Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ushetu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote ninaendelea kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kibali na baraka zake tele kwa kunirudisha tena Bungeni. Pia, ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu kwa ushindi mkubwa alioupata kwa Watanzania, na leo kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wenzangu ni siku yake ya kuzaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninawapongeza sana wananchi wa Jimbo la Ushetu kwa kuniamini, kwa kunirudisha tena mara ya pili, nami ninaendelea kuwaahidi wananchi wa Ushetu kwamba tuko pamoja na mimi sitawaangusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Spika, Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Mawaziri wote mliopata kibali cha Mheshimiwa Rais. Mimi ninaendelea kuwapongeza sana wote, endeleeni kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwa siku zake 100 hasa kwenye suala la michezo amefanya kazi kubwa sana. Kwenye ukurasa wake wa 36 alisema kwenye kile kitabu ukurasa wa 36 amesema michezo ni uchumi, hatuwezi kupata matokeo makubwa bila kuwekeza. Mheshimiwa Rais amewekeza sana kwenye michezo na leo tumeshuhudia sisi Watanzania, timu yetu ya Taifa imeingia kwenye 16 bora ya Kombe la AFCON, isingelikuwa bahati mbaya inawezekana Taifa Stars ingeleta kombe hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana walijipanga vizuri, vijana walipewa motisha vizuri na kupitia goli la mama, timu zetu za Simba, Yanga, Azam pamoja na Singida leo ziko kwenye 16 bora. Mheshimiwa Rais ameandika historia kubwa kwenye michezo hapa nchini. Tuendelee kumwombea kwa Mwenyezi Mungu, tuendelee sana kumsaidia na kumwombea afya njema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa mikopo ya akina mama kwa upande wa Jimbo la Ushetu, kwa siku 100 za Mheshimiwa Rais wetu, tayari shilingi 1,720,000,000 zimetolewa kwa wananchi wa Ushetu ikiwemo wanawake shilingi 836,000,000, vijana shilingi 835,000,000, na wenye ulemavu shilingi 55,000,000 nani kama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kwenye barabara, tulikuwa na changamoto kubwa ya madaraja, toka uhuru yalikuwa hayapitiki. Mheshimiwa Rais ameletwa shilingi 18,600,000,000 kujenga madaraja ya kisasa. Daraja la Ng’wabomba lilishindikana toka uhuru, shilingi 2,900,000,000 tayari limekamilika, lakini pia Daraja la Ubagwe ambalo wananchi wameteseka kwa muda mrefu, shilingi 4,100,000,000 nalo limeshakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Daraja la Kasenga pale Ulowa kwenda kwa jirani yangu pale Tabora, shilingi 5,100,000,000 daraja la urefu wa meta 80, ni karibu uwanja wa mpira, nalo limekamilika. Pia, tuna Daraja la Sunga, ndugu zangu wa Ng’hwande pale ni mashahidi, tayari pale shilingi 4,200,000,000 zimewekwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nalo daraja limekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hospitali Mheshimiwa Rais hajatusahau. Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu, shilingi 3,500,000,000 nayo imekamilika na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais ameniletea watumishi. Juzi kwenye siku 100 tayari ajira 131 zimemwagwa kwa wananchi wa Ushetu wakiwemo watumishi wa afya 64 na elimu sekondari 56, tayari wameripoti kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nidhamu ya watumishi kwa upande wa Ushetu ni kubwa sana, wanahudumia vizuri wananchi wetu. Ni pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Rais. Leo Mheshimiwa Rais anakuja na Bima ya Afya kwa Wote, ninawaomba, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kwenye hotuba yake na tunanukuu kwamba anakuja na fyekeo kwa wazembe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu wasiwepo watu wa kwenda kushindwa kuwahudumia wananchi waliolipa bima yao kwa sababu ya uzembe wao na hulka zao. Ninaomba Mheshimiwa Waziri haya yafanyie kazi kuhakikisha tunamsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye suala la kilimo, mwenzangu hapa wa Sikonge amesema wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani, mbolea ya CAN ambayo inatumiwa na wakulima wengi hapa nchini ilikuwa imefika shilingi 120,000, leo wananchi wanachukua kwa shilingi 63,000 kwa bei ya ruzuku. LPK ilikuwa imefika shilingi 160,000, leo wananchi kote na ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi wanachukua kwa shilingi 73,000. Mbolea ya urea ambayo pia maeneo mengi tunaitumia ilifika shilingi 160,000, leo wanachukua kwa shilingi 73,000. Nani kama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan? Ni mama amefanya kazi ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye kilimo cha pamba, matrekta zaidi ya 800 yamemwagwa. Wakulima wa pamba walikuwa wanalimiwa kwa shilingi 100,000, au shilingi 60,000 kwa heka moja, leo kote wanalimiwa kwa shilingi 30,000 kwa heka moja. Vijana wa BBT wamemwagwa kule kuwafundisha, watoke kwenye uzalishaji wa kilo 300 au 500 kwa heka moja, tunaenda kuzalisha kilo 1,000 kwa heka moja kwenye eneo la pamba. Wanunuzi tayari wameshapeleka wataalamu. Kwa hiyo, ninaendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado kwenye upande wa tumbaku kama alivyosema ndugu yangu, hali ya uzalishaji ilishuka. Tulikuwa na kilo 240,000, zikashuka mwaka 2015, 2018-2020 zikabaki kilo 68,000, lakini leo zimepanda mpaka kilo 240,000,000 na bei imetoka wastani wa dola 1.75 na sasa ni dola 2.02 na madaraja yetu ambayo wakulima wengi wanayapata L10F ni dola tatu, L1 ni dola tatu, L20F ni dola tatu, C1O dola tatu, madaraja ya dola tatutatu yameongezeka, ni wastani wa shilingi 8,000/= kwa kilo. Ni historia kubwa ameiandika Mheshimiwa Rais kwenye nchi yetu, lazima tumwombee Mheshimiwa Rais wetu, amefanya kazi kubwa sana kwenye suala la ushirika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumbaku ilifika mahali wakulima wakapangiwa uzalishaji, mwenye uwezo wa kulima eka tano, anaambiwa alime eka mbili, mwenye uwezo wa kuzalisha kilo 10,000, azalishe kilo 5,000. Mheshimiwa Rais aliikataa na leo wakulima wanalima kulingana na uwezo wao. Mheshimiwa Rais ametende mambo makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye vyama va ushirika Mheshimiwa Rais tayari kwenye vyama ameanzisha mfumo wa MUVU ambao unasajili wakulima, unasajili vyama vyote. Leo mpaka Mkulima wa Sikonge, Mkulima wa Kigoma, Mkulima wa Songea kwenye upande wa ushirika utamjua yuko wapi? Ana shamba gani? Yuko maeneo gani? Vifaa vya kupima udongo tayari vimepelekwa. Vyama zaidi ya 6,300 vimesajiliwa, wakulima 3,279,000 wote wamesajiliwa kwenye mfumo, tayari wapo kwenye mfumo wa MUVU.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, mizani ya kidigiti ambayo huwezi kumwibia mkulima sasa hivi kwenye maeneo ya ushirika, zaidi ya mizani 4,400 imenunuliwa na vyama vya ushirika. Warajisi wote wa mikoa yote ya Tanzania bara wamepatiwa magari. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo wanaushirika, historia ya Mheshimiwa Nyerere aliyoiacha, Mheshimiwa Rais ameimaliza. Benki ya Ushirika imeanzishwa na inamilikiwa na wakulima kwa zaidi ya 51%. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la sekondari, sisi Ushetu tumepewa zaidi ya shilingi 1,700,000,000, leo shule zetu za msingi zimekarabatiwa zote. Leo ninachukua hatua kuipongeza Shule ya Msingi Nyabusaru iliyoko katika Halmashauri ya Ushetu, ni shule ya kata ambayo imewekewa mazingira mazuri na Mheshimiwa Rais ambapo zamani zilikuwa zinadharaulika sana, imekuwa ya kwanza kwenye mtihani wa Darasa la Nne kitaifa kutoka kwenye shule za kata. Mheshimiwa Rais ameweka mazingira popote, na mimi ninawaalika Waheshimiwa Wabunge, shule ile nafasi zipo, leteni watoto wenu, alama zote 300 zilipigwa pale kwenye shule ya msingi. Kwa hiyo, ni kazi kubwa ya mazingira mazuri aliyoiweka Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa sekondari kwenye Jimbo la Ushetu, ni zaidi ya shilingi 6,300,000,000 zimepelekwa kwa Mheshimiwa Rais, shule mpya sita na shule ya watoto wenye vipaji ya shilingi 1,600,000,000 imejengwa na imeshakamilika, watoto tayari wameanza kusoma. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana, nami ninaendelea kumpongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku 100 za Mheshimiwa Rais, wananchi wanaona, ajira zimeongezeka, na juzi tu amemwaga tena ajira nyingine 5,000. Huyu mama jamani, hebu ninaomba tumpigie makofi ya kutosha. Amefanya kazi kubwa mno. Leo ushindi alioupata zaidi ya 97% ni halali yake mama wa watu. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni kama vile alivyosema Mheshimiwa Mbunge moja hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye michezo amefanya, kwenye mambo ya ushirika; kwetu sisi wakulima, amefanya; kwenye elimu amefanya; kwenye afya amefanya; kwenye barabara amefanya; na kwenye umeme amefanya. Sasa Waheshimiwa Wabunge leo kwenye umeme mnaona vitongoji vyenu vyote zaidi, kwenye jimbo langu, vitongoji 134 vilivyokuwa vimebakia, leo tayari wakandarasi wako kazini, tushindwe wenyewe. Maji ya Ziwa Victoria tayari shilingi 44,000,000,000 mkandarasi yuko site kazi inafanyika. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ya kusema ni mengi, lakini kubwa sana twendeni tukamsaidie Mheshimiwa Rais, tukawaambie Watanzania nini kimefanyika katika majimbo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)