Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuongea tena mara ya pili katika siku ya leo. Nimefurahi sana kuongea leo ili nami pia niweze kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Siyo hivyo tu, kumpongeza kwa birthday yake leo na kweli hata kama hatupo huko, lakini tumemtakia birthday njema siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninampongeza sana Mheshimiwa Spika na wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuliongoza Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nitoe shukrani nyingi kwa Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuingia Bungeni, nafasi ambayo niliipambania kwa miaka 10 bila kupata, lakini sasa nimefanikiwa kuingia Bungeni. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru wanawake wa Dodoma kwa kuweza kuniamini na kunipa kura nyingi sana. Kati ya kura 1,581 niliweza kupata kura 1,524. Kwa hiyo, ninawashukuru sana wanawake wa Dodoma, wameniamini sana na mimi nitawawakilisha vyema Bungeni. Siyo hivyo tu, nitafanya utumishi uliotukuka kuweza kuwatumikia wanawake wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitamani sana kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais, niliiona ni hotuba ya kiongozi tena iliyo thabiti kabisa, kiongozi mwenye madaraka, lakini upande wa pili ili-sound kama hotuba ya mama tena mama mlezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niongee maeneo machache ambayo ninamsikia Rais wangu akiongea kama mama. Pale alipoingia tu na kuanza hotuba yake kwa kuonyesha masikitiko yake kwa matukio yaliyotokea Oktoba 29, hiyo ilikuwa ni sauti ya mama. Pia, alipoendelea kuwasamehe wale vijana ambao waliingia kwenye mkumbo hiyo pia ilikuwa ni sauti ya mama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, aliongea sasa kama mama, akasema, nikimaliza nafasi yangu sipendi kusemwa kwa majengo, miundombinu, barabara, maghorofa, lakini niache tabasamu kwa Watanzania. Hiyo niliona ni sauti ya mama ndani ya hotuba ya Rais wa nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ilikuwa ni dira yetu ya miaka mitano ambayo tutaifuata na inaenda sambamba kabisa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Niliona Rais ame-summarize Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye hotuba fupi aliyoitoa kwenye Bunge lako Tukufu hiyo tarehe 14, Novemba, 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijikite kwenye hotuba hiyo na mawazo yangu niyatoe kwenye uchumi na uwekezaji wa wananchi. Amesema: “malengo yetu ya kiuchumi ni kupandisha kasi ya ukuaji wa uchumi kutoka 5.6% hadi zaidi ya 7%.” Kwa hiyo, alikuwa na maana kwamba economic growth yetu itaenda zaidi ya 7%. Pia, akasema kwamba itaongeza ukuaji wa huduma za kijamii ambazo ni muhimu sana, hata tuzo nyingi amepata kwa ajili ya huduma za kijamii, kujenga hospitali, kujenga zahanati mpaka vijijini, kujenga vituo vya afya na kujenga hospitali za rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu hahitaji kutoka mkoa kwenda mkoa mwingine tayari hospitali za rufaa zimejengwa kwenye kila mkoa na hapo moja kwa moja ameokoa maisha ya mwanamke na mtoto. Hivyo, wanawake tumerefushiwa maisha yetu, hatufi mara nyingi kwa kujifungua au kwa njia ya uzazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais huyu mwanamke amejipambanua kwa kutujengea vituo vya afya na zahanati kuanzia chini vijijini, kwenye tarafa zetu, kwenye wilaya zetu na hospitali za rufaa zipo kwenye kila mikoa yetu. Hivyo, kongole nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, amejikita katika kujenga miundombinu wezeshi ya kiuchumi. Hapo ndiyo tunaona barabara, madaraja yanajengwa, anafanya uwekezaji rafiki ili tuweze kufanya maendeleo ya kiuchumi. Nami ninampongeza tena Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano. Pia, anasema ataimarisha masoko na mitaji na kuhamasisha uwekezaji wa ndani, anatia moyo Watanzania kuwa wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa tunafikiri wawekezaji ni wazungu. Mzungu akija ndio anatetemekewa kuwekeza, lakini sasa hivi tunatiwa moyo wawekezaji wa ndani kuwekeza kwenye viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi. Ana kitengo maalumu cha kuwatia moyo wawekezaji wa ndani, lakini akigusa moja kwa moja, ni kutia moyo shughuli zetu za madini, na pia kuwawezesha au kuwadhamini mikopo hao wawekezaji wa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami niseme tu ukweli tumaini hili ni kubwa sana kwa wanawake na vijana pamoja na watu wa makundi maalum kwa sababu zile 10% za kila halmashauri bado zinaendelea. Alipotamka hivi tu, nafikiri wanawake na vijana wote tulifurahi. Hilo ni tumaini kubwa sana kwa wanawake wa Kitanzania kwamba tutaendelea kupata hizo 10% za mikopo, na bado ataendelea pia kufanya mifuko yote ya uwekezaji iliyo chini ya ofisi yake ya kiuchumi, yapata mifuko 74, nayo pia itaendelea kuwasaidia wanawake, vijana na makundi maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Dodoma sisi tumenufaika sana na hizi 10%. Kwa miaka minne tu wanawake wamepokea shilingi bilioni 1.6, kwa Dodoma Mjini peke yake. Siyo hivyo tu, tumeendelea kunufaika na mifuko kama TASAF na tumeenda kunufaika na mifumo mingine kama Women Development Funds. Kwa hiyo, sisi tunaendelea kunufaika na mambo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutuwazia vizuri wanawake, vijana pamoja na makundi maalum kwenye jamii yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, ni hilo tumaini sasa la shilingi bilioni 200 ambazo nazo pia zinaenda kwa wajasiriamali wote, lakini wanufaika wakubwa watakuwa ni hao hao wanawake, vijana na makundi maalum pamoja na wazee wameongezwa hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapongeza sana hotuba hii, ina mashiko. Tunawaomba tu watendaji kwenye Wizara mbalimbali na sekta mbalimbali watumie vizuri maneno haya yaliyowekwa kwenye hii hotuba ili wanufaika wawe watu wote ikiwepo wanawake wote hasa wa vijijini. Tukiwa kwenye kampeni, tulipokwenda vijijini, wanawake wengine hawajawahi kusikia na kupata hii mikopo. Hivyo basi, yatengenezwe mazingira rafiki ambayo mikopo hii itaweza kuwafikia wanawake waliopo vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, elimu hiyo ya fedha ambayo tuliongea hata asubuhi iendelee kutolewa mpaka kule vijijini ili wanawake, vijana na makundi haya maalum yaweze kupata elimu ya fedha ili sasa waweze kurasimiwa biashara zao na waweze kukopesheka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono sana hotuba ya Rais wangu mpendwa kabisa. Mungu ambariki, ampe maisha mema na leo ni birthday yake, tunamhitaji akiwa na afya njema aendelee kufanya majukumu yake, ahsante sana. (Makofi)