Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia hoja ambayo iko Mezani ya Hotuba ya Ufunguzi wa Bunge kutoka kwa Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kweli, ni bahati iliyo njema, ni tajamara na sudi kupata nafasi ya kuingia hapa katika Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo jambo rahisi. Sisi sote tunajua tuliyopitia huko, kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu tumeweza kufika hapa kuwawakilisha wananchi wetu. Wananchi wametutuma hapa tusemee changamoto zao, tushukuru kwa tuliyoyapata na tuendelee kuomba tena, ili changamoto za maendeleo zipunguke, ziondoke.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nami nashukuru chama changu kwa imani, pamoja na wajumbe na wananchi wa Kilombero kwa kunipa dhamana hiyo. Kama walivyosema Wabunge wengine, nami nasimama hapa katika Bunge lako Tukufu kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa yale makubwa ambayo ametufanyia na anayoendelea kutufanyia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyosema wenzangu, tunaona Mawaziri wakihangaika kila kona chini ya kiongozi wao, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, wakipambana katika kuhakikisha nchi yetu inaenda kwa usalama na amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana na wananchi wa Kilombero wameniambia, Mheshimiwa Asenga tunakutuma mara ya pili, nenda kashukuru, tulikuwa hatuna barabara ya lami. Hapa kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais, ukurasa wa 28, anazungumzia habari za barabara za lami kwa majimbo ambayo hayajapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunajua adha ya kukosa barabara ya lami na barabara hiyo ilikuwa chini ya Wizara ya Fedha, wakati huo Mheshimiwa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu alikuwa Waziri wa Fedha, ndiyo ilikuwa barabara pekee iko chini ya Wizara ya Fedha, siyo Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumza tuna kilometa 67 za lami tunateleza tu. Wananiambia, Mheshimiwa Asenga nenda kashukuru, kamshukuru Mheshimiwa Rais. Tunawashangaa hao watu wa mjini huko wanavyoleta vurugu, sisi hatutaki vurugu na ndiyo maana Kilombero, tarehe 25 ile, sijui 26, tulikuwa salama na amani. Vijana wa Bodaboda walikuja kwangu, hasa wale pale Msikitini Mjini, wananiambia mwambie OCD Mheshimiwa Asenga, Mbunge, sisi hatuna nongwa, kwa nini anatuambia tufunge saa 12?
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunataka amani, sisi watoto wa masikini, tukiendesha bodaboda ndiyo tunakula. Tukiendesha bodaboda, tukitoka ndiyo nguo zetu zinafuliwa. Sisi tunalinda amani. Kwa hiyo, wamenituma, kazi yangu kubwa hapa ni kuja kusema ahsante kwa yale ambayo tumeyapata na kusema tunaomba tena kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu Wilaya inaundwa sisi hatuna Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya; leo ninavyozungumza na wewe, tunayo hospitali hiyo, na Mheshimiwa Rais ametuletea shilingi milioni 800 tunajenga wodi ya akina mama, wodi ya watoto na wodi ya wanaume. Mwenyezi Mungu ambariki sana Rais Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tulisimama hapa katika Bunge lililopita, tukasema umeme unakatika sana. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezungumzia hiyo, ametuletea shilingi bilioni 25, tumejenga substation Kilombero na Mheshimiwa Rais amefika pale, umeme haukatiki tena Ifakara. Mwenyezi Mungu amlinde sana Rais Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamsihi na kumnasihi Rais wetu, Mwenyezi Mungu amjalie kifua kikubwa, kwa sababu Mwenyekiti wangu wa vijana Mheshimiwa Sadifa ametoka kusema hapa; alikuwa Mwenyekiti wetu wa Vijana wa Taifa, tulikuwa tukienda naye, na anatutuma twende tukawatetee Marais waliopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mijadala mbalimbali tunamwambia Mheshimiwa Rais asife moyo kwa sababu kuna wananchi hawatampenda wote, lakini hawatampenda kwa hulka zao. Tuliona hivyo kwa mzee wetu Mkapa, yalizungumzwa yaliyosemwa; tuliona kwa mzee Jakaya, amekuwa madarakani anamaliza kipindi chake, maneno yote, mzee anaondoka madarakani watu wanakumbuka mazuri yake kwamba hata kilometa 11,000 za lami alifanya yule mzee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwambia Mheshimiwa Rais, kama walivyosema kwa Rais Dkt. Magufuli, na wanaendelea kusema hana jema, wapo. Sasa sijui kama wanasemea gerezani au wanasemea wapi? Lakini wanaendelea kusema, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli hana jema, pamoja na Mwenyezi Mungu kamchukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Samia atafanya atamaliza, kuna watakaomshukuru na hao watakaoendelea kusema maneno yake. Tunamwomba Rais wetu asife moyo, yasimnyong’onyeze, kwamba anakata tamaa, ndizo hulka zetu sisi. Atakapomaliza, mwaka mmoja akija Rais mpya utasikia hakuna kama Samia hapa. Kama tulivyozungumza, hakuna kama Mheshimiwa Dkt. Magufuli, kama tulivyosema hakuna kama mzee Jakaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninasema hapa kumpa moyo Rais wetu, kumwambia akaze buti asonge mbele. Madhali akijithibitishia yeye ni muislam. Wazanzibar hawa wenzetu katika Muungano ni watu wema kweli. Ukienda Zanzibar mtu anaweza akakupeleka hata kilometa tano anakuonyesha sehemu ambayo wewe huijui. Ni waungwana. Wasivunjike moyo kwa changamoto hizi tunazozipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi na wananchi wa Kilombero hatuwezi kumbeza Rais wetu kwa sababu kuna mtu yuko nje ya nchi huko kasema sijui kuna wizi sijui kuna namna gani? Yeye na familia yake, watu wanaibeza, Rais wetu asivunjike moyo. Rais akisema mtoto wake akae sehemu hapa apate nafasi, maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kama mimi mtoto wa fundi cherehani ninapata nafasi Bunge la kwanza kuteuliwa kuwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Wanu tuko naye kipindi cha tatu, kupewa Unaibu Waziri nongwa mpaka mnaandika huko kwenye mitandao, nongwa! Nchi imeuzwa, wameuza watoto, hivi Abdul leo ukimwangalia na wema wake ule, anavaa sandals na kanzu atauza nchi yetu!
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndiyo waliyoyasema wakati wa Ridhiwani hapa, brother wangu. Ridhiwani aliambiwa magorofa ya bandari; hata nilikuwa sijui wakati ule kama ya bandari. Nikamwuliza, mzee maghorofa yale mapacha ya kwako kumbe, mimi ninakufa njaa tu hapa! Nitoe bwana. Akasema, uongo tu. Kila mali ya Ridhiwani. Leo kiko wapi? Tunakula pamoja naye canteen pale brother wangu. Kwa hiyo, akina Abduli hawa Mungu awape nguvu tu, haya yatapita tutasonga mbele pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, niseme kwamba sisi tunataka kufungua Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro. Tumesaini Barabara ya Ifakara kwenda Malinyi baadaye itakwenda Songea. Tumesaini Barabara ya Ifakara kwenda Mahenge, Lindi, tumesaini Barabara ya Ifakara kwenda Mlimba. Ee, Mwenyezi Mungu ninakuomba umjalie Rais Samia apate fedha barabara hizi zianze, wananchi wetu wapate raha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake amesema kwamba uwekezaji mkubwa wa dola bilioni 42 unakuja katika gesi, tunaunga mkono. Tunaunga mkono uwekezaji wa Bandari ya Bagamoyo iunganishe na Kwala, SGR iende katika Bandari ya Dar es Salaam. Tumeokoa shilingi bilioni 256 katika uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulibezwa hapa, tulitukanwa, mjadala ulikuwa nchi nzima kuhusu uwekezaji wa bandari. Leo nani anasema kwamba tumeokoa shilingi bilioni 256? Hakuna. Ninarudia kumpa nguvu Mheshimiwa Rais, ninamwambia akithibitika mbele ya Mwenyezi Mungu jambo hili akiulizwa na Mwenyezi Mungu siku ya hukumu anaweza kujitetea, lina maslahi na wananchi wa Tanzania, alifanye, asirudi nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wataendelea kupinga na kusema; na madhali Mwenyezi Mungu sio Athumani, tumepata mifano ya nchi nyingine hapo yametokea kama ya Tanzania. Watanzania wameamka sasa, wanasema kumbe nchi yao inachochewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, alikuja Mheshimiwa Rais Kilombero akatuzindulia kiwanda cha sukari. Wananchi wamesema tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa uzinduzi wa kiwanda cha sukari, lakini nikamwambie Mheshimiwa Rais, tunaomba bei ya sukari ichangamke ili wakulima wa muwa tuweze kulipwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami ninawasilisha katika meza yako hapa, na Waheshimiwa Mawaziri wako hapa, Mheshimiwa Rais alikuja pale. Mheshimiwa Rais alipita na mimi nikachomekea, kwamba, kuna kiwanda cha Mang’ula Mechanical and Machine Tools, kikianza kupata mwekezaji vijana wetu wengi watapata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema mbele zako hapa, kiwanda kile kikianza wananchi watapata ajira na vijana wangu watapata ajira. Bunge lililopita Mheshimiwa Rais amenisaidia fedha kupitia TANESCO, shilingi milioni 400 ku-control mto unaopita Ifakara Mjini, kujenga tuta upande mmoja, kuelekeza maji Mto Kilombero ili maji yaende katika Bwawa la Mwalimu Nyerere ili tupate maji ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamenituma baada ya kushukuru niseme hapa, bado shilingi milioni 400 za kujenga tuta upande wa pili ili tuendelee kuthamini chama chetu, tuendelee kumthamini Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)