Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tanganyika
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Mpango. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kura nyingi alizozipata na kupewa dhamana ya Watanzania. Pia ninawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wote wawili; Waziri anayeshughulikia mpango Mheshimiwa Profesa Kitila na Waziri wa Fedha kwa kuleta mpango ambao ni mzuri endapo utatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nijikite zaidi kwenye eneo ambalo Watanzania wengi wanategemea hasa kwenye suala zima la kilimo. Watanzania wengi wanategemea sekta ya kilimo ambayo ndiyo inaendesha maisha yao. Kwenye mpango tumeona mipango mizuri ya Serikali, lakini tunakazia kwenye eneo la utekelezaji. Ili wananchi waweze kuendelea, ni vyema Serikali sasa ikajikita kwenda kusimamia miradi ya kilimo hasa cha umwagiliaji. Eneo hili ni muhimu ili wananchi waweze kuwa na uhakika wa uzalishaji kuliko ilivyo kwa sasa wanalima kilimo cha kubahatisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mipango mizuri iliyofanywa na Serikali hasa kwenye ruzuku ya pembejeo, wamejitahidi sana, Serikali wamepeleka mbolea na pembejeo nyingi, lakini bado wakulima wetu wanalima kilimo cha kubahatisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa mwaka 2025 ulioishia mwaka 2025, Serikali ilikuja na mkakati wa kilimo cha umwagiliaji, lakini bahati mbaya sana karibu miradi yote ya umwagiliaji ni mibovu na haijafanya kazi. Kwa hiyo, tunaomba kwenye eneo la usimamizi waende wakasimamie ili kilimo kiweze kuwainua Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wengi wanalima kilimo cha kujikimu. Sasa tunataka watoke kwenye kilimo hicho cha kujikimu waende kwenye uzalishaji ambao utakuwa na tija sambamba na kuwapa vifaa vya uzalishaji ambavyo vitawawezesha Watanzania kuzalisha na nchi iweze kupata ziada ya kuuza mazao sehemu ya nje ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kilimo kinaenda sambamba na viwanda; ili mkulima aweze kunufaika tunahitaji sasa tupate viwanda ambavyo vitawasaidia Watanzania kuweza kuweka thamani ya mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna eneo la uvuvi, na tuna eneo la ufugaji. Tanzania ni nchi ambayo bado uvuvi ni eneo dogo sana linalotoa mchango kwenye pato la Taifa. Eneo hili tunapaswa kuwasaidia wananchi. Nchi zilizoendelea sasa hivi wanapata fedha nyingi sana kwenye uvuvi, ni kwa sababu wamewekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba uwekezaji mkubwa, kwani nchi yetu ina eneo la bahari kuanzia eneo la Mtwara mpaka Tanga, lakini bado hakuna kitu ambacho kinaweza kuwawezesha hawa wafugaji, wavuvi ambao wanafanya shughuli za uvuvi kwenye maeneo haya. Tuwape fedha, tuwawezeshe vitendea kazi ili waweze kuwa na uzalishaji mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi wa kisasa unahitaji vifaa, uvuvi wa kisasa unahitaji vizimba ambavyo vimetumika katika maeneo mengi ambayo wanazalisha. Tunaomba kwenye maeneo haya yafanyiwe kazi. Pia tuangalie eneo la mifugo. Kwenye mifugo kama hakuna uwekezaji hasa wa kutenga maeneo ya malisho na maeneo ambayo watanyweshwa mifugo wapate huduma, hatuwezi kupata mifugo mizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina nafasi ya kupata masoko ya nje, kama tutakuwa tumewekeza kwenye eneo hili. Ninaomba tuwekeze kwenye maeneo haya. Kwenye eneo la madini, nchi yetu ina madeni mengi, lakini tupo nyuma sana kwenye utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti tunaoutegemea kwa sasa ni wa wachimbaji wadogo wadogo. Kwa bahati mbaya hawa wachimbaji wadogo wadogo wakivumbua madini, wanakuja kufukuzwa na watu wanaoitwa wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana tuwekeze kwenye utafiti. Utafiti ndiyo utakaotufanya sisi tutoke kwenye hatua tuliyopo kwa sasa. Leo tunazungumzia machimbo ya almasi, toka madini haya ya almasi yalivyogunduliwa pale Mwadui, miaka yote, miaka nenda rudi hiyo almasi ni ya hapo hapo Mwadui. Ni kwa sababu hakuna utafiti uliofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba maeneo ya madini tuwekeze zaidi utafiti, kwani nchi itanufaika kwa sababu tuna madini ya aina mbalimbali kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mazingira, nchi yetu ina misitu mingi ambayo imemilikiwa na Serikali, lakini bado hatujanufaika kwenye maeneo haya ya uhifadhi wa mazingira. Nchi nyingine zinanufaika kwa kiwango kikubwa. Kuna sera ya utunzaji wa mazingira pamoja na uhifadhi unaopata na hewa ya ukaa (Carbon). Niombe sana, Serikali kwenye maeneo haya iweze kuangalia kwa jicho pana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wananufaika sana, wanapata fedha nyingi. Ninawaomba wenzetu ambao wapo kwenye suala la usimamizi, waweze kutafuta masoko tuweze kuuza kwa wanunuzi ambao ndio wanaonunua kuliko ilivyo sasa tunawapa middleman ambao wapo katikati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninaishauri Serikali hata maeneo ambayo misitu inamilikiwa na Serikali kwa maana ya (National Park) na wao waweze kunufaika kuliko ilivyo kwa sasa wanufaikaji ni misitu ambayo iko chini ya Serikali za Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye eneo la miundombinu. Pamoja na yote mazuri tutakayoyafanya, kama hatujakuwa na uwekezaji mzuri kwenye maeneo yale ambayo yanaweza yakakuza uchumi, tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwenye eneo la mpango mmezungumzia ukuzaji wa uchumi hasa kwenye eneo la Liganga na Mchuchuma. Sasa ili uweze kuchimba hayo machimbo ya makaa ya mawe na chuma ni lazima ujenge reli ya kutoka Mtwara kwenda Liganga ifike kwenye eneo la Ziwa Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga bandari karibu kila eneo na tunaipongeza sana Serikali. Bandari ya Mtwara ni nzuri; Bandari ya Dar es Salaam imekuwa na mapato mazuri; Bandari ya Tanga kumechangamka, lakini zipo bandari zilizopo kwenye maziwa makuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Karema tumejenga bandari kubwa ambayo bado haijafanya kazi. Kwenye Mpango, lazima twende sambamba na uwekezaji nje ya nchi ya DRC Congo ili tuweze kupata rasilimali zitakazoifanya bandari ile iweze kufanya kazi, sambamba na kujenga barabara ya kutoka Karema kuja eneo la Kabungu ili iwe kiunganishi kwa ajili ya kuifanya Bandari ya Dar es Salaam iweze kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana wa kunipa nafasi. Nami ninataka kuungana na wenzangu waliosema ni vyema mifuko yote iliyowekwa kisheria tusiingize kwenda kupunguza, itatufanya tusipate hiyo miradi ya maendeleo. Mfuko wa Reli, Mfuko wa Barabara, Mfuko wa Maji vinategemea sana upatikanaji wa hizo fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)