Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuwa mzungumzaji wa kwanza kwenye hoja iliyopo Mezani. Kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya na uzima wa kuwa mahali hapa. Kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuchaguliwa kwa kishindo kikubwa na kuwa Rais na hatimaye kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi hiki cha 2025/2030. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa niwapongeze pia Mawaziri, waliowasilisha hoja zilizopo mbele ya Bunge lako Tukufu, kwa kuanzia na Mheshimiwa Prof. Alexander Mkumbo, ambaye ni Waziri katika Ofisi ya Rais akisimamia eneo la Mipango na Uwekezaji; na Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar, ambaye ni Waziri wa Fedha kwa mawasilisho yao ambayo wameyatoa mbele ya Bunge letu Tukufu na sisi sasa tunao wajibu wa kutoa mapendekezo yetu, namna bora ambavyo mipango hii takribani yote mitatu itakwenda kuongeza tija katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Rais, aliyoitoa wakati anafungua Bunge hili, alieleza bayana kwamba anatamani itakapofika mwaka 2030 nchi yetu iwe katika kipato cha juu cha kati. Maana yake nini? Maana yake ni kwamba zipo sekta ambazo zimetajwa katika mpango ni lazima tuzipe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaziona sekta mbili ambazo ningependa nitoe mchango wangu. Sekta ya kwanza ni sekta ya kilimo, ambayo kwa sasa inachangia zaidi ya takribani 26% katika pato la Taifa. Sekta nyingine ni sekta ya madini ambayo sasa imefikia wastani wa 10.1% kwenye pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini haya mapendekezo tunayoyatoa yakienda kufanyiwa kazi baada ya kipindi kifupi kufika hiyo 2030 tunaweza tukafikia hicho kiwango cha kati cha juu cha uchumi kama ambavyo ninakwenda kueleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza kwenye kilimo bado nina imani kwamba 65% ya Watanzania wamejiajiri katika kilimo; na hawa ni wale ambao shughuli yao akiamka asubuhi, akishinda mchana, akilala jioni anawaza kilimo. Ukiacha zile kama 15% hivi za wengine ambao wanajishughulisha na kilimo na shughuli nyingine kufikia 80% au 65% ndio wanabeba jukumu la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu, katika viwanda malighafi zinazotokana na mazao mbalimbali ni zaidi ya 65% kwenye uzalishaji wa viwanda. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba, sisi tukitaka tuwe na uchumi mkubwa na uchumi shirikishi, ni lazima tuingize fedha nyingi katika kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninataka kusema bado hatujakuwa na mipango madhubuti ya kuhakikisha kwamba pamoja na miradi ya umwagiliaji ambayo inaendelea kujengwa kote nchini, lakini bado tupo nyuma sana. Kwa hiyo, ni vyema tukapiga hatua za haraka ili tuweze kufikia haya malengo ambayo ninayasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani, tunazo takribani hekta milioni 44 ambazo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini ninavyozungumza sasa tunazo hekta 500 na mpango wetu ni kwamba ikifika 2030 tufike hekta 1,200; kwa hiyo, utaona bado tupo nyuma sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi zaidi ya 146 ya umwagiliaji ambayo inatekelezwa kote nchini. Miradi 428 imefanyiwa usanifu. Ningependa kuona kwamba hapa juhudi kubwa inaongezwa ili miradi hii ikikamilika wananchi wengi wawe wamejiajiri katika sekta ya kilimo. Tayari tuna geographical advantage kwamba sisi tunauza zaidi katika Ukanda wa SADC na ukanda wa Afrika Mashariki mpaka Afrika ya Kati. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo tulitumie vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji amesema tuna tija ndogo kwenye kilimo. Kwa hiyo, ni lazima tuongeze chachu ya kuongeza tija katika kilimo. Mapinduzi ya viwanda yaliyotokea katika karne ya 19 kwenye Bara la Ulaya yalitokana kwanza na mapinduzi ya kilimo. Ni lazima tuanze na mapinduzi katika kilimo. Tija itaongezeka, pia malighafi zitapatikana na kwenda kuchechemua kasi, ambayo amesema; kasi ndogo ya ukuaji wa viwanda, itakwenda kuwa kasi kubwa tu endapo tutakuwa na malighafi za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tija tunazopaswa kuongeza ni pamoja na kuokoa mazao yanayoharibika kabla ya kwenda kwenye masoko, na kuongeza miundombinu wezeshi katika maeneo ya mashambani ili mazao yaweze kutoka mashambani na kwenda katika maeneo ya viwandani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango yetu inapaswa kuwa jumuishi, himilivu na shindani. Ninapenda kusema, dhima na malengo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo ya Taifa umeweka vipaumbele, lakini kwa masikitiko makubwa Profesa ameweka kipaumbele namba 10 kuweka msukumo katika maendeleo vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani hii ndiyo ingekuwa kipaumbele namba moja. Tutakapoweka msukumo wa maendeleo vijijini, maana yake kule ndiko uzalishaji ulipo na ndiko ajira za Watanzania wengi zitapatikana, na hili tatizo la ukosefu wa ajira pia tunaweza tukapata majawabu yake kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ningependa kutoa mchango ni kwenye sekta ya madini. Sekta hii ya madini pamoja na kwamba tuna madini mengi, lakini bado Taifa letu hatujaweza kujitambulisha vizuri kwamba sisi tumejikita katika eneo gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika madini, tunayo madini ya kipekee kabisa ya Tanzanite, ambayo dunia nzima yapo Tanzania peke yake, lakini hayajatutangaza vyema na kuona kwamba sisi ni watu wa namna gani? Bado tuna reserve kubwa sana ya dhahabu, ambapo inasadikika kuwa tuna zaidi ya tani 1,600 za dhahabu. Tunayo madini ya aina mbalimbali mengi. Shida kubwa ipo kwenye data.
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini yetu tunayo, lakini hatuna data za uhakika. Niombe sana kwenye mpango huu tuhakikishe kwamba tunaiwezesha GST ili iweze kufanya utafiti wa kijiolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi yenye miamba ambayo yanasadikika kuwa na madini ni 16% peke yake ambayo yameshafanyiwa utafiti. Zaidi ya 84% hayajafanyiwa utafiti. Kwa hiyo, inawezekana hata hapa ndani ya Bunge kuna madini, hatujui. Kwa hiyo, ni vyema tukaongeza nguvu katika eneo hili la utafiti wa kijiolojia ili tuwe na data za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maana ya kuwa na data? Tunapokuwa na data tunajijengea uwezo hata wa kujenga ushawishi wakati tunaingia mikataba. Sasa hivi sehemu kubwa ya mikataba yetu inategemea zaidi aidha wachimbaji wadogo au wachimbaji wakubwa ambao wamekuja na wamefanya utafiti wenyewe. Tutakapokuwa na data za kwetu wenyewe ni rahisi hata wawekezaji kutoka nje wakija tunazitumia data kama sehemu mojawapo ya kuanza kufanya proper bargaining.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tunashindwa kufanya bargaining ya kueleweka kwa sababu hatuna uhakika na kilichopo ardhini. Sambamba na hilo, kwenye madini huku ni vyema sana tukatengeneza dira ya madini angalau ya miaka 10 au 15; kwamba tunataka madini yetu yawe namna gani? Pia tuweke malengo, na malengo haya yawe yanapimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo amesema kwenye hotuba yake, kwamba angetamani kuona kwamba siku madini haya yatakapokwisha, basi vizazi vitakavyokuja baadaye tuwaonyeshe kwamba tuliwahi kuwa na madini na rasilimali hizi hapa ama tuwaonyeshe miradi ya kielelezo ambayo imetokana na rasilimali ya madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu tukatengeneza dira ya madini ya kati ya miaka 15 mpaka 25 yenye malengo yanayopimika ambayo yanaelekeza tunataka nini? Tunaweka vigezo. Ni vigezo gani tutavifikia hapo na sekta zipi tunazipanga kuziinua kupitia pato linalotokana na madini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, ahsante sana.