Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia jioni ya leo katika hotuba ya Mheshimwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze na kumshukuru Mungu, Muumba Mbingu na Dunia na kila kilichopo, kwa neema kwa kunipa kibali, watu wa Kigoma Kaskazini kunichagua kwa kura nyingi za kishindo. Niseme nawapenda sana wananchi wa Kigoma Kaskazini, na nipo hapa kuwatumikia kwa namna yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimsikiliza Mheshimwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nilimsikiliza vizuri na nimesoma vizuri hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais, kwa mtu yeyote mwenye akili timamu na mwenye kulipenda Taifa lake ilikuwa ni hotuba bora ambayo inaonesha dira ya Watanzania. Sasa Watanzania tunachokitaka, ni utekelezaji wa yale Mheshimiwa Rais aliyoyasema katika hotuba yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza katika hoja mbalimbali nikianza na hoja ya kilimo. Ni ukweli usiopingika kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo katika Taifa letu la Tanzania. Asilimia 80 ya Watanzania wanategemea kilimo, na hata sisi tupo hapa leo wengi, tumesomeshwa na wakulima. Maana yake hatuna budi kama Taifa kuwa na mikakati bora ya kusaidia kilimo chetu, lakini tuwe na mikakati bora ya kupata viwanda ambavyo vitasababisha vijana kupata ajira na kutoka kwenye changamoto ya ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi hapa katika mazao ya biashara, ndani ya Mkoa wangu wa Kigoma tunalima zao la Michikichi. Malaysia kwa historia zao la Mchikichi walichukua mbegu katika Mkoa wa Kigoma, Kata ya Simbo, leo Malaysia ni nchi ya tatu kwa kuzalisha mafuta yanayotokana na mchikichi, lakini ukija Tanzania zao la michikichi ambalo tunalima sana Mkoa wa Kigoma katika Jimbo langu la Kigoma Kaskazini, bado hatujaona manufaa makubwa yanayotokana na zao la mchikichi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali kwamba, katika dira ambayo Mheshimiwa Rais ametupatia kama Taifa twende tukawekeze katika zao la mchikichi, tukawashawishi wawekezaji waje wawekeze viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kigoma tupo mpakani mwa Congo, tupo mpakani wa Burundi. Warundi, Warwanda, na Wakongo wanaweza wakaja wakachukua mafuta yetu na hata nchi nyingine nasi tukawa nchi ambayo tunasafirisha mafuta kwa wingi kutoka Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, ushauri wangu katika zao la mchikichi ni kwamba mpaka sasa hatuna bodi katika zao la mchikichi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia zao la pamba tuna bodi, ukiangalia zao la kahawa tuna bodi, lakini zao la michikichi hatuna bodi. Sasa Mheshimiwa wa Kilimo, ambaye yuko hapa ananisikiliza, ni muda muafaka kuhakikisha kwamba, zao hili la michikichi tunapata bodi, ili tuweze kusimamia kwa ukaribu, tuweze kuzalisha kwa wingi na kuwa nchi ambayo tunasafirisha mafuta duniani na maeneo mbalimbali ya dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie suala zima la afya. Hakuna asiyejua kwamba, afya ni kila kitu kwenye maisha ya mwanadamu. Bila afya hatuwezi kuwa na Taifa ambalo ni imara. Ili tuwe na Taifa imara tafsiri yake ni lazima tuwe na wananchi ambao afya zao zimeimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hotuba ya Mheshimiwa Rais ameonesha dira ya kuanzisha bima ya afya kwa Watanzania wote na ni kiu ni kuhakikisha kwamba, wote tunapata bima ya afya kwa sababu, tukienda kwenye majimbo yetu sisi ni mashahidi, vijijini kuna watu wanapoteza maisha kwa sababu, wamekosa pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu anakwenda hospitali hana bima hana pesa, tafsiri yake ni anaweza akapoteza maisha kwa sababu ya umasikini wake. Kwa hiyo, kama leo tutakwenda katika mpango wa Bima ya Afya kwa Watanzania wote itawasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi hapa natamani sana kupendekeza, inawezekana sana kama Taifa tukaweza kuwatibu Watanzania wote bure, inawezekana kabisa. Kwa mfano, ndani ya chama changu tulitoa solution kwamba, katika pato la Taifa hata tukitenga asilimia mbili pointi tano ya kuweza kuwasidia Watanzania tunaweza tukahudumia Watanzania milioni 11 ambao watapata bima ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi naamini kabisa kama tutajipanga vizuri, na kama Mheshimiwa Rais alivyotuambia Watanzania, natarajia tunakokwenda mbele huduma za afya zitakuwa bora. Tunaposema sema huduma ya afya hatuzungumzii majengo pekee yake, shida ya Watanzania ni majengo na huduma bora ya afya. Sera inasema kila kata kutakuwa na kituo cha afya, lakini sasa kuna maeneo ambayo hata ndani ya jimbo langu, hatuna vituo vya afya, kuna vijiji ambavyo hatuna hata zahanati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani ni fursa, kupitia Hotuba hii ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inatoa matumaini kwa Watanzania tujitahidi. Mawaziri ambao mmepewa dhamana kusimamia hizi Wizara twende tukahakikishe kwamba, tunaboresha huduma bora ya afya. Moja ya kero kwenye afya ni suala la wananchi kuzuiwa kutoa maiti hospitali. Mheshimiwa Rais amesema kwamba, watu wapewe maiti, lakini watafute waende wakalipe deni.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua nia ya Rais ni njema, kuwasaidia Watanzania, lakini mnaonaje tukawasaidia hata tukafuta kabisa tozo ya kutoa maiti hospitali?
Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana kwa sababu, leo imagine, labda mimi nimefiwa na mume wangu halafu narudi nyumbani, mmenipa mwili nikazike, nina-stress za kufiwa, halafu natafuta hela ya kwenda kulipa deni hospitali. Katika hali ya kawaida inahitaji Roho Mtakatifu, lakini siyo kazi rahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natamani sana, sisi kama Wabunge, katika hili tuwasidie wananchi ikiwezekana tufute kabisa kodi ya kutoa maiti. Tukiamua tunaweza, kama Taifa, kuwasaidia Watanzania, mtu amekufa... (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiza, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Engineer Aisha Ulenge.
TAARIFA
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpe hii taarifa mzungumzaji kwamba, anapokuwa anachangia ajue the logic behind bima ya afya. Tutakapokwenda kuingiza bima ya afya, wananchi wote wakawa wanatibiwa kwa bima ya afya issue ya maiti kuzuiwa itakuwa haipo. So, anatakiwa a-read between the lines katika kupata concept halisi ya bima ya afya, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiza, taarifa unaipokea? Ahsante.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, taarifa hiyo siipokei na tusichangie kwa mihemko, lengo letu ni kujenga kama Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ametoa hili, lakini kwa ushahidi, leo kuna hospitali ambazo bado watu wanazuiwa maiti. Kwa hiyo, ninapochangia hapa, lengo langu ni jema katika kuhakikisha kwamba, tunawapunguzia mzigo Watanzania na tusilete mihemko wala matabaka ya chama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninazungumzia suala hilo la maiti, kwa hiyo, mimi natamani Watanzania tuwapunguzie mzigo...
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa Husna.
TAARIFA
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Mbunge haruhusiwi kuzungumza hoja ambayo hana ushahidi nayo, kwa sababu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwamba, ndani ya siku 100 hataki kuona maiti inazuiliwa na alitoa maelekezo namna ya kufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hilo sasa kama Mheshimiwa Mbunge ana ushahidi na hospitali ambayo imezuia maiti ni vizuri akatupatia, ili kuweka takwimu sahihi, nashukuru (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taarifa ya Mheshimiwa Mbunge unaipokea? Muda pia umeisha, umalizie, ahsante.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa hiyo siipokei na ninaendelea kusisitiza, lengo langu ni kuhakikisha kwa pamoja, sisi na Mawaziri tumsaidie Mheshimiwa Rais. Hospitali zote ambazo bado watu...
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
WABUNGE FULANI: Aaah!
MBUNGE FULANI: Mnapoteza muda.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umeisha, naomba umalizie sentensi ya mwisho.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba unilinde, kwa sababu wameniingilia, naomba uniongezee dakika mbili.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika Taarifa. Hatujamwingilia, sisi hatuna uwezo wa kumwingilia.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, Taarifa ni sehemu ya kuchangia.
Mheshimiwa Jacqueline sijakuruhusu. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, unapotoa taarifa kwa Mbunge anayechangia, hakuna muda wa ziada. Taarifa ile ni kwamba, unamwongezea au unatoa ufafanuzi kutokana na hoja anayosema. Kwa hiyo, muda umeisha, malizia sentensi ya mwisho Mheshimiwa.
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, sikutumwa na Wana-Kigoma Kaskazini kuja kubishana, nimekuja kujenga hoja. Mwisho ni suala zima ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushukuru kwa sababu, alitoa maelekezo, akina mama wajawazito wanaoambiwa wapeleke beseni, wembe, mpira, mpaka kibana kitovu cha mtoto, sasa ni marufuku. Ni muda wetu kuhakikisha kwamba, hawa akina mama kweli, wakienda hospitali wanapata hivyo vifaa na kupata huduma iliyo bora. Ahsante. (Makofi)