Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa asilimia nyingi za uchaguzi wa Oktoba, 2025. Tunampongeza sana kwa kuaminiwa na wananchi kwa kura nyingi na sisi tunamtakia heri sana katika majukumu yake, na bahati nzuri, leo ninachangia ikiwa siku pekee ya kuzaliwa kwa Mheshimiwa Dkt. Samia. Nami ninamtakia heri katika siku yake hii muhimu ya kuzaliwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru kipekee sana wananchi wa Jimbo la Busega kwa kuniamini tena kwa mara ya pili kuwa mwakilishi wao hapa Bungeni. Nitawatumikia kadiri Mwenyezi Mungu atakavyonijaalia, ninawashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nichangie kidogo maeneo machache juu ya hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa kwetu iliyokuwa na dira na mpango wa kufika 2030 kama alivyohutubia mahali hapa na tunaamini kabisa Mheshimiwa Rais ataenda kufanya kazi kubwa kwa sababu tumeona mfano katika miaka hii yake mitano iliyopita. Tumeona maendeleo makubwa kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Busega tumeona maendeleo makubwa, (vituo vya afya vinne, hospitali ya wilaya imekamilika, mradi wa maji mkubwa, barabara zimetengenezwa, bajeti ya barabara imeongezeka kutoka shilingi milioni 714 mpaka shilingi 2,447,000,000. Hizi ni juhudi kubwa za Dkt. Samia kwa wananchi hususan wananchi wa Busega. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Busega wamenituma nimshukuru kwa niaba yao kwa miradi mikubwa kwa hii miaka mitano ambayo alikuwepo. Tuna imani kubwa yale aliyoyaahidi katika hotuba yake yanaenda kufanyika kwa sababu ya namna aliyofanya kwa miaka ile mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niseme kidogo eneo la nishati. Ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa 29 utaona namna gani amejipanga katika eneo la nishati hasa katika suala zima la umeme. Sasa tuna vitongoji ambavyo vina umeme 39,003 kati ya vitongoji 64,359 vya nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ukiangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Rais amesema ifikapo 2030 vitongoji vyote vitakuwa na umeme na haya yanajionesha sasa hivi. Kwa nini, ninasema yanajionesha sasa hivi? Miradi inayoendelea katika vitongoji vyetu ni vitongoji 2,562 ambavyo miradi yake inaendelea itakayoenda kupatiwa umeme na itakapokamilika, tutakuwa tumebaki na vitongoji takribani 22,000 plus ambavyo vitakuwa havina umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuona kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia yuko serious na kazi, ukitaka kuona Mheshimiwa Dkt. Samia amedhamiria kazi katika eneo la nishati, kama alivyosema ifikapo 2030 vitongoji vyote vitakuwa na umeme. Sasa tarehe 17 Januari, 2026 tumesaini vitongoji 9,009 kupelekewa umeme katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia ongezeko la vitongoji 9,009 ni kubwa sana na vitongoji sasa baada ya mradi huu wa vitongoji 9,009 kukamilika tutakuwa tumebaki na vitongoji 13,785 ambavyo vitakuwa havina umeme. Kwa kasi ya Mheshimiwa Dkt. Samia kama tumeanza mwezi wa 11, ameapa, na leo ni mwezi wa kwanza, ni miezi miwili plus. Siku zake 100 tumesaini mkataba wa vitongoji 9,009, maana yake vitongoji 13,785 vilivyobaki sidhani hata kama 2030 itafika ukiangalia katika hotuba yake alivyosema 2030.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina imani kwa kasi hii aliyonayo Mheshimiwa Dkt. Samia inawezekana isifike 2030, vitongoji vyote vitakuwa na umeme kama ambavyo tumeona kasi yake kubwa katika maeneo yetu. Hii inadhihirisha kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia amedhamiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inadhihirisha kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia amedhamiria. Ukisoma dira yetu ya 2050 ambayo imetolewa hivi karibuni, imeonesha ifikapo 2050 mwananchi mmoja atakuwa anatumia kilowatts 3,000 kwa mwaka ikilinganishwa na sasa hivi mwananchi moja anatumia kilowatts 170 kwa mwaka. Ongezeko hili ni kubwa na ukiona hivyo maana yake Mheshimiwa Dkt. Samia amedhamiria kwa wananchi wake katika eneo la nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Dkt. Samia anaingia, eneo la nishati uzalishaji wa umeme katika nchi yetu ulikuwa megawatts 1,685. Tunavyozungumza, leo uzalishaji wa umeme sasa umefikia megawatts 4,100. Haya ni mapinduzi makubwa na dhamira kubwa ya Mheshimiwa Dkt. Samia kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wanabusega tunampongeza na tunamtakia heri katika utekelezaji wa haya ambayo tunayapanga kwa miaka ile mitano kufikia 2030. Tunaye Waziri Mkuu mchapakazi, na tunao Mawaziri, tumeona namna ambavyo wamepokea kazi kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia. Ninaamini watafanya vizuri na kuyafikia yale malengo makubwa ya Mheshimiwa Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ninataka kusema, ukisoma ukurasa wa 25 mpaka 26 amezungumzia eneo la madini. Tumeona wazi eneo hili pia tumelitengeneza vizuri na tumekua na uzalishaji mkubwa wa madini katika nchi yetu. Katika maeneo ya madini tunaona pato la Taifa limeongezeka kutoka 6.8%, mwaka 2012/2013 mpaka kufikia 10.1% mwaka 2024/2025. Haya ni mapinduzi makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia ukusanyaji wa maduhuli umetoka shilingi bilioni 173.7 mwaka 2012/2013 mpaka kufikia shilngi trilioni 1.057 mwaka 2024/2025. Haya ni mapinduzi makubwa katika nchi yetu ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia amedhamiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa huko nyuma tulikuwa hatuna mfumo wa kununua dhahabu kupitia BOT. Sasa tunavyozungumza leo Mheshimiwa Dkt. Samia ameanzisha mfumo wa kununua dhahabu kupitia Benki yetu ya Tanzania (BOT).
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyozungumza, miezi kama miwili iliyopita, taarifa zilivyotoka tayari tumekusanya tani 16 kwa miezi 14 na hizi ni taarifa za miezi miwili iliyopita. Leo tumefika tani 17 na kufanya nchi yetu sasa itapanda kutoka aliposema Comrade Festo pale asubuhi, nchi ya sita. Nchi ya sita ni pale tulipokuwa na tani 16. Ninaamini watakapotengeneza taarifa za sasa, kwa sababu tumeshafika tani 17 tutapanda zaidi hata kuwa wa nne Barani Afrika. Haya yote ni mapinduzi makubwa ya Mheshimiwa Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ukurasa wa 26 wa hotuba yake, tunaenda kununua mashine ya kuchenjua madini (multipurpose refinery) na hii tunaenda sasa kuwasaidia vijana katika suala zima la kupata ajira. Watapata ajira vijana, lakini uzalishaji wa dhahabu pia utaongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikwambie nini faida ya ununuzi wa dhahabu kupitia BOT? Bei imepanda na sasa wananchi wanaona ni bora kuuza dhahabu kwa kupitia mfumo wa BOT kuliko kuuza dhahabu zao kwa wafanyabiashara wengine kwa sababu bei imeongezeka. Wananchi wetu sasa kama BOT siku hiyo hainunui dhahabu, wanaacha kuuza wanasubiri mpaka siku ambapo BOT itatangaza mnada wa dhahabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni maono mazuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia kwa ajili ya wananchi wetu hasa wachimbaji wadogo wadogo wanaonufaika na bei ya dhahabu ambayo inanunuliwa kupitia mfumo wetu wa BOT.
Mheshimiwa Naibu Spika, tungekuwa nje ningepiga makofi kwa ajili ya Mheshimiwa Dkt. Samia ili aone namna gani dhamira aliyonayo na sisi kama Wabunge tunamuunga mkono. Kazi yetu kubwa tumuunge mkono Mheshimiwa Dkt. Samia, Waziri Mkuu na Mawaziri ili kuyafikia malengo ya Mheshimiwa Dkt. Samia kwenye eneo la nishati na eneo la madini. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)