Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie mpango uliopo mbele yetu leo. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazoendelea kufanya kwa Taifa letu. Pia niwapongeze Mawaziri wa wizara zetu mbili ambao wameleta mpango hapa ili tuweze kushauri na kujadili kwa kina juu ya mustakabali wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niseme mambo kama matatu au mawili hivi. Tumeona kwenye mpango uliowasilishwa kwetu hapa asubuhi, pato la mwananchi mmoja mmoja kwa mwaka katika mwaka 2024/2025 ni dola za Kimarekani 1,277; lakini pia GDP yetu kwa 2024/2025 inasadikika kuwa Dola za Kimarekani bilioni 87.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika mpango ambao umeelezwa hapa, mpango wa nne ambao utaisha mwaka 2030/2031 inasadikika yaweza kuwa pato la mwananchi mmoja mmoja kufika dola za Kimarekani 1,638 na GDP kufikia dola za Kimarekani bilioni 118.1.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukisoma Dira ya Taifa ambayo itakwenda mpaka 2050/2051 GDP inasadikika kuwa dola za Kimarekani trilioni moja na pato la mwananchi mmoja mmoja ifikapo 2050/2051 iwe dola za Kimarekani 7,000. Leo tuna 1,277; tunafikaje 2030/2031 dola za Kimarekani za pato la mwananchi mmoja mmoja kuwa 1,638 na 2050/2051 pato la mwananchi mmoja mmoja dola za Kimarekani 7,000? Tunafikaje hapa? Ni lazima kuanzia leo tuanze kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji. Tunazo sekta za uzalishaji mfano, sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima leo tukubaliane hapa kwamba kilimo ni biashara na mkulima ni mwekezaji. Ni lazima tuwachukulie wakulima kama wawekezaji kwenye nchi yetu ili tuweze kupandisha pato la mwananchi mmoja mmoja. Tunajua wazi kuwa Watanzania takribani 80% ni wakulima; lakini kati ya hao wakulima 80%, 65% ni wakulima ambao hawana ofisi. Yaani anatoka nyumbani anaenda kulima; akitoka kulima anarudi nyumbani kwake, ndiyo amemaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ni lazima tumwezeshe huyu mwananchi wa kipato cha chini cha leo ambacho ni dola za Kimarekani 1,277 kwa mwaka afikie dola za Kimarekani 1,638 mwaka 2030 au dola za Kimarekani 7,000 mwaka 2050/2051. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tukiwekeza katika kilimo cha umwagiliaji tutatoboa. Mwananchi mmoja mmoja tukiwekeza katika kilimo cha umwagiliaji, kwa sababu ni lazima tukubaliane sote, sisi wakati tunalima kule enzi za zamani mbolea wala haikuwa kipaumbele; pembejeo siyo kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini mwananchi akilima yakiwepo maji enzi hizo, mwananchi atapata. Kwa hiyo, ni kitu ambacho hakipingani. Ili tulime, cha kwanza, tunategemea maji. Sasa maji tunayapataje? Ni lazima tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wanatamani kuvuna hata mara mbili kwa mwaka, lakini watavunaje mara mbili kwa mwaka kama wanategemea mvua? Haitawezekana. Ili wavune mara mbili kwa mwaka au mara tatu ni lazima tuwe na kilimo cha umwagiliaji. Tutengeneze mabwawa kwenye maeneo yetu, ikiwepo Busega.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna maeneo potential kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Ukienda kule kata za Lutubiga, Shigala, na Lamadi utakuta maeneo mazuri kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, ni lazima tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji. Tukiwekeza mahali hapa, kwanza tutakuwa tumemsaidia mwananchi katika kipato chake, mwananchi mmoja mmoja kutoka hizi dola za Kimarekani 1,277 kufika huko tunapotaka leo kwenye dola 1,638. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi akiwa na uhakika na maji atalima na atapata kipato, na tutapandisha kipato katika mazao ambayo tutakuwa tumetarajia. Nchi kama nchi, leo tumeona tumeambiwa hapa na Mheshimiwa Shangazi, kilimo kinachangia takribani 26%. Tukiwekeza katika eneo hili, ifikapo 2030 tunaweza kuwa tumefika kwenye 40% hata 50% kwa sababu sehemu mojawapo tuliyo na uhakika na ajira ni eneo la kilimo pamoja na eneo la viwanda na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, twendeni tukawekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji ili wananchi wetu waweze kunufaika na kilimo ambacho leo wanataabika na upatikanaji wa maji kwenye maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tunatambua wazi kwamba ili tumsaidie mwananchi huyu ni lazima pia makato yanayojitokeza kwenye kilimo tuyapunguze. Wakati mwingine mwananchi analima kwa tabu, wakati mwingine hatuendi kumsaidia wakati wa kulima, lakini wakati wa kuvuna anapokwenda kuuza tunakuwa na makato mengi, ambapo hatumsaidii mwananchi anayetegemea kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatakiwa sasa ifike sehemu Mheshimiwa Waziri, hasa Waziri wa Kilimo aliangalie sana hili, ili tumsaidie mwananchi tumpunguzie makato ambayo hayana tija. Nitoe mfano mmoja, sisi Mkoa wa Simiyu ni wakulima wa pamba. Ukilima pamba unapata pembejeo. Unapewa pembejeo kwa mkopo ambapo utakuja ulipe wakati wa kuuza pamba yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na hilo. Mimi sina tatizo, lakini wananchi hawa wanakatwa shilingi 300 kwa kilo ya pamba unapoenda kuuza kugharamia pembejeo bila kufuata ni kiasi gani mwananchi huyu alichukua pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani mwananchi alipe kulingana na kile alichokopa na kulingana na kile alichopewa. Kama mwananchi amepewa pembejeo; tuchukulie pembejeo kilo 100 akazalisha pamba kilo 10,000 na mwingine hapa amepewa pembejeo kilo 100 akazalisha pamba kilo 1,000 kuna tofauti kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote wamechukua pembejeo kilo 100, lakini uzalishaji huu unatofautiana kulingana na vile ambavyo wewe umetunza eneo lako na ulivyotunza kilimo chako, lakini mwisho wa siku katika kurudisha ule mkopo unalipa kulingana na vile alivyozalisha shilingi 300/= kwa kilo bila kujali ni kiasi gani ulikopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningetamani mtu aliyekopa kilo 100 akatwe kulingana na kilo 100 alizokopa na wala siyo kukata lumpsum ambapo tunawanyonya wananchi wadogo wadogo ambao wanategemea kilimo, na leo tunataka wafike kwenye pato la mwananchi kwa mwaka 2030/2031, 1,638 US Dollars. Hawatafika kama tutakuwa tunawalimbikizia makato makubwa kiasi hiki ambayo wao yatawakatisha tamaa kwenye suala zima la kulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani kuishauri Serikali iliangalie hili. Kwenye ushuru huko kuna kitu kinaitwa Pay As You Earn. Sasa ninatamani na huku kwenye zao la pamba na lenyewe kuwepo na kitu kinaitwa Pay As You Use, yaani ulichotumia ndicho ambacho urudishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme tuna haja ya kuliangalia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nimeona kwenye Mwongozo wa Uandaaji wa Mpango na Bajeti, Waziri wa Fedha amesema hapa kwamba wale Maafisa Masuuli wanaosimamia mifuko maalumu, waweze kutenga asilimia tano kwa ajili ya kupeleka kwenye uzalishaji wa kiuchumi kwenye maeneo mengine. Mimi la kwenye uchumi huko sina tatizo, tatizo langu ni kutenga asilimia tano kwenye mifuko mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema tu hapa kwamba tunayo mifuko ya maji, tuna mfuko wa barabara, tuna mfuko wa TRC, tuna Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote; yakikatwa asilimia tano, tunadidimiza sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Watanzania walio wengi bado wana shida ya maji, leo Watanzania walio wengi bado wana shida ya barabara. Tumeweka vyanzo kwa ajili ya ku-boost barabara, kwa ajili ya ku-boost maji, kwa ajili ya ku-boost maendeleo ya mawasiliano kwa wote...
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tena tunakuja na mpango tukate asilimia tano ili tupeleke kwingine wakati huku bado hatujamaliza. Hili siungi mkono, ninaunga mkono maelezo ya Kamati kwamba tuachane na hii habari, hizi fedha ambazo tumetenga kwa ajili ya mifuko, tuiache kama ilivyo, tupeleke kwa wananchi. twende tukatekeleze miradi ya maji, miradi ya barabara na miradi mingine. Wakandarasi bado hawajalipwa, leo tunataka tukate tena! Haiwezekani. Mimi kwa hili siungi mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja ya Kamati. Ahsante sana. (Makofi)