya watoto 5119 mpaka sasa wamepata scholarship ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, scholarship hiyo siyo mkopo, ni grant, ni ruzuku, unapewa for free ilimradi uwe umefaulu masomo ya sayansi. Takribani shilingi bilioni 30 imeshakwenda huko. Tunavyozungumza sasa, kuna watoto wamekaa camp pale Arusha wanapigwa msasa kwa ajili ya kwenda nje ya nchi, kwenda kusoma course za sayansi kwenye sayansi, nuclear science, wanaenda kusoma kwenye artificial intelligence, wanakwenda kusoma zile course ambazo tuna upungufu mkubwa au hatuna wataalam nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, haitazami Tanzania kama tunavyoitazama sisi leo hapa. Ameshaona mahitaji ya nchi yetu kwa miaka mingi ijayo, amewekeza kwenye maeneo ambayo yataleta tija,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa, malizia.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: …pengine hata kipindi ambacho yeye hatakuwepo katika Kiti cha Urais.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Nakutakia kila la heri, ninaunga mkono hoja. (Makofi)