Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bahi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KENETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa nikushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaanza kwa kuunga mkono hotuba hiyo. Pia nichukue nafasi hii kwa dhati niwashukuru wananchi wa Jimbo la Bahi kwa imani kubwa waliyoionyesha kwangu na kunirejesha tena katika kipindi hiki cha pili. Nami ninataka niwahakikishie kwamba nitawatumikia kwa moyo thabiti kabisa kulinda imani ile ambayo wameionyesha kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi kile cha miaka iliyopita ambayo amefanya kazi kubwa, na sasa wananchi wameonyesha imani, walimpa kura za kutosha ili kuweza kuwatumikia kwa kipindi cha miaka hii mitano mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita zaidi katika suala zima la sekta ya kilimo. Mheshimiwa Rais aliweza kutoa nukuu kwamba kilimo ni biashara, mkulima ni mwekezaji. Kupitia katika hotuba yake, aliweza kuainisha zaidi kwamba Serikali ambayo alikuwa anaahidi kwamba ataenda kuchagua watendaji wawe thabiti katika kusimamia, ni vipengele na malengo ambayo ameweza kuyaainisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi yetu 75% ya Watanzania ni vijana chini ya miaka 35, lakini kila mwaka workforce inayoingia ni kiasi cha Watanzania 800,000 mpaka 1,000,000, inakuwa ni workforce ambayo iko tayari kwa ajili ya kuingia kwenye sekta hasa ya kilimo ambayo inaajiri Watanzania wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake alisema kwamba pamoja na mambo mengine anakusudia kuanzisha kitu kinachoitwa Youth Investment Window. Lengo lake kwanza anasema ni kutoa shilingi bilioni 200 ambayo itasaidia katika kuwekeza kwa vijana na wanawake kuingia kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona fedha nyingi zimewahi kuja wakati wa kilimo kwanza na maeneo mengine tukazipeleka kwenye mabenki. Hata hivyo, ninaishauri Serikali kwamba ije na model ambayo kweli itasaidia vijana wetu waweze kujiajiri kwenye kilimo. Jambo lingine ambalo Mheshimiwa Rais alisema ni kukuza kilimo kutoka asilimia nne mpaka 10%, ambao ni mkakati wa ten – thirty. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumebakiwa na miaka mitano tu kufikia 2030. Ninaiomba sana Serikali kupitia Wizara ya Kilimo wafanye mapinduzi makubwa, na watambue kwamba 85% ya Watanzania bado wanatumia jembe la mkono. Kwa hiyo, ipo haja ya makusudi kabisa kwamba tutoke katika mkwamo ule ambao mimi ninasema bado upo, sasa tufanye mapinduzi makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kununua matrekta kwa pamoja lakini yapo majembe yanayokokotwa na ng’ombe, hapa tunaweza tukafanya. Tuna viwanda vyetu hapa nchini vinavyozalisha na bei yake ni kuanzia shilingi 160,000 mpaka shilingi 200,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukitoa kodi zote tukaweka na ruzuku, wananchi wetu wanaweza kununua majembe haya kwa shilingi 80,000 mpaka shilingi 60,000. Lengo lake ni nini? Unaongeza workforce ambapo utakuwa umerahisisha wananchi waweze kuzalisha zaidi kupitia majembe yanayokokotwa na ng’ombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jambo ambalo Mheshimiwa Rais amelionesha kwenye hotuba yake ni kufanya kilimo kivutie kwa kuajiri vijana wengi, lakini hawawezi kuwaajiri vijana hawa kwa kupitia jembe la mkono. Huwezi ukawaajiri vijana hawa kwenye kilimo kwa kutegemea mvua na amesema kabisa ni lazima tujikite katika kilimo chaa umwagiliaji pamoja na kilimo cha mbogamboga (horticulture).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaiomba sana Wizara ya Kilimo kupitia bajeti inayokuja ya Mwaka wa Fedha wa 2026/2027 tuone mapinduzi makubwa sana, hasa ni namna gani fedha zimetengwa kwa ajili ya kwenda kuwaingiza vijana katika sekta nzima ya uzalishaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina fursa kubwa. Sisi tunategemewa na nchi za SADC katika kuwalisha chakula, hususan mahindi na mchele. Ipo haja kubwa ya nchi yetu kuweka kipaumbele kikubwa katika kuzalisha. Jambo hili linaenda na Dira ya Taifa ambayo na yenyewe inaongelea habari ya uzalishaji mkubwa wa kilimo. Kwa hiyo, kwenye suala zima la kilimo na nchi yetu tukitaka iajiri watu wengi ni lazima tuweke utaratibu wa makusudi tuweze kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya kuajiri vijana kwenye kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Mheshimiwa Rais anaongea habari ya kukuza viwanda, nami ninataka niseme kwa mkoa huu wa Dodoma, Serikali iangalie Dodoma iwe ni logistic hub. Kwanza, tuna miundombinu ya reli ya kisasa (SGR) ambapo tutaweza kusafirisha mizigo yetu kwa urahisi hapa, lakini Serikali inajenga kiwanja kikubwa cha Kimataifa hapa Msalato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha kiwanda cha mbolea ambacho kina wafanyakazi kama 2,000 lakini viwanda vikubwa Dodoma bado hatuna. Mji huu ni mji mkubwa, lakini ni mji wa kutegemea mshahara mwisho wa mwezi. Hatuna mzunguko mkubwa wa fedha za viwanda. Ni bora Serikali iweke scheme makusudi ya kuweza kuongeza viwanda katika mji wa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja 100%, ahsante sana.