Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nami ninaanza kwa kushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wa Wanasikonge, kwenye hotuba hii nzuri ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningeomba kabla sijaendelea, uniruhusu niweze kutoa tathmin ndogo sana ambayo niliiona kwenye jimbo langu nilipotembelea wakati ninawashukuru wananchi kwa kazi kubwa waliyoifanya tarehe 29 Oktoba, 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Sikonge lina jumla ya kata 20, vijiji 71, vitongoji 287 na kwa sasa lina wakazi 372,800 na hii ni kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 pamoja na projection rate ya asilimia 3.1 Kwa hiyo, kwa hivi sasa tuko 372,800. Katika jimbo langu hilo niliweza kutembelea kata zote na nilibahatika kufanya mikutano zaidi ya 46. Ninafurahi kusema kwamba idadi ya watu walioongea wao wenyewe kwenye mikutano hiyo walifika 678. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema kwamba kati ya hao watu 678 watu 230, sawa na 34%, waliongelea changamoto ya barabara katika maeneo yao. Vilevile, watu 142 sawa na 21%, waliongelea ufinyu au upatikanaji wa maeneo ya shughuli za kiuchumi katika wilaya yetu ya Sikonge.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, watu 88 waliongelea changamoto ya maji ambao ni sawa na 13%. Pia 12% sawa na watu 81, waliongelea changamoto ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya pamoja na upatikanaji wa madawa. Hali kadhalika, watu 54 sawa na asilimia nane, waliongelea sekta ya elimu na hasa waliongelea juu ya umaliziaji wa majengo ya shule, uchakavu wa madarasa pamoja na upungufu wa walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wengine watu 34 waliongelea mambo mengine ikiwemo utawala bora, athari za wanyamapori, upatikanaji wa mbolea na hususan ya ruzuku, vilevile mawasiliano na hasa ujenzi wa minara ya simu, hicho ndicho nilichokiona huko jimboni kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija sasa kuchangia hoja. Kwanza kabisa, wananchi wa Jimbo la Sikonge wanampongeza sana na wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mambo makubwa aliyowafanyia Wanasikonge. Sisi Wanasikonge ni wakulima, Mheshimiwa Rais amefanya jambo kubwa ambalo hatukulitarajia wala halikuwa katika ndoto zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na shida ya mbolea, lakini Mheshimiwa Rais ametumwagia mbolea ya kutosha na isitoshe mbolea yenyewe kwa bei ya ruzuku, tunamshukuru sana. Kama haitoshi, sisi ni wakulima wa zao la tumbaku, kuna kipindi tumbaku iliyumba kwa sababu tulikosa masoko, lakini Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa. Ametutafutia masoko na sasa hivi tunauza tumbaku yetu kwa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, mliopo niwaambie tu msimu uliopita, zaidi ya shilingi bilioni 110 zimeweza kuingia pale Sikonge, tufanye nini sasa Wanasikonge? Kweli tarehe 29 Wanasikonge walijitoa kwa wingi na Mheshimiwa Rais amepata zaidi ya 98% kwenye Jimbo la Sikonge. Hizi 98% hazijaja kwa bahati nzuri, wala bahati mbaya, hapana. Ni kwamba yeye mwenyewe alizitafuta kwa sababu alifanya makubwa ndani ya Jimbo la Sikonge. Tunamshukuru sana na Wanasikonge wanampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija katika suala la maji, leo hii sisi kule Sikonge maji ya kutoka Ziwa Victoria yameingia. Bado kuna changamoto ndogo ndogo, lakini wataalam wanasema kwamba ifikapo Februari Wana-Sikonge wanapata maji ya uhakika kutoka Ziwa Victoria. Sasa Wanasikonge tuseme nini? Hivi tungeenda tukampe nani hizo kura kwa mambo haya mazuri aliyotufanyia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la umeme ndiyo usiseme, wachangiaji wamesema. Leo hii Mheshimiwa Rais anamalizia vitongoji vilivyobaki. Leo katika Jimbo langu la Sikonge nikichukua na hivi ambavyo ametupa sasa hivi siyo zaidi ya vitongoji 50, ndiyo vimebaki ambavyo havina umeme, na ninaamini hata kabla ya 2030 tayari vitongoji vyote vitakuwa vimepata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninarudia kusema tena, 98% aliyoipata haikuwa kwa bahati mbaya wala bahati nzuri isipokuwa alizitafuta yeye mwenyewe kwa kazi kubwa aliyoifanya. Tunamshukuru na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija sasa kwenye tathmini hii. Kimsingi kinachoonekana hapa kwa wananchi wa Sikonge, changamoto kubwa namba moja waliyonayo ni barabara katika maeneo yao. Hata hivyo, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, katika hotuba yake ukurasa wa 28 amesema waziwazi kabisa kwamba anaenda kuongeza bajeti na uwezo wa TARURA. Kwa hali hiyo, sisi Wanasikonge imetupa faraja kubwa sana kwa sababu hii ni changamoto kubwa sana katika eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba Jimbo la Sikonge ni kubwa, ni kubwa sana. Kuna kutoka Makao Makuu ya kata kwenda vijijini, kwa mfano, kutoka pale Sikonge uende Kijiji cha Igalula, ni zaidi ya kilometa 26 kwenda kwenye kijiji. Ni kubwa mno. Kimsingi ni kwamba Jimbo la Sikonge linalingana na baadhi ya nchi jirani. Hivyo tunaomba sasa, TARURA watakapokuja na Wizara, waje na formula, kanuni nzuri ambayo kwa kweli ile bajeti ita-reflect ule ukubwa wa jimbo na mtandao wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana, ninawaomba sana ndugu zangu wa TARURA, ndugu zangu wa Wizara, hebu mjaribu kuliangalia hilo, mje na formula nzuri ili kusudi tuweze kupata ile bajeti kulingana na mtandao wa barabara jinsi ulivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo vilevile limewagusa sana Wana-Sikonge ni ufinyu wa maeneo ya shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji pamoja na urinaji wa asali. Ninamshukuru sana leo hii Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na wizara kwa jibu lake zuri la Serikali kwamba Kamati ya Mawaziri imeshapewa hiyo kazi na imeshaifanya hiyo kazi, kinachosubiriwa sasa ni taarifa ili kusudi hawa wananchi waweze kuongezewa maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba sana, Mheshimiwa Waziri Mkuu uko hapa, ninaomba sana ile kamati sasa itoe hiyo taarifa ili kusudi hawa wananchi waweze kupata hayo maeneo na hii migogoro midogo midogo ambayo inajitokeza iweze kwisha na watu waendelee na shughuli zao za kiuchumi. Tunaomba sana hilo kwa kweli, wafanye namna hiyo. Wakifanya namna hiyo, kwa kweli sisi hizi changamoto ndogo ndogo watakuwa wametuondolea kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni jambo la maji. Kama nilivyosema hapo awali, tayari hivi sasa tunayo maji ya Ziwa Victoria. Ninawaomba tu ndugu zangu wataalamu na Serikali kwamba ijaribu sasa kuangalia kwa sababu tunaenda kwenye gridi ya Taifa ya Maji na kwa hivi sasa kuna kata tisa za awali katika Jimbo la Sikonge ambazo ndizo zitafaidika na huo mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba, kwa vile sasa zinakuja kuingia kwenye mfumo uliopo, kwenye mtandao wa maji uliopo, kwa kweli tunaamini kuna kata tatu zinaenda kufaidika, na yale maji ni mengi na yana pressure ya kutosha na miundombinu ipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaamini kwamba Kata ya Usunga na yenyewe itafaidika, Kata ya Kiloleli na yenyewe itafaidika lakini vilevile na Kata ya Kipanga nayo itafaidika kutokana na huo mradi kwa sababu miundombinu ipo tayari. Maji yakishafika pale ni kuingia tu kwenye ile miundombinu, yanafika na kwenye hizo kata. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba badala ya kuwa na kata zile tisa, sasa tutakuwa na kata 12 na katika zile kata 20, tutabakiwa na kata nane ambazo sasa kwa bajeti ya kuchimba visima, ninaamini wananchi wa Sikonge tutawafikia kwa 100% hata kabla ya 2030.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)